NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI NA NANE

Baadhi ya vyombo vya habari vya ndani vilitoa habari hii kwa mbwembwe, kila mhariri alikipamba chombo chake kwa kichwa cha habari alichoona kinafaa kusema. Mhariri mmoja aliandika, MAUZAJI YA DAWA ZA KULEVYA YAKAMATWA DAR. Mwingine akaandika, MAUZA UNGA MIKONONI MWA SERIKALI. Lakini gazeti hili nalo likapambwa na kichwa cha habari kinachosema, WANAJESHI WAINGILIA KATI VITA DHIDI YA WAFANYABIASHARA WA DAWA ZA KULEVYA. 

Mimi nilishangazwa na jinsi waandishi wa habari walivyoipata habari hii na kuichapisha haraka kwenye vyombo vyao vya habari. Nikaamini kuwa hilo ndilo jukumu lao, lakini pia walituharibia mambo fulani, ambayo bado yalikuwa hayajakaa sawa.

"Walikuwa wapi hawa waandishi wa habari", tulijiuliza baada ya kusoma habari hii kwa urefu, karibu kila chombo cha habari kiliandika jinsi tukio hili lilivyofanyika, lakini wakashindwa kubaini jambo moja, jinsi Raymond Kenoko, Afisa Ukaguzi uwanja wa ndege alivyokamatwa kama kuku.

Tuliyapitia magazeti yaliyokuwa mezani, mmoja akishika hili, mwingine anashika lile, wakati tukipata kifungua kinywa, tulisoma haraka haraka habari hii iliyokuwa ikitugusa sisi. Baada ya kufungua kinywa ndani ya Mghahawa huu ulioko kando ya Barabara ya Temeke, karibu na kituo cha mafuta eneo la Mchicha tukatafuta sehemu ya kawaida, tukachukua vyumba, tukapumzisha akili. Tukalala kwa muda.   

*********************

Ilikuwa saa mbili kamili za asubuhi, Hawa Msimbazi na mwenzake Tony Sime, walipofikishwa katika Mahakamni, wakituhumiwa kufanya makosa ya kuingiza dawa za kulevya nchini. Mahakama ilifurika watu wa kila aina, wapo waliofika kusikiliza, wapo waliokuja kuona, pia walikuwepo waliofika kwa ajili ya kuangalia mbinu za kuwaokoa watu hao.

Baada ya kufikishwa kizimbani, mwendesha mashitaka wa serikali alisimama na kuileza mahakama. "Mheshimiwa Hakimu, walioletwa mbele ya mahakama yako tukufu ni watuhumiwa wawili Bi. Hawa Msimbazi na Bw. Tony Sime, waliokamatwa jana usiku wakijaribu kuingiza nchini dawa hatari za kulevya aina ya heroine", alisema mwendesha mashitaka halafu akawageukia.

"Bi. Hawa Msimbazi na mwenzako Bw. Tony Sime, mnashitakiwa kwamba, mnamo tarehe 22, mwezi huu, huko eneo la Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, mlikamatwa mkijaribu kuingiza shehena kubwa ya dawa za kulevya, ambazo hata hivyo zilikamatwa. Kweli si kweli?".

"Si kweli Mheshimiwa", Hawa na Tony walijibu kwa pamoja. Lakini pia walionekana kushangazwa sana na hali hiyo, walijiuliza mpango wa wao kufikishwa mahakamani haraka kiasi hicho ulifanywa saa ngapi, hata taratibu zote zikawa zimekamilika na sasa wamesimama kizimbani kujibu shitaka.

Hawa na Tony waliamini kuwa, Carlos Dimera alikuwa katika mipango kabambe wa kuwatoa kwenye mikono ya sheria kabla ya kuburutwa mahakamani. Lakini hakujuwa kuwa mara tu baada ya wao kukamatwa usiku, Kanali Emilly na Teacher walikutana na kuandaa mashikata dhidi ya watu hawa ili kuziba mianya ya matumizi mabaya ya pesa.

Mara baada ya kufikishwa mahakamani, Hawa na Tony nao hawakuchelewa kumleta mwanasheria wao, ambaye alisimama kwa ajili ya kuwatetea. Mwendesha mashitaka wa serikali alipomaliza kuileza mahakama jinsi watu hawa walivyomatwa na kielelezo ambacho ni dawa za kulevya, mwanasheria huyo alisimama na kujitambulisha.

"Mheshimiwa Hakimu, naitwa Lutazaa Kyaruzi, ni mwanasheria wa kujitegemea, nimekuja kuwawakilisha wateja wangu, Hawa Msimbazi na Tony Sime. Hakimu aliandika majina yake kwenye kumbukumbu zake, halafu akamuuliza mwendesha mashitaka wa serikali. 

"Mwendesha mashitaka, unasemaje?".

"Mheshimiwa Hakimu, kwa niaba ya serikali niko tayari kuwahoji washitakiwa", mwanasheria wa serikali alimwambia Hakimu.

"Unaweza kuanza", Hakimu aliweka wazi. Mwanasheria wa serikali alitoka mahari alipokuwa ameketi, akasogea karibu kabisa na kizimba walichosimama Hawa na Tony. Aliwaangalia kwa sekunde kadhaa kisha akageuka.

"Hawa Msimbazi, una mahusiano gani na Tony Sime?", alihoji mwanasheria wa serikali.

"Tony ni mchumba wangu, tumepanga kuoana mapema mwaka huu", alisema Hawa.

"Uchumba wenu umedumu kwa muda gani sasa?".

"Miaka mitatu sasa".

"Miaka mitatu ya uchumba?" alihoji mwanasheria wa serikali.

"Ndiyo, unaona ajabu, mbona wengine wanakuwa wachumba hata kwa miaka kumi, sisi miaka mitatu, ndiyo tumepanga kufunga ndoa sasa". Hawa Msimbazi alibainisha.

"Kabla ya kukamatwa na hii shehena ya dawa za kulevya, kazi gani nyingine mlikuwa mkifanya tofauti na hii ya kuuza dawa za kulevya?", alihoji mwanasheria wa serikali. Haraka mwanasheria wao wakasimama.

"Mheshimiwa Hakimu, naomba wateja wangu wasihusishwe na dawa za kulevya, mwanasheria mwenzangu anapashwa kuuliza maswali ya kisheria, naomba mheshimiwa uwalinde wateja wangu".

Hakimu aliwaangalia kwa muda mfupi, akajaribu kutabasamu, akaangalia huku na huku, akatoa miwani aliyovaa, akasugua macho yake kwa viganja vya mkono, akavaa miwani, akasema.

"Endelea".

"Kabla hamjakamatwa na hii heroine, mliyokuwa mkijaribu kuingiza hapa nchini, kazi gani nyingine mlikuwa mkifanya tofauti na biashara hii halamu. Nasubiri jibu". alihoji mwanasheria wa serikali.

"Tafadhali, nakuomba usinihusishe na mzigo ambao siujii, mimi nilifika uwanja wa ndege kupokea malighafi za kiwanda zinazotumika kwa ajili ya kutengeneza tembe za kutibu malaria", Hawa Msimbazi alijitetea.

"Mheshimiwa Hakimu, mzigo uliokamatwa ni dawa za kulevya aina ya heroine, kumbukumbu zinaonyesha kuwa mzigo huu umetumwa kutoka Colombia, ukahifadhiwa kwa muda Adis Ababa, Ethiopia, hatmaye ukawasili Dar es Salaam jana, bahati nzuri, wahusika walikuwa macho, madawa hayo yakakamatwa", mwanasheria wa serikali alifafanua.

"Usilazimishe jambo ambalo si kweli, usichume dhambi kwa kusema uongo, kama mwenzangu alivyoeleza, sisi tunapokea mizigo ya kila aina kutoka kwa wakala wetu, hatuwezi kujua ametuma nini, kwa kuweka kumbukumbu sahihi, tunamiliki kiwanda cha kutengeneza tembe mbalimbali, mzigo tuliopokea ni kwa ajili ya tembe za malaria, sasa unaposema ni dawa za kulevya, tunakushangaa", Tony Sime aliyekuwa kimya kwa muda mrefu alieleza.

Lutazaa Kyaruzi alisimama na kurekebisha tai yake, ikiwa ni ishara ya kuomba kusema. Hakimu alimruhusu. 

"Ni muda gani mnasafirisha mizigo kama hii kutoka nje ya nchini?", Kyaruzi alimhoji Hawa.

"Miaka zaidi ya kumi sasa, tunasafiri, wakati mwingine tunapokea kutoka kwa wakala wetu huko nje", Hawa alijibu akitabasamu.

"Huko nje ya nchi, mzigo yenu inafungwa na nani, mnafunga nyie wenyewe au wakala anayehusika", Kyaruzi alihoji.

"Ah, mizigo yetu binafisi tunafunga wenyewe, malighafi za kiwanda tunamwachia wakala, sisi tunapokea mzigo baada ya kufika Dar es Salaam", Hawa alijibu huku Hakimu akiandika maelezo yake.

"Kwa hiyo wakala anaweza kukosema, mfano unaweza kuhitaji malighafi hii, yeye akakutumia aina nyingine kwa bahati mbaya?", Kyaruzi alihoji.

"Hilo linawezekana, iliwahi kutokea pia hapo nyuma, wakala alituma malighafi tofauti, lakini baadaye akarekebisha, sasa jana tumekamatwa hata kabla hatutajua mzigo ulioingizwa nchini", Hawa alijitetea.

"Kwa hiyo unaieleza mahakama kuwa wakala anaweza kufunga mzigo tofauti na ukaingizwa nchini bila nyie kujua, na hilo ni kosa la wakala".

"Ndiyo".

"Kwa maana hiyo, mnaitaka serikali iwaombe radhi kwa kuchafua majina yetu, hususan kwenye vyombo vya habari vya leo, ambavyo vimeandika kuwa mmekamatwa na dawa za kulevya?". Kyaruzi alimwambia Hawa.

"Yaani watuombe radhi kabisa, kwanza wametudhalilisha mbele ya jamii, pili jamii imeamini kuwa sisi ni wahalifu, waingizaji wa dawa za kulevya, wakati hatuhusiki kabisa na biashara hiyo", Tony alieleza huku mwanasheria wao akimgeukia Hakimu.

"Mheshimiwa Hakimu, kama ulivyosikia, wateja wangu wamekana kuhusika na mzigo uliokamatwa jana, yawezekana ni njama au mbinu za kibiashara, au makosa ya wakala wao huko nje. Kutokana na hali hiyo, wanaiomba mahakama yako iwaachie huru na serikali iwambe radhi kwa usumbufu waliopata", Kyaruzi alimwambia Hakimu.

"Watuombe radhi kabisa", aliongeza Hawa, huku mwanasheria wa serikali akisimama kutoa ufafanuzi.

"Hawa Msimbazi na Tony Sime, huyo wakala wenu alituma hizi dawa ya kulevya kwa nani hapa nchini".

"Nimesema sijui, usilazimishe, pia usinihusishe kabisa na mzigo huo, siujui, mbona hunielewi".

"Hujui nini Hawa, wakati mzigo huo umetumwa moja kwa moja kuja kwenu?. Ndiyo maana mkaupokea", mwanasheria wa serikali aliwaambia, Hawa na Tony wakashindwa kujibu.

"Mheshimiwa, mzigo uliokamatwa ni mali ya watuhumiwa hawa mbele yako, haiwezekani kabisa wakala huko nje atume mzigo kwa mtu asiyemjua, tena mzigo huo usafirishwe kwa mapesa mengi, kingine cha kusikitisha mheshimiwa, taratibu za nchi zinaelekeza kuwa mzigo kabla haujachukuliwa sehemu husika lazima ukaguliwe na kubaini ni mzigo gani, hawa wanasema wakala wao amekosea, wakaguzi wetu pia wamekosea, iko haja ya kuangalia upya watumishi wetu. Mheshimiwa, mzigo uliokamatwa ni dawa za kulevya, hii imethibitishwa na mkemia mkuu wa serikali", alieleza mwanasheria wa serikali huku Hawa na Tony wakimwangalia kwa hofu.

"Mheshimiwa, watu hawa ni wahalifu wazoefu, kuingiza dawa za kulevya nchini ndiyo kazi yao, sasa basi, ili iwe fundisho kwa watu wengine, wenye mtazama kama wao, upande wa serikali tunaomba watu hawa wapewe adhabu kali kwa ajili ya usalama wa kizazi kijacho", mwanasheria wa serikali alisema huku hakimu akiandika maelezo yake kwa makini zaidi.

Hakimu aliinua macho akawaangalia tena watuhumiwa hawa, halafu akazama tena kuandika. "Watuhumiwa watarejeshwa mahabusu mpaka kesho muda kama huu, ambapo mahakama itatoa hukumu", Mheshimiwa Hakimu alieleza huku akisimama na kutoka kizimbani.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru