KIKOSI CHA KISASI

SURA YA NANE 

MAUAJI YA KISHENZI 

III

Ofisi za 'Agence Sozidime' zilikuwa ziko sehemu ya Gombe mtaa wa Avioteuurs karibu na jumba la sinema liitwalo Cine Rac. Habari zote hizi zilikuwa kwenye kadi ambayo Tete alikuwa amempa Willy, hivyo haikuwa vigumu kwa Willy kuipata ofisi hii. Wailly aliipata ofisi hii karibu na 'Cine Rac' kama ilivyokuwa imeelezwa kwenye kadi. Ofisi yenyewe ilikuwa ndani ya nyumba moja ndogo ambayo ungefikiri ni nyumba ya mtu binafsi ya kuishi. Ilikuwa imezungukwa na michongoma mirefu ambayo ilikuwa inaimeza nyumba, na mbele kulikuwa na lango kubwa. Mbele ya lango ndipo kulikuwa na ubao mkubwa uliokuwa umeandikwa kwa maandishi makubwa sana, 'AGENCE SOZIDIME'. Willy aliingia kwenye lango hili na kusimama. Mlinzi aliyekuwa pale mlangoni alimwonyesha ishara ya kupita moja kwa moja. Ndani alikuta nafasi kubwa ya maegesho akaegesha gari lake. Kulikuwa na magari mengine yapatayo karibu ishirini ambayo yalimfanya Willy kutambua kuwa kampuni hii ilikuwa na maofisa wengi. Vile vile alipoangalia mazingira ya nyumba na ofisi hii alihisi kuwa zamani lazima ilikuwa nyumba ya mtu binafsi. Alisukuma mlango wa mbele wa nyumba hii ambao ulikuwa umeandikwa kwa karatasi iliyoandikwa SUKUMA.

Kuingia alijikuta yuko kwenye sebule kubwa iliyotandikwa zulia moja safi sana toka ukuta hadi ukuta. Chumba hiki kilizungukwa na makochi mazuri sana yakiandamana na meza ndogo ndogo. Hewa ya humu ndani ilikuwa baridi sana kitu kilichoonyesha kwamba mashine ya kuleta baridi 'air condition ilikuwa inatumika. Nyumba nzima ilikuwa kimya isipokuwa mashine ya kupiga chapa iliyokuwa ikisikika tokea vyumba vya ndani. Willy alijikuta anaangaliana moja kwa moja na Tete ambaye uzuri wake uliongezea uzuri wa chumba kizima. "Karibu Willy," Tete alimkaribisha Willy wakati alipomuona. Mwili mzima wa Willy ulisisimkwa kwa kusikia sauti nyororo ya msichana huyu, pamoja na macho ya msichana huyu yaliyokuwa yakimtazama kama kwamba yanamwambia 'usijaribu kunisahau'. Willy alisogea akataka kujibu, lakini sauti ikakwama, akatoa kohozi, na kwa sauti ya kubabaika alijibu, "Asante". Kusema kweli msichana huyu alikuwa mzuri nadiriki kurudia kukueleza tena, mimi nina imani kama wewe ndiye ungekuwa mahali pa Willy ungepatwa na kizunguzungu na ungeweza kuanguka chini, maana nasikia kuna watu wamewahi kupatwa na mkasa huo. Lakini kwa vile ni Willy alikaza roho na kumsogelea msichana huyu. "Habari za toka jana," Tete alimsalimu.

"Nzuri ulifika salama?"

"Nilifika ingawaje gari langu lilinifanyia uhuni kidogo." Alijibu Tete huku akiendelea kumwangalia Willy kwa macho malegevu. Moyo wa Willy ulipiga haraka haraka akajibu, "Pole sana."

Tete naye moyo wake ulikuwa unapiga haraka haraka, maana naye kwa sababu asizozijua alijukuta anaguswa vibaya sana moyoni kwake na kijana huyu ambaye asubuhi hii alikuwa akipendeza zaidi kuliko alivyokuwa amemuona usiku uliopita.

"Karibu kaa kwenye kiti, nimeisha kufanyia miadi na Meneja wa Biashara ambaye yuko tayari kuonana na wewe. Nilifanya miadi na Mkurugenzi lakini ana shughuli nyingi sana wiki hii hatakuwa na nafasi. Subiri nimuulize Meneja wa Biashara kama yuko tayari sasa hivi," alieleza Tete. Willy alikaa kwenye kochi. Kwenye meza iliyokuwa mbele yake kulikuwa na magazeti mengi. Aliyaangalia akaona gazeti la 'Salongo' la siku ile akaanza kuliangalia huku akingojea Tete arudi. Alichunguza gazeti hili na kwenye pembe moja ndani ya gazeti alikuta kitu ambacho alikuwa akikihitaji kukiangalia. Kulikuwa kumeandikwa kwa kifupi sana habari za ajali waliyoifanya na wale watu waliokuwa wanamfuata Ozu. Gazeti lilisema tu kwamba mtu mmoja alikutwa barabara ya Poids Lourds amepigwa risasi na gari aliyokuwa akiendesha ikiwa imepata ajali. Liliendelea kusema polisi walikuwa bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hili.

"Yuko tayari kukuona," Tete alimweleza.

"Asante," Willy aliweka gazeti chini akaanza kumfuata Tete ambaye alifungua mlango wakaingia ndani, wakamkuta msichana wa kizungu ndiye alikuwa mwandishi mahsusi wa Meneja wa Biashara.

"Oh asante sana, karibu Willy," msichana huyo wa kizungu ambaye naye alikuwa mzuri sana alimkaribisha Willy.

"Asante," alijibu Willy huku wakisalimiana.

"Wille. Lucie atakushughulikia, tutaonana ukitoka," Tete alimwambia na kumminyia jicho, kitu kilichomshinda Willy na kubabaika hata hakuweza kujibu. Baada ya Tete kuondoka Lucie alimsindikiza Willy ofisini kwa meneja wake.

"Bwana Max tafadhali onana na bwana Willy," Lucie aliwafahamisha.

"Oh bwana Willy karibu, nimepata habari zako toka asubuhi," alijibu Max

"Asante sana, nami nimefurahi kufika ili tuweze kuzungumza," walielezana huku wakishikana mikono. Lucie alitoka akawaacha waendelee na mazungumzo yao. Willy alivuta kiti akaa huku akimwangalia meneja huyu wa kizungu tayari kuanza mazungumzo naye.

"Nimepata habari kuwa unawakilisha kampuni moja ya wakala ya nchini Zambia," Max alisema.

"Ndiyo mimi ni mwakilishi wa kampuni iitwayo 'Zambia Overseas Agency' na natumaini umewahi kuisikia," Willy alifungua mkoba wake, akatoa kadi yake ya kibiashara kati ya kadi alizokuwa ametayarishiwa na Chifu kabla ya kuondoka mjini Lusaka. Max aliiangalia kisha naye akatoa akampa Willy.

"Ni jambo zuri kwa kufika kwako hapa kutuona kwa mazungumzo ya kibiashara, Kusema kweli kampuni yetu ni kubwa na ina uhusiano wa kibiashara na nchi nyingi sana. Ilikuwa bahati mbaya tu kuwa bado tulikuwa hatuna uhusiano wa kibishara na makampuni ya Zambia. Hivi tunakukaribisha sana," mazungumzo haya alizungumza max.

"Asante sana, kusema kweli bwana Max kampuni yetu ndiyo wakala wa makampuni mengi nchini Zambia. Kwa sasa hivi Shirika la Mazao la Zambia ambalo ni kati ya makampuni tunayowakilisha linahitaji kuuza mahindi nchi za nje, hivi limetupa jukumu la kutafuta wanunuzi. kutojkana na habari za kibiashara Zaire inahitaji sana mahindi, Kwa hivi nimefika hapa kuwaona baada ya kupata habari kuwa kampuni yenu ndiyo inawakilisha makampuni mengi ya humu nchini na makampuni ya njeyanataka kufanya biashara nchini huku. Natumaini mtanitatulia shida yangu," alisema Willy.  

"Ahaa, nimekuelewa kwa ufasaha sana. Kusema kweli Zaire inahitaji sana mahindi, na kwa sasa hivi inaagiza mahindi kutoka Rhodesia. Tukiangalia na upande mwingine Zaire ikiwa ni nchi ya Kiafrika na mwanachama wa OAU na Umoja wa Mataifa si vizuri kisiasa kufanya biashara na serikali ya walowezi ya Rhodesia. Lakini kutokana na hali halisi ya kiuchumi ilivyo Zaire imebidi kufanya biashara na Rhodesia. Litakuwa jambo la maana sana bwana Willy kama Zambia itakuwa tayari itakuwa tayari kuisaidia Zaire kibiashara ili iweze kupunguza biashara na Rhodesia na hatmaye kuikomboa kabisa Zaire kutoka mikononi mwa walowezi kiuchumi," Max alimweleza. Willy aliyekuwa anasilikiliza maelezo ya mzungu huyu ambaye alikuwa ameanzisha mazungumzo yanayoingiliana na siasa kali iliyokuwa inamgusa moyo, alimtilia mashaka sana mtu huyu kama kweli alikuwa anazungumza kutoka moyoni mwake au alitaka kumsikia yeye Willy amesimama wapi. Hivi alijibu.

"Jambo hili niachie nitalishughulikia, kwani umefikia wapi?" Max aliuliza.

"Niko Hoteli Memling,"

"Utakuwa hapa mjini kwa muda gani?"

"Leo ni Jumatano... nitakuwa hapa mpaka wiki ijayo", alijibu Willy.

"Vizuri bwana Willy, mimi nitakupasha habari kati ya kesho au kesho kutwa, maendeleo nitakayokuwa nimeyafanya juu ya suala hili. Nitazungumza na Wizara ya Kilimo na Mashirika yanayohusika. Usiwe na shaka jambo hili limefika mahali penyewe," Max alieleza huku akisimama, akaenda ukutani akawasha mashine ya kuleta baridi. Kitendo hiki kilimgutua kidogo Willy lakini akaona kweli hali ya joto ilikuwa imeanza kuingia.

"Lini umefika hapa mjini?" Max alimuuliza.

"Toka Jumatatu," alijibu Willy kisha aliendelea na mazungumzo ya kibishara kwa muda kidogo halafu Willy akaamka tayari kwa kuondoka. "Nashukru sana bwana Max nafikiri sasa nitaondoka. Mimi nitakuwa nasubiri kusikia toka kwako," Willy aliaga.

"Karibu tena siku nyingine", Max alijibu naye akasimama kumsindikiza Willy. Max alimsindikiza na kuingia kwenye ofisi ya Lucie.

"Asante sana Lucie, mimi ninaondoka," Willy aliaga.

"Asante karibu tena," Lucie alijibu. Max alimsindikiza Willy mpaka mapokezi ndipo akamuaga.

"Oh Willy nitakupigia simu."

"Asante nitaisubiri," walipeana mikono Max akarudi ofisini kwake huku Willy akibaki anazungumza na Tete.

"Vipi mazungumzo yenu yameambua chochote cha maana?" Tete aliuliza.

"Oh yamekuwa mazuri kiasi ambacho sikutegemea" alijibu Willy.

"Nashukuru imetokea hivyo. Je leo mtakuwa wapi?" Tete aliuliza.

"Sijajua bado mpaka nimwulize Mwadi ambaye ndiye mwenyeji wangu. Je ulikuwa unasemaje?" Willy aliuliza.

"Basi nitampigia simu Mwadi", Tete alijibu kwa mkato.

"Haya vizuri, nitajua toka kwake," alijibu Willy. Kisha waliagana na kuahidiana kuwa huenda wangeonana jinsi ile baada ya kila mmoja wao kuzungumza na Mwadi. Willy aliingia ndani ya gari lake huku akiwa na mafikira mengi sana juu ya ofisi hii. Baada ya kufikiria mambo kadhaa yaliyomtia wasiwasi juu ya ofisi hii kuwa itambidi arudi na kuingia ndani ya ofisi hii wakati itakapokuwa imefungwa, hasa wakati wa usiku kwa siri ili aweze kutuliza wasiwasi wake. Alipoangalia saa yake aliona ni saa tano, akaamua kufika madukani kidogo.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru