KIKOSI CHA KISASI

SURA YA TISA

USIKU WA KAZI 

III

Wakati Willy na wenzake wakielekea gereji Baninga. Kofi aliwaeleza namna gereji ile ilivyokaa maana aliwahi kufika kwenye gereji hii alipokuwa ameharibikiwa na gari, safari moja alipokuwa hapa mjini Kinshasa. "Gereji yenyewe imezungukwa kwa ua wa seng'enge na uwanja wake ni mkubwa kuliko G.A.D. Kuna stesheni ya petroli nje tu ya gereji, na stesheni hii ni mali ya gereji hii. Hivi nina imani kuwa tanki la petroli la stesheni hii litakuwa ndani ya ua wa gereji kwa usalama. Kuna majengo mawili makubwa mojawapo likiwa ni ofisi na moja linatengeneza kivuli cha magari. Kitu kingine cha kufikiria ni kwamba katika sehemu hii ya Kintambo kuna kambi ya jeshi ambayo iko karibu nusu maili kutoka kwenye gereji hii. Nafikiri maelezo haya yatawapa mwanga jinsi gani tutakavyoiingilia gereji hii", alimaliza Kofi.

"Kama ni hivyo, mimi naona ya kwamba uzi uwe ule ule. Tukifika pale mashambulizi yetu yawe ya moja kwa moja. Ozu kazi yake itakuwa kutafuta mdomo wa tanki uko wapi wakati sisi tukipambana na walinzi watakaokuwepo. Ozu akishapata mdomo huu, atapiga risasi hewani kutupa ishara, halafu atafanya kama alivyofanya kule na kuondoka. Shambulizi hili itabidi tulifanye kwa muda mfupi sana ili tusiwape nafasi wanajeshi kutuwahi. Kwani ikiwa watasikia mlio wa bunduki lazima watakuja. Nataka wafike wakati sisi tumeishaondoka," alishauri Willy.

"Hamna taabu silaha tulizonazo zinatosha kabisa kuzuia jeshi zima", alisema Ozu ambaye alikuwa anafurahishwa sana na matukio ya usiku huu. Yeye kama wenzake alipenda sana kashikashi za namna hii. Walipofika barabara ya Bangala walisimamisha gari karibu na shule halafu walichukua silaha zao na kuanza kukiimbilia gereji Baninga. Kila mtu alichukua sehemu yake. Ozu ndiye alikuwa aingie kwa mbele. Kofi kwa nyuma na Willy kwa pembeni. Wote walipokuwa wameshika nafasi zao walingojea Kofi aanze mashambulizi kama walivyokuwa wamepanga.

Kofi aliruka ua wa seng'enge na kutumbukia ndani ya gereji na pale pale akaanza kusambaza risasi. Wale walinzi waliokuwa pale wengine walianza kusinzia. Mara waliposikia mlio wa bunduki walishika bunduki zao na kuanza kukimbia bila mpango. Willy aliruka seng'enge kwa upande wa pembeni na kuanza kushambulia vile vile. Ozu naye aliruka upande wa mbele na kuanza kushambulia vile vile. Walinzi wa hapa waliingiwa na kiwewe maana walisikia mashambulizi yanatoka kila sehemu. Hii iliwafanya waende ovyo na hivi ikawa rahisi kwa Willy na wenzake kuwashambulia. Ozu aliangalia stesheni ya petroli ilipokuwa na akahisi sehemu gani tanki lingeweza kuwa. Huku akiwa anashambulia alienda sehemu ile na kuanza kutafuta. Willy na Kofi walikuwa wanashambulia vizuri sana na walikuwa wameua walinzi wengi. Walinzi waliobaki waliendelea kujihami kwa kupiga risasi mfululizo bila kukoma, ili kuzuia mashambulizi yaliyokuwa yanakuja. Kwa ajili ya kiwewe hawakujua kuwa kwa kufanya hivi wangeweza kumaliza risasi, mkasa ambao walijikuta wamo baada ya muda mfupi. Hivi walianza kukimbia ovyo.

Ozu aliona mdomo wa tanki akapiga risasi hewani. Kisha akaanza kulishambulia kufuli, na baada ya kulisambaza kwa risasi akafungua mdomo wa tanki. Willy na Kofi walisikia ishara hii waliruka na kutoka nje ya ua. Wakati Willy anaruka alimuona mlinzi mmoja naye anaruka ua karibu na yeye, Willy alimfuata na kumkamata. Mara Kofi naye alifika wakamvuta yule mtu na kukimbia naye. Tanki la petroli lilikuwa karibu na seng'enge, hivi Ozu alitafuta tambara akalipata, akalichovya ndani ya petroli, na halafu karuka ua wa seng'enge. Alipofika nje ya seng'enge aliwasha lile tambara moto, akalitupa kwenye mdomo wa tanki lilipokuwa limefunikwa na akaanza kukimbia kule walikoacha gari.

"Tayari", aliwaeleza wenzake ambao walikuwa na mateka wao. Aliingia ndani ya gari wakaondoka. Kazi hii ilikuwa imefanywa kwa dakika nne. "Je huyu mnampeleka wapi?", Ozu aliuliza. 

"Atatusaidia kazi moja sasa hivi," Willy alijibu.

"Mbele kidogo kwenye barabara ya Kasavubu baada ya kona ya Kasavubu na barabara ya Bangala kama unaelekea mjini walikuta kibanda cha simu. Willy alisimamisha gari na kumuamuru yule mtu ateremke. Willy, Ozu na yule mtu waliteremka na kumuacha Kofi akiwa ameliwasha gari tayari tayari kwa kuondoka wakati wowote. Walipofika kwenye kibanda cha simu Willy alimweleza mtu huyu, "Kama unataka kuishi nipe nambari za simu ya gereji Papadimitriou. Nikipiga nikiwapata, nitakupa simu uzungumze nao. Waeleze maneno haya. Gereji Baninga imeshambuliwa lakini hawa watu walioshambulia tumepambana nao wakakimbilia hapa shuleni, sasa tumewazingira tunarushiana risasi tunaomba msaada, umeelewa?" Willy alimuuliza.

"Ndiyo", yule mtu alijibu kwa woga. Mtu yule alitoa nambari za simu ya Papadimitriou bila kusita. Willy alipiga na ikapokelewa mara moja akampa yule mtu. Yule mtu alizungumza nao, na baada ya kujitambulisha aliwaeleza maneno aliyokuwa ameelezwa kusema na Willy, na baada ya kuzungumza tu Willy akakata simu. Halafu akamkata huyu mtu mkono na shingo akaanguka chini akiwa amezirai.

"Twenze zetu sasa gereji Papadimitriou," aliwaeleza wenzake huku wakiingia ndani ya gari.

"Ahaa, nimekuelewa sasa kwanini umefanya hivyo. plani nzuri sana," alisema Ozu. Mara wakasikia mlipuko mkubwa mno uliotetemesha sehemu yote hii ya Kintambo.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru