KIKOSI CHA KISASI

SURA YA KUMI

MAPAMBANO BADO YANAENDELEA

Ilikuwa yapata saa nne za asubuhi Willy alipoamka. Kwani usiku ule walikuwa wameingia kitandani kiasi cha saa kumi ya asubuhi baada ya pilika pilika kubwa walizokuwa wamezifanya. Wote walikuwa wamerudi nyumbani kwa Robert, kwani waliogopa kurudi mahotelini kwao wakihisi kuwa wangekuwa wanangojewa na magaidi hawa. Alipoamka alienda akaoga halafu akaelekea sebuleni kuangalia kulikuwa na nini. Aliwakuta Ozu na Kofi wameisha amka na walikuwa jikoni wanakaanga mayai.

"Loo, hata mimi njaa inaniuma afadhali nimewahi", Willy alisema. 

"Njoo ujisaidie," Ozu alijibu.

Wote watatu walikaa jikoni wanakula mayai ya kukaanga bila chai wala kahawa.

"Robert yuko wapi?" Willy aliuliza.

"Aliacha ujumbe kuwa tusiondoke tumsubiri mpaka atakapokuwa amerudi," Ozu alijibu.

"Mliwahi kuzungumza naye usiku tuliporudi?" Willy aliuliza.

"Ndiyo alikuja chumbani kwetu na tukamweleza kwa kifupi tu mambo yalivyokwenda. Tuliagana kuwa tungezungumza kwa kirefu asubuhi hii," alijibu Ozu.

Wakiwa bado wanazungumza, walisikia gari linapiga breki mbele ya nyumba. Ozu alipochungulia alimwona ni Robert alikuwa amerudi. Wote walihama jikoni na kwenda kuketi sebuleni.

"Huu ndiyo utakuwa mwisho wa kujipikia, msichana wangu anarudi leo kutoka Brazzaville," Robert alisema huku akiketi chini.

"Hakuna haja, sisi wenyewe ni wapishi hodari", alijibu Kofi.

"Lo, msichana wangu ni mpishi stadi kweli chakula chake akipika ni kitamu kama yeye. Ozu alikusanya sahani zao walizotumia kwa kula mayai akazirudisha jikoni. Willy alienda chumbani kwake akaichukua ile bahasha aliyokuwa ameichukua kule G.A.D. akarudi nayo sebuleni. Willy alimweleza kwa kirefu Robert juu ya shughuli waliyokuwa wameitekeleza usiku ule.

"Kwa ujumla makambi wa wadhalimu hawa tumeyateketeza, sasa lililobaki ni kuwakamata watu hawa wanaohusika ili kuvunja kabisa kikundi hiki kinachojiita 'White Power'. Sasa namna ya kuwakamata na kupata ushahidi kamili wa kuweza kuiridhisha Serikali ya Zaire kuwa kweli hawa ndio wamehusika na mauaji mengi yaliyotokea katika Bara la Afrika, ndilo tatizo kubwa lililobaki", Willy alimalizia.

Kisha alifungua ile bahasha akaanza kutoa makaratasi yaliyokuwemo. Mlikuwa na makaratasi mengi yaliyokuwa yanazungumzia mambo ya biashara ya spea za magari. Kwanza Willy aliyapitia makaratasi haya haraka haraka huku akiyapitisha kwa wenzake.     

Karibu na kuyamaliza makaratasi mengi yaliyokuwa ndani ya ile bahasha. Willy aliona barua moja iliyokuwa inatoka kwenye Kampuni moja iitwayo Baseh Overseas Speres Supplies (S. African) Ltd. Ilikuwa imeandikwa kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya 'Sozidime Agence' ikimtaka amweleze mkurugenzi wa gereji iitwayo 'Garage du Peuple' kuwa ajitayarishe kupata spea kutoka kwa kampuni za watu wafuatao.

1. Leon Fadaka
2. Nelson Chikwanda
3. Komba Matengo
4. Omo Nene
5. Edger Mongo
6. John Lupala
7. Mateo Chiunia
8. Lumala Nchitole
9. Stephen Magwasa
10. David Makandala 

Maelezo zaidi yatafuata baadaye. Willy aliweka chini makaratasi mengine akasema.

"Mwishowe tumepata kitu tulichokuwa tunatafuta hebu sikilizeni niwasomee barua hii," Willy alieleza kisha akawasomea. Wenzake wote waliinuka na kumzunguka Willy ili kuiangalia ile karatasi kwa macho yao, karatasi hii ilikuwa nakala. "Unaona sasa, ukichukua kifupi cha Kampuni hii, inakuja BOSS. Hii ina maana kikundi tunachoshughulika nacho ni kikundi cha Shirika la kijasusi la Afrika Kusini (BOSS). Robert alivyokuwa amebuni ni sawa kabisa", Willy alieleza.

"Afadhali sasa tumekuwa na uhakika na ushahidi angalau kidogo kuwa Kampuni ya Sozidime Agence pamoja na magereji mengi ya hapa mjini Kinshasa ni ofisi za Boss zinazoendeleza udhalimu katika Afrika. Inaonekana magereji yanayohusika ni mengi, 'Garage du Peuple' mimi ninaifahamu ni gereji moja kubwa sana iliyoko kwenye sehemu za viwanda huko Limete. Kama tulifikiria kazi imekwisha inaonekana kuwa ndiyo imeanza", Robert alieleza.

Hakika kazi ndiyo imeanza, majina yote yaliyokuwa yametajwa Willy alikuwa anawajua watu hawa, bila shaka hata wewe umeweza kugundua kuwa majina matano ya kwanza yalikuwa ya watu waliokuwa wameisha uawa. Wale watano waliobaki vile vile walikuwa ni maofisa wa juu sana waliokuwa wanaongoza harakati za ukombozi kusini mwa Afrika. Hivi Willy alianza kuwaelezea wenzake juu ya watu hawa.

"Tuna bahati kuwa tumeipata orodha ya maofisa wa wapigania uhuru ambao Afrika Kusini imeamua kuwaua, watano tayari wameishauawa na watano walikuwa mbioni kuuawa. Robert inakubidi umwarifu Chifu juu ya orodha hii bila kuchelewa. Na umuulize karatasi hii tuifanyeje." Willy alimweleza Robert. Willy aliangalia hiyo karatasi tena, akakuta ilikuwa imeandikwa tarehe 15 Juni miaka mitatu iliyokuwa imepita waliyaangalia makaratasi mengine na wakawa wamekusanya maelezo kamili kuhusu kikundi hiki kiitwacho 'White Power' ambacho sasa walijua kwa dhati kuwa ni tawi la BOSS.

"Kama tulivyo kwishasema hawa watu wote tunaopambana nao ni majasusi wa Boss. Boss imeingia katika nchi huru ya Afrika na kuweka mizizi huku ikiwa imekaa raha mustarehe ni jambo la kusikitisha sana," Kofi alisema kwa masikitiko makubwa.

"Hilo ndilo tatizo tulilonalo Afrika," alijibu Ozu.

"Haya tuyaache yalivyo kwanza tumsikilize Robert naye atueleze ya kwake kama kuna maelezo yoyote", Willy alisema.

Robert aliyekuwa amesimama alienda na kukaa chini halafu akasema.

"Nina mambo mengi sana ya kuwaelezeni, jana usiku mlipoondoka nilizungumza na Chifu nikamweleza yote kama tulivyokuwa tumeamua. Yeye alinieleza kuwa tuendelee katika hali hii hii mpaka hapo atakapotupatia maelekezo mengine. Asubuhi hii niliondoka nikaenda ofisini ambako nilituma habari kwa Chifu juu ya matukio ya jana usiku kama Ozu alivyokuwa amenieleza kwa kifupi", alinyamaza kidogo ili kupitisha mate halafu akaendelea.

"Baada ya kupeleka habari kwa Chifu nilimtafuta rafiki yangu wa C.N.D. nikazungumza naye ili nijue serikali ina msimamo gani juu ya matukio ya jana usiku. Habari alizonipa ni kuwa serikali inaendelea na uchunguzi mkali sana. Wale wenye magereji yaliyolipuliwa wameisha andika maelezo kwa kifupi kuwa wanafikiri wenye magereji wenzao ambao walikuwa wanawaonea wivu wa kibiashara ndio wamefanya uhalibifu huu. Vile vile alinieleza kuwa hii Kampuni ya Sozidime Agence ambayo ndiyo wakala wa magereji haya yaliyolipuliwa imepiga makelele mengi sana, na kutaka serikali ichunguze tukio hili, na kuwakamata wanaohusika na kuwapeleka mbele ya mahakama. Alisema Mkurugenzi wa Sozidime ni mtu ambaye anaheshimiwa sana serikalini na ana nguvu nyingi sana kwa Serikali maana Mawaziri wengi ni marafiki zake. Amewahi kuwasaidia sana katika mambo yao ya kibiashara, hivi neno lake lolote lazima lishugulikiwe kikamilifu. Hivyo polisi na C.N.D wamo katika uchunguzi wa matukio yote ya jana, tokea ya Mwadi, Kabeya na wenzake mpaka yale ya usiku", Robert alinyamaza tena kidogo ili kupumua halafu akamwangalia Willy na kuendelea.

"Juu ya mauaji ya Mwadi, Willy inasemekana unahusika. Watu wa pale hotelini wameeleza kuwa wewe ulikuwa na uhusiano naye, na kuwa tangu Mwadi ameuawa ulikuwa bado haujaonekana. Hivi sasa kuna polisi pale Hotelini Memling anakusubiri ili kukuuliza juu ya mauaji hayo, hivyo lazima uwe tayari kwa maswali. Baada ya kuachana na huyo rafiki yangu wa C.N.D nilikwenda kuangalia kama Kadima Kashimuka amerudi kutoka Zambia. Kwa bahati nimepata habari kuwa amerudi leo asubuhi, na kwa vile kutakuwa na mkutano saa sita Wizarani kwao atakuwa ofisini mchana mpaka saa tisa wakati wanapotegemea mkutano huo kwisha. Hayo ndiyo niliyopata katika uchunguzi wangu", alimalizia Robert.

"Umefanya kazi nzuri sana. Sasa inaonyesha jinsi BOSS inavyoweza kujiingiza ndani kabisa ya Serikali ya Zaire na kujijenga thabiti. Hii inaonyesha kuwa kiungo hasa cha ujasusi katika eneo hili la Afrika ni hii Kampuni ya Sozidime. Kwa hivyo tukiiangusha Sozidime tutakuwa tumevunja kabisa mikondo ya kijasusi ya BOSS katika Afrika. Ni imani yangu kuwa tukifikia hapo tutakuwa tumemaliza kazi yetu. Ninachowaomba ni kila mtu akae anafikiria jinsi gani tutaweza kuikamata ofisi hii bila kugombana na serikali ya Zaire kitu ambacho ndicho kinafanya kazi yote hii iwe ngumu", Willy alieleza.

"Sasa unasemaje juu ya huyu Kadima?" Robert aliuliza.

"Hivi sasa mimi ninaondoka kwenda hotelini kwangu ili niweze kupambana na hao polisi ili niweze kujisafisha. Saa nane na nusu ningojee pale nje ya ofisi zenu nitakupitia hapo. Jaribu kufanya kila njia umfahamu kwa sura huyo Kadima, ili hiyo saa tisa tukamsubiri hapo ofisini kwake na tutajua la kufanya hapo hapo", Willy alishauri.

"Sawa, nitajitahidi", alijibu Robert.

"Sisi tunaondoka tukaiangalie hiyo Garage du Peuple ili tuwe na ramani yake kamili. Inaonekana huenda katika gereji hii ndiko kuna mkubwa zaidi wa hawa wengine, huenda ndiyo sababu tulikuwa bado hatujaigungua", Ozu alieleza.

"Lakini mjiangalie sana, sababu watu hawa watakuwa kama Simba aliyejeruhiwa wanaweza kufanya lolote," Willy alionya.

"Usiwe na wasiwasi tutajitahidi kujiangalia", Ozu alijibu.

"Kwa hiyo saa ngapi tutaonana hapa?" Kofi aliuliza.

"Kiasi cha saa kumi tuwe wote hapa", Willy alijibu.

Willy alienda kwenye simu akapiga simu. "Hapo ni STK?" aliuliza.

"Ndiyo, STK uwanja wa ndege," alijibiwa.

"Naomba kuzungumza na Ntumba".

"Subiri". Alijibiwa. Baada ya muda kidogo aliitikiwa;

"Hallo Ntumba hapa".

"Willy hapa, habari yako?"

"Nzuri Willy, habari yako?"

"Nzuri," Willy alijibu, "Habari za Brazzaville?"

"Nzuri tu," alijibu, "Ehe lete habari ninapewa miadi au vipi?" Ntumba alisema kwa sauti ya kejeli.

"Samahani Ntumba, nina tatizo naomba unisaidie."

"Mwanaume wewe, kila siku wewe una tatizo tu, tatizo langu mimi hutaki".

"Ukiweza kunisaidia tatizo hili tatizo lako nitalimaliza mara moja".

"Haya sema tatizo lako, mimi niko tayari masaa ishirini na nne kukusaidia, shauri yako wewe unayeniponda!" Ntumba alijibu.

"Jana ulikwenda wapi toka ulipotoka kazini?" Willy aliuliza.

"Kwanini unauliza? Mimi nilikuwa nyumbani na sikutoka kabisa jana", alijibu Ntumba.

"Sasa sikiliza kwa makini. Mimi nina tatizo kidogo na polisi, mimi nimewaambia kuwa tulikuwa wote toka jana kiasi cha saa kumi na moja mpaka leo asubuhi. Nimewaambia kuwa tulikuwa nyumbani kwako na kwamba hatukutoka mpaka asubuhi. Naomba wakikuuliza useme hivyo hivyo, tafadhali sana," Willy aliomba.

"Umefanya nini, mwanaume wewe?" Aliuliza Ntumba.

"Usitake kujua tafadhali. Je utafanya hivyo?" Willy alitaka kuhakikisha.

"Siwezi kukuangusha nitafanya hivyo. Je jioni nitakuona?" Ntumba alisema. 

"Asante sana", alijbu Willy akikata simu. Alipomaliza kuzungumza kwenye simu, aliagana na wenzake na kuelekea mjini.

ITAENDELEA 0794296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru