MAKONDA AWATAJA WAUZA DAWA ZA KULEVYA


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (pichani) amewataja baadhi ya Wasanii, Maofisa na Askari wa Jeshi la Polisi Nchini wanaotuhumiwa kushirikiana na watu wanaohusika kufanya biashara hatari ya kuuza na kusambaza dawa za kulevya Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Makonda amesema Serikali ya Awamu ya tano haitawavumilia kabisa watu wanaohusika na biashara ya dawa za kulevya na wanaochukua pesa za wafanyabiashara hao kwa ajili ya kuwalinda. Ametoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuwakamata maofisa wa Jeshi hilo waliotajwa kushirikiana na wauza dawa za kulevya wawekwe mahabusu mpaka pale uchunguzi utakapokamilika.

"Nimepata taarifa baadhi ya Maofiusa na askari wa Jeshi la Polisi wanajihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya, wengine wamekuwa na utaratibu wa kuchukua pesa kila Jumamosi kwa wauzaji wa madawa ya kulevya na ndio maana biashara hii imeendelea kuwepo kwa sababu askari waliopewa dhamana ya kulinda nchi wanahusika kuwalinda wahusika hawa",. Makonda amewaambia waandishi wa habari leo.

Wakati huo huo Makonda amewataka wote waliotajwa kuhusika katika kashifa hiyo ya madawa ya kulevya kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam kesho kwa ajili ya mahojiano. Baadhi ya waliotajwa ni pamoja na Msanii wa runinga, Wema Sepetu, Mwanamuziki wa kizazi kipya 'TID', Dogo Hamidu, Chiody Benz, Babu wa Kitaa, Rachel na Mr. Blue.

Polisi waliotajwa na Mkuu wa Mkoa kuhusika katika kashfa hiyo ni pamoja na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni (RPC) Christopher Fuime, Swai (Oysterbay), Neri (Oysterbay), Willy (Oysterbay),, Inspekta Wayi (Kataki), JB (Chang'ombe), Dotto (Kijitonyama), Makomed (Oysterbay), WP Groly (Kawe), Sajenti Steven (RCO Kinondoni), Noel, Inspekta Fadhil (RCO Kinondoni), Sajenti Stere (RCO Kinondoni) na James (RCO Kinondoni).

Makonda amesema amefikia uamzi huo akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam. Amesema hawezi kuendelea kuona Mkoa wake unakuwa kitovu cha biashara haramu ya dawa za kulevya zinazoathiri vijana wa taifa la kesho.

"Nimejitolea kwa lolote liwalo, niko tayari kufa nikitetea jambo hili, mimi kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nitakuwa mnafiki kama sintawataja watu hawa, naagiza wafike Polisi Kituo 
cha Kati kesho wawekwe mahabusu kupisha uchunguzi. Walioko nje wa Dar es Salaam warudi haraka iwezekanavyo", amesema Makonda.

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru