NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI NA TATU

Baadhi ya maofisa walikuwa wameugeuza uwanja wa ndege kuwa njia ya kupitisha dawa za kulevya. Raymond Keneko, alikuwa Afisa Mwandamizi Kitengo cha Ukaguzi wa mizigo. Kiutendaji ukimuona utaamini kuwa ni mtu makini, mwenye msimamo wa kati, asiyeyumbishwa katika kazi zake. Lakini alikuwa mmoja wa watu hatari, dhaifu waliopenda kupokea zawadi kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa, bila kujua kuwa zawadi hizo ni kishawishi.

Ndiyo kwanza Kenoko alikuwa amefikisha umri wa miaka arobaini na saba. Akiwa mmoja wa watumishi wachache wa uwanja wa ndege waliokuwa wakipokea pesa nyingi kutoka kwa mzungu Carlos Dimera, kila wakati mzigo wa dawa za kulevya unapokuwa njiani kuletwa Jijini Dar es Salaam. 

Asubuhi hii wakati Kenoko akipata kifungua kinywa nyumbani kwake, alipokea ujumbe kutoka Hawa Msimbazi, ukimjulisha kuwa malighafi za kiwanda cha kutengeneza vidonge vya malaria zilizokuwa zimekwama nchini Ethiopia baada ya kukosa usafiri sasa tayari kuletwa Tanzania. Kutokana na uzito wa ujumbe huo, Raymond Kenoko alilazimika kuacha kila kitu mezani, akafanya maandalizi yake na kuondoka haraka kuelekea kazini.

Mkewe na watoto waliyajua vizuri majukumu yake, hivyo hawakushangazwa na kitendo cha kuacha chakula mezani. Alipofika ofisini, aliwapanga vizuri watu wake, aliweka kila jambo katika mstari, akipita kila idara inayohusika na ukaguzi wa mizigo akiweka mambo sawa. Baada ya kila jambo kuwa limefanikiwa, aliwasiliana na Hawa Msimbazi.

"Nakujulisha kuwa kazi yangu imekwisha, kazi imebaki kwenu dadangu, njia zote za kuingia na kutoka ziko wazi. Mwambie Carlos asihofu, kila idara imejulishwa kuhusu kuingia kwa mzigo huo, bahati nzuri ni kwamba wakuu wa idara zote wamepewa amri kuushughulikia mzigo wenu haraka, wanasubiri mgao wao", Raymond Kenoko alimjulisha Hawa Msimbazi.

"Umesomeka kakangu, Carols mwenyewe amesema malipo yako yataongezwa, kazi unazofanya kwa upande wetu zinastahili nyongeza, mimi kama mwakilishi wake, naahidi kuongeza posho zaidi", alisema na kukakata simu. Kisha aliwasiliana na Carlos Dimera.

"Habari ya asubuhi bosi?", Hawa alimsalimia Carlos.

"Niko salama, una habari gani nzuri?", alihoji Carlos Dimera.

"Habari nzuri ni kwamba Uwanja wa ndege kumeeleweka. Taratibu zimekwenda vizuri, Mr. Raymond anasema kwa upande wao hakuna shaka, kazi imebaki kwetu, tena amenihakikishia kuwa idara zote zinazohusika kupokea mizigo zimejulishwa kuhusu kuingia kwa mzigo huo, hali ni shwari".

"Nimekupata Condeliza Rise, maana hauna tofauti kabisa na mwana mama wenye jina hilo, kazi alizofanya akiwa Waziri wa Mambo ya Nje Marekani, zilitosha kumfanya awe kivutio kwa wanawake wenzake duniani. Ngoja niwasiliane na wakala ili mzigo usafirishwe kwa ndege ya usiku leo.

"Fanya hivyo bosi, kilichonisisimua zaidi ni kwamba, huyu Raymond ambaye ndiye Afisa mkaguzi, anasema njia ziko wazi".

"Asante Hawa, wapange watu wako vizuri mkaupokee mzigo huo, sitaki kusikia jambo baya limewakuta", Carlos alibainisha.  

"Tuko tayari kwa mapokezi na kwa lolote, napata faraja kwamba, Raymond amesema hali ni nzuri kuliko wakati wote, hususan baada ya Waziri aliyekuwa akiwafuatilia na kuweka kamera za CCTV uwanjani hapo kuhamishiwa wizara nyingine, hii imetuongezea nguvu na matumaini", Hawa alisema.

"Oke, niwatakie kazi njema na mapokezi mema, lakini tuwasiliane, kila hatua mtakayokuwa mnijulishe, lolote laweza kutokea", Carlos alieleza wasiwasi wake.

"Ni kweli bosi. Tutakujulisha", aliongeza Hawa Msimbazi. Baada ya Carlos kuongea na Hawa. Alifanya mawasiliano ya mwisho na wakala.

"Habari ya asubuhi kaka?", Carlos Dimera alisalimia.

"Huko Tanzania ni asubuhi, Addis Ababa ni mchana, tunakula chakula, leta taarifa?". 

"Ndio maana nikakupigia. Najulisha kuwa hali ya Dar es Salaam ni shwari kabisa, vijana wako tayari kupokea mzigo, kulikuwa na mvua za rasharasha na mawingu ya hapa na pale, lakini sasa yamedhibitiwa, itakuwa vizuri mzigo ukiingia Dar es Salaam leo usiku. Hali ni nzuri", Carlos Dimera alieleza.

"Mzigo uko tayari, kilichokuwa kikisubiliwa ni taarifa za awali kutoka kwenu, hata hivyo Mamlaka za usalama nchini hapa Ethiopia zilianza kuhoji kuwepo kwa mzigo huu, lakinimaofisa wetu makao makuu Bogota, Colombia waliwasiliana na mamlaka za hapa na kuzijulisha kuwa mzigo huu unaopita, naamini utaingia leo Dar es Salaam", alieleza wakala.

"Asante na samahani kwa kuchelewa kutoa taarifa za awali, hii imetokana na hali ya usalama nchini Tanzania kuwa si ya kuaminika wakati huu, kiasi fulani mambo hayaeleweki. Serikali ya sasa haitabiriki, kwa kuwa mipango imekaa vizuri sasa tuko tayari kupokea mzigo, ambao utawafanya vijana wengi wa nchi hii kupoteza mwelekeo baada wakivuta dawa hizi za kulevya", Carlos alieleza na kukata simu. 

Ndio kwanza nilikuwa nimeamka kutoka usingizini, kuchelewa kwangu kuamka si kwamba mimi ni mtu mvivu, la hasha, hali hii ilitokana na mimi kuchelewa kulala usiku kutokana na kazi nilizofanya. Kama wewe ni binadamu mwenye huruma, utaona ni jinsi gani mimi nilistahiri kulala mpaka muda huu.

Ilinilazimu kulala KB Hoteli iliyoko Mabibo ili asubuhi niweze kuonana na shemeji yangu Mama Feka, ambaye pia alifikia katika hoteli hii. Kilichonitoa usingizini ni kelele ya mwito wa simu iliyopigwa na Peter TWite, Vinginevyo ningeendelea kuuchapa usingizi, nilijivuta taratibu na kupokea simu.

"Jambo Mkuu", sauti ya Peter ilipenya masikioni mwangu.

"Oh Peter, Jambo. Habari ya asubuhi".

"Habari nzuri mkuu, nakujulisha kazi uliyonituma, vijana wako kwenye pointi kama ulivyoshauri, kuwatambua kila mmoja amevaa fulana na kofia nyeusi za NSSF. Ili kuepusha usumbufu, nimewajulisha wavae kofia ziangalie nyuma, maana anaweza kutokea mtu mwingine amevaa vile ikawa shida", Peter alieleza.

"Asante Peter, kama nilivyokufahamisha, usishughulike na jambo lolote mpaka nitakapokujulisha, usizime simu, usiwe mbali na eneo lako, kuna kazi moja itabidi uifanye majira ya saa tisa alasiri hivi. Usiniangushe", nilisisitiza.

"Siwezi, siwezi kabisa kukuangusha mkuu. Utakapokuwa tayari kunituma kazi yoyote utanifahamisha, nafahamu wakati tuliomo bosi, niamini tafadhali".

"Usijali Peter, wewe endelea mpaka nitakapokujulisha vinginevyo". 

"Tuko pamoja".

Niliwasiliana na Luteni Fred Libaba nikamjulisha mahali nilipokuwa, niliagiza awachukue Luteni Claud Mwita na Sajenti Julius Nyawamiza, awalete KB Hoteli chumba namba kumi, floo ya pili. Nikamjulisha kuwa wakifika wanipigie simu. Ningia maliwatoni, nikafanya usafi wa mwili wangu, nilikoga, nikanyoa ndevu na kujiweka vizuri, halafu nikashuka chini kwa ajili ya kifungua kinywa.

Sebastian alikuwa mmoja wa rafiki zangu, kazi yake ilikuwa dereva taksi, alifanya kazi zake sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam. Kijana huyu ndiye aliyenileta hapa usiku, nikamfahamisha pia anifuate saa mbili asubuhi na tayari alikuwa amefika kunichua.  
"Umelala saa ngapi Seba?", nilimuuliza.

"Hizi kazi zetu hatuna muda wa kulala, dereva taksi halali kaka, unaposubiri wateja, ndiyo nafasi ya kulala hiyo", alieleza Sebastian.

"Nitakuwa na wageni, nahitaji kutumia gari yako kwa shughuli zangu binafsi. itakuwa siku ya leo na kesho, nitakulipa", nilimwambia.

"Hakuna shaka kaka, funguo za gari hizi hapa, ukimaliza mambo yako utanijulisha, iwe siku mbili, wiki au mwezi". 

Baada ya kupata kifungua kinywa, nilisimama, wakati najiandaa kurejea chumbani kwangu, Fred, Claud na Nyawaminza waliingia. 

"We Fred, ina maana mlikuwa karibu sana?", nilimuuliza.

"Hata sisi tumelala Mabibo, niliwaambia wenzangu, Teacher asipolala Sinza, basi atalala Mabibo, utabiri wangu umekuwa sahihi", alieleza Fred. 

Tulipanda ngazi tukaingia chumba namba kumi, "Karibuni, baada ya kutoka nyumbani kwa Carlos usiku, niliona vyema kulala hapa. shemeji yangu Mama Feka yuko chumba namba nane, kwa kuwa tumekutana wote hapa, ngoja nimwite aje mbele yenu, itakuwa vizuri mkimfahamu", niliwaeleza wote wakatingisha vichwa kukubaliana nami.

Nilisimama kwa sekunde kadhaa nje ya mlango wa chumba namba nane, nilijiuliza maswali kadhaa, ambayo majibu yake yalielekea kunishinda. Nilijiuliza kuhusu kazi ninayotaka kumtuma mwana mama huyu, ni sahihi au namuingia katika matatizo. Hata hivyo nilipiga moyo kinde, nikagonga mlango, akaniruhusu kuingia. Mama Feka alikuwa amevaa kaptula na fulana, zilizomfanya apendeze sana.

Jasho jingi lilikuwa likimtoka mwilini kwa sababu ya mazoezi, aliponiona akasitisha mazoezi na kunisalimia, "Sema shem wangu, umelala salama?".

"Niko salama kabisa shem, ama kweli wewe ndiye Cnthia Rothrock wa ukweli, nimelala hapa chumba namba kumi, niko na wenzangu, wanahitaji kukuona, ukimaliza mazoezi yako, njoo room namba kumi tuzungumze kidogo", nilimwambia.

"Dakika moja", alisema Mama Feka nikatoka nje na kumwacha akijiandae. Maana vitu vingine vya shemeji sina ruhusa ya kuviona.  
ITAENDELEA 0784296253  

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru