NOTI BANDIA

SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE

Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa hivi kupita, risasi zikarindima tena huku nafsi zetu zikiwa zimejawa na hofu kubwa. Ghafla taa ndani ya chumba hiki ziliwashwa, vijana wawili nadhifu sana waliingia ndani ya chumba hiki kwa kasi ya ajabu, silaha zao zikiwa mikononi wakazikata kamba zilizofungwa kwenye miguu na mikono yetu kwa visu vikali. Ukweli ni kwamba Vijana hawa sikuwahi kuwajua kabisa.

"Poleni sana bosi, tutaongea baadaye", alisema mmoja wa vijana hawa baada ya kuzikata kamba tulizofungwa kwa kisu chake imara.

"Usijali", niliwaambia huku zikinyoosha viungo vya mikono yangu. Risasi zikasikika tena nje, mmoja wa vijana hawa akatufahamisha kuwa tusihofu ilikuwa kazi ya Peter Twite, ambaye alikuwa nje ya chumba hiki kuimarisha ulinzi wetu.

Bahati mbaya ni kwamba, hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa katika vurumai hiyo, Carlos Dimera, Mzee wa Mtemba na  vijana wao kadhaa walifanikiwa kutoroka salama kutoka katika eneo hilo. Kazi nzuri iliyofanywa na Mama Feka ilikuwa imenusuru maisha yetu.

Ilikaribia kuwa saa tano za mchana, Wakati wote sikujuwa tulikuwa sehemu gani, baada ya kutoka ndani ya chumba hiki, nilishangazwa kuona kumbe tulikuwa kwenye ofisi za karakana ya Tazara, kando ya barabara ya Nyerere. "Mmmh inakuwaje", nilijiuliza kwa sauti baada ya kumuona Peter Twite akinijia.

"Pole sana mkuu, tuondoke haraka eneo hili, watu wengi sana wameuawa hapa, tuondoke kabla polisi hawajafika, wanaweza kutuleta nongwa, tukacheelewa", alisema huku akinishika mkono kunisabahi.

"Ni kweli kabisa Petet, hii inaweza kutuchelewesha pia", nilimwambia, sisi tukaingia ndani ya gari alilokuwa akiendesha Twite, tukaondoka kuelekea sehemu za Vingunguti. "Wapi Fred?" Niliuliza.

"Fred, tuliwasiliana saa tatu hivi, akaniuliza kama nimesikia taarifa za mauaji ya Hakimu aliyehukumu kesi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, nikamwambia nimesikia, akaniuliza kuhusu kutoroka kwa watuhumiwa hao mikononi mwa polisi, nikamjulisha kuwa taarifa hizo ni kweli, mwisho akanifahamisha anawatafuta lakini hawapati, baada ya hapo sijamsikia tena na simu yake haipatikani", alieleza Twite wakati anavuka kwenye njia ya reli ya Vingunguti.

"Twende Green Pub, nadhani patafaa kwa mazungumzo kidogo wakati tukifikiri na kutafakari tuwafanye nini watu hawa", nilisema, wakati Peter Twite akizungusha usukani wa gari tukaingia Barabara ya Nyerere na kuelekea eneo la Vingunguti.

"Watu hawa wamejipanga vizuri kutenda uhalifu", Nyawaminza alisema baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu.

"Inaonyesha hivyo. Lakini tuwe makini sasa, maana jana tu nimekamatwa mara mbili, naamini wanatumia mawasiliano ya mitandao kujua mahali tulipo, sasa tusiamini mtu yeyote", niliwaasa.

"Hakika. Mimi bado najiuliza ilikuwaje wakaingia kwenye ofisi za umma pale karakana na kuzitumi kama sehemu zao, ingekuwa siku za mapumziko kama sikukuu ama Jumamosi, Jumapili nisingehofu, lakini leo siku ya kazi?" alihoji Twite.

"Tutajua baadae. Hawa ni wahalifu wakubwa, wanachofanya ni kuvamia na kuua wahusika, wanatumia eneo hilo kwa muda halafu wanasepa. Wengine hutumia maeneo hayo nyakati za usiku, lakini hawa wako vizuri mpaka wakati huu mchana kweupe?" nilisema wakati Twite amesimama kwenye taa za kuongoza magari za Jeti.

Tulikuwa na magari matatu, ambayo hayakufauatana kwa karibu kutokana na hali ya usalama. Peter alichepuka tukaingia kwenye barabara mbovu ya vumbi, baada ya kuvuka kizuizi cha reli ya kati, akaingia kulia kama tunarudi katikati ya Jiji. Tukazipitka ofisi za Kiwanda cha BECO, Nilikuwa makini kuangalia kila gari lililokuwa mbele au nyuma yetu, hatmaye tukaingia Green Pub.

"Ipo njia ya mkato hapa, lakini nilipita Jeti kwa sababu za usalama", Twite alidokeza.

"Nilikusoma, ndiyo maana nikawa kimya", nilijibu wakati tukitafuta sehemu nzuri ya kuketi. Bahati nzuri mwenye sehemu hii rafiki yangu Kinyami Mwitazi ananifahamu, alipotuona alituelekeza sehemu nzuri tukaketi. Bada ya kila mmoja kuagiza kinywaji chake, tukagawanyika, wale vijana wakatafuta sehemu yao mbali kidogo tofauti na sisi.

"Peter, najiuliza sijui hata nikushukru kwa maneno gani. Maana sijui hata ilikuwaje ukajuwa kuwa tumefungiwa pale Karakana?" nilianzisha mazungumzo.

"Ni hadithi ndefu, lakini tumshukru sana Mama Feka, nadhani atafika hapa muda si mrefu. Bosi ulicheza sana kumuingia dada huyu katika kazi hii, bila yeye sijui ingekuwaje?" Peter alidokeza.

Mara Pikipiki kubwa aina ya Honda XL CC 250 ikasimama upande wa pili wa Reli, juu ya pikipiki hiyo kulikuwa na vijana wawili nadhifu, mmoja wa kiume na mwingine mwanamke wote wakiwa wamevalia miwani ya tinted usoni. Msichana mrembo sana alishuka, baada ya kuangalia huku na kule akatembea kuelekea mahali tulipoketi.

"Unamfahamu huyo?" Peter aliniuliza.

"Bila shaka ni Mama Feka, ama kweli ametakata", nilisema. Yule kijana aliyemleta aliinua mikono, akatupungia halafu akaondoka.


 "Na huyo?".

"Huyo ni kjana wetu, miongoni wale ulioagiza wakae kwenye pointi wakiwa na Pikipiki, vijana hawa hawajalala toka tuanze kazi hii, kama tukiimaliza salama, tusiwasahau, utazani wamewahi kufanya kazi hizi", Peter alishauri.

"Ni kweli kabisa Peter".

Baada ya kutushika mikono, Mama Feka alivuta kiti karibu yangu akaketi. "Poleni sana Teacher, nasikia usingizi sana lakini usijali, karibu tutashinda vita nitapata wasaa mzuri wa kulala", alieleza.

Akaanza kutueleza habari zote, toka nilipokamatwa kule Hoteli Bela Vista Kinyerezi, alivyoniwezesha kutoroka pale kiwanda cha Blanket Keko, kutekwa kwa Julius Nyawaminza, Claud Mwita na hatimaye mimi.

"Shemeji yangu Teacher, kazi hii ni ngumu, lakini nakiri kuwa baada ya wewe kuniingiza katika jambo hili imesaidia kujua mambo mengi, sasa nazijua sababu za watu kuniita Cthia Rothrock, nimewiva sana, angalieni saa zenu", alisema wote tukainamisha vichwa kuziangalia saa zetu, ilikaribia kuwa saa saba mchana.

"Inakaribia saa saba mchana. Binafsi nimsifu na kumpongeza sana Peter, baada ya kutambua kuwa simu zenu zimeingizwa kwenye mtandao wa mawasiliano na kila mlichofanya pale pale kilionekana, sikuona sababu ya kuwasiliana na simu zenu, nilitengeneza laini yangu ya siri, ambayo nimeitumia kwa ajili ya kuwasiliana na Peter tu. Na kweli imesidia kuokoa maisha yenu, nilichanganyikiwa sana nilipomuona Mzee wa Mitemba, yule Mzee akiitwa maeneo kama yale, mmmh usitehgemee kutoka salama, tumshukru sana Mungu", alisema.

"Ilikuwaje wakatoroka wakati tulikuwa tumeizingira ofisi ile?, tena ajabu ni kwamba tumeua watu ambao hawahusiki kabisa", Peter alihoji.

"Pale ndani ya ofisi ile, chini kuna milango miwili ya siri, ukibonyeza kitufe inafunguka unazama na kuna njia ya kutokea sehemu nyingine kabisa, tumepita huko", alieleza Mama Feka.

"Hawajakushtukia?", niliuliza.

"Wee, siyo rahisi, unajuwa wakati nawasiliana na Peter, kidogo Carlos anishtukie, lakini nilikuwa nimefanya ujanja fulani, nilifungua sehemu ya game, nikawa nacheza huku natuma ujumbe, kwa kuwa simu yangu niliitoa sauti, basi ilikuwa kazi rahisi kujibu kila swali Peter aliloniuliza".

Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, akaanza kutueleza tena habari za kutisha na kusikitisha sana, "Watu wengi sana wamepotea, nimeona mambo mengi ya kutisha sana, namshukru Teacher alinijenga kisaokolojia kabla sijaingia huko. wale watu ni hatari sana. Naomba mnisikilize kwa makini sana", tukajiweka tayari kumsikia huku nywele zikinisiimka kichwani, sikuamini kama Mama Feka angetusaidia kiasi hiki. Kimya kimya nilituma ujumbe wa maandishi kwa Kanali Benny Emilly ili naye afike sehemu hii maana tulikuwa tunajiandaa kuingia vitani.

"Mkishindwa kuwakamata leo, itakuwa ndiyo salama yao, hawatakamatwa tena, wamepanga kutokomea leo, hivi tunavyongea hapa kuna meli ndogo iko ufukweni mwa Bahari, itaondoka nadhani itakuwa saa kumi Alasiri, wana kikosi kizuri sana, wanao vijana mahiri katika mapigano, ili kazi yetu iwe rahisi lazima tujipange sawasawa", alishauri.

"Tumekusikia", nilimwambia, halafu nikawageukia wenzangu, "bila shaka wote tumemsikia Mama Feka?".

"Naam", walijibu huku tukiendelea na vinywaji. Mara simu yangu iliita nikapokea. Ilikuwa simu kutoka kwa Kanali Emilly.

"Angalia upande wako wa kuume ulipoketi, kuna Pick Up single cabine rangi ya kijani, ina kiturubai nyuma, njoo ingia tuzungumze".

"Nakuja bosi", nilisema huku nikisimama. "Jamani, ngoja nimsikilize kigogo, nendeleeni nakuja", nikawaacha na kuelekea kwenye gari lililokuwa limeegeshwa mbali na eneo tulipoketi. Nilipokaribia dereva wa gari hilo alishuka na kunielekeza niingie upande wake.

"Jambo Mkuu", nilimsalimia Kanali Emilly baada ya kuongia ndani ya gari hii.

"Jambo, habari ya kupotea Teacher?. Mpaka nikapatwa na hofu kubwa. Ulipatwa na nini Kapteni?"

Nikaanza kumweleza kilichonitokea hata nikatekwa na kutoroka kule Kiwanda cha Blanketi. Nikaeleza jinsi tulivyoponea chupchup kuuawa kwenye ofisi za Karakana ya Tazara, maelezo haya kiasi fulani yalionekana kumuumiza rohoni.

"Poleni sana vijana wangu. Siku zote Mungu humsaidia asiye na hatia, yule anayeonewa. Teacher mwanangu, mpaka sasa adui anaelekea kuchanganyikiwa, cha msingi tusilegeza kamba, au unasemaje?"

"Hakika".  
 
"Mmekwama wapi?".

Nikaanza kumweleza kuhusu mpango ulio mbele, "Hatujakwama Mkuu, tunachofanya sasa ni kujadili plani B, kuvamia eneo fulani ufukweni mwa Bahari. Taarifa zilizopo ni kwamba wamepanga kutoroka leo jioni wakitumia Meli ndogo ambayo tayari imejazwa shehena ya dawa za kulevya kwa ajili ya kuelekea Mombasa. Na sisi hatutawapa nafasi hiyo, Leo ndiyo mwisho ama wao ama sisi", nilisema.

"Amina", Kanali Emilly alisema kwa ishala huku akiangalia juu.

"Samahani, Afande nakuomba shuka kwenye gari twende uongee na vijana, uwape hamasa, vita si lelemama, habari kutoka kwenye vyanzo vyetu ni kwamba adui ana nguvu na vifaa vya kisasa kama silaha na mitambo", nilimwambia akahamasika, akafungua mlango tukashuka kuelekea kwa wapiganaji. Wote wakasimama, machozi ya furaha yakamtoka.

ITAENDELEA 0794296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU