RUKSA ILIONGEZA KASI YA UCHUMI - MZEE MWINYI


RAIS Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, 'Mzee wa Ruksa' (pichani) amesema pamoja na Ruksa kuongeza uchumi wakati utawala wake, Taifa lilikubwa na changamoto nyingi ambazo kama asingesimama imara kuzikabili zingesababisha mpasuko kwa wananchi.

Mzee Mwinyi aliyepata umaarufu mkubwa kwa jina la Mzee Ruksa, aliyasema hayo Dar es Salaam Decemba 9, mwaka huu wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara uliopatikana Decemba 9, 1961 kutoka kwa Mwingereza. Mzee Mwinyi alikuwa akizungumza moja kwa moja katika Televisheni na Radio za Taifa (TBC). 

Katika mahojiano hayo maalumu, Mzee Ruksa alisema wakati wa utawala wake, changamoto kubwa kwa Serikali yake ilikuwa madai ya Waislam waliolalamika kulishwa nyama za Nguruwe bila ridhaa yao. Akifafanua Mzee Ruksa akasema, mgongano huo wa waumi wa dini ulitokana na baadhi ya bucha Jijini Dar es Salaam, kuuza nyama za Nguruwe pamoja na Ng'ombe kwa wakati mmoja.

"Hii ilikuwa changamoto kubwa kwa Serikali yangu ya Awamu ya pili, wakati huo mimi nilikuwa Visiwani Zanzibar, nikaletewa taarifa kuwa hali ni mbaya Bara, bucha zinazouza Nguruwe pia zinauza nyama ya Ng'ombe. Kwamba kisu kinachokata nyama ya Nguruwe hicho hicho tena ndicho kinatumika kukata nyama ya Ng'ombe, manung'uniko yakashika moto, kuwa kule bara kuna jambo hili", anasimulia.

Mzee Ruksa anaeleza kuwa, manung'uniko ya Waislam yalishika kasi zaidi hata kuchochea mgogoro mkubwa na uhasama wa dini kati ya Waislam na Kikristu jambo ambalo lilivuka kiwango na kufikia hatua kwa waumini wa dini hizi kutishiana kupigana. 

"Nikatoa tamko kuwa kuanzia sasa kula Nguruwe iwe Ruksa, kula Panya iwe ruksa, yaani kila mtu ale kitu atakacho, lakini asimlishe mtu mwenzake. Ruksa kula bila kuingiliwa, jina la Ruksa likashika kasi", anabainisha.

Akasisitiza kuwa, kila mmoja anaruhusiwa kuabudu dini kwa imani yake. Wakristu, Wahindu na Waislam. Akaagiza kila kikundi kisiingilie kikundi kingine. Mzee Mwinyi anasema msimamo huo ulileta amani na utulivu nchini, kila upande ukaheshimu upande mwingine. 

Rais huyo Mstaafu wa Awamu ya pili anasema, jina la Ruksa liliendelea kushika kasi zaidi pale alipoamua kuwa kila biashara ni Ruksa kufanyika nchini. "Biashara nyingi wakati huo zilikuwa zikifanywa na Mashirika ya Umma tu, akawahamasisha watanzania kukazana katika biashara ili waweze kukuza uchumi na kulipa kodi.

"Nikaagiza kuanzia sasa biashara Ruksa, kujenga nyumba ruksa, vitu vyote ruksa vije. Tulikuwa na sababu ya kuruhusu kutokana na shida ya wakati huo, kulikuwa na maduka maalum, Sukari na nguo zilikuwa kidogo. Mfano kesho una harusi ya mwanao unapangiwa bia, Kanga na Sukari. Mambo haya ndiyo yalichangia jina la Ruksa kusambaa zaidi", anafafanua.

Anasema Taifa limepiga hatua tofauti na wakati huo, ambapo kukosekana kwa vitu alivyovitaja kulichangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa rushwa, akidai kuwa wakati huo Nchi ilikuwa tegemezi. Lakini akawataka watanzania wasiridhike kwani safari ya kuelekea kwenye mafanikio bado inaendelea.

Kama ilivyo kawaida yake, Mzee akarudia maneno yake ya kila siku kuwa anapenda kuona amani ikitawala nchini, huku akiviasa vyama vya siasa vitufikishe salama. Akavitaka vyama vya siasa kuacha kuingilia uhuru wa watu.

"kuwepo kwa vyama vya siasa ni changamoto kwa Serikali iliyoko madarakani kuongeza kasi ya maendeleo, "Lakini kwanini kuna uhasama wa vyama. Kwanini tusizikane eti kwa sababu ya itikadi ya vyama?" Anahoji Amiri Jeshi huyu wa zamani.

Mzee Ruksa akamalizia kwa kusema siasa haikuja Nchini Tanzania kwa ajili ya kuliwagawa Taifa. Akawataka watanzania kutumia siasa kujenga nchi moja.


Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU