KIKOSI CHA KISASI


SEHEMU YA NNE 

'WP'

III

Willy bila ya kujua kuwa alikuwa ameingia ndani ya mji ambao ndiyo Makao Makuu ya kikundi kiitwacho 'WP' kikundi maalumu cha 'Boss' ambacho kazi yake ilikuwa kuendesha hujuma dhidi ya harakati za Ukombozi wa Kusini mwa Afrika na vile vile kupiga vita harakati zozote zinazofanywa na wanamapinduzi wa Afrika ili kuendeleza fikra za kimaendeleo katika Afrika huru, aliendelea na safari kwenye barabara hii ya Patrice Emery Lumumba akitokea uwanja wa ndege kuelekea mjini. Akiwa kwenye barabara hii Willy mawazo yake yalimfikiria Marehemu Patrice Emery Lumumba, alikuwa amesoma habari za Lumumba na alikuwa mmoja wa wapenzi wake. Hivi moyo wake ulisisimkwa kufikiria kuwa alikuwa akiendesha kwenye barabara hii ambayo ilikuwa imeitwa kama kumbukumbu ya shujaa huyu wa Afrika.  

Ghafla akiwa amesafiri kama kilomita kumi na tano hivi akiendesha njia panda ya 'Echangeur de Limete' mawazo yake yaliiendea gari moja iliyokuwa nyuma yake ikiwa imehakikisha kuwa inabaki nyuma ya gari lake na huku katikati yao kukiwa na magari mawili au matatu. Willy alikuwa amejenga silika ya namna hii kiasi cha kwamba alikuwa akiweza tu kuhisi kitu bila sababu maalumu. Kwa sababu alikuwa akiiamini sana silika yake, mara mawazo yake yalilitilia mashaka gari hili kuwa huenda linamfuata, alikata shauri kuthibitisha. Hivyo aliendelea na safari yake huku akiliangalia gari hilo ndani ya kioo cha kuendeshea gari. Kila alipopunguza mwendo na mengine kumpita, gari hili lilihakikisha kuwa nalo linapunguza mwendo kubaki pale pale. Na kila alipokuwa anaongeza mwendo nalo linaongeza mwendo. Hivi alihakikisha kuwa gari hili lilikuwa linamfuata. Alipofika kwenye kona ambapo barabara ya P.E Lumumba na barabara ya Bongolo zinapokutana alikata shauri kuingia barabara ya Bongolo ili aweze kulikwepa hili gari aliloamini kuwa lilikuwa linamfuata. Alipoingia barabara ya Bongolo gari hili nalo aliliona baada ya muda mfupi lilikuwa nyuma ya gari lingine likizidi kumfuata. Kisha alikata na kuingia barabara ya L'universete, tena baada ya muda mfupi aliliona gari hilo likiwa nyuma ya gari lingine likiwa bado linamfuata. Jambo hili lilimshangaza sana Willy maana yeyote aliyekuwa akimfuata alikuwa mjuzi sana katika kazi yake. Kitu kilichomshangaza sana ni kuwa alikuwa ameingia Kinshasa hata saa haijamalizika, na wala mjini alikuwa hajafika na tayari alikuwa ameanza kufuatwa.

Hili jambo lilikoroga mawazo yake kiasi kikubwa sana. Kwa mawazo yake alikuwa akitegemea kuwa ingemchukua muda kabla hajaweza kutambulika, lakini hii ilionyesha kuwa tayari usalama wake ulikuwa hatarini tokea dakika hii, aliamua kuweka mawazo yake pamoja na viungo vyake katika tahadhari. Alisogeza mkoba wake na kufungua zipu, akatoa bastola iliyokuwa juu. Kwani baada tu ya kuagana na Ntumba aliendesha gari mbali kidogo na uwanja wa ndege kisha akasimama na kufungua mkoba kwenye sehemu yake ya siri na kutoa bastola moja. Maana katika kazi ya akina Willy ilikuwa vigumu kukaa tu bila kuwa na silaha karibu hasa ugenini kama hapo ambapo alikuwa ameingia tayari kwa mapambano yoyote yale ambayo yangeweza kutokea. 

Huku akiwa anaendesha, mkono wake mwingine ulishughulika na kutoa bastola hii ambayo alikuwa ameiweka juu tu. Alipokwisha kufanya hivi aliichomeka bastola yake ndani ya suluali mbele kwenye kitovu na kuendelea na safari yake huku akifikiria amfanyie nini mtu huyu. Vile vile alionelea ni jambo la busara kama naye angeweza kumfahamu mtu huyu ni nani na kwa sababu gani alikuwa akimfuata. 

Aliendelea na safari yake akaingia mtaa wa Sendwe kutoka mtaa wa L'universete, alipoangalia bado gari hilo ingawa kwa mbali bado lilikuwa bado likimfuata. Kutoka mtaa wa Sendwe aliingia mtaa wa Funa. Alipoingia mtaa wa Funa vile vile alipunguza mwendo na alipolina hilo gari sasa lilikuwa peke yake linafuata, alikata na kuingia kwenye Stesheni ya Petrol iliyoko mbele ya 'Funa Klabu' halafu akakata shauri kwenda moja kwa moja na kuegesha gari lake katikati ya magari yaliyokuwa yameegeshwa na watu ambao walikuwa wamekuja kuogelea mchana huu katika bwawa la 'Funa Klabu'.

Baada ya kuegesha gari lake, haraka alitelemka huku akiwa ameinama alikimbia kati ya haya magari na kuinuka umbali kidogo toka kwenye gari lake. Alipokuwa akiinuka ndipo lile gari lililokuwa likimfuata lilikuwa linaegeshwa karibu tu na gari lake na ndani ya gari hili mlikuwa na kijana wa umri kama miaka 30 hivi. Alivaa suti ya Abakozi, miwani ya jua na alionekana kijana muungwana kabisa. Alitazama huku na kule kwa mshangao halafu akaliendea gari la Willy na kuliangalia kwa mbali. Kisha akaelekea kwenye bwawa. Willy alipopata nafasi hii, alikimbia mbio tena huku akiwa ameinama katikati ya magari na bila kuonana na watu mpaka karibu na lile gari lililokuwa likimfuata. Gari lenyewe alipochungua ndani yake aliona hamna kitu. 

Alipoangalia kule kwenye bwawa alimuona yule kijana anarudi huku akionekana mwenye kuwa na mshangao na wasiwasi. Willy alikata shauri kujificha pembeni ya gari la pili kutoka kwenye gari la huyu kijana, bila kumuona huku akiangalia nambali za gari la Willy kijana huyu alifungua mlango wa gari lake na kuingia ndani ya gari lake tayari kwa kuondoka. 

Willy alimnyemelea polepole kwa kutambaa chini na wakati alipokuwa anawasha gari moto, na Willy naye akawa yuko sawa na mlango wa dereva. Huku akiwa na bastola mkono alifungua mlango wa dereva kwa ghafla kuhamaki yule kijana alijikuta akiwa anaangalia ndani ya mtutu wa bastola. "Hapo hapo rafiki yangu usijitingishe hii itakuonyesha kuwa si adamu nzuri kufuatafuata watu," Willy alimwambia kijeuri.

ITAENDELEA 0784296253 

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru