NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI NA NANE

Boing 787, mali ya Shirika la Ndege la Uholanzi, iliwasili na kutuwa taratibu kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius K. Nyerere, Jijini Dar es Salaam, majira ya saa nne na dakika arobaini na tano usiku. Baada ya abiria wa Dar es Salaam kutoka ndani ya ndege hii. Kazi ya kutoa mizigo ilichukuwa masaa kadhaa, hatmaye kila abiria alitoka na mzigo wake, baada ya kutimiza masharti.

Mimi na wenzangu, Claud Mwita, Julius Nyawaminza na Fred Libaba, tulikuwa tumewasili uwanjani hapa masaa mawili kabla ya ndege hii kushuka katika ardhi ya Tanzania, wakati huo tukitumia magari manne tofauti. pia tukiwa tumejiwekea usalama wa kutosha. Tulijipanga vizuri kwa lolote. Ili kufanikisha kazi iliyokuwa mbele yetu, Claud na Nyawaminza, walitumia gari ndogo aina ya Toyota IST rangi ya Blue yenye vioo vyeusi ambavyo mtu hawezi kuona ndani.

Nje kabisa ya uwanja, liliegeshwa gari lingine lililochaa aina ya Suzuki Escudo, vijana wawili waliovalia mavazi machakavu, Tumain Changasi na China Kilinda, walionekana wakihaha kurekebisha sehemu ya gari hii, Ukweli ni kwamba vijana hawa walikuwa hapo kwa kazi maalumu, 

Claud aliyekuwa akiendesha gari IST, aliliingiza gari upande wa pili kwenye maegesho ya taksi. Kama ilivyo kawaida baadhi ya madereva taksi wanaoegesha magari yao eneo hili walilifuata gari hilo ili kumfahamisha dereva kuwa sehemu hiyo magari ya watu wa kawaida tofauti na taksi hayaruhusiwi.

Vijana wawili wawili ambao ni madereva taksi haraka walilifikia gari hili na kugonga kioo upande wa dereva, Taratibu Claud alishuka kioo hicho na kuacha ufa kidogo ili aweze kuwasikiliza. 

"Ondoa gari, eneo hili ni kwa ajili ya taksi tu", alisema mmoja wa vijana hawa aliyeonekana kuwa na jazba, Clauud alimwangalia kwa sekunde kadhaa halafu akauliza..

"Kwenu, ondoa gari ndiyo salamu?".

"Salamu ya nini, nimesema ondoa gari lako, hii ni sehemu ya taksi tu, vinginevyo gari lako litafungwa minyororo na faini yake ni elfu hamsini, mimi nakusaidia usipigwe faini wewe unaleta jeuri, ukitaka salamu tii sheria kwanza", kijana huyo aliongeza kwa jazba.

Ok, kama unaona fahari, enedelea kupaza sauti yako", alisema huku akipandisha kioo cha mlango cha upande wake na kuwaacha vijana hao wakiendelea kusuburi. Walisimama kwa dakika kadhaa halafu wakaondoka huku wakilalama.

Kabla ya kufika eneo hili, nilikuwa nimewaelekeza wenzangu kila kitu. Fred akiwa peke yake alitumia gari ndogo aina ya Toyota Starlet, rangi nyekundu iliyochoka kidogo, aliliegesha gari hilo karibu na sehemu ya kutokea abiria, bahati nzuri Fred hakupatwa na misukosuko ya kuulizwa maswali kama wenzake.

Mimi nikitumia gari ndogo pia, Toyota Corolla, ambalo pia mtu akiwa ndani huwezi kumuona kutokana na vioo vyake kuwa vyeusi, nililiegesha gari kwenye barabara ndogo inayotoka kituo cha mafuta cha PUMA. Karibu yangu kuliwekwa bango linalokataza magari kuegeshwa mahali hapo, nikalipuuza/

Niliwakumbuka vijana wetu wa bodaboda ambao Peter Twite aliwaweka sehemu mbalimbali kwa kazi maalumu, nikajuwa huu ndiyo muda wao itakapobidi.

Tulikuwa tumejipanga vizuri. Hatukufanya kosa hata kidogo, tukiwasiliana kila baada ya dakika chache, hatmaye, Fred alinidokeza kwa njia ya simu kuwa mambo yamewiva. Nikajuwa kazi imeanza, nilichukua bastola yangu iliyokuwa kwenye  droo ya gari nikaiondoa usalama.

Mara nikaliona gari wanalotumia Claud na Nyawaminza linapita taratibu mbele yangu, mapigo ya moyo ya moyo wangu yakanienda kasi. Baada ya muda mfupi, Mitsubishi Pajero lenye rangi nyekundu ambalo dereva wake aliwasha taa, kuashiria hatari lilipita likikifuatwa kwa nyuma na gari kubwa Lori aina ile ile ya Mitsubishi, dereva wa gari hilo alijaribu kuyapita magari yote yaliyokuwa mbele yake, akaliingiza kwenye Barabara kuu ya Julius Nyerere kwa ajili ya kuelekea mjini huku gari lingine likiwafuata kwa nyuma.

"Kumekucha", nilimwambia Claud kwa njia ya simu ya mkononi, "Endesha kwa mwendo wa kasi kidogo, yapite magari ya adui, angalia msifanye chochote, nitalianzishea mimi", nilimwambia wakati naingiza gari langu kwenye barabara ya Nyerere.

Magari yoteyalipokipita kituo cha mafuta cha OILCom, karibu na stendi ya daladala ya Kipawa, mimi nilikuwa karibu yao zaidi. Haraka niliwasha taa za mbele, nikaanza kulichezesha gari langu, nikimbana dereva wa gari la mbele kumtaka aegeshe gari hilo kando ya barabara, vivyo hivyo, Fred alifanya kwa gari kubwa lililobeba mzigo, magari yote matatu yalichepuka kutoka barabara kubwa na kuegeshwa kando.

Hawa Msimbazi aliyekuwa katika mawani meusi, akionekana kama haelewi chochote, alishusha kioo upande wa pili wa dereva, "Nini unatuvamia kama sisi wahalifu?", aliuliza,macho yake yalipokutana na yangu akaanza kugwaya.

"Habari ya kwako, samahani kwa usumbufu, bila shaka unajuwa kwa nini tumewasimamisha hapa?", nilimuuliza.

"Hapana, sijui kwanini tusimamishwe, mzigo wetu ni malighafi za kiwanda kwa ajili ya kutengeneza tembe za kutibu malaria. Tunaziingiza nchini baada ya kufuata taratibu zote za serikali", Hawa Msimbazi alieleza huku akishuka kutoka ndani ya gari hilo.

"Una hakika?", nilimuuliza baada ya Fred kusongea karibu. Claud na Nyawamiza wao walibaki ndani ya gari wakiangalia usalama wetu.

"Hakika kabisa, taratibu zote za kuingiza mzigo huu zimefanyika, upekuzi umefanyika, hatujaingiza mzigo tofauti na matakwa ya serikali", alisisitiza.

"Si kweli, fungua tuhakikishe", niliagiza.

"Wewe ni mtaalam wa kugundua aina ya poda zinazoingizwa nchini na kupelekwa viwandani?, haifunguliwi mpaka ifike sehemu husika, hii ni malighafi hatari, unaweza kunusa sumu ukafa, tukaulizwa kwanini tuliruhusu". 

"Nimesema fungua tuhakikishe", nilimwambia kwa sauti ya ukali kidigo, baada ya kujiuliza akarudi ndani ya gari na kujaribu kupiga simu, lakini nilikuwa mwepesi kuchukuwa simu hiyo. Nilitoa kisu changu kidogo kilichokuwa mfukoni nikazikata kamba.

Kulikuwa na shehena kubwa ya dawa za kulevya, aina tofauti tofauti, nilimwangalia mwanamama huyu kwa hasira, wakati huo alikuwa akiniangalia kwa macho ya hasira pia, akitweta  nikaliona gari la akina Tumaini linasogea kwa ajili ya kuimalisha ulinzi, 

"Unamfahamu, mtu mmoja anaitwa Raymond Kenoko?", nilimuuliza.

"Raymond Kenoko?, Mmmm, simjui", alijbu baada ya kutafakari.

"Humjui mtu aliyefanikisha mpango wenu wa kuingiza dawa za kulevya hapa nchini?. Mtu aliyewatengenezea mazingira ya kutoa huu mzigo".

"Nimesema simjui, hivyo usilazimishe kujibu swali ambalo sijui".

"Sawa, mtakutana mahakamani, huu ni ushahidi wa kutosha kabisa kuwatia hatiani, haya ni madawa ya kulevya aina ya heroin", nilimwambia.

"Kama ni madawa ya kulevya mimi siyajui, usinihusishe na mzigo huo, si wangu". Hawa Msimbazi alieleza msimamo wake.

Tuliwachukuwa watu hawa na kuwahifadhi sehemu ambayo pesa haiwezi kutumika, nilijione mwenye bahati kufanikisha nusu ya zoezi hili, Hawa Msimbazi na wenzake walikuwa kimya wakitafakari kilichotokea. Shehena kubwa ya dawa za kulevya iliyokuwa iingizwe nchini imekamatwa na kufuta ndoto zao za kupata utajiri.

Gari moja ambayo hata sisi hatukuitilia shaka, ilisimama hatua kadhaa, kutoka mahali tulipokuwa, watu wanne walitoka ndani ya gari hiyo na kutuangalia kwa hasira, Fred alipojaribu kuwafuata walirudi ndani ya gari na kuondoka kwa mwendo wa kasi, wakiacha vumbi. Hata hivyo Claud alijaribu kulifuata gari hilo, likapotelea eneo la Vingunguti.


*************************

Carlos Dimera ndiyo kwanza alikuwa amerejea kutoka kwenye starehe, habari za kukamatwa kwa Hawa Msimbazi na vijana wake wengine zilionekana kumshitua sana, Jakina Nombo na wengine walikuwa wameduwaa wasijue cha kufanya.

"Kwanza niwafahamishe, huyu ni mchumba wangu, anaitwa Sweety", Carlos alisema huku akiwaangalia vijana wake, halafu akamgeukia Sweety, "Mpenzi, hawa ni wafanyakazi wangu, jione uko huru, usihofu kuwa na sisi, kilichotokea tutakirekebisha, ni ajali katika kazi", alieleza Carlos.

"Asante, nakushukuru sana baby kwa kunitambulisha, habari zenu?", Mama Feka alisalimia.

"Habari nzuri, mbaya yote ni habari", Nombo alisema.

"Oke, sasa nataka kujuwa, ilikuwaje mkaleta taarifa za uongo, kuwa Teacher ameuawa, Nombo wewe ndiye ulileta taarifa hiyo, ilikuwaje kuleta taarifa ambazo huna hakika nazo?", Carlos alihoji kwa sauti ya kutetemesha.

"Bosi Carlos, huu si wakati wa kulaumiana, waswahili walisema maji yakimwagika hayazoleki, cha msingi ni kuangalia nini kifanyike kuwaokowa wenzatu, halafu mambo mengine yatafuata", Jakina alieleza.

"Ndiyo, lakini ni vyema kujuwa, ukisema tuangalie mbele, bila kukumbuka nyuma, hatuwezi kufanikiwa, taarifa iliyopo ni kwamba Teacher aliuawa wakati wa shambulizi, gari yake iliteketezwa vibaya kwa mjibu wa Nombo. Leo ameharibu mipango yetu, mtu mmoja Teacher ambaye siamini kabisa kama ana mbinu za kutushinda", Carlos alieleza kwa hasira.

"Hakika ninaposikia habari hii, nashindwa kuamini bosi, tulimfuatilia Teacher kuanzia mwanzo mpaka anaingia Benjamin Mkapa, gari aliyoingia nayo ni ile ile iliyopigwa kombora, mtu mmoja alikufa katika shambulizi hilo, siami", Simba alibainisha.

"Yule ni mpelelezi wa siku nyingi, huenda aligundua kitu akampa mtu mwingine kuendesha gari hilo, kama yuko hai basi ni mjuzi wa hali ya juu, mbinu za ziada zinahitajika", Nyati aliongeza.

Mama Feka alikaa kimya akiwasikiliza kwa makini, kiasi fulani aliogopa maneno ya watu hawa, alimuonea huruma Teacher, akajiona mwenye bahati kufanikiwa kuingia ndani ya ngome hiyo, lakini pia akijiuliza, iwapo atabainika itakuwaje.

Waliongea mambo mengi, wakipanga hili na lile, hatimaye wakaweka azimio kuwa mzigo mwingine wa dawa za kulevya ulikuwa stoo uhamishwe haraka iwezekanavyo, kupisha upekuzi wa polisi baada ya hapo utarejeshwa na kuingizwa sokoni.

"Walichofanya ni kupunguza kasi tu, lakini hii itatuongezea kasi zaidi, mtu mjinga, mtu asiyependa kuishi maisha ya kifahari, wenzake wanakula kuku na bata, yeye anakosa usingizi kwa ajili ya kuziba mianya ya wengine", Carlos alilalama.

"Binadamu hatulingani bosi", Nombo alisema.

"Wakati huu msilale, fanyeni kazi usiku huu mpaka alfajiri tupate taarifa za Hawa na wenzake wamewekwa kituo gani cha polisi, shilingi ngapi inahitajika kumaliza jambo hilo, mzigo uhamishwe, kazi zingine zote zisimame mpaka hapo nitakapowajulisha vinginevyo.

"Ametuchokoza, ajiandae kulia", Jakina alieleza huku akisimama.

Ni wakati wa kuwashirikisha wageni, wamesafiri kutoka huko kuja hapa nchini kwa kazi moja, kufanikisha jambo hili", aliagiza Carlos. 

ITAENDELEA 0784296253 

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru