KIKOSI CHA KISASI

SURA YA NANE 

MAUAJI YA KISHENZI 

V

Ilikuwa saa kumi na mbili za jioni wakati Willy alipoondoka nyumbani kwa Robert, ili kuelekea Bandalungwa nyumbani kwa Mwadi. Wenzake aliwaacha bado wanapumzika. Kiasi cha saa kumi na mbili na robo ndipo Willy alikuwa anaegesha gari lake nje ya nyumba ya Mwadi. Alifungua mlango wa gari akaenda kubisha hodi mlangoni, lakini hakupata jibu lolote. Alishangaa sana kwa kutomkuta Mwadi nyumbani na hali alikuwa amemuahidi kuwa atakuwa anamsubiri. 

Kisha aliamua kumsuburi kidogo, kwani aliona kulikuwa na umuhimu wa kumsubiri ili waende wote kwa Tete. Maana aliamini kuwa angeweza kupata maelezo mengi zaidi kutoka kwa Tete kwa kumtumia Mwadi. Alimsubiri hapo nje kiasi cha robo saa zaidi mpaka akaanza kuingiwa na wasiwasi. Alienda akaujaribu mlango kama umefungwa, akakuta uko wazi kitu ambacho kilimwonyesha kuwa Mwadi hakuwa ameenda mbali. Alipoingia ndani tu, mara kengele ya tahadhari ikalia kichwani mwake maana aliona matone ya damu chini kwenye zuria. Alirudisha mlango haraka na kutoa bastola, huku akichunguza huko na huko. Alifungua mlango wa chumba cha kulala kwa ghafla na kuingia ndani. Loo tishio alilolikuta ndani mle ni lile ambalo hatawahi kulisahau.

"Mama yangu mzazi" Willy alilalamika kwa hasira. Mwadi alikuwa amekatwa na huku amelazwa kitandani na ametumbuliwa matumbo nje. Yalikuwa mauaji ya kishenzi ambayo Willy alikuwa hajawahi kuyaona. Haraka haraka Willy alichukua shuka akaifunika maiti ile, akaangalia huku na huku lakini hakukuwa na kitu chochote cha maana kwa uchunguzi akamuapia Mwadi kwa sauti, "Mungu mmoja, mpenzi wangu Mwadi, watu waliokufanya hivi, nitakulipizia kisasi kwa mkono wangu. Maana umekufa kwa ajili yangu. Nitakukumbuka daima," Alipokwisha kusema maneno haya alitoka haraka haraka na kufunga mlango wa chumba na wa mbele akiwa amejawa na hasira na uchungu mwingi aliamua kwenda Ndolo. Mawazo yake yalikuwa yamemtuma kuwa, mauaji ya Mwadi lazima yalikuwa yameletelezwa na uhusiano wa yeye, na vile vile alihisi kuwa lazima angekuwa anajua habari fulani fulani juu ya mauaji haya, maana Tete na Mwadi walikuwa wamepigiana simu mchana na ndiye mtu aliyejua Willy atakuja kwa Mwadi na vile vile kuwa Mwadi atakuwa nyumbani. Akiendesha kama mwendawazimu alielekea Ndolo nyumbani kwa Tete. Alipofika Ndolo alikumbuka kuwa Mwadi alikuwa amemwambia kuwa Tete alikuwa na nyumba yake iliyokuwa inatazamana na uwanja wa mdogo wa ndege wa Ndolo. Alienda mpaka sehemu hii akaikuta nyumba nambari 16 ambayo ilikuwa imezungukwa na seng'enge pamoja na michongoma. Kulikuwa na lango kubwa, lakini wakati huu lango hili lilikuwa wazi. Willy aliingiza gari lake moja kwa moja ndani ya ua. Alikuta kuna gari moja ndogo aina ya 'MG Sports' akahisi kuwa hii ilikuwa gari ya Tete kwa sababu alikuwa ameiona pale Sozidime. Huku akiwa katika tahadhari kubwa alitelemka ndani ya gari na wati huo huo Tete naye alikuwa amefungua mlango wa mbele ya nyumba.

"Ooh karibu Willy, mbona uko peke yako, Mwadi yuko wapi?", Tete alimkaribisha Willy na kumuuliza.

Willy alijibu, "Asante." Jibu hili lilimtatanisha Tete lakini hakusema kitu. "Nani mwingine yuko hapa nyumbani kwako," Willy aliuliza huku amepandwa hasira wakati wameingia ndani ya kurudisha mlango.

"Hamna mtu mwingine," Tete alijibu kwa woga maana aliona sura ya Willy imebadilika kiasi kwamba alionekana kama mzee. Willy alimshika Tete, akaanza kumtwanga makofi, "Niambie nani amemuua Mwadi la sivyo nitakuua na wewe," Willy alimwambia kwa harira. Tete ambaye alikuwa ameanza kupiga makelele kwa kupigwa makofi alinyamaza ghafla baada ya kusikia maswali haya ya Willy. 

"Niache , unasema nini?" Tete aliuliza huku macho yote yamemtoka na uso wake ukapoteza rangi naye vile vile akaonekana kama mzee. Kuona hivi Willy alimuachia akamjibu.

"Mwadi ameuawa kishenzi kabisa naamini wewe unajua nani amemuua kwa sababu ni wewe na mimi tuliojua mienendo ya leo ya Mwadi.

Kusikia hivi Tete alianza kulia kwa uchungu mwingi. "Sikiliza Tete, mimi sikuja hapa kukuangalia unalia, ninachotaka kujua nani amemuua Mwadi, au niulize hivi mtu gani amekuuliza habari za Mwadi leo?" Willy alimuuliza. Tete aliinua macho yake akamwangalia Willy kisha akasema kwa sauti ya uchungu. 

"Mwadi alikuwa rafiki yangu sana, tumefahamiana muda mrefu toka tuko shule. Siamini kama amekufa".

"Kama kweli alikuwa rafiki yako mimi nataka kulipizia kisasi. Sasa lazima unisaidie, kuna mtu amekuuliza habari za Mwadi leo?" Willy aliuliza baada ya kuona Tete analalamika. Tete alianza kufikiria jinsi mpenzi wake Muteba na rafiki yake Kabeya walivyokuja saa kumi ile baada ya kutoka kazini na kumuulizia juu ya Willy na Mwadi na sasa alishangaa kusikia Mwadi ameuawa. Hakuamini kuwa Muteba angeweza kufanya jambo hili. Kufikiria hivi kulimfanya machozi mengi yazidi kutiririka kwani alijukuta katika hali ya kutatanisha sana. Alianza vile vile kumfikiria huyu kijana aliyesimama mbele yake alikuwa na nini kiasi awe kwamba uhusiano wake na Mwadi umefanya akina Kabeya wamuue Mwadi, hata yeye alianza kuogopa. Kutokana na maswali aliyokuwa ameulizwa na akina Kabeya naye alianza kuamini kuwa wangeweza kuwa ndio wamemuua Mwadi, kwani walisema walikuwa wanaenda kumwona. Alisikia uchungu na huzuni kubwa juu ya Mwadi na akili yake ilivurugika aliposikia ya kwamba Muteba, mpenzi wake alikuwa anahusika na mauaji haya.

"Niambie Tete, muda unakimbia?" Willy aliuliza baada ya kuona kuwa Tete kweli kuna kitu alikuwa anakifahamu.

"Kwa nini usiende Polisi ukapige ripoti?" Tete aliuliza.

"Mimi sina haja ya Polisi, kama una haja ya Polisi nenda wewe, mimi ninataka unielekeze nani unafikiria?" Willy alijibu kwa mkato. Tete aliamua amweleze, maana kwa sababu asizozijua alikuwa anamchukia sana Kabeya, Hata alikuwa amewahi kumweleza Muteba juu ya chuki yake kwa Kabeya, lakini Muteba hakutilia manani jambo hili. Alikuwa anahisi kuwa Kabeya alikuwa mtu mbaya katika matendo yake, hata aliwahi kumfikiria kuwa angeweza kuwa jambazi. Sasa wasiwasi wake ulikuwa umethihirika, ila kilichokuwa kinamsikitisha ni kwa nini Muteba ajiingize kwenye matendo maovu ya mtu huyu. Alimjua Muteba fika, hivi alishangazwa na kitendo hiki ambacho kilikuwa hakilingani naye, kwani alikuwa mtu tajiri na mwenye kuheshimika kama yeye Tete alivyomjua kwa binafsi hivi aliamua amweleze Willy kwani kumficha kungekuwa na maana kwamba alikuwa amefurahishwa na mauaji ya Mwadi. kitu ambacho kingemhangaisha moyoni mwake. Aliinua kichwa chake akaangalia juu kwenye dari huku machozi yanaendelea kumtoka. Akiwa kama mtu ambaye yumo mwenye njozi alizungumza taratibu. "Nilifika hapa nyumbani kiasi cha saa kumi na robo hivi kutoka kazini. Kwa sababu Mwadi alikuwa ameeleza kuwa mtakuja nilifika hapa mapema ili kuwaandalia chakula cha jioni. Saa kumi na nusu hivi nikapata wageni. Wageni hawa walikuwa na rafiki yangu Muteba na rafiki yake Kabeya. Nilifurahi kumwona Muteba kwa sababu nilikuwa nimemtafuta kwenye simu bila kumpata. Niliwakaribisha halafu mimi nikaenda jikoni kuendelea na shughuli zangu. Kisha wote wawili wakaja jikoni ndipo Muteba akaanza kuniuliza juu ya uhusiano kati yako na Mwadi. Kwanza nilishangaa wamejuaje hizi habari lakini nikafikiria kuwa huenda walikuwa wameonana na Mwadi na amewaeleza. Najua kuwa Kabeya alikuwa anamtaka hivyo kuwapo kwake nilikuelewa. Niliwaeleza yote ninayojua kati yako na Mwadi. Vile vile waliniuliza lini ulifika hapa mjini, nikawaeleza kuwa ulifika Jumatatu iliyopita. Walizungumza wao wenyewe mambo fulani kuhusu majina, na Kabeya akasema kuwa Mwadi lazima ndiye anajua kwa nini jina lako halikuwemo. Sikuelewa maana yake na wala sikutilia maanani kiasi cha kuwauliza. Hivyo Kabeya aliaga akamwambia Muteba anaenda kumuona na Mwadi. Muteba alibaki nyuma, kwani nilimweleza kuwa wewe na Mwadi mngefika hapa kututembelea na kuwa nilikuwa nimemtafuta kwenye simu muda mrefu bila kumpata, na kwa vile alikuwa amekuja nilimuomba abaki kusudi tuwasubiri wote. Akakubaliana na mimi akasema naye alikuwa anapenda kuonana na wewe lakini anaomba aende nyumbani kwanza akabadilishe mavazi ndipo arudi. Tokea hapo hajarudi tena. Hayo ndiyo ninayoyajua", alimalizia Tete huku akiendelea kutazama juu.

"Huyu rafiki yako Muteba yeye anashughulika na nini?" aliuliza Willy kwa sauti ya huruma.

"Yeye ni mfanyabishara ana gereji yake inayoitwa Garage Baninga." Kusikia hivi moyo wa Willy uligonga haraka haraka kwani ilionekana watu wote wenye magereji hapa mjini Kinshasa walikuwa wameunda kundi la ujambazi.

"Mmefahamiana toka lini?"

"Tuna mwaka na nusu sasa. Maana tulifahamiana baada ya mimi kurudi mjini hapa kutoka Brazzaville ambako nilikuwa nafanya kazi, kwani mjomba wangu yuko huko. Wakati natafuta kazi ndipo nilionana naye na ni yeye aliyenitafutia kazi huko Sozidime," Tete alieleza. Willy alianza kuona mwanga mkubwa sana sasa. Kumbe Sozidime ilikuwa na uhusiano na haya magereji ya majambazi. Kitu hiki kilimpa dukuduku kubwa sana moyoni.

"Unajua huyu Kabeya anakaa wapi?" Willy aliuliza.

"Anakaa huko Yolo-Sud, barabara ya Ezo, nyumba nambari 32." Tete alijibu.

"Tete tafadhali sana usimwambie mtu yeyote kuwa umenieleza mambo haya jaribu kurudia hali yako ya kawaida, na hata mpenzi wako Muteba usimweleze, maana maisha yako yanaweza kuwa hatarini ukieleza mambo uliyonieleza. Mimi nakwenda nitakuja kukuona tena. Kifo cha Mwadi nimeapa nitalipiza", alisema Willy huku uchungu unampanda tena.

"Lakini hasa wewe ni nani, maana mawazo yangu yanaanza kukufikiria kwamba wewe si mfanyabiashara. Jinsi unavyofanya na jinsi ulivyo kama mcheza sinema." Tete alimuuliza huku sasa akiwa anamwangalia Willy.

"Kiasi unachokijua kinakutosha, kunijua sana kunaweza kukawa hatari kwako", alijibu Willy huku akisimama.

"Usiniache hapa Willy twende wote, nasikia woga tafadhali usiniache," Tete alianza kulia tena. Kwa vile Willy alikuwa bado ana shughuli ya kufanya alimwambia, "Wewe nenda ukalale kama una pombe kali, kama vile Whisky, kunywa halafu lala, mimi nitakuona baadaye," alimwacha Tete analia Willy aliondoka akaingia ndani ya gari na kukata shauri kwenda nyumbani kwa Kabeya. Aliomba amkute Kabeya nyumbani maana alikuwa amepatwa na hasira juu ya mauaji ya Mwadi. Alikuwa anajiona kuwa yeye ndiye chanzo cha kifo cha Mwadi, hivi mzigo wote wa kifo hiki aliamua kuubeba yeye mwenyewe binafsi. Wakati anaelekea nyumbani kwa Kabeya, mawazo yake yalikuwa yanafanyakazi sana. Habari alizokuwa amezipata kwa Tete zilianza kuleta picha yote ya mambo yalivyo. Ilikuwa inakaribia saa mbili wakati Willy alipowasili sehemu ya Yolo-Sud. Alitafuta barabara ya Ezo mpaka akaipata. Kuangalia nambari za nyumba alikuta ameingilia kwa juu kwani alikuta yuko nyumba nambari 110 hivi alianza kutelemka pole pole kwenye barabara hii mpaka akaiona nyumba nambari 32, akapitiliza mpaka mbele kidogo, akasimama na kutelemka na kuanza kurudi pole pole huku akiwa amejiweka tayari kabisa kwa mapambano ya aina yoyote.

Nyumba ya Kabeya ilikuwa imezungukwa na ua wa michongoma mifupi. Ilikuwa nyumba ndogo lakini nzuri. Willy alisikia furaha kwani aliona taa inawaka ndani ya nyumba hii kitu ambacho kilimaanisha kuwa kulikuwa na mtu ndani. Willy aliamua kuingilia nyumba hii kutokea nyuma. Hivi alizunguka nyumba hii kwa kupitia kati ya ua wa nyumba ya jirani na nyumba hii, na alitembea kana kwamba yeye ni mwenyeji wa sehemu hiyo ili wasiweze kumtilia mashaka. Alipofika nyuma ya nyumba hii aliruka ua na kutumbukia ndani ya ua wa nyumba hii. Alipotumbukia alianza kuizunguka nyumba hii kwa kunyatia na huku anasikiliza kama kulikuwa na mtu ndani. Alisikia mtu anapiga mluzi ndani, akawa na uhakika kabisa kuwa Kabeya alikuwepo maana ni mara chache kumsikia mtu asiyekuwa mwenye nyumba kupiga mluzi saa kama hizi ndani ya nyumba. Alikagua madirisha ya vyumba vya upande wa kulia akakuta yote yamefungwa. Alirudi nyuma ya hii nyumba akatoa funguo zake malaya, akaufungua mlango wa kutokea uani kwa uangalifu na utaratibu sana bila kufanya lolote. Alipoingia ndani alijikuta yuko jikoni. Huku akiwa katika tahadhari, bastola mkononi alifuata kule mluzi ulikokuwa unatokea. Alipofungua mlango wa jikoni alijikuta yuko sebuleni. Juu ya meza moja iliyokuwa na chupa ya primus, meza yenyewe ilikuwa karibu na makochi, hii chupa ilikuwa nusu na glasi iliyokuwa imejaa pombe. Hii ilimuonyesha Willy kuwa kulikuwa na mtu mmoja tu hapa ndani. Muziki ukiwa unatoka taratibu kwenye radio, mluzi uliendelea kusikika kutoka kwenye chumba kilichokuwa kushoto kwa Willy alipokuwa amesimama. Akisha viweka vitu vyote hivi maanani aliamua kuunguruma. Kabeya ambaye alikuwa na uhakika kuwa ni yeye.

Alinyata alikwenda mpaka kwenye ule mlango wa chumba na ghafla ule mlango wa chumba ulifunguka huku Willy akiwa ameiweka bastola yake mkononi ikiwa imemlenga mtu huyu aliyekuwa ndani ya chumba hiki akivaa nguo baada ya kukoga kama alivyoonekana.

Mtu huyu aliingiwa na hofu kubwa kwani ilionekana hakuwa kabisa anategemea kuwa jambo kama hili lingeweza kumtokea. "Weka mikono juu," Willy alimwambia huku anarudisha mlango. Mtu huyu ambaye alikuwa anafunga mkanda wa suruali, akiwa bado hajavaa viatu alifanya kama alivyoagizwa. "Nasikia ulikuwa unanitafuta, nimekuja sasa. Mwadi amenieleza kuwa ulikuwa kwake kiasi cha saa kumi na moja unaniulizia. Niulize mimi mwenyewe sasa maana Mwadi alishindwa kukujibu," Willy alimweleza kwa kebehi. 

Kabeya alitetemeka kusikia maneno haya maana alikuwa ana uhakika kuwa alikuwa amemuua kabisa Mwadi kabla hajaondoka. "Mimi sijui unavyozungumza," Kabeya alijibu kwa hofu kwani sura ya Willy ilionyesha chuki kubwa sana,

"Sikiliza Kabeya, wewe ulikuwa unanitafuta mimi Willy, na ndiyo sababu umemuua Mwadi kwani Mwadi hakuweza kukueleza lolote juu yangu. Ukweli ni kwamba Mwadi alikuwa hajui lolote, lakini wewe hukutaka kumwamini mpaka umemuua, sasa mimi mwenyewe nimekuja niulize, la sivyo utaenda kuonana na Mwadi huko kwa Mungu mkashitakiane vizuri," Kabeya alijui sasa ndiyo mwisho wa maisha yake, maana jinsi alivyokuwa ameingiliwa alikuwa hana hamu tena kabisa. Moyo wake wote wa ujasiri uliyeyuka kama kipande cha samli kwenye kikaango. Alianza kujuta kwa nini alimsikiliza Muteba ajiunge naye. Kila wakati alikuwa akijuta siku moja mwisho wake utakuwa mbaya, pesa kupenda pesa kulikuwa kumemponza, aligwaya Kabeya rohoni.

"Kama huwezi kuniuliza mimi, mimi nitakuuliza wewe. Hii GAD Garage ni mali ya nani?" Bila hata kufikiria Kabeya alijibu.

"Ni mali ya mzungu mmoja aitwaye Jean, ni raia wa Ubelgiji".'

"Umefanya naye kazi kwa muda gani?"

"Miaka mitatu na nusu sasa".

"Je Muteba mna uhusiano gani?"

"Ni rafiki yangu, na tunatoka sehemu moja huko jimbo la Shaba. Ni marafiki wa siku nyingi. Muteba ndiye aliyenitafutia kazi na kunijulisha kwa Jean."

"Nieleze yote unayoyajua juu ya njama zinazofanyika kati ya gereji Baninga, Papadimitriou, GAD na kampuni ya wakala ya Sozidime. Usinifiche kwani kunificha unanunua tiketi ya kifo. Mimi ndiye jaji wako, naweza nikakuhukumu kufa au kukusamehe kutokana na ambavyo utakuwa tayari kushirikiana na mimi," Kabeya ambaye kwa kuogopa kufa alikuwa amesahau masharti yote ya 'WP' alianza kuropoka. "Wote wanachama wa 'WP' moyo wa Willy ulishtuka akauliza. 'Wp' maana yake ni nini?" Kabla Kabeya hajajibu walisikia gari linafunga breki mbele ya nyumba hii. Kabeya akakumbuka kitu kilichokuwa kimemruka mawazoni ya kwamba Charles alikuwa aje kumpitia hapa ili waende kwenye shughuli ya kuwasaka akina Ozu na Kofi. "Nani huyo?" Aliuliza Willy.

Kabeya akiwa amepata imani kidogo kuwa Charles akishirikiana naye angeweza kuokoka alijbu, "Sijui ni nani", Willy alijua amedanganywa. Charles akiwa pamoja na kijana mwingine waliingia moja kwa moja nyumbani kwa Kabeya kwani ni kitu ambacho walikizoea.

"Hey Kabeya uko wapi?" Charles aliuliza.

"Nakuja Charles," alijibu kwa sauti ya wasiwasi Kabeya.

Willy alijua sasa mambo yameiva kwa Charles ndiye alikuwa amekodi gari lile lililokuwa linamfuata Ozu kutoka S.T.K. Mawazo ya Willy yalifanya kazi haraka sana kwa sababu alijua sasa hali ya hatari hata kwake ilikuwa imetangazwa. Ilibidi acheze vizuri mchezo huu la sivyo wangeweza kumletea matatizo. Alisikia Charles anazungumza na mtu mwingine akajua wako watu wawili, hapo sebuleni. Aliangalia saa yake akaona muda umekwenda. Alimuonyesha ishara Kabeya afungue mlango atoke nje, huku akiwa amemlenga bastola. Kabeya alianza kupata moyo tena wa kijasiri akaamua hapa ndipo atajaribu kuokoa maisha yake. Willy alikuwa akimwangalia kila hatua yake. Kabeya alifungua mlango taratibu akatoka nje, Willy akiwa anamfuatia bastola mkononi. Ghafla kama umeme Kabeya alijitupa. Willy akafyatua risasi ikamkosa. Charles akatupa kimeza kidogo kilichopiga bastola na kutoka mikononi mwa Willy. Yule kijana mwingine alitoa bastola yake na kupiga risasi upande wa Willy, lakini aliruka kutoka pale kabla risasi haijafika, akamfikia Kabeya ambaye alikuwa anaanza kusimama na kumsukumia kwa nguvu sana kwa yule kijana mwenye bastola wakagongana huku bastola inafyatua risasi ovyo.

Charles ambaye alikuwa bado akili yake haijajua hasa nini kinatokea alimtwanga Willy teke la tumbo, lakini Willy akawahi kumshika na kumsukuma kwenye kochi ambalo alianguka nalo. Aliona bastola yake ilipokuwa kumbe na Kabeya ambaye alikuwa ameanguka juu ya yule kijana alikuwa na yeye ameiona. Hivi Willy alipoirukia na Kabeya naye alirukia wakafika wakati mmoja. Willy alimpiga kichwa kabeya na kuruka pembeni kabla yule kijana mwenye bastola hajapiga risasi. Yule kijana alipopiga risasi zilimkosa Willy lakini zilimpata Kabeya ambaye alikuwa hajiwezi kutokana na dhoruba ya kichwa alichopata toka kwa Willy. Risasi hizi zilimpiga Kabeya kichwani na kumjeruhi vibaya sana. Kitendo hili kilimshtua yule kijana, na kushtuka kwake kulimpa muda Willy kumrukia na kupiga teke bastola ile na ikaanguka sehemu nyingine ya chumba. Charles alikuwa amejiweka tayari lakini woga ulimwingia baada ya kuona kuwa Kabeya alikuwa amejeruhiwa vibaya sana kwa mikono yao wenyewe. Hata hivyo alijikaza akatupa konde moja safi sana, lililompata Willy na kumfanya apepesuke. Yule kijana alichukua nafasi hii akampiga Willy ngwala na kumuangusha chini. Charles alimrukia hapo chini lakini Willy alimwahi na kumpiga farasi teke akaanguka upande ule mwingine na wakati huo huo Willy akawa amesimama na kukabiliana na yule kijana mwingine. Yule kijana alitupa ngumi ya kwanza Willy akaiona, akatupa ya pili akaiona, akatupa ya tatu Willy akaiona na pale pale akatupa shoto lake alilokuwa ameliweka kwa nguvu zote na kumtwanga huyo kijana ambaye alianguka chini na kushindwa kuinuka. Willy alimgeukia Charles ambaye alikuwa amesimama kutoka pale akamwambia. 

"Mimi nachukia wazungu ambao wanaokuja kufanya udhalimu katika Afrika, leo utaniambia." Akiwa amepandwa na mori na huku Charles naye akiwa amejawa na hasira walikabiliana kama mafahari ya ng'ombe. Charles alibadilisha akaanza kupiga karate, kumbe hakujua karate Willy ndiyo alikuwa mwenyewe. Walizipiga wakazipiga. Willy akaona huyu mtu anamchelewesha akambadilishia mitindo ya karate kama mitatu halafu akamfungia kazi ya kung-fu. Alimpiga na dhoruba moja ya kung-fu ambayo Charles hakuweza kuizuia, ikamdhoofisha sana. Willy alimrukia akashika kichwa chake na mabega akapanda na kuvunja shingo lake na kumuua pale pale. Wakati anazipiga na Charles alikuwa vile vile anaangalia kama yule kijana ameamka ama vipi. Mara hii alipogeuka baada kumuua, alikuta yule kijana anainua bastola huku akitetemeka karibu kufyatua risasi. Wily aliwahi tena kuruka kabla risasi hazijamiminika pale alipokuwa, na pale aliporukia palikuwa karibu na pale Kabeya alipokuwa amelala na bastola yake ilikuwa karibu pale. Hivi alipotua pale tu alinyanyua bastola na kuwahi kumpiga yule kijana risasi na kumwua pale pale.

Willy alisimama bastola mkononi akamwendea Kabeya. Hali ya Kabeya ilikuwa mbaya sana kiasi cha kwamba angeweza kukata roho wakati wowote. Willy alimtingisha na kumuuliza, 'WP' ni chama gani," Kabeya aliinua macho na kumwangalia Willy huku sauti ikiwa inafifia alisema, "White po... po... power," halafu akakata roho. Willy aliondoka ndani ya nyumba hiyo huku akitembea haraka haraka aliingia ndani ya gari lake na kuelekea nyumbani kwa Robert. 

ITAENDELEA 0784296253

Comments

 1. Chapa KAZI kama Willy....ninasema piga kazi wewe ndio Nyakasagani hupangiwi urushe lini na wakati gani...bro CHAPA KAZI

  ReplyDelete
 2. iko poa nasubiri kwa ham nini kitaendelea

  ReplyDelete
 3. iko poa nasubiri kwa ham nini kitaendelea

  ReplyDelete
 4. Nyakasagani tunasubiri mzigo mkuu au tukuchangie Airtel money uturushie via WhatsApp!!

  ReplyDelete
 5. ???????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????

  ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru