KIKOSI CHA KISASI

SEHEMU YA TANO

MWANZO WA MAPAMBANO

III

Ilikuwa saa tatu wakati Willy alipofika Vatcan Klabu. Alikuta magari yamejaa kiasi cha yeye kukosa maegesho. Hivi aliondoka na kwenda kuegesha gari lake kwenye mtaa wa Kasavubu. 

Vatcan Klabu ni Klabu nzuri sana. Watu wenye heshima zao hufika hapa ili kustarehe. Hamna fujo na kila mtu ambaye anafika hapa inabidi kujiheshimu. Hivi watu wa madaraka Serikalini, makampuni, watu tajiri na mabalozi mara nyingi ndiyo hufika hapa ili kustarehe. Kwa sababu Robert alikuwa akipewa heshima za Kibalozi, mara kwa mara alikuwa akifika kustarehe katika klabu hii ambayo ndiyo ya hali yake. Ingawaje Kinshasa ni mji unaojulikana Ulimwengu mzima kwa kuwa na bendi nyingi zenye ujuzi wa hali ya juu katika mambo ya muziki, lakini Vatcan Klabu ni Klabu kubwa ambayo haina bendi bali kuna 'disco'. 

Baada ya kuegesha gari lake, Willy alienda moja kwa moja mpaka kwenye lango la ua wa Klabu hii ambapo alifunguliwa na kukaribishwa na askari aliyekuwa pale. Alipita na kwenda mpaka kwenye mlango wa klabu ambao ulifunguliwa na mtu mwingine na kukaribishwa ndani. Ndani ya Vatcan Klabu mna nafasi kubwa sana. Wakati unapoingia ndani ya klabu karibu na mlango kuna vyumba vitatu vitatu kila upande. Mbele ya vyumba hivi kuna uwanja wa kuchezea dansi huku ukiwa umezungukwa na sehemu nyingi za kukaa na mbele yake ndipo kuna kaunta ya klabu hii. Hivi Willy alipoingia alikuta watu wameisha jaa alipita akaangalia chumba hadi chumba bila kumuona robert, alipotokea kwenye uwanja wa muziki ambao kwa wakati huo ulikuwa hauna mtu ndipo alipomuona Robert kushooto kwake akiwa amekaa na kijana mwingine. Kwa vile alikuwa hana haja ya kuonana na mtu mwingine ila Robert alikata shauri kwenda kulia kwake ambapo alipata meza iliyokuwa haina kitu na kukaa. Robert alikuwa amemuona alijitafadhalisha kwa kijana aliyekuwa amekaa naye na kuhamia mezani kwa Willy. 

"Habari za saa hizi?" Robert alimpa Willy hali.

"Safi tu, naona umeisha wahi kabisa kabisa," alimtania Willy.

"Ee bwana, chelewa chelewa mbaya," alijibu Robert kimatani vile vile. 

"Robert alimwita mfanyakazi na kumwagiza vinywaji. Yeye alikuwa amehama na kinywaji chake. 

"Utakunywa nini Willy?".

"Anipe Dimple kubwa na tonic soda."

"Umesikia, kalete haraka, mimi niongezee Martel", Robert alimsisitiza mfanyakazi.

"Kabla sijaanza mambo mengi, nimepata habari kutoka Lusaka kwa Chifu, ameniambia nikueleze kuwa Petit Ozu na Mike Kofi watawasili hapa kesho mchana na ndege ya shirika la ndege la Nigeria, ambayo itatua mjini hapa saa nane kamili. Hivi ndizo habari nilizopata."

"Asante sana, nitawashughulikia watakapofika." alijibu Willy huku akipokea kinywaji, "Sasa tuendelee unipe hata kama ni kwa muhtasari tu mambo yalivyo hapa." Robert alisafisha koo kwa kohozi ili apate kueleza vizuri. 

"Mimi nimefika hapa mjini Kinshasa toka mwisho wa mwaka jana. Nilijaribu sana kuchunguza kifo cha Meja Komba lakini bila mafanikio. Nimeweza kuwa na uhusiano na afisa mmoja wa C.N.D ambayo ndiyo idara ya upelelezi ya hapa, ili niweze kupata habari zingine kutokana na upelelezi waliokuwa wameufanya, lakini na wao vile vile hawakuweza kufika popote. Jambo hili liliweza kunifanya nihisi mambo mawili, aidha Komba alikuwa ameuawa kwa mpango ambao Serikali iliujuwa kikamilifu au alikuwa ameuawa na kikundi cha kijasusi ambacho ni chenye ujuzi wa hali ya juu. Hili jambo la kwanza nililitilia wasiwasi maana baada ya kufanya upelelezi sana ilionekana uliokuwa umefanywa na Serikali ya Zaire ulikuwa umefanywa kwa dhati na kiukweli.  Hivi nilibaki na jambo la pili ambalo nimekuwa nalifanyia upelelezi bila kufika popote hadi hapa majuzi ndugu Mongo alipouawa. Suala hili la kuwepo kwa kikundi cha ujasusi kinachoendesha uovu limeweza kuthibitika kwangu kutokana na mauaji haya ya juzi. Tatizo lililopo hapa Kinshasa ndugu Willy ni kwamba, nchi hii ina watu wa nje wengi na inafanya biashara na nchi nyingi sana hata Afrika ya Kusini na Rhodesia. Hivi ni rahisi sana kwa majasusi wa kutoka nchi hizo kuweza kuingia nchini hapa na kufanya uovu kama huo. Kwa mfano katika upelelezi wangu nimekuta kuwa kila mwaka Zaire inapata bidhaa toka Afrika Kusini zenye zaidi ya thamani ya R40m. Vitu hivi hutumwa kupitia Rhodesia na Zambia kwa Reli na kwa bahari mpaka Matadi. Lakini vile vile bidhaa nyingine inaingia Zaire kwa njia ya barabara kwa kupitia Rhodesia na Zambia. Kwa mfano hivi karibuni kumekuwa na mkataba kati ya Zaire na Rhodesia ambapo malori makubwa kiasi cha mia mbili yanaingia Zaire kutoka Rhodesia kila mwezi. Mia moja na ishirini ya malori hayo hubeba makaa ya mawe na yaliyobaki hubeba mahindi. Kutokana na mipango kama hii ni rahisi sana kwa majasusi ya Afrika Kusini na Rhodesia kuingia mjini hapa wakiwa aidha kama madereva wa magari haya au makarani. Vile vile utakuta kuwa kampuni za Afrika Kusini za biashara ziko na wakala wao hapa mjini Kinshasa. Kwa mfano Zaire ina mpango wa kupeleka bidhaa yake Japan kwa kupitia Afrika Kusini, na mkataba wa tani 125,000 za shaba ziendazo huko Japan kwa mwaka ulitiwa saini ya kusafirisha tani hizo kupitia kampuni moja iitwayo Grindrod Cots Stevedoring iliyoko mjini East London, Afrika Kusini. Kampuni hii ina wakala wake mjini hapa. Kutokana na ukweli wa mambo haya ulivyo ni wazi kuwa, ni rahisi sana kuwa na ukanda wa kijasusi wa Afrika Kusini ukifanyakazi yake hapa unapoona ya kuwa watu wanaouawa ni wale wenye uhusiano na wapigania uhuru wa Kusini mwa Afrika. Kutokana na hali hii mimi ningeshauri tuanze upelelezi mkali kwa watu wa makapuni haya yenye asili ya Afrika Kusini", alimalizia Robert.

Willy ambaye alikuwa amesikiliza maneno yote haya kwa makini alimuuliza, "Marehemu Mongo alikuwa amefikia hoteli gani?"

"Intercontinental hoteli", Robert alijibu.

"Uliwahi kukagua vyombo vyake uliposikia ameuawa?".

"Ndiyo, nilifika pale nikiwa pamoja na ofsa huyu wa C.N.D. Kusema kweli tulikuta chumba kile kimepekuliwa sana ingawaje kwa ustadi ambao mtu wa kawaida hawezi kugundua. Hatujui mtu aliyekuwa amekipekua alitaka nini au alichukua nini sababu hatukuona kitu cha maana kilichochukuliwa. Vitu vyake vingi hata zile karatasi za maelezo ya mkutano wa Libreville tulizikuta. C.N.D wamejaribu kupata alama za vidole bila mafanikio. Hii ina maana kuwa walitumia mifuko ya mikono 'gloves', Baadaye siku ile nilifanya upelelezi wangu kwa watu kadhaa na pale Intercontinental ambao walikuwepo tokea Ndugu Mongo anawasili pale kama waliwahi kuona kitu chochote cha kutilia mashaka lakini hawakunipa jambo lolote la maana.

"Alikuwa akilala chumba namba ngapi?", Willy aliuliza. 

"Nambari 501".

"Hili gari marehemu alikuwa amepewa na nani?".

"Lilikuwa la Wizara ya Mambo ya Nchi za nje".

"Alikuwa akiendesha mwenyewe?".

"Wakati alipopatwa na ajali alikuwa mwenyewe".

"Jaribu kupeleleza ni wakati gani alipewa hilo gari. Na kabla ya kupewa hilo gari lilikuwa wapi. Ni mahala gani alipokuwa ameliegesha, na kama kuna mtu maalumu aliyelishughulikia gari hilo kabla marehemu hajapewa. Kwani alikuwa na muda gani Kinshasa tangu kufika kwake hadi kuuawa?".

"Yeye aliwasili hapa saa nne za usiku, kesho yake saa tano ndipo alipopatwa na ajali hii," Willy alifikiri sana kisha akasema. 

"Vizuri Robert, nitaenda kuyafikiria maelezo yote uliyonipa usiku huu na uamzi wangu nitakueleza kesho nini tufanye. Umekuwa ukifanyakazi na maelezo yako ni ya  kufaa sana. Mazishi yatakuwa kesho saa ngapi?".

"Saa nne asubuhi, na atazikwa kitaifa", Robert alijibu. 

"Mimi nitahudhuria mazishi".

"Na mimi nitakuwepo", alijibu Robert.

"Kwa hiyo tuta...", Willy alikatwa kauli na jamaa mmoja aliyefika kwenye meza yao akiwa ameandamana na msichana mmoja.

"Hallo Robert, habari za leo?" 

"Oho Kalenga, habari zenu, karibu bibie", Robert aliwakaribisha hawa watu.

"Asante asante," alijibu Kalenga huku akikaa.

"Willy onana na Bwana na Bibi Kalenga Mbizi. Bwana Kalenga ni Meneja Maslahi katika kampuni ya Fiat, yeye ndiye aliyenifanyia mpango wa kununua gari yangu ya Fiat 132 GLS. Na huyu ni ndugu willy Chitalu kutoka Lusaka, yeye ni mfanyabiashara. Ni wakala wa makampuni ya nchi za nje katika Zambia", Robert aliwafahamisha.

"Vizuri kuonana". 

"Vizuri kuonana", walijibishana.

Pombe ziliagizwa na muziki ulianza kuwa moto moto, hivi kundi hili likageuka kutoka mazungumzo waliyokuwa nayo na kuwa kundi la starehe, maana saa hizi watu wa kila aina wliojuana na Robert walipoingia walienda kukaa kwenye meza hiyo hiyo.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU