KIKOSI CHA KISASI

SURA YA SITA 

WASIWASI 

IV 

Ilikuwa yapata saa mbili kamili Willy alipoingia mtaa wa Kimbondo katika sehemu ya Bandalungwa. Aliendesha pole pole huku akiangalia namba za nyumba kila mara, na kusimama ili kuona vizuri. Mwishowe aliona nyumba nambari 79. Aliposimamisha gari tu mbele ya nyumba hii. Mlango ulifunguliwa na Mwadi akatokeza kuja kumpekea.

"Karibu Willy, nilikuwa na wasiwasi mkubwa kuwa huenda umeponda miadi yetu".

"Lo, hiyo isingewezekana Mwadi, nilikuwa bado nakuja ila tu nilicheleweshwa na watu fulani waliofika tuweze kuzungumza mambo ya biashara. Unajua tena mambo ya biashara!" Willy alieleza huku wanaingia ndani.

"Karibu keti," Mwadi alimkaribisha Willy. Willy aliketi kwenye kochi.

Nyumba ya Mwadi ilikuwa ndogo yenye sebule na chumba kimoja cha kulala, ikiwa pamoja na jiko, bafu na choo. Sebule ilikuwa na vyombo vizuri vya gharama ya juu ambavyo vilifanya chumba kuonekana maridadi kabisa, hasa ukiongezea kwamba hiki chumba ni cha msichana na wewe mwenyewe unajua jinsi wasichana wanaojipenda wanavyofanya.

"Hapa ndipo ninapoishi".

"Mahali pazuri sana Mwadi".

"Asante," alijibu Mwadi, "Utakunywa nini bia au Whiski?"

"Nipe bia", alijibu Willy.

"Skol au Primus?".

"Nipe Primus".

Mwadi alifungua barafu na kutoa bia mbili za Primus, kisha akazifungua na alichukua bilauri na kumimina.

"Karibu", alisema huku akimkabidhi Willy kinywaji. Willy aliinua bilauri yake na Mwadi akainua ya kwake, kisha Willy akasema. "Triniens."

"A la sante ya Willy," alijibu Mwadi wakagonganisha bilauri zao wakaanza kunywa. Muziki taratibu ulitokea kwenye santuri, Willy aliamka akaenda kuchagua sahani za santuri ambazo zilikuwa nyingi sana, hii ilionyesha kuwa Mwadi alikuwa mpenzi wa muziki maana nikitaka kusema ukweli alikuwa na maktaba nzima ya muziki. Sahani zilipangwa kwenye kabati kubwa, na kila fungu la sahani lilikuwa na karatasi ambayo iliandikwa majina ya kila wimbo. Willy alitafuta kati ya rekodi alizozipenda, akapata rekodi moja ya Orchestra Shamashama iitwayo 'SHAMASHAMA' akaiweka kwenye santuri na kuicheza.

Wakati Willy anashughulika na muziki Mwadi alishughulika jikoni kutayarisha chakula. Willy alipokuwa ameweka sahani na santuri za kutosha kwenye santuri alimfuata Mwadi jikoni huku amebeba bia yake. "Nimekuja unionyeshe jinsi ya kupika maboke", Willy alisema.

"Bahati mbaya nimeishapika 'maboke' yameiva, ingekuwa vizuri kama ungewahi kabla sijapika. Hata hivyo kama bado upo tutapika wote siku moja".

"Haya, kati ya siku hizi za karibuni tutakuja tupike maboke wote", walikubaliana.

Mazungumzo matamu kati yao yaliendelea mpaka wakati wa chakula, Willy alikula 'maboke' chukula ambacho alikuta kitamu sana na kilikuwa kimepikwa vizuri sana. Kusema kweli alikula sana.

"Kweli Mwadi mpenzi, kwa muda mrefu sijala chakula kitamu namna hii, chakula hiki sintakisahau maishani. Asante sana," alisema Willy alipomaliza kula.

"Bila ya asante Willy", alijibu Mwadi kwa moyo wa furaha. 

Ilipofika saa tatu na nusu, walikata shauri waende kwenye dansi.

"Unaonaje tukienda kwenye muziki," alishauri Mwadi.

"Hata mimi nilikuwa na mawazo hayo hayo," Alijibu Willy. "Chagua mahala pa kwenda maana wewe ndiye mwenyeji hapa".

"Wewe unapendelea bendi gani?." Aliuliza Mwadi.

"Nimekuachia uchague wewe, bendi unayopenda ndiyo hiyo hiyo itakuwa chaguo langu", Willy alijibu. 

"Mimi napendelea Orchestra Veve ya Verckys."

"Vizuri twende huko huko. Leo wanapiga wapi?"

"Wapo Parafifi Bar", alijubu Mwadi. 

"Haya kajitayarishe twende".

Mwadi aliingia chumbani na kuanza kujitayarisha. Willy alibaki sebuleni akisikiliza muziki huku akiendelea kunywa bia. Mwadi alipomaliza kuvaa alijitokeza sebuleni. Alikuwa amevalia vitenge toka juu mpaka chini katika staili ya Kizaire. Kusema kweli alionekana wakupendeza sana. Willy alithibitisha ya kwamba alikuwa amepata msichana mzuri wa kutosha.

"Ama kweli nina bibi", Willy alisema Mwadi alipojitokeza.

"Mimi ndiye nimepata bwana wa sheria yake basi," alijibu Mwadi kimatani.

Baada ya kutaniana hivi waliamua kuondoka. Kwa sababu Willy alikuwa amepita hotelini kwake jioni ile na kubadili nguo hakukuwa na sababu kwake kubadili tena, maana alionekana nadhifu wa kutosha. Hivi waliondoka moja kwa moja kuelekea Parafifi Bar. 'Parafifi Bar' ni bar mojawapo maarufu sana mjini Kinshasa ambapo vijana wengi hupenda kwenda na kustareheshwa na muziki wa bendi mbali mbali ambazo huwa zinafika hapa kuwaburudisha. Bar yenye iko kwenye kona ya mtaa wa Assossa na mtaa wa Victoire.

Willy na Mwadi walipofika kwenye bar hii ilikuwa kiasi cha saa nne na nusu na tayari magari yalikuwa yamejaa sana kuonyesha kuwa watu wengi walikuwa wamewahi. Walihangaishwa kidogo na mahali pa kuegesha gari maana sehemu yote ya karibu na bar ilikuwa imejaa, kwa bahati mtu alikuwa akitoka, wakapata mahali pa kuegesha. Walifunga gari lao na kuelekea kwenye mlango wa kuingilia ambapo walikata tiketi za kuingilia kwa wote wawili. Willy alilipa Zaire tatu.  

Watu kama walivyokuwa wamehisi, walikuwa wamejaa tayari. Muziki ulikuwa unaendelea na watu kadhaa walikuwa uwanjani wakilisakata rumba. Walitafuta mahala pa kukaa na kwa sababu Mwadi alikuwa anafahamika sana pale walifanyiwa msaada na kupata mahala pa kukaa. 

"Tumepata nafasi nzuri, maana ni karibu na watu wanapochezea. Hii itatupa nafasi ya kuona mitindo ya dansi ya hapa mjini Kinshasa," alieleza Mwadi.

"Na hasa, maana huu ndio mji wenyewe kwa muziki. Tena inafurahisha sana kuwaona hawa wapiga muziki macho kwa macho maana sisi tumezoea kuwasikia mwenye redio na santuri tu," alijibu Willy kisha waliagiza vinywaji.

"Mimi niagizie Whisky ndiyo itaniletea nishai upesi. Maana mimi bila nishai nakuwa mzito katika kucheza dansi," Mwadi alieleza.

"Hamna taabu, hata mimi Whisky ndiyo itanifaa kwa wakati huu," Willy alijibu. Hivi waliagiza whisky na walipoiletewa wakanywa huku wakiendelea na mazungumzo ya hapa na pale. Ilipofika saa sita ndipo muziki ulipopamba moto. Watu walikuwa wengi sana sasa, na wengi wao wakiwa wawili wawili walikuwa uwanjani wakilisakata rumba, kila mmoja akijaribu kuonyesha ujuzi wake. Akiwa Willy waliendelea kuzungumza huku Willy macho yake yakiwa uwanjani ambapo alifurahishwa sana na mitindo ya dansi iliyokuwa ikitokitolewa na wachezaji. Vijana wa Orchestra Veve nao ilipofika wakati huu, wakaanza kupiga zile nyimbo tamu tamu. Ulipoanza kupigwa ule wimbo uitwao 'Natamboli motu' Mwadi alisimama na kumwambia Willy, "Tukacheze wimbo safi sana huu. Unajua maana yake?" alimuuliza Willy huku wakiingia uwanjani.

"Hapana," alijibu Willy.

"Unasema kichwa changu hakifanyi kazi, na mimi Willy kichwa changu, nacho hakifanyi kazi sasa hivi kwa ajili yako," alisema Mwadi huku wanaanza kucheza. Willy alizubaa tu kwa maneno ya huyu msichana ambaye alionekana alikuwa amejawa na mapenzi makali juu yake, hivi hakujibu neno. 

Mwadi naye kama wasichana wengi Kinshasa alikuwa anajua namna ya kulisakata rumba sawasawa, kiasi kwamba wakati mwingine Willy alikuwa akijisahau na kusimama huku akifurahia jinsi Mwadi alivyokuwa akikatika maungo hasa kiuno. Wasichana wote waliokuwa uwanjani utafikiri walikuwa wakishindana, maana kila mmoja alicheza na kujinyonga kwa mtindo wake.

Baada ya wimbo huo vijana wa Veve walipiga wimbo mwingine uitwao 'Zonga Andowe' yaani kwa kiswahili 'Rudi Andowe'. Bila kwenda kupumzika Mwadi na Willy waliendelea na kucheza nyimbo hizi tamu. Hivi ndivyo walivyostarehe usiku huu ambao wote wawili walijuana katika ulimwengu wao wa kipekee.

Wakati walipokuwa wamerudi mezani pao wanaburudika na vinywaji hali ya kimapenzi ilikuwa imepamda sana rohoni mwao , "Mwadi sikujua ungeweza kuwa msichana wa kusisimua hivi. Sasa hivi najiona kama niko juu ya dunia", alidiriki kusema Willy.

"Mimi je? Mimi ndiye siwezi hata kueleza, maana naona hata haya kukueleza jinsi moyo wangu ulivyokufa juu yako, ee Willy wangu mtoto wa Kizambia", alisema Mwadi kwa sauti ambayo ungefikiri anataka kulia. Wakiendelea na mazungumzo yao ya kimapenzi mara Willy aliona watu wanaangalia sehemu uliko mlango wa kuingilia. Maana 'Parafifi Bar' ina mlango mmoja tu na huku ikiwa imezungukwa na sehemu zote na nyumba na nyumba ya ghorofa. Willy alipogeuza kichwa chake kuona watu wanaangalia nini, moyo wake uliruka mapigo. Maana aliona msichana mzuri ajabu akielekea sehemu waliyokuwa wamekaa na huku macho yote ya wanaume kwa wanawake waliokuwepa hapo, yakimwangalia na kuthibitisha kuwa kweli huyu alikuwa ni mrembo hasa.

Msichana huyu alikuwa mrefu wa kutosha, na rangi yake, rangi ya shaba. Alikuwa na nywele nyingi nyeusi sana na nzito na jinsi alivyokuwa amezichana zilitoa sura ya ki- Afro. Uso wake ulikuwa na umbo la moyo. Alikuwa na macho makubwa yaliyozungukwa na nyusi nyeusi nzito na kope nzito. Pua yake ilikuwa ndogo na ya kuchongoka kiasi cha kupendeza. Midomo yake ilikuwa ile ambayo kila mtu alitamani kuibusu, maana ilijaa ujana. Mashavu yake yalijaa kiasi cha kufanya sura ya uso mzima wa msichana huyu kuonekana ya kupendeza sana. Kifua chake kilijaa matiti ambayo yalikuwa yamejaa kabisa kiasi cha kwamba hata ungeyaminya ungesikia ugumu wake. Na bila shaka yalikuwa na joto la kutosha. Tumbo lake lilinyooka jembemba utafikiri hali chakula. Miguu yake ilikuwa mirefu kiasi kinachohitajina na ilikuwa imeshiba kiasi kwamba ukiangalia hutapenda kutoa macho yale kwa jinsi ilivyoumbika vizuri, nyuma alikuwa amejengeka kwa namna ya peke yake, kiasi kwamba siwezi kukuelezea mpaka umuone wewe mwenyewe mrembo huyu. Kwani matako yake pamoja na sehemu za mgongo kuteremka chini, alikuwa ameumbwa kwa mahesabu ya peke yake. Alikuwa na shingo la urefu uliotakiwa kupendeza umbo lake zima. Alikuwa amevaa 'maxy ya kijani kibichi ambayo ilizidisha rangi yake ya shaba kung'aa. Msichana huyu ndiye alikuwa na haki ya kiitwa kisura.

Willy aliendelea kumwangalia msichana huyu akisogea. Alikuwa akitembea taratibu kwa hatua zilizokuwa zinatupwa kwa mahesabu. Msichana huyu aliangalia huku na kule lakini kwa chati sana kiasi kwamba mpaka uwe mtu mjuzi kama Willy ndipo ungeweza kutambua. Hii ilimtambulisha Willy kuwa msichana huyu alikuwa akijua kuwa yeye ni mrembo sana hivi kila jambo alilolifanya alilifanya kwa sheria yake. Miondoko yake ilikuwa vile vile ya peke yake, ili kukamilisha urembo wa msichana huyu ambaye nimeshindwa maneno ya kuelezea urembo wake, afadhali siku moja ukipata nafasi fika Kinshasa umtafute mrembo huyu ili ujue uzuri ni nini. Alipozidi kusogea mahali walipo Willy alihisi kuwa huenda alikuwa anamtafuta mtu. Mwadi alimgusa Willy kwenye mkono na kumshitua kutoa mawazo huko yalikokuwa.

"Msichana mzuri sana au siyo Willy?" Aliongea Mwadi huku akumwangalia Willy machoni. Willy hakutambua kwa nini Mwadi aliuliza swali hili, lakini ili aweze kueleza ukweli wake alijibu. 

"Ndiyo ni msichana mzuri sana". 

"Ni rafiki yangu." Mwadi alijibu kwa mkato. Willy alishangaa kusikia msichana huyu tena ni rafiki wa MWadi. "Kweli maajabu hayataisha ulimwenguni," alijisemea rohoni. Kabla mshangao wake haujaisha msichana huyu akawa amefika kwenye meza yao. Alikuwa akitabasamu, tabasamu lililofanya nywele za Willy kusimama na jasho kumtoka mwili mzima. 

"Eee Mwadi, mbote," yule msichana alisamu katika Kilingala.

"Mbote," alijibu Mwadi huku naye akitabasamu.

"Sango nini?" 

"Malamu," alijibu Mwadi kisha akamkaribisha, "Approchez".

"Merci," alijibu yule msichana. Kisha yule msichana akamgeukia Willy macho yao yakaonana. Macho ya huyu msichana yalikuwa malegevu lakini yenye nguvu fulani ambazo zilimwingia hata Willy.

"Mbote", Willy alisalimiwa.

Willy alitabasamu, na baada ya kusita kidogo alijibu "Mbote," Mara moja yule msichana alihisi kuwa huyu kijana aliyekuwa na Mwadi si mwenyeji wa Kinshasa na wala Zaire. Moyoni mwake msichana huyu alivutiwa sana na kijana huyu aliyekuwa na Mwadi akakata shauri kuvuta kiti, akakaa.

"Nafikiri inabidi niwafahamishe," Mwadi alisema.

"Litakuwa jambo la maana", alijibu Willy. 

Mwadi alimwangalia yule msichana akamwambia, "Huyu ni Willy Chitalu ni raia wa Zambia. Yeye ni mfanyabiashara na yuko hapa katika mapumziko ya kikazi kwa muda mfupi." Kisha alimgeukia Willy na kumfahamisha, "Huyu msichana ni rafiki yangu anaitwa Tete. Yeye anafanya kazi na kampuni iitwayo Agence Sozidome." Baada ya kufahamishwa walishikana mikono na kusalimiana. "Habari za siku nyingi," Mikono ya msichana huyu ilikuwa laini sana, kiasi cha kuufanya mwili mzima wa Willy usisimke.

"Mimi nilipomuona tu huyu rafiki yako nilijua si kinois," Tete alimweleza Mwadi.

"Unajua kinois ni nani?" Mwadi alimuuliza Willy huku akicheka.

"Kinois ni mtu yeyote ambaye maskani yake ni hapa hapa mjini Kinshasa bila kujali anatoka wapi", Mwadi alieleza.

"Kwa hiyo hata mimi nikihamia hapa nitaitwa kinois."

"Bila wasiwasi", alijibu Mwadi.

Willy alimwagizia Tete kinywaji, huku wakiendelea na mazungumzo ambayo yalinoga zaidi kwa kuongezeka kwa Tete.

"Kampuni unayofanya kazi inashughulika na mambo ya wakala au siyo?" Aliuliza Willy maana neno Agence ina maana wakala.

"Ndiyo kampuni yetu ni wakala ya makampuni mengi sana ya nje ambayo yanapenda kufanya biashara na Zaire," alijibu Tete.

"Ahaa, kumbe tuko kwenye kazi sawa maana hata mimi kampuni yangu inashughulika na shughuli za Wakala, inaitwa 'Zambia Overseas Agency'. Hata safari yangu hii kama Mwadi alivyokueleza ni ya mapumziko na kikazi. Huenda itakuwa vizuri nikifika ofisini kwenu ambako naweza kuonana na wakubwa wako wa kazi ambao wanaweza kunieleza vizuri juu ya makampuni ambayo naweza kufanya nayo biashara", Tete alifurahi sana kuona kuwa ameweza kukutana na mfanya biashara ambaye angeweza kuletea kampuni yake biashara. Maana ofisini kwao walikuwa wameelezwa kuwa kila walipo wao ni wawakilishi wa makampuni yao.

"Itakuwa vizuri. Kampuni yetu ni kampuni kubwa na inajulikana sana. Hata imeweza kuwa Wakala wa makampuni ya Afrika Kusini katika Zaire. Kwa mfano miezi miwili iliyopita tuliweka saini mkataba kwa niaba ya Serikali ya Zaire, mkataba ambao ulikuwa kati ya Serikali na kampuni moja ya Afrika Kusini iitwayo Grindrod Cots Stevedoring ya mjini East London wa kusafirisha tani 125,000 za shaba ziendazo Japan kwa kupitia kwao. Hii itakuonyesha jinsi kampuni yetu ilivyo maarufu. Mimi naamini kuweza kuwa na uelewano mzuri zaidi kati yetu na makampuni ya Zambia kuliko nchi nyingine yoyote", Tete alisisitiza.

Kwa kusikia maneno haya moyo wa Willy ulipiga haraka haraka maana maelezo haya yalikubaliana sana na maelezo aliyopewa na Robert juu ya uhusiano wa Zaire na Afrika Kusini kibiashara. Vile vile alikumbuka wasiwasi wa Robert kuwa makampuni yanayoshughulikia maslahi ya wafanyabiashara wa Afrika Kusini, yanaweza kutumiwa kijasusi na nchi hiyo ambayo iko mstari wa mbele katika kupinga maendeleo ya nchi huru za Kiafrika na zile ambazo bado zinapigania uhuru. Bila kuonyesha dukuduku lake Willy alisema, "Ni jambo la bahati sana kuonana mimi na wewe, na inabidi nimshukuru Mwadi kunifahamisha kwako. Hii kampuni yenu ni ya Kizaire au ni ya watu kutoka nje?" Aliuliza Willy.

"Hii kampuni inaongozwa na Wabelgiji. Lakini wamekuwa hapa kwa muda mrefu sana, na wameweza kufanya biashara na nchi karibu zote za Afrika.

"Vizuri basi, nitafika ofisini kwenu kesho. Ofisini zenu ziko wapi?"

Tete alifungua kimfuko chake kidogo akatoa kadi ya biashara akampa Willy, "Hiyo itakupa maelezo yote." Tete alisema. Willy aliangalia kadi hiyo akajibu, "Asante sana."

"Mimi nitaondoka Mwadi, maana nilikuwa napita tu. Muteba alikuwa amenipigia simu tuonane 'Vis-a-vis bar ambako O.K Jazz wanapiga leo, lakini nimemsubiri sana hakuja. Nilitoka nikaenda nyumbani kwake hayuko vile vile nilifikiri yuko hapa lakini pia hayupo. Nikimuona atanikoma." Tete alimweleza Mwadi.

"Lazima atakuwa amepata matatizo. Ninavyomjua Muteba alivyokufa juu yako, hawezi kuwa hakufika hivi hivi tu," Mwadi alijibu huku akitabasamu.

"Wacha maneno yako," alijibu Tete huku akisimama. Willy na Mwadi nao walisimama na kumuaga mrembo huyu. 

"Haya tutaonana kesho," Willy alisema.

"Vizuri, mimi nitakuwepo. Maana ukifika tu mapokezi utanikuta mimi pale," alijibu Tete.

Aliondoka taratibu, huku mamia ya watu waliokuwepo hapa wakifurahia miondoko ya mrembo huyu wa aina ya peke yake. Willy alijiona mtu mwenye bahati sana kufahamiana na mrembo huyu kwani hata watu walibaki wakiwaangalia Tete alipokuwa ameondoka.

Willy na Mwadi waliendelea kunywa na kucheza kwa muda mfupi, na kwa vile Mwadi alianza kulewa aliomba waondoke. Walipotaka kuondoka vijana wa Veve wakiongozwa na mwanamuziki mashuhuri Verckys walipiga wimbo mmoja uitwao 'Toweli Nini' yaani 'Mnagombea nini.' "Muziki mtamu sana huo, tukacheze ndiyo uwe wa mwisho", alishauri Mwadi.

Baada ya wimbo huu waliondoka na kelekea Bandalugwa nyumbani kwa Mwadi, na ilikuwa saa tisa walipofika nyumbani. Wakiwa wana nishai ya kutosha, waliingia ndani na tayari kwa kupumzika.

"Willy mimi ninakupenda sana," alisema Mwadi huku akijitoa kabisa kwa Willy.

"Na mimi vile vile," alisema Willy akimvuta na kuanza kumbusu, busu motomoto. Hali hii ya kimapenzi iliwajaa, wakaanza kufanya mapenzi ambayo yaliwafanya wote kutosheka kabisa. Wakiwa wanapumzika, Mwadi akiwa anambabata Willy kifuani alisema. "Willy mimi mapenzi yangu kwako yalianza toka siku ile uliyoingia tu pale hotelini. Nilipokuona tu mwili wangu wote ulisiimkwa sana nikajua nimepata mwanaume ambaye mwili wangu umempenda, na niliamini kuwa wewe tu ungeweza kunitosheleza kimapenzi.

"Kweli," alijibu Willy huku akisikia usingizi.

"Kweli kabisa, hata kuna mtu mmoja huwa ananilipa mimi kwa kumpatia majina ya wageni wanaoingia hapo hotelini, hata jana aliniomba majina ya watu walioingia hapo hotelini kwetu, lakini bila sababu moyo wangu haukupenda nimpe jina lako, sijui kwa nini nilifanya hivi, huenda ni kwa sababu nilikuwa nimekupenda sana kuanzia wakati huo". Kusikia maneno haya Willy aliyekuwa anasinziasinzia, mara moja usingizi wote ulimtoka na akili yake ikawa katika hali ya tahadhari. 

"Mtu gani huyo", aliuliza Willy kana kwamba hana haja ya kujua.

"Mtu mmoja anaitwa Kabeya,"

Kwa kutaja jina hili Willy alistuka.

"Majina hayo huwa anayahitaji kwa nini?" Willy aliuliza.

"Sijui mimi huwa anayahitaji kwa ajili gani. Huwa nikisha mpa ananilipa basi yanakwisha. Sasa jana aliniambia nimpe majina ya watu walioingia jana na niendelee kumpa majina hayo mpaka atakaponiambia yeye mwenyewe, akasema atanilipa mara tatu ya kawaida.

"Huyu mtu anafanya kazi wapi?"

"Aliwahi kuniambia siku moja kuwa anafanya kazi gereji moja iitwayo G.A.D. iliyoko barabara ya T.S.F. sehemu za Gombe."

"Na unasema jina langu hukumpa?".

"Ndiyo, kwani nilifanya vibaya?".

"Hapana, ulifanya vizuri sana", Willy alifikiria habari hizi alizokuwa amezipata, akaonaa mtu mwenye bahati sana, na kufikiria kuwa Mungu ndiye alikuwa amepanga yeye apendane na msichana huyu ili aweze kupata habari hizi alizozipata. Kwani huyu Kabeya ndiye kile kikaratasi alichokikuta mfukoni mwa yule mtu aliyejiua kilikuwa kikimtaja. Hivyo alijua sasa amepata mahali pa kuanzia kesho yake. Alipanga kesho yake aende kwenye gereji hii ya G.A.D. ajue nini kiko pale.

Mawazo haya yakiwa yanapita kichwani mwake alimvuta Mwadi na kumkumbatia.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru