KIKOSI CHA KISASI

SEHEMU YA TANO 

MWANZO WA MAPAMBANO

II

Baada ya kuondoka nyumbani kwa Pierre, Jean aliendesha gari lake moja kwa moja mpaka kwake 'G.A.D'. Alikuta kazi ya kutengeneza magari inaendelea kama kawaida. Alikaguakagua kazi kisha akawaita faraghani wafanyakazi wake wawili ambao walikuwa wakisimamia kazi. Mmoja aliitwa Kabeya Mwabila na mwingine Charles Besaleti, mwenye asili ya Kibeligiji. "Jamani kuna kazi muhimu", aliwaeleza. "Tunatakiwa tuchunge kiwanja cha ndege na mahoteli yote kuhakikisha kuwa hakuna mgeni ambaye anaingia mjini hapa bila sisi kuwa na maelekezo yake. Mnaweza kuweka watu wengi mnavyoweza na kutumia kiasi chochote ili mradi jambo hili lishughulikiwe kikamilifu. Kufanyika lifanyike kwa siri kama kawaida kiasi cha kwamba Polisi au CND* haiwezi kututuhumu. Tumeelewana?". alimaliza Jean. 

"Tumeelewa, hilo hamna taabu, litafanyika kwa makini kabisa maana kila hoteli tunaye mtu kwenye orodha yetu ya mshahara ambaye kazi yake ni hiyo kila tuhitajipo maelezo," alijibu Charles. 

"Sitaki kusikia makosa, Kazi hii ifanyike kikamilifu kabisa, watu mnao, pesa zipo, ninachohitaji ni utekelezaji." Jean aliwatilia mkazo. 

"Usitie shaka, kazi itakwenda kama siku zote," Kabeya alimhakikishia na wote wawili wakatoka ndani ya ofisi ya Pierre tayati kufanya kazi.

*CND* Idara ya Upelelezi ya Zaire.

"Wewe shughulikia mahoteli na mimi nitashughulikia njia zote za kuingia Kinshasa, hasa uwanja wa ndege na kwenye kivuko cha kwenda Braville." Charles alimshauri mwenziwe.

"Vizuri, mahoteli yote nitayashughulikia mimi na pale patakapokuwa lazima nitapashughulikia mwenyewe".

"Oke, basi tulishughulikie mara moja".

Kila mmoja aliondoka na kupita kwa vijana waliokuwa wanashughulikia magari, wakiitwa mmoja mmoja hapa na pale tayari kwenda kwenye shughuli hii maalumu ambayo kimsingi ndiyo ilikuwa kazi waliyoajiriwa. Haya mambo ya kutengeneza magari ilikuwa geresha tu, ili kuivuruga serikali isijue maovu yao.

Ilikuwa yapata saa tisa kasoro robo wakati Kabeya ambaye alikuwa ofisini mwake huku akipiga simu mahotelini kwa wadukuzi wake alipofika Memling Hoteli kwenye orodha yake. 

"Hapo ni Memling Hoteli?" aliuliza.

"Ndiyo".

"Mwadi yupo?" Mwandi ndiye alikuwa kwenye orodha ya mshahara ya 'WP' hapa Memling Hoteli kutokana na habari alizokuwa akizitoa kuhusu wageni. Kwa vile alikuwa akilipwa vizuri kwa kutoa habari ambazo alifikiria hazina madhara, alikuwa anaona kama ni bahati kwa upande wake alipoambiwa na Kabeya kufanya hivyo kwa malipo hayo.

"Ndiyo, yupo subiri", alijibiwa. Baada ya muda kidogo aliweza kuunganishwa na Mwadi. 

"Halo Mwadi hapa".

"Ohoo Mwadi, Kabeya hapa habari yako?" Moyo wa Mwadi ulistuka kidogo kumsikia ni Kabeya, ingawaje alikuwa anajua habari alizokuwa anazitoa kwa Kabeya hazikuwa mbaya, lakini wakati mwingine alikuwa akiingiwa na wasiwasi hasa kwa vile sura ya Kabeya ilikuwa ikionyesha uovu mwingi sana. Kwa hivi alipopata simu mchana huu kutoka kwa Kabeya moyo wake ulishtuka sana, bila kuwa na sababu kamili.

"Mzuri, habari yako na wewe?".

"Mzuri tu".

"Unasemaje, maana mimi namaliza kazi nataka kwenda kupumzika".

"Nina kazi kidogo tu Mwadi, ile ya kila siku. Naomba unipe majina na maelezo ya wageni walioingia hotelini kwako toka jana hadi leo na vile vile endelea kunipa kwa siku hizi zitakazofuata. Malipo yako yatakuwa mara tatu ya kawaida. Tafadhali maelezo hayo yanahitaji kabla ya saa kumi leo. Yatakuja kuchukuliwa mahali pa kawaida. Sawa Mwadi?" Mwadi ambaye mara moja mawazo yake yalikwenda kwa kijana yule ambaye alikuwa amewasili mchana ule alisita kidogo kisha akasema. 

"Sawa Kabeya nitashughulikia".

"Asante", alijibu Kabeya na kukata simu.

Mwadi alibaki huku akiwa na wasiwasi, na alikuwa hajui kwa nini roho yake ilikuwa haipendi kufikiria juu ya kutoa maelezo ya huyu kijana Willy Chitalu kwa Kabeya. 

"Sijui ni kwa sababu nimempenda?" alijiuliza. Mawazo mengine yalimjia yakiwa yanamshauri kuwa maelezo haya yalikuwa yakitakiwa kwa ubaya ndiyo sababu walikuwa wako tayari kumlipa mara tatu ya kawaida. Hata hivyo moyo wake nao ulikuwa na wasiwasi na Willy maana kijana huyu alimsisimua sana. Mwishoni aliamua kuwa afadhali atengeneze orodha na kumpelekea Kabeya bila ya kina la Willy, kusudi kama maelezo haya yatakuwa kwa ubaya, ubaya huu usije ukamdhuru kijana huyu ambaye moyo wake ulikuwa umempenda bila kijana mwenyewe kujua. "Afadhali mimi nipate matatizo kuliko yule kijana," alijisemea. 

ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. japo kwa ufupi sana mapambano yameanzia hapo!!safi mkuu

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru