KIKOSI CHA KISASI

SURA YA NANE

MAUAJI YA KISHENZI 

II

Wakati Willy anaondoka nyumbani kwa Robert saa tatu hivi mkutani mkali ulikuwa ukiendelea nyumbani wa Pierre huko Limete. Mkutano huu ulikuwa umeanza saa moja ya asubuhi lakini ulikuwa bado unaendelea. Mazungumzo hasa katika mkutano huu yalikuwa yanahusika na tukio lililokuwa limetokea usiku ule huko 'Garage Papadimitriou'.Pierre ambaye alikuwa ametoa maneno makali sana kwa kushindwa kwao katika tukio hili, alikuwa saa hizi amesimama na huku anatembea toka pembe mpaka pembe ya chumba kitu ambacho kilionyesha kuwa alikuwa na mafikira mengi sana.

"Hili tukio ndilo liwe la mwisho kwetu kushindwa. Ni aibu kubwa kuona ya kwamba kundi tulilolijenga muda mrefu liweze kuingiliwa na kutingishwa na watu wawili. Hapana watu hawa lazima watafutwe na wauawe mara moja, maana sijui BOSS italipokea vipi tukio hili wakati mjini hapa imeweza kuweka watu wake mashuhuri na wenye vyeo vya juu kabisa wapatao watano, na eti ipate habari kuwa wapelelezi wawili na wakiwa na wakiwa Waafrika wameweza kuingia ofisi mojawapo ya 'WP' na kuua watu wake chungu nzima. Hapana jamani lazima jambo hili sasa limegeuka linahitaji tulishughulikie sisi wenyewe, huenda hawa vijana wetu hawana ujuzi wa kutosha," alieleza Pierre kwa uchungu.

"Sawa Patroni jambo lililotokea jana limekuwa ni fundisho kubwa sana. Kosa ni langu kwa sababu niliwadharau watu hawa, nilifikiri wasingeweza kuwa na ujuzi kiasi cha kuweza kutuingilia namna ile. Lilikuwa kosa kubwa mno watu hawa ni hatari sana na wana ujuzi kama sisi au zaidi," alikiri Papa. 

Muteba na Jean waliokuwa wamesikiliza maelezo ya Papa kwa makini sana, waliendelea kunyamaza kwani mambo mengi yalikuwa yakipita mawazoni mwao. Walijua ya kwamba wakati umefika sasa ambao wao wenyewe ndio watatumika na wala hawatamtuma mtu. Walitambua kuwa muda wa mapumziko umekwisha kwani kwa muda mrefu sana wamekaa kibwana mkubwa na kuishi kifahari lakini sasa wakati wa kulipa umefika.

"Mbona mmeduwaa namna hii?" Pierre aliwashtua.

"Mimi niko tayari kabisa kupambana na watu hawa na wala wasikupe taabu," aliropoka Muteba.

"Na mimi vile vile niko tayari ni siku nyingi sijapata muda wa kashikashi kama huu naamini naamini nitaufurahia sana. Nitawaonyesha watu hawa kuwa sisi sio vipimo vyao," alijitapa Jean.

"Kama tulivyopata bahari, watu hawa hawakurejea tena mahotelini kwao jana usiku. Lakini nina imani mchana huu watu hawa lazima watarudi kubadilisha nguo zao. Hivi itabidi tuwe na watu wa kuangalia mahoteli haya, na wawe na ujuzi wa kuweza kumfuata mtu bila ya yeye kutambua. Ni dhahiri kuwa watu hawa wanatembea kwa tahadhari kubwa, na wanalindana kutokana na tulivyojifunza na tukio la jana, hivi itabidi kati yetu tuongoze watu watakaofanya kazi hii na kama mtu akipata nafasi nzuri anaweza kufanya mashambulizi." Pierre alieleza. Muteba na Jean walijitolea kuwa wangeongoza watu hawa.

"Nashukuru," alijibu Pierre. "Lakini kumbukeni watu hawa ni hatari, mkipata nafasi nzuri msiwape nafasi waueni pale pale mimi sijali tena litakalotokea. Hasara waliyokwisha tupa ni kubwa mno kiasi kwamba sijali tena. Mimi nitakuwa gerejini kwangu, ripoti zote mtaniletea huko. Na kama mimi nitawahitaji nitawaeleza.

Wote walisimama wakaondoka kimya kwenda kwenye uwanja wa mapambano. Walipokuwa wameishaondoka Pierre alienda kupiga simu. "Hallo Sozidime hapa," sauti ya msichana alijibu.

"Hapa ni Garege du Peuple, Mkurugenzi yupo?" Aliuliza Pierre.

"Ndiyo yupo".

"Nipe nizungumze naye," Pierre aliomba.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru