NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI NA SABA

"Mnanipeleka wapi jamani?", Raymond Kenoko alihoji, wakati naingiza gari kwenye Barabara ya Nyerere kuelekea mjini, baada ya kuiacha barabara inayoingia Uwanja wa ndege.

"Uwe mpole kaka, sehemu ambayo utaweza kujibu maswali yetu vizuri", nilimwambia kwa sauti ya ukali kidogo. Nilifungua droo ya gari nikatoa kitambulisho changu, nikamuonyesha.

"Nimekosa nini jamani?", alihoji kwa sauti ya kukata tamaa huku mikono yake ikitetemeka.

"Sikiliza kaka, sisi ni watu wema kabisa, watumishi wenzio katika serikali, huna budi kutulia na usijaribu kufanya lolote ambalo linaweza kuyahatarisha maisha yako", Fred alimwambia.

"Nimekuelewa kaka, sasa napaswa kufanya nini? kama kuna tatizo linahitaji ufafanuzi tuzungumze tu, dunia ya sasa hakuna siri, mnilinde jamani", Raymond Kenoko alieleza.

"Sikiliza Mzee Ray, tunakuhitaji kwa mazungumzo ya dakika ishirini hivi, halafu tutakuacha utarudi kazini kwako, cha msingi ni ushirikiano, wewe unajua kwa nini tumekukamata, naamini hivyo", nilimwambia.

"Hapana, hakika sijui lolote", alisisitiza.

"Sawa, kama hujui tutakusaidia kujua, cha msingi ni wewe kuwa na ushirikiano", Fred alisema.

Tulipofika kwenye makutano ya barabara za Nyerere na ile inayokwenda Vingunguti, tuliiacha barabara ya Nyerere, nikachepuka na kuingiza gari kwenye barabara ndogo ya dharura, inayopita kushoto, pembeni mwa barabara hii ya Nyerere, nikaliongeza gari mwendo.

"Mtanisaidiaje?", alihoji.

"Kuhusu nini?", Fred alimuuliza. 

"Kuhusu kusaidiana ili tumalize jambo hili lisifike mbali, maana ukipuuzia upole, kitakuwa kidonda", alibainisha.

"Ni kweli, lakini ni jambo gani wakati wewe umesema hujui kwa nini tumekukamata?", nilimwambia.

"Kwa vyovyote vile kutakuwa na sababu, haiwezekani maofisa kama nyie mnikamate tu bila sababu, lazima ipo sababu ndiyo maana nikasema tuzungumze kirafiki, tusiharibiane kazi. Tusaidiane", alijitetea.

Mara simu yangu ya kiganjani ikaita, Kanali Benny Emilly alitaka kujua tumefikia wapi, maana kabla hatujatoka uwanja wa ndege kuelekea Transt Motel nilimjulisha wapi atusubiri, nilimweleza kila kitu akatuelekeza mahali alipo.

Tulipofika kwenye ofisi za kiwanda cha sigara cha Master Mind, kilichoko kando ya barabara hii, geti la kuingia liliachwa wazi, hivyo niliingiza gari moja kwa moja. Kama unavyojua sheria inaturuhusu kutumia ofisi yoyote ya umma na binafsi mahali popote, wakati wowote kwa ajili ya usalama wa nchi. Kanali Emilly alikuwa amefika mapema sehemu hii na kuandaa ofisi ya muda, kwa ajili ya kazi hii.

Meja Iddi Satara, mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Kanali Emiily alinionyesha ishara nikalisogeza gari mahali alipokuwa, wakati haya yanafanyika Raymond Kenoko alibaki ameduwaa asijue la kufanya.

"Mtanisaidiaje?", alijitetea kwa mara nyingine.

"Amini tutakusaidia, twende kwanza uongee na mkubwa, cha msingi uwe mkweli, vinginevyo utaozea jela, haki ya Mungu", nilimwambia wakati tunatoka ndani ya gari, tukaelekea kwenye ofisi ya Kanali Emilly ya muda.

Kanali Emilly aliketi mbele ya meza kubwa iliyozungukwa na viti kadhaa vya wageni, ilikuwa ofisi ya kuvutia sana, Meja Satara alimuonyesha Raymond sehemu ya kuketi, bila ajizi akaketi.

"Karibu bwana Raymond Kenoko, Afisa Mkaguzi Mwandamizi wa Uwanja wa ndege. Naitwa Kanali Benny Emilly, kwa ufupi mimi ndiye nimewatuma vijana wangu wakukamate, ili ufike mbele yangu ujibu maswali mawili matatu, halafu tunakuachia, kikubwa hapa ni ushirikiano, tusaidie tukusaidie, bila shaka umenielewa?", Kanali Emilly alimwambia.

"Ndiyo baba, niko tayari kujibu maswali yako na kutoa ushirikiano unaotakiwa", alijibu kwa hofu.

"Una muda gani sasa toka umepata ajira serikalini?", Kanali Emilly alimuuliza.

"Miaka kama ishirini na sita hivi", alijibu.

"Miaka kama ishirini na sita, unaonyesha kuwa huna hakika", Kanali Emilly alihoji.

"Ni miaka ishirini na sita, hakika ni ishirini na sita sasa", alisisitiza.

"Umeoa?".

"Ndiyo baba, nimeoa".

"Una watoto?".

"Yes, nina watoto watatu".

"Wazazi wako hai?".

"Hapana, wote ni marehemu".

"Una nyumba ndogo, namanisha mke mwingine?".

Akaonekana kubabaika, baada ya kutafakari kwa sekunde kadhaa akasema, "Yupo rafiki wa kike, lakini hayuko karibu sana, unajua hali ya maisha sasa ni ngumu".

Kanali Emilly aliendelea kumuuliza Raymond maswali mengi ambayo aliyajibu vizuri. Pamoja na maswali hayo ya kirafiki, akili ya Raymond ilikuwa katika dimbwi la mawazo, akijiuliza kimya kimya, hususan swali la Carlos. Fred alipomwita kwenye gari, alijitambulisha kama kijana wa Carlos, ndiyo maana akakubali kupanda gari, sasa alijiuliza kwanini watu hawa walimtaja Carlos lakini baadaye wakamkamata na kumweka chini ya ulinzi.

"Unamfahamu mwana mama mmoja anaitwa Hawa Msimbazi?", Kanali Emilly alimuuliza Raymond.

"Hapana, simjui".

"Humjui, na huyu mzungu anayeitwa Carlos?", swali hili lilimchanganya kidogo, akaweweseka.

"Simjui pia", alisema huku akitingisha kichwa chake kukataa kwa msisitizo.

"Unamjua", nilirukia.

"Siwezi kusema kitu ambacho sikijui, haki ya Mungu simjui Hawa wala Carlos", alisisitiza kwa mara nyingine.

Kanali Emilly alisimama, alitoka mahali alipokuwa ameketi akatembea hadi kwenye mgongo wa Raymond. Mzee huyu alikuwa na huruma kwa kila kiumbe kilichotengenezwa na Mungu, lakini pia alikuwa katili kwa viumbe vilivyokuwa hatari kwa maisha ya viumbe wengine. Alipenda kucheka sana, lakini pia alikuwa mwenye hasira sana.

"Unadhani sisi ni wapumbavu, unadhani hatuna kazi zingine za kufanya mpaka tukulete hapa, nilitegemea utakuwa muungwana, utajibu maswali yangu vizuri kama tulivyoanza, kumbe naongea na mpumbavu. Sikiliza, naomba ujibu swali langu. Unamfahamu Carlos Dimera", Kanali Emilly alihoji kwa sauti ya kutisha.

Raymond aliinamisha uso wake chini, akabaki kimya. Kanali Emilly aliendelea kusimama nyuma yake, akisubiri jibu.

"Sikiliza, wewe ni raia wa Tanzania, tena mtumishi wa umma, Carlos ni mzungu, ametoka mbali sana, mpaka anafika hapa nchini, taarifa zake zote tunazo, mpaka anawasiliana na wewe kuhusu mzigo uliokwama Adis Ababa, Ethiopia tunajua, nashangaa kwanini unaficha jambo ambalo liko wazi kabisa", nilimwambia.

"Mr Raymond, unakumbuka kabla hatujapanda gari uliniuliza swali gani, ulisema ni huu mzigo unaoingia leo au mzigo mwingine, sasa unaficha nini inaeleweka hivyo", Fred alimwambia.

"Raymond, unataka usaidiwe au uishie jela?", Kanali Emilly alimuuliza.

"Naomba nisaidiwe", alisema huku machozi mengi yakimtoka.

"Tutakusaidiaje wakati hutaki kufunguka, jaribu kusema ukweli ili tuangalie jinsi ya kukusaidia", Meja Satara alieleza.

"Kabla sijasema chochote naomba mnihakikishie usalama wangu, huyu Carlos ni mtu hatari sana, anaweza kuniangamiza", Raymond alieleza.

"Kuhusu hilo ondoa shaka, tutakulinda kwa gharama yoyote", Fred alimwambia.

"Na vipi kuhusu familia yangu?" alihoji.

"Kuhusu familia yako, wako chini ya uangalizi wa jeshi la polisi kabla hata hatujakukamata, hivi tunavyoongea hapa mkeo na watoto wako mikononi mwa polisi, lakini kwa ajili ya usalama wao tu", nilimwambia akaonekana kushangaa.

Baada ya maelezo hayo, Raymond alieleza kila kitu kuhusu Carlos, alieleza jinsi alivyotambulishwa kwake na Denis, Afisa Ukaguzi mstaafu, ambaye sasa ni marehemu, alieleza jinsi alivyofahamiana na Hawa Msimbazi na mengine mengi, pia alieleza mbinu wanazotumia kuingiza dawa za kulevya nchini, na mkakati wa kuua yeyote anayeonekana kuingilia biashara yao.

"Asante, kazi yako imekwisha, Meja Satara, hakikisha huyu jamaa anapelekwa mahabusu ya siri mpaka nitakapojulisha vinginevyo", Kanali Emilly aliagiza.

"Hakuna tatizo mkuu", Meja Satara alieleza huku akijiandaa kuondoka na Raymond.

"Mlisema mtanisaidia, imekuwaje?".

"Tulisema tutakusaidia baada ya kazi hii kwisha salama", nilimwambia. Kiasi fulani nilifurahi kumkamata mtu huyu, maelezo yake yalitufanya tupate mwanga. Niliwapigia simu Claud na Nyawaminza kuwafahamisha kilichotokea wakaeleza furaha yao.


**********************

Wakati huo Mama Feka alikuwa kwenye foleni ya kununua tiketi ya kuingia California Dreema. Alivaa vizuri kiasi cha kumfanya mwanaume yeyote kuingiwa na tamaa, baada ya kupata tiketi yake alipenya mlango na kujitosa ndani ya ukumbi huu. 

Muziki laini ulikuwa ukipenya masikioni mwa wapenzi wa starehe, kila mmoja alionekana akicheza na mpenzi wake, huku wengine wakiwa wameketi kwenye meza za pembeni wakiupiga mtindi.

Kama ilivyo kawaida yake, Mama Feka alipita akatafuta sehemu nzuri ambayo anaweza kuonekana kwa urahisi, alifanya hivi baada ya kuwa amemuona Carlos Dimera na wapambe wake wakiwa wameizunguka meza iliyojazwa vinywaji vya kila aina.

Ili aweze kuonekana, Mama Feka alianza kulicheza rhumba, alicheza vizuri huku akigeuka kila upande, kijana mmoja aliyekuwa karibu yake alivutiwa na mwana mama huyu, hivyo akajisogeza na kumuomba wacheze. Lakini hilo lingemfanya auhalibu mtego wake, alichofanya Mama Feka ni kumkwepa kijana huyo, akaendelea kucheza peke yake, kijana huyo kwa aibu akajiondoa eneo hilo.

Jakina alifanikiwa kumuona Mama Feka, hakufanya ajizi, haraka alizifikisha habari kwa Carlos, ambaye alikuwa ameketi kwenye meza ya vinywaji na akina dada kadhaa.

"Bosi, unamuona yule mbabe wa Supermarket?", Jakina alimwambia Carlos Dimera.

"Yuko wapi?" Dimera alihamaki.

"Yule anacheza peke yake pale".

"Oh, nimemuona, sasa sikiliza, tafuta mbinu ya kuwafanya hawa malaya wengine wasinisogelee, asije akaniona mhuni. Kwa vile wewe na yeye damu zenu zimetofautiana, acha niende mimi mwenyewe, nimuombe tucheze kidogo", Carlos alimwambia Jakina huku akielekea mahali alipokuwa Mama Feka.

"Helo, habari yako?" Carlos alisalimia baada ya kumshika bega. Haraka Mama Feka aligeuka na macho yao kukutana.

"He, na wewe unakuja huku?" Mama Feka alihoji.

"Mimi ni mtu wa starehe, lazima nifike sehemu kama hizi, nimekuja kukuomba tucheze kidogo", Carlos aliomba.

"Unataka ucheze na mimi wakati mlitaka kunipiga kule Supermakrt?".

"Ilikuwa bahati mbaya, waswahili mnasema wanaogombana ndiyo wanaopatana, pole kwa yaliyotokea, msamehe kijana wangu hakuwa na nia mbaya", Carlos alieleza.

"Sawa, nimekuelewa, karibu tucheze", Mama Feka alifurahi kupata nafasi hiyo, wakaanza kucheza huku wameshikana.

"Unaitwa nani?" Carlos alihoji.

"Sweety".

"Oh, jina zuri sana, unafanyakazi gani Sweety?".

"Niko nyumbani tu, nimemaliza shule, ndiyo natafuta kazi".

"Umesomea nini?"

"Mambo ya Maabara", Mama Feka alidanganya.

Oh, very god, umepata kazi, mimi namiliki kiwanda kikubwa cha madawa".

"Asante, na wewe unaitwa nani?".

"Carlos, au ukipenda unaweza kuniita Carlos Dimera".

"Wewe ni Mtaliano?".

"No, hapana, si kila mzungu Mtaliano. Mimi ni raia wa Colombia", Carlos alifafanua.

"Unafanya kazi gani?".

"Yaani mimi nifanye kazi, mimi ni mfanyabiashara, business men".

"Unafanya biashara gani?".

"Ohoo, sasa hapa umekuja kustarehe au kunihoji". 

"Hapana, nilitaka tufahamiane tu". 

"Utanifahamu tu, si bado tuko pamoja". 

"Sawa", wakaendelea kucheza.

Mama Feka akamshukru Mungu kwa kazi aliyoifanya kwa muda mfupi, aliyakumbuka maneno ya Teacher kuwa Carlos ni mtu hatari, lazima awe makini, akaupiga moyo wake konde na kujiweka tayari kwa lolote, akimtanguliza Mungu katika jukumu hilo zito, lililoko mbele yake.

ITAENDELEA 0784296253  

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU