NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI NA NNE

"Tumsubiri kidogo, anakuja, alikuwa katika mambo ya kujiweka sawa kiafya", niliwajulisha wenzangu, waliokuwa kimya, wakainua vichwa vyao juu kuonyesha ishara kuwa wamenielewa. 

Wakati tunamsubiri Mama Feka, niliona ni vyema nitumie nafasi hii kuwaeleza habari ya usiku. "Fred, niliwahi kukwambia siku zote usiamini maneno ya mtu, wakati tunamsubiri Mama Feka, labda nitumie nafasi hii kukujulisha kuwa Carlos Dimera si binadamu wa kawaida, ni aina ya mnyama tena hatari zaidi ya chui", akanitolea macho na kunishangaa.

"Ehee, imekuwaje bosi, maana kiasi fulani umenishitua?", alihoji Fred kwa shauku kubwa.

"Sikiliza Fred, huyu mzungu rafiki yako, au sijui ni nani kwako, anamiliki kikosi kikubwa cha uhalifu hapa jijini, sasa nakwambia tukifanya mchezo tumekwisha, take care", nilimwambia.

"Si rafiki yangu kabisa, kumbuka nilikwambia habari za huyu mzungu nilielezwa na rafiki yangu mmoja wa polisi, binafsi sijawahi hata kukutanishwa nae", alijitetea.

"Basi elewa hivyo, mimi nilimtilia shaka mapema kabisa, ndiyo maana nimejiridhisha baada ya kufika nyumbani kwake usiku. Huyu mzungu ndiye chanzo cha mambo yote ya uhalifu hapa jijini, sasa nasema ama zake ama zangu, amejiandaa vizuri sana, lakini sisi pia tuko vizuri, au vipi jamani?", niliwauliza wenzangu huku wote wakiniunga mkono.  

"Sasa ajiandae kukutana na mkono wa sheria, watu kama hawa siku zao ni arobaini, mwisho wake umetimia, kama ulivyosema, ama zake ama zetu, naamini tutashinda", Julius Nyawaminza alieleza kwa hasira.

Niliwaeleza kila jambo, jinsi nilivyoingia nyumbani kwa Carlos Dimera, hali ya ulinzi ilivyokuwa na mipango yao ya uhalifu waliyokuwa wakipanga. "Walikuwa katika sherehe, eti wakisherehekea kifo changu, cha ajabu hawakuweka ulinzi wa aina kabisa, wameamini nimekufa, siku wakiniona watatamani ardhi ipasuke". 

"Kama ndivyo kwanini tusiwakamate mapema ili kuokoa muda?", Claud alihoji na kuongeza, "Maana kila kitu kiko wazi, sasa sijui tunasubiri nini mkuu?".

"Ni kweli kabisa Claud, kama inawezekana wakamatwe wakati ni huu sasa", Nyawaminza alirukia kuunga mkono maneno ya Claud.

"Hapana, tusikurupuke kufanya jambo ambalo halina tija kwa taifa. Sikilizeni, ingekuwa kazi ni kuwakamata tu, ningewaita hata usiku tukawamata kama kuku, lakini tutakuwa tumefanya kazi ya bure, lazima muelewe kuwa nchi yetu inatawaliwa kwa mjibu wa sheria, huwezi kumtia mtu hatiani bila kuwa na ushahidi. Fred... unadhani inawezekana, haya sawa, tutamfikisha mahakamani kwa kosa lipi?", niliwauliza.

"Hakika bosi, itakuwa vigumu kumkamata mtu bila ushahidi, nashauri tufanye kila njia wakamatwe na ushahidi", alishauri Fred, wote tukamuunga mkono.

"Leo tutafanya kazi moja ndogo, lakini yenye faida kubwa kwetu. Fred jiandae tutakwenda kumkamata mtu mmoja anaitwa Raymond Kenoko, huyu jamaa ni Afisa wa Uwanja wa ndege, Claud na Nyawaminza nitawaelekeza cha kufanya, halafu...", kabla sijaendelea mlango uligongwa, Mama Feka akaingia.

"Habarini za asubuhi", Mama Feka alisalimia.

"Oh, nzuri, nzuri", tulimwitikia kwa pamoja. suluali ya blue na fulana ya njano, alizovaa zilimfanya apendeze sana, aliingia na kusimama mfano wa mtu anayesubiri kupandishwa kizimbani.

"Pole na safari shem wangu, pole kwa kukukatisha usingizi wako, pole kwa kila nililokukosesha kulifanya asubuhi ya siku ya leo", nilimuomba radhi.

"Usijali shem", Mama Feka alisema kwa mkato huku akitabasamu.

"Jamani, huyu mwana mama ni shemeji yangu kabisa, ametoka Nyamuswa kwa ajili ya kushiriki mahafari ya chuo kikuu huria, lakini kabla hajafika huko chuoni nikamuomba aonane na sisi kwa ajili ya mambo fulani fulani ambayo tutamuomba atusaidie", niliwaeleza wenzangu wakatingisha vichwa. 

"Kazi gani tena shem? Mbona unanitisha jamani".

"Usiogope molamu, labda nieleze moja kwa moja utanielewa". Nilitumia nafasi hiyo kuwatambulisha wenzangu kwake ili awafahamu, halafu niliendelea. "Hapa jijini limeibuka kundi moja hatari la wafanyabiashara wa dawa za kulevya, hawa jamaa ndiyo wanauzia watu madini feki kama umewahi kusikia, wanateka watu na kuwapora mali zao mchana na usiku, wanaibia watu kwa mtindo wa noti au dolla bandia, mji umechafuka kwa ajili yao, sasa sisi hatukubaliani nao", nilimwambia.

"Umenikumbusha mbali, mwanangu aliwahi kuibiwa kwa mtindo wa madini feki, wakachukua ada yote ya shule, hao watu ni wauaji kabisa", alieleza Mama Feka.

"Pole, sasa kinara wao yuko hapa ni mzungu, huyu mzungu ndiye anafadhili mambo haya, lakini kumkamata imekuwa ngumu kidogo", nilieleza.

"Kuna ugumu gani shem?, mtu kama huyo si anakamatwa tu jamani, mwanangu alilia sana siku hiyo, alikuja na chupa akidai ameuziwa madini, iliniuma sana jamani, kwa hiyo ulitaka nieleze ilivyokuwa?", aliuliza.

"Hapana shem, kuna jambo moja la msingi sana ambalo tumelijadili na wenzangu kwa muda mrefu, baada ya kutafajari kwa kina, tukaishia kukuchagua wewe utusaidie kufuatilia mambo fulani, ambayo yatatuwezesha kumtia hatia mtu huyo", nilimwambia akacheka.

"Ehe, mnataka mimi nifanye nini?", alihoji.

"Tunataka tukutume ujiingize upande wake iwe rahisi kwetu kumkamata na ushahidi, unasemaje shem?", nilimuuliza.

"Heeee, shem hivi inawezekana mtu akajipeleka mwenyewe jehanam, si hatari hiyo, kwanza mimi nimekuja Dar kwa kazi nyingine, aaah itakuwa ngumu, hivi nitaanzaje kujiingiza huko?", alilalama Mama Feka huku akisimama.

Nilishika kichwa, nikainamisha uso wangu chini, nilianza kutafakari hili na lile nikitafuta majibu lakini nikakosa. Wenzangu, Claud Mwita, Julius Nyawaminza na Fred Libaba nao walikuwa kimya wakiniangalia.

"Keti tafadhali shem". Nilitumia nafasi hiyo kumweleza mambo mengi yanayoweza kumfanya binadamu akaonekana shujaa kwa watu, nilimuomba arejee alipokuwa ameketi. Nikasimama, nilitembea kutoka kona moja ya chumba hiki kwenda upande mwingine. 

"Samahani shem, si kusudio langu kukuingiza kwenye moto, kukutuma ujiingize upande ule si kwamba tutakuacha tu, tutakuwekea ulinzi wa hali ya juu, tutakufuatilia wakati wote, kuhusu usalama wako ondoa shaka", nilieleza.

"Sawa, lakini nitaanzaje kujiingiza upande wao, kwanza wataniamini vipi?".

"Tunataka kujaribu kitu kimoja, tumepata taarifa kuwa huyu mzungu Carlos Dimera, anapenda sana wasichana wazuri, kila anapowaona hupagawa, ndiyo maana nikasema kwako itakuwa rahisi atanasa, na akinasa hatutakuacha tu, tutakufuatilia kila hatua utakayokuwa", nilimwambia.

"Mmmm, sasa naanza kukuelewa, unataka nitumie mbinu zangu huyo mzungu Carlos anipende au sivyo?".

"Ndivyo tunavyotaka", Nyawaminza aliyekuwa kimya kwa muda mrefu akitafakari aliongeza. 

"Majaribu haya, sina jinsi, niko tayari kuwasaidia sasa natakiwa kufanya nini?".

"Tutakuwezesha kwa pesa na mavazi. Tumepata ratiba kuwa huyu mzungu kila siku lazima afike Msasani Shopaz Plaza kwa ajili ya kununua vitu vidogovidogo vya kula, halafu huenda Seaclif Hoteli, akitoka hapo, hujirusha kwenye muziki, California Dreema. Shem, hakikisha wewe pia unapatikana maeneo hayo, akikuona tu atakushobokea, lakini uwe mwangalifu sana", nilimuasa.

"Kazi hiyo niachie mimi, nawahakikishia huyu mzungu kwangu atanasa, chezea Cnthia wewe, niko tayari kuanza kazi hiyo", alisema Mama Feka hofu ikiwa imemtoka.

Niliwasiliana na Peter Twite kumjulisha hatua tuliyokuwa, nilitumia nafasi hiyo kumwelekeza ratiba ya kazi atakapokuwa na Mama Feka. Tulimpangia kazi ya kumpeleka  sehemu alizopangiwa, yaani Shopaz Plaza, Seaclif Hoteli na California Dreema. 

ITAENDELEA 0784296253     

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru