NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI NA TISA

Watu wote walikaa kimya ndani ya chumba cha mkutano. Carlos Dimera alionyesha dhahiri hali ya woga na hasira, akivuta sigara kubwa iliyosokotwa kwa karatasi ngumu, alitembea kutoka kona moja ya chumba hiki kwenda kona nyingine huku akitafakari kwa kina kilichokuwa kimetokea. Alijitahidi kuvuta sigara hiyo mpangilio na kupuliza moshi mwingi hewani. Hali iliyowafanya wafuasi wake wapatwe na hofu.

Mama Feka au Sweety, kama alivyojitambulisha kwa Carlos, alikuwa mmoja wa watu waliokuwa ndani ya chumba hiki cha 
mkutano wa siri, akishiriki kama mjumbe wa kawaida. Lengo la Carlos ilikuwa kumshirikisha mama huyu katika biashara ya dawa za kulevya.

Mzungu huyu aliutambua urembo wa Mama Feka, awali alikuwa ameteta na Jakina, kuwa unapokuwa na msichana mrembo kama 
huyu kwenye biashara yako asilimia tisini mambo yatakuwa shwari. Hata aliposhiriki kikao hiki wajumbe walilitambua kusudi la Carlos, wakampokea Mama Feka kwa mikono miwili.

Mfano wa mtu aliyeshikwa na kigugumizi, Carlos alivunja ukimya uliokuwepo kwa kusema. ..."Imenishangaza mno, watu makini, watu mnaojitambua, kuyachezea maisha yenu mbele ya Simba mwenye njaa, sielewi nini kimewalevya mpaka mnazidiwa maarifa na wajinga?. Haiwezekani, Hawa na Tony wakamatwe kama kuku, halafu, shehena yote ipotee. Lakini cha ajabu na kusikitisha zaidi, wenzetu hawa wamefika mahakamani. Mmmmm, imenifedhehesha sana Nauliza kila baada ya dakika kuhusu hatima ya jambo hili, wakubwa wanataka kujua nini mkakati wetu au tumejipangaje kumaliza tatizo hili, pesa si tatizo, mtu mmoja, mtu mmoja mpuuzi hawezi kufanya tuonekane wapuuzi", alitembea tena kutoka upande mmoja wa chumba hiki kwenda upande mwingine huku wajumbe wakimwangalia.

"Inachosema ni hakika bosi, lakini usitishwe na ukimya huu, ukadhani labda tumeridhishwa na jambo hili, niseme wazi kuwa adui anaishi kwa mbinu, ambazo hakika siku zake za kuishi sasa zinahesabiwa, hivi tunavyoongea, vijana wetu wako katika msako mkali kujua mjinga huyu yuko wapi. Naamini msako huu utafanikiwa haraka iwezekanavyo, kwani tunatumia vifaa vya kisasa", Nombo alieleza.

Haraka Jakina akasimama, tofautu na mwenzake aliyeongea ameketi. "Kama ulivyosikia bosi, mahakama ilikuwa itoe 
hukumu ya kesi hii leo, lakini kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa, hukumu imeahilishwa mpaka kesho ili tuweze 
kujipange. Nakuhakikishia Hawa na Tony kesho wakati kama huu watakuwa huru, mwanasheria wetu pia ni mtu makini sana, cha msingi tuwe wavumilivu, tumalize tatizo hili ndipo tujiulize wapi tulijikwaa", Jakina alieleza.

"Maneno mazuri sana, lakini hayana ufumbuzi wa jambo hili, kila mmoja anaongea kwa mtazamo, kama tunaweza kuwatoa Hawa na Tony kwenye mikono ya sheria, swali langu ni je, huu mzigo utapatikana au utapotea?. Tunapojadili jambo nyeti kama hili, lazima tuangalie uwezekano huo pia", alihoji.

"Swali zuri bosi. Mara tu baada ya Hawa na Tony kukamatwa, haraka tuliwasiliana na watu wetu katika vitego mbalimbali vya usalama wanaopokea mshahara kutoka kwetu, kuwajulisha kilichotokea, hakika ushirikiano wao ni mkubwa mno. Kama unavyojua msimamo wa serikali sasa, unapofikishwa mbele ya mahakama na ushahidi, moja kwa moja unakumbwa na kifungo, lakini maofisa hao ndiyo waliofanikisha mahakama kusogeza hukumu ya kesi hii mbele ili tuweze kujipanga", alisema Nombo.

"Baby naomba uketi", Mama Feka alimwambia Carlos kwa sauti ya mahaba. Sauti ya Mama Feka, ilimfanya Carlos, atabasamu kidogo.

"Asante Sweety wangu, usijali mpenzi, mambo yanapokwenda ndivyo sivyo, lazima tuketi na kutafakari njia sahihi, usiogope Sweety mpenzi, uwe na amani nitaketi", Carlos alisema, halafu akaendelea. ..."Jamani, tupunguze maneno, tupunguze porojo, jukumu lililo mbele yetu ni zito mno, yatupasa kujipanga vyema, Hawa na Tony ni watu kutoka miongoni mwetu. Nasema kwa gharama yoyote lazima watakuwa huru kutoka katika mikono ya sheria. Nataka kuona jambo hill linafanyika haraka iwezekanavyo, hebu jiulize mfano ungekuwa wewe ingekuwaje?", Carlos alihoji baada ya kutoa agizo.

Lakini Carlos na kikosi chake walikuwa wamekosea jambo moja. Hawakujua kama, Mama Feka alikuwa hapo kwa kazi maalumu, alitumia simu yake ya kiganjani kwa usiri wa hali ya juu kurekodi mazungumzo hayo na kuyatuma wakati huo huo moja kwa moja kwenye simu ya Teacher. Carlos Dimera na wafuasi wake waliendelea kujadiliana hili na lile, waliongea mambo mengi, wakipanga hili na lile, hatimaye wakafikia mwafaka. 

"Nitalala usingizi mnono iwapo nitasikkia Teacher amekufa, sasa naagiza, kwa gharama yoyote ya pesa, atafutwe ikiwezekana auwawe haraka kabla ya hukumu kesho, uwepo wake unaweza kuharibu mipango yetu", Carlos alisisitiza, huku kila mmoja akipewa jukumu lake.

Hata hivyo, Carlos Dimera aliamua kutumia uzoefu wake wa siku nyingi katika kazi hizi za hatari, aliwatuma kwa siri, vijana wawili Gabriel na George, bila kuwashirikisha wenzake. Hawa walikuwa wakiishi nchini Tanzania kwa siri, wakisubiri matukio kama haya. Vijana hawa wenye uzoefu mkubwa wa mambo ya ujasusi walipewa jukumu la kumtafuta Teacher.

Carlos, aliwaamini sana vijana hawa, waliokuwa wakifanya mazoezi wakati wote, aliujuwa vizuri muziki wao, Ni vijana 
ambao wakitumwa kukileta kichwa cha mtu yeyote, wanaweza, kutokana na imani yake kwao, aliwaagiza kumleta Teacher mbele yake akiwa hao ili athibitishe kuwa ndiye, halafu amuue yeye mwenyewe. Hili alilifanya kwa siri kubwa, bila hata Sweety kujuwa.

Mara nyingi majasusi hutumia mbinu tofauti katika kufanikisha mambo yao, Gabriel na George waliishi nchini kwa siri, hakuna mtu aliyefahamu uwepo wa majasusi hawa. Hata Jakina aliyekuwa karibu zaidi na Carlos hakuwajuwa vijana hawa. 

Gabriel na George walikuwa majasusi waliohitimu mafunzo ya juu ya ujasusi katika vyuo mbalimbali duniani, walilingana kwa kimo na umri, walionekana kama mapacha, lakini ukweli ni kwamba kila mmoja alikuwa na sifa zake, 

George akiwa amezaliwa katika mji wa Kano, nchini Nigeria, huku Gabriel akiwa raia wa Afrika Kusini. Vijana hawa walikutana katika chuo kimoja nchini Cuba, ambako walishabihiana kwa kila kitu, hata walipohitimu mafunzo yao ya ujausi walipangwa pamoja, baada ya kununuliwa na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya kwa ajili ya kulinda maslahi yao. 

*************************

Wakati huo huo, mkutano mwingine wa siri, ulifanyika katika Hoteli ya King Air katikati ya Jiji la Bogota, nchini Colombia, ambapo Wafanyabiashara wakubwa, matajiri wa dawa za kulevya walikutana kwa siri kama ilivyo kawaida yao. 

Watu hawa walikutana kujadili mafanikio ya biashara yao pamoja na shehena yao kubwa ya dawa za kulevya kukamatwa Jijini Dar 
es Salaam, Tanzania na watu wao kufikishwa mahakamani.


Emilio, mfanyabiashara kigogo, aliyefika Dar es Salaam, kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kuingiza dawa hizo, ambazo awali zilikwamba Ethiopia, alitakiwa kuwaeleza wakubwa hawa kwa nini shehena hiyo ikamatwe baada tu ya kuingia Tanzania.

"Inawezekana hatukuwa makini wakati wa kusafirisha shehena hii? Tanzania kama Tanzania ndiyo njia yetu ya kusafirisha dawa za kulevya kwenda katika nchi nyingine za ukanda wa mashariki. Leo tujiulize, nini kimetokea mpaka shehena hii hii kubwa ikamatwe?", Mfanyabiashara tajiri, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa mtandao huu, Enock Jonson, alihoji. 

"Ni wakati wa Emilio kutoa maelezo, ndiye mtu wetu pekee aliyesafiri hadi Dar es Salaam, lengo la safari ilikuwa kuweka mambo sawa, sasa kama hali ya usalama nchini humo ilikuwa hairuhusu, ilikuwaje wewe ukaruhusu shehena hiyo kuingizwa bila kuwa na uhakika wa hali ya usalama nchini Tanzania", Stephan Bad ambaye kiutendaji ndiye msimamizi mkuu wa biashara ya dawa za kulevya alihoji.

Emilio alikohoa kuweka koo lake sawa, alipaswa kueleza ukweli. Tabia ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya kumuua mwenzao haikuwa tatizo. "Naomba kueleza kuwa wakati naingia Dar es Salaam juzi, njia zote zilikuwa vizuri na wazi kabisa, tukumbuke kuwa nilikwenda Dar es Salaam, baada ya shehena hiyo kukwama, Adis Ababa, Ethiopia, Carlos alikuwa amenieleza kuwa hali haikuwa nzuri wakati huo, lakini baada ya kuweka mambo sawa, hali ikawa shwari, sasa si wakati wa kulaumiana, vijana wanajaribu kila njia kuweka mambo sawa. Tusubiri". 

"Wakati mwingine tuwe makini na jambo hili, tusikurupuke kutoa maamuzi", Stephan Bad alieleza. "Hakika, lakini nimesikia kuwa nchini Tanzania sasa njia nyingi zimefungwa, serikali ya nchi hiyo imekuwa macho zaidi, lakini watu wetu Dar es Salaam wamefikishwa mahakamani leo, Carlos amenihakikishia kuwa watatoka kesho, 

Hakimu wa kesi hiyo ni mtu wa upande wetu, inasemekana alishinikizwa atoe huku leo, lakini pesa imefanya kazi yake, 
ametumia vifungu vya sheria kuweka mambo sawa, jambo hili litakwisha kesho", Emilio alidokeza.

"Punda afe mzigo ufike, nchini Tanzania hatuna mkataba na mtu zaidi ya Carlos Dimera, hao wengine ni vibaraka tu, lazima mtambue kuwa tuna nguvu kubwa Dar es Salaam, hao waliokamatwa tuwaache wafungwe, ili iwe rahisi kuupata huo 
mzigo, nakuhakikishia wakifungwa hawa itakuwa na nafasi nzuri kwetu kuupata mzigo huo", Stephan Bad alieleza msimamo wake.

"Itakuwa ngumu zaidi, Carlos amenihakikishia uwezekano wa kuwatoa upo, hakuna sababu ya kuwatosa", Emilio alishauri.

"Hapana, wakati mwingine tumia akili yako ya ziada, fahamu kuwa watu hawa wakifungwa, serikali itatangaza kuteketeza shehena ya dawa hizo, lakini kabla hazijateketezwa zinarejeshwa kwetu, wahusika wanateketeza maboksi na makuti ya mnazi chini ya ulinzi mkali, hatimaye mzigo unaingia sokoni, ndivyo tunavyofanya", Stephen Bad alieleza.

"Ushauri mzuri, Carlos aelezwe kuhusu jambo hili, japokuwa siamini kama anaweza kukubaliana nasi", Emilio alidokeza.

"Hili ni agizo, asikubali yeye nani? Nakuhakikishia Emilio, kama tuna nia njema ya kuupata mzigo huo, hatuna budi kuwatosa Hawa na Tony, waliokamatwa, lakini ukijaribu mbinu nyingine tumeumia", Stephan Bad alisisitiza.

"Hofu yangu ni kwamba tunaweza kukosa mama na mwana", Emilio alidokeza.

"No. Usihofu kabisa, nakuhakikishia hii ndiyo njia salama ya kupata mzigo huo, unakumbuka kilichotokea Msumbuji na Congo? sasa una shaka gani?", Enock Jonson alihoji.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu, hatimaye kikao kiliafiki kuwa, Hawa na Tony watoshwe. Carlos Dimera alipewa taarifa ya siri kuhusu mwafaka huo, akautafakari msimamo huo. Lakini hakuwa tayari kuutekelezq. 

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU