KIKOSI CHA KISASI

SURA YA SITA 

WASIWASI

II

Wakati Ozu na Kofi wanaelekea nyumbani kwa Robert, katika ofisi za gereji G.A.D. kulikuwa na kikao cha dharura cha 'WP', viongozi wote wanne wa 'WP' walikuwepo katika kikao hiki. Pierre alikaa huku anavuta mtemba wake katika hali ya majonzi kabisa. Wenzake walikaa kimya wakisubiri atasema nini. Maana alikuwa amepata habari za kifo cha Mulumba lakini mpaka dakika hii walikuwa hawajapata habari zozote za Kasongo. Jinsi mambo yote yalivyotokea, walikuwa wamehisi na hiki ndicho kitu kilikuwa kinawapa wasiwasi mkubwa sana. 

"Jamani hapa ndio tumefikia muda wenyewe. Huu ndiyo utakuwa muda wetu mgumu tangu ianzishwe 'WP', maana kwa mara ya kwanza 'WP' imeingiliwa kiasi cha vijana wao mmoja kuuawa na mwingine kutekwa nyara. Jambo hili naamini wote tulilitegemea na ndiyo sababu tumeunda kundi kubwa lenye nguvu la kuweza kuvunja nguvu zozote za upinzani. Hivi tupo hapa sasa hivi kulishughulikia suala hili kikamilifu. Toeni wasiwasi," alisema Pierre katika hali ya kuwatia wenzake moyo, maana alijua mambo yameharibika.

"Sisi, Patron hatuna wasiwasi, tuko tayari kabisa kupambana na hawa watu kikamilifu," alijibu Jean huku wengine wakitingisha vichwa kuonyesha kuwa wanamuunga mkono. 

"Nafikiri sasa tuanze mipango ya kushughulika na jambo hili. Kitu cha kwanza ninachotaka kujua, Mulumba na Kasongo walikuwa watu wenye ujuzi kiasi gani?" aliuliza Pierre. 

"Mulumba na Kasongo ni kati ya vijana wetu ambao walikuwa na ujuzi wa juu katika kumfuata mtu na wasiweze kutambuliwa. Ndiyo walikuwa wamefanya kazi hii kwenye matukio yote tuliyofanya sehemu mbali mbali katika Afrika na wakawa wameimudu vizuri sana. Kwa mfano, waliweza kumfuata Nelson Chikwanda yule tuliyemuua Lagos Nigeria kwa muda wa wiki moja bila kugunduliwa na wakaweza kutueleza nyendo zake zote kiasi ya kuwa ilikuwa rahisi kwa Masamba kumpiga risasi na wote wakaondoka bila kugunduliwa. Vile vile kwa upande wa kutumia silaha walikuwa na ujuzi wa hali ya juu sana. Wote wawili waliweza kutumia silaha kila aina, ukiongezea kuwa Mulumba alikuwa na ujuzi wa hali ya juu katika karate. Kwa ujumla Patroni, vijana hawa walijua kazi yao vizuri sana na ndiyo sababu waliwekwa mahali pa maana kama uwanja wa ndege," alieleza Jean.

"Hii ina maana kuwa watu hawa wawili walioingia si wa kuchezea", alizingatia Muteba.

"Ndiyo si wa kuchezea. Kutokana na habari kamili nilizozipata toka 'Boss' kwa kupitia wakala jioni hii kabla sijapata habari za mambo haya yaliyotokea, ni kwamba huyu mmoja aitwaye Petit Osei ni mpelelezi maarufu sana. CIA imekuwa inamwangalia kwa muda mrefu sana na inamtambua vizuri sana, na ndiyo sababu walipomnasa kwenye kanda zao za kipelelezi akija hapa baada ya tukio hili kubwa sana kutokea ilibidi kupasha mashirika mbali mbali wanayoshirikiana nayo, habari za safari ya mtu huyu. huyu wa pili hajulikani kabisa, ila alionekana akitembea na Osei mjini Lagos na CIA ikajuwa lazima walikuwa na safari moja. Na kweli wamesafiri pamoja na wote wana pass za Nigeria ambazo bila shaka ni za bandia. Vile vile wanatumia majina ya bandia, Osei anajiita Petit Ozu na mwenzie Mike Kofi. Kusema kweli CIA na Boss imeshaturahisishia kazi lililopo ni kuwasaka tujuwe wamefikia hoteli gani na kisha tuwafyagilie mbali, ndipo watambue 'WP' maana yake nini," alieleza Pierre kwa sauti ya uchungu. 

"Kama ni watu wa ujuzi kiasi cha kwamba CIA inawatambua na wako kwenye orodha yao basi ni wajuzi kweli. Kwa hiyo mambo waliyowafanyia Mulumba na Kasongo ni kipimo chao. Hii ina maana kuwa lazima tokea sasa jambo hili liwe chini ya uangalizi wetu moja kwa moja maana sasa tunashughulika na watu wenye ujuzi kama sisi," alishauri Papa. 

"Maelezo yako sawa kabisa, inatulazimu kufanya hivyo. Bila shaka itakuwa rahisi kwetu kuwapata upesi na kuwafutulia mbali maana sisi tunao watu na vifaa vya kutosha. Hii ni faida tunavyowazidi wao," Pierre alisema.

"Kasongo watakuwa wamempeleka wapi?" Aliuliza Muteba.

"Hili ndilo jambo ambalo linanikera. Kitu ninachoogopa wasije wakamlazimisha Kasongo akalopoka maneno ambayo yanaweza kuwafanya wakavumbua siri yetu hii ambayo tumeweza kuificha kiasi cha kwamba Serikali ya hapa haijatugundua. Hivi inatubidi usiku huu tutumie kila tulichonacho kutambua Kasongo yuko wapi," Pierre alinena. "Kuropoka Kasongo hawezi kuropoka, maana wamepewa amri ya kawaida ya 'WP' kuwa, mtu akishikwa na ukahisi kuwa unateswa kiasi ambacho huwezi kuvumilia unameza kidonge cha sumu na kujiua. Kama sisi wote tunavyojua, kama Kasongo amelazimishwa kusema lazima ameishajiua, maana afadhali ajiue kuliko kurudi 'WP' huku akiwa ametoa maelezo juu ya 'WP'. Anajuwa vizuri kuliko kufanya hivyo, maana haya maelezo niliwapa tangu nilipowachukua chini yangu. Kwa hiyo mimi nina imani asilimia mia moja kuwa Kasongo ameisha kufa hivyo hakuna haja ya kupoteza muda kumtafuta. Jambo la maana sasa la kufanya ni kuwatafuta hawa watu wawili tuweze kujua wapi walipo ili tukawafutilie mbali kabla hawajaleta madhara," alijigamba Jean.

"Kama una uhakika huo vizuri. Sasa lililopo ni kutaka kujwa hawa watu wamefikia hoteli gani," Pierre alisema.

"Hilo lisikupe taabu, Kabeya anazo njia za kuweza kutupatia hoteli pamoja na vyumba wanavyolala. Hebu nikawaone ofisi ya pili maana nilimwambia yeye na Charles wasitoke ofisini mpaka hapo nitakapowaeleza," alijibu Jean huku akiondoka kwenda kuwaona Kabeya na Charles. Wakati Jean ametoka mazungumzo kati ya hawa wengine yaliendelea. 

"Jean atakapokuwa ametupatia hoteli walizomo, Muteba na kundi lako mtamshughulikia Kofi, wakati wewe Papa utamshughulikia Ozu. Nataka kufikia kesho saa kama hizi tuwe na mpango kamili wa kuwaua hawa watu au wawe wameishauawa tayari," alitoa amri Pierre. 

"Hamna taabu Patroni, kazi rahisi sana, tukishaweza kuwaweka machoni kazi yao imekwisha," Papa aliwahakikishia.

Jean alirudi akiwa na uso wa furaha furaha, na kuwaeleza, "Vijana wangu wanafanya kazi nzuri sana. Kila mtu ambaye ni mgeni anayeingia hapa mjini na kuchukua chumba ndani ya hoteli yoyote kubwa na zile za hali ya katikati, majina yao yanapelekwa moja kwa moja kwa Kabeya. Kwa hiyo wageni wote walioingia Kinshasa anayo, Hata majina ya Kofi na Ozu ameisha yapokea lakini alikuwa bado hajaweza kujuwa ni kwa ajili gani wameingia hapa mjini. Kwa kifupi Petit Ozu yuko Hoteli Regina chumba nambari 108 na Mike Kofi yuko Hoteli Intercontinental chumba nambari 401," 

"Lo, kazi nzuri Jean, kazi nzuri kabisa, namna hii bila shaka kazi yetu itakwenda sawa. Sasa kazi imebaki kwenu yaani kwako Papa na Muteba, Jean atawasaidia katika kuwapa habari na katika kuwawinda hawa watu wawili. Tusipumzike mpaka tutakapokuwa tumeweza kunasa nyendo zao na kuwa tayari wakati wowote kuwashambulia," alisisitiza Piere.

"Usiwe na wasiwasi Patron, sisi sasa tunakwenda kushughulikia jambo hili kikamilifu. Vijana wote wako katika tahadhali, na usiku huu huu tutakujulisha mambo yalivyo," alieleza Muteba huku wote wakisimama tayari kuondoka kwenda kuanza kazi hii muhimu.

"Sawa, mimi nitakuwa nyumbani nikisubiri kutoka kwenu wakati wote," Pierre alisema huku anaingia ndani ya gari lake na wenzake nao wakiwa tayari kwenda kwenye uwanja wa mapambano.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru