NOTI BANDIA

SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA

Nilizinduka na kujikuta ndani ya chumba kidogo chenye joto kali na giza nene, mikono na miguu yangu ilikuwa imefungwa madhubuti kwa kamba ngumu. Upande wa mikono yangu ulifungiwa kwenye nondo za dirisha, huku miguu ikifungwa upande mwingine kwa lengo la kunizuia kabisa nisiweze kugeuka. Hakika nilikuwa kwenye kitanzi cha mauti.

Kichwa changu kilikuwa katika maumivu makali, nadhani yalisababishwa na aina ya vifaa walivyotumia adui zangu wakati wakiniteka nyara. Nilijaribu kuinua kichwa juu kuangalia jinsi nilivyofungwa sikuweza, nikapoteza matumaini ya kuishi tena katika dunia hii.

Akili yangu ilifanya kazi haraka, nilijiuliza jinsi nilivyofika ndani ya chumba hiki. Baada ya kutafakari kwa kina, nikakumbuka kuwa wakati napata kinywaji pale Bella Hotel, eneo la Kinyerezi, alikuja mtu mmoja akaketi karibu yangu, nakumbuka wakati tunaongea na mtu huyu niliguswa na kitu katika miguuni yangu, nikapoteza fahamu. "Nani hasa wamenileta katia chumba hiki. Kwanini hawakuniua kama kusudi lao lilikuwa hivyo", nilijiuliza.

Kutokana na giza nene lilolokifunika chumba hiki, sikujua eneo nililokuwa, hata kama kungekuwa na mwanga bado ilikuwa vigumu kujuwa. Milijilaumu kuwaacha wenzangu, Julius Nyawaminza, Claud Mwita na Fred Libaba, nilijiuliza jinsi watakavyopata shida kunitafuta bila mafanikio. Lakini pia niliona vizuri wao kuendelea pale nilipofikia. Nilijiuliza hili na lile, nikakosa majibu ya haraka, nikaishia kukubali matokeo. 

Niliwakumbuka watoto wangu wapendwa, Warioba, Changasi na Masey, ambao walikuwa bado wadogo sana wakihitaji msaada wangu, niliwahurumia jinsi watakavyolia baada ya kusikia kifo changu. nijaribu kukumbuka tena niko wapi nikakosa jibu la haraka. Nilimkumbuka mama yangu mzazi, Nyamadoho, nilijiuliza jinsi atakavyolia baada ya kupata taarifa za kuuawa kwangu. 

Joto kali ndani ya chumba hiki, lilizifanya nguo zangu za mwilini kulowa maji ya jasho, nilijaribu kwa mara nyingine kupima kiwango cha kamba nilizofungwa upande wa mikono na miguu, zilifungwa kwa uhakika. 

Nilisikia watu wakitembea nje ya chumba hiki, halafu mlango ukafunguliwa, mimi nikafumba macho na kurejea katika hali yangu ya awali, ya mtu aliyezimia. Watu wawili waliingia ndani, mmoja aliwasha taa, mwingine akasogeza sikio karibu yangu.

"Bado hajaamka huyu. Nadhani, bado masaa machache atakuwa amezinduka, daktari alisema pigo alilopata litamchukua masaa matatu hadi manne, kwa vile mtu mwenyewe anafanya sana mazoezi", mmoja wa watu hawa alieleza.

"Mimi sikuona sababu ya kumuacha hai mpaka sasa, watu wa aina hii ni hatari sana, kwa vile bosi ametaka kumuua kwa mikono yake, basi tusubiri azinduke", alisema mtu wa pili.

"Namsikilitikia sana, maana atakufa kifo kibaya mno, Carlos alivyo na hasira na mtu huyu, anaweza hata kumla nyama", alisema mmoja wa watu hawa, huku mapigo ya moyo wangu yakinienda kasi. 

Halafu wakaingia watu wengine zaidi ya sita, akiwemo mzungu Carlos Dimera. Mmoja wa watu hawa alikuja moja kwa moja karibu yangu na kunimwagia maji mengi kichwani, mengine yaliingia katika masikio, nikajidai kushituka na kujaribu kuvuta kamba ili nisimame.

"Tulia wewe masikini mjinga, umerukaruka hatimaye umeingia kwenye anga zangu. Teacher... ulifanikiwa kututia hasara, umevuruga mipango yetu, lakini waswahili walisema siku za mwizi ni arobaini, leo arobaini yako imetimia. Niliahidi kuwa siku moja nitakuchinja kwa mikono yangu, siku hiyo imefika", Carlos alisema huku akicheka.

"Ni kweli... kama ulivyosema, siku za mwizi ni arobaini, lakini mimi si mwizi, hata wewe arobaini yako itafika, heri yangu mimi ambaye arobaini imenikuta nikitetea watuwanyonge, jiulize arobaini yako itakuwaje?" nilimwambia.

"Kwa taarifa yako nguvu yetu ni kubwa, mtu mwenye pesa hafungwi kaka, ndiyo maana nikasema leo ndiyo mwisho wa maisha yako, wenzako wengi walijaribu wakashindwa, nilijiuliza wewe utaweza? Sasa utauawa baada ya mahakama kutoa hukumu ambayo itawashangaza wengi, Hawa na Tony hawana hatia, pamoja na hilo, madawa uliyokama uwanja wa ndege yatarejeshwa mikononi mwetu..., oh pole sana Teacher kwa kupoteza muda wako", Carlos alieleza kwa kebehi.

"Sidhani kama hakimu atakuwa mpuuzi kiasi hicho, mpaka akubali kuharibu kazi yake, hata kama nitakufa leo, sijui kifo gani? Lakini siogopi, maana kifo ni kifo tu, hata wewe siku yako itafika, sijui utajibu nini mbele za mungu", nilimwambia, akasogea karibu yangu na kunipiga kibao kwa hasira.

"Sina muda wa kubisha na mtu mjinga, wengine tunatafuta maisha mazuri, wewe unatafuta kifo, jiandae kufa, kibaya zaidi ni kwamba hata ndugu zako hawataiona maiti yako", alitamba.

"Hewezi kujisifu kwa kumpiga maiti, ungekuwa mwanaume ungenitafuta wewe ili nikuonyeshe kazi, bila shaka habari yangu umewahi kuisikia ndiyo maana ukakodi majasusi kutoka nje ambao siku chache zijazo watakuwa mikononi mwa serikali, kuniua mimi usidhani utakuwa umemaliza tatizo, serikali ipo tu", nilisisitiza.

"Hilo unasema wewe, wenzako katika serikali wanapenda kuishi katika maisha mazuri ndiyo maana nikasema hukumu itakayotolewa leo kuhusu Hawa na Tony, itakushangaza hata  wewe na wengine wasiojitambua".

"Mimi najitambua, ndiyo maana nikasema haiwezekani, labda kwa mtu mjinga kama wewe ndiye utaamini hivyo", nilisema kwa hasira huku nikisikia maumivu makali katika mwili wangu.

"Simba na Nyati, mchapeni huyu mpuuzi", Carlos aliagiza, wakaanza kunitandika ngumi za tumboni, walinipiga jinsi walivyoweza, nilisikia maumivu makali, lakini kwa vile nilijua hii ndiyo siku yangu ya mwisho, sikujali.

"Nyie vibaraka, mnaotumwa kuwahujumu wenzenu, shauri yenu, siku yenu itafika, mtalia na kusaga meno", nilisema huku nikipiga kelele.    

Baada ya kunipiga sana, mmoja alizima taa, wakatoka ndani ya chumba hiki wakafunga mlango na kuniacha nikiwa nimefungwa madhubuti ndani ya chumba hiki, niliomba mizimu ya kwetu inisaidie, nilimuomba marehemu bibi yangu Matobela, aliyenilea toka nikiwa mchanga. Nilikumbuka jinsi bibi alivyonitokea siku niliyopata ajali katika maeneo ya Gairo, nikitoka Dodoma kurejea Dar es Salaam usiku, bibi akiwa ndani ya mavazi meupe na alinisimamia nikafika salama. Hivyo nilimtegemea leo pia. 

Maumivu makali katika mwili wangu nusura nipoteze tena fahamu. Nilimkumbuka Kanali Benny Emilly, Mkuu wa kitengo cha upelelezi, nilijiuliza jinsi atakavyohaha kunitafuta, jinsi atakavyoumizwa na taarifa za kuuawa kwangu, nilijilaumu kwa makosa ya uzembe niliyofanya hata nikakamatwa kama kuku.

Wakati nikiendelea kutafakari, mara nikahisi nyayo za mtu zikiukaribia mlango, sekunde chache baadae taratibu mlango wa chumba hiki ulifunguliwa, mtu mmoja aliingia kwa mwendo wa kunyata. Kutokana na hali ya giza ndani ya chumba hiki, niliangalia kwa makini, alipowasha taa mimi nikafumba macho.

"Teacher, Teacher, Teacher amka", sauti nyepesi ya Mama Feka ilisikika katika masikio yangu.

"Naam", niliitika.

"Nilidhani umezimia tena?", alihoji huku akitoa kisu kidogo kwenye matiti yake na kuzikata kamba zilizofungwa kwenye mwili wangu. "Naomba unisikilize, kuna ulinzi mkali sana huku nje, ukitoka muda huu hutaweza, cha msingi endelea kuwa humu ndani, Carlos anasuburi mahakama imalize kutoa hukumu halafu aje kukuchinja, usihofu, wewe jiweke sawa ili wakija uwe vizuri", alieleza Mama Feka.

"Lo, Mama Feka, ni wewe kweli Molamu au malaika kashuka kutoka mbinguni, hakika umekuja kuniokoa wakati ambao sikutegemea kabisa, amini siwezi kufa tena, nitajitetea kwa nguvu zangu zote, jinsi ulivyoingia nilidhani Ninja", nilitania.

"Kama ulivyonielekeza".

"Tuko wapi hapa?, nilimuuliza.

"Utapajua baadaye, si wajuwa Dar es Salaam mimi mgeni", akazima taa. 

"Umejuwaje niko ndani ya chumba hiki?".

"Tutaongea baadae Teacher, wako kwenye kikao cha mwisho, wanasubiri taarifa ili Carlos aongee na wewe tena, halafu akuchinje, ndiyo nikatoka kama nakwenda kujisaidia, muda huu si wa kuongea, nikichelewa watanitafakari", alieleza Mama Feka na kutoweka.

"Kila la heri", nilimwambia huku nikisimama kuweka viungo vyangu vya mwili vizuri, nilitumia nafasi hiyo kufanya mazoezi ya viungo, niliruka na kupiga push up kadhaa, baada ya kuuandaa mwili wangu kwa kazi, niliuvuta mlango taratibu ili nitoke, kumbe Mama Feka alipotoka aliufunga kwa nje. Ikanibidi kusubiri kitakachotokea.

Vifaa vyangu kadhaa vya kazi, ambavyo mimi huvificha sehemu mbalimbali ya mavazi yangu, vilikuwa vimechukuliwa isipokuwa kamba ndogo sana, ambayo niliifungia kiunoni kwangu, kwa muda mfupi nikabaini kuwa watu walioniteka walikuwa wajuzi wa hali ya juu katika tasnia hii. Lakini niliamini kuwa nilikuwa mjuzi zaidi yao. Nilijiuliza kama walikuwa wajuzi wa mambo kwanini wasije wao binafsi kama wao, waliujuwa muziki wangu ndiyo maana walijiandaa, wangekiona cha moto.

Mara nikazisikia nyayo za watu zikiusogelea mlango, haraka nilitumia nafasi hiyo kutoa balbu juu, nikasimama karibu na sehemu ya kuwashia taa. Mlango ulifunguliwa, mtu wa kwanza aliingia akaelekea sehemu ya kuawashia taa, alipobonyeza kitufe ili taa iwake, giza liliendelea kutawala.

"Balbu imeungua", alisema.

"Haiwezekani, imeungua saa ngapi? Labda kuna sababu", alihoji mwingine wakati nae akiingia ndani.

Kutokana na hasira niliyokuwa nayo, niliruka na kumpiga mmoja karate ya shingo, nikamsindikiza za teke la kifua akaenda chini, wakati mwenzake akijiuliza nini kimetokea, nilimdaka na kumgeuza mbele nyuma, huku nimembana vizuri kwenye koromero, akashindwa kutoa sauti. Niliwaua haraka sana, halafu nikawaburuza kuwatoa pale mlangoni.

Walikuwa wamevaa mavazi yaliyofanana, suluali nyeusi, makoti ya rangi ya blue na kofia nyekundu, nilichukua mavazi ya mmoja wao aliyekuwa na umbo kama langu nikavaa, niliwapekuwa, kila mmoja alikuwa na silaha kubwa aina ya AK 47, niliitwaa silaha moja na nyingine nikachomoa magazini, nikiwa na matumaini tele. Mimi nikiwa na aina hii ya silaha hata uniletee Kombania nzima ya jeshi, hawaniwezi.

Nilitoa magazini, nikahakiki idadi ya risasi zilizokuwa ndani, kila magazini moja, zote zilikuwa na ujazo sawa, yaani risasi. Bahati nzuri ni kwamba bunduki hii ilikuwa zimekatwa kwenye mtutu wa mbele ili risasi zinapotoka zisitoe sauti. 

"Jamal, Jamal..., fanyeni haraka", sauti kutoka nje ilisikika. 

"Njoo uone", nilisema kwa sauti ya kubana. Akasukuma mlango na kujitosa ndani, alivaa kama wenzake, huyu alikuwa na bunduki aina ya SMG ikiwa begani. 

"Unasemaje?" nilimuuliza kwa sauti ya kutisha, aliposikia sauti yangu, akaamini kuwa mimi siyo Jamal, akakurupuka ili atoe bunduki begani, lakini alikuwa amechelewa, nilimpiga risasi ya kifua, akaanguka chini. Nilimvua bunduki yake nikatoa magazini, sasa nilikuwa na risasi za kutosha, kukabiliana na adui wa aina yoyote. Nikajidhatiti na kutoka ndani ya chumba hiki.

Nilijiuliza wapi watu hawa wamepata aina hii ya silaha za kivita, silaha ambazo haziruhusiwi kwa watu binafsi,  nilitafuta sehemu nzuri, nikajibanza kisubiri kitakachotokea. Sikuwa na saa lakini ilikaribia kuwa saa nane, tisa au kumi za alfajiri, kutokana na utabiri wangu.

Ukuta mkubwa uliopambwa kwa nyaya za umeme juu uliizunguka ngome hii, nilisikia kelele za mashine zikifanya kazi huku na huko, ilionekana sehemu hii ilikuwa ya viwanda, nilitoa kamba yangu niliyojifungia kiunoni nikaikata kidogo, nilitumia kipande hicho kufunga magazini mbili za risasi pamoja, moja ikiangalia chini na nyingine juu, nilifanya hivyo ili magazini moja itakapoishiwa risasi iwe rahisi kwangu kuchomoa na kupachika nyingine haraka.

Pamoja na kuvaa mavazi kama wao, lakini nilitembea kwa kunyata, maana sikujua wanazotumia mawasiliano gani kwenye ngome hii, taratibu nilitafuta mlango mkubwa wa kutokea, nilipouona, nikafanya kazi nyingine ndogo, kutafuta sehemu waya za umeme zinazolinda ukuta huu zilikotokea, hii pia nilifanikiwa.

Kwenye langu kuu kulikuwa na askari wasiopungua sita, wote wakiwa na silaha aina ile ile AK 47, hawa walikuwa wakitembea huku na huku kuangalia usalama wa eneo hilo. 

Mara nikawaona watu wawili wakitoka kuelekea kwenye mahabusu yangu, chumba ambacho nilikuwa nimefungiwa, walivaa sawa na mimi, koti la blue, suluali na kofia nyekundu. Niliwafuata taratibu, nilipowakaribia, niliachia risasi kadhaa zikawapata, mmoja alikufa pale pale, mwingine akapiga kelele za kuomba msaada kutokana na maumivu aliyopata. Kumbe nilikuwa nimechokoza mzinga wa nyuki. 

Risasi zilipigwa mfululizo pale nilipokuwa, bahati nzuri nilikuwa nimelala kifudifudi, nilisubiri wasogee, halafu nikaachia tena risasi kadhaa zikawapata. Kumbe walikuwa wengi, wengine wakitoka ndani, hivyo ilinipasa kutumia hesabu zaidi.

Nilipanda juu ya ukuta uliokuwa mbele yangu, niliweza kuwaona vizuri, niliachia tena risasi nikaua kadhaa, nikaruka na kukimbilia upande mwingine, nikiacha eneo hilo likichakazwa kwa risasi. Nilikuwa nimejibanza eneo lingine, walipoona kimya wakasogea, nikatumia nafasi hiyo kuwafyatulia risasi, nikaua askari wao kadhaa na kuhama haraka sehemu niliyokuwa. Wakaichakaza tena sehemu hiyo kwa risasi.

Kelele za askari zilisikika kutoka kila pembe ya ngome hii, wakisema, "piga risasi huyo, ua kabisa", lakini mimi nilikuwa na kusudi moja tu, kumsaka Dimera, aliyenipiga kibao wakati nimefungwa kamba. Mara nikamuona Dimera, Mama Feka na vijana wawili wakiingia ndani ya gari, lango kubwa likafunguliwa na gari hilo kutokomea nje.

Ilikuwa nafasi nzuri kwangu kumshambulia Dimera, hata kumuua kwa risasi, lakini niliogopa kitu kimoja, ningeweza kuhatarisha maisha ya Mama Feka. Wakafanikiwa kutoweka huku nikirusha risasi bila mpangilio, askari waliokuwa mlangoni walikimbia nami nikapata upenyo na kutoka.

Nilipotoka nje, sikuyaamini macho yangu, kumbe mahabusu yangu ilikuwa ndani ya kiwanda cha Blanket, kilichoko Keko. Nilijiuliza imekuwaje watu hawa watumia sehemu hii, kutokana na muda, niliahidi kulifuatilia baadaye. Nikaondoka.

ITAENDELEA 0784296253 

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU