KIKOSI CHA KISASI

SURA YA KUMI 

MAPAMBANO BADO YANAENDELEA 

VI 

Kofi na Ozu baada ya kuchukua plani yote ya gereji Du Peuple, pamoja na maelezo yote waliyoyataka tayari kwa mashambulizi ya jioni. Waliondoka na kuelekea Hoteli Regna ambako Ozu alikuwa amefikia. Ozu alibadilisha nguo na kuchukua silaha zingine alizokuwa amezitayarisha kwa mapambano zaidi.

Chakula cha mchana walipatia hapa hapa, na baada ya hapo waliondoka kuelekea Hoteli Intercontinental ili Kofi naye akajiweke tayari kwa ajili ya jioni.

Ilikuwa saa tisa na nusu walipoingia Hoteli Intercontinental baada ya kuridhika kuwa hakuna mtu aliyekuwa amewafuata. Lakini kwa bahati mbaya vijana wa 'WP' waliokuwa wakiwangojea hapo Hoteli Intercontinental walipowaona bila wao kujua. Ozu alienda kwenye bar wakati Kofi alipanda juu kwenda kubadilisha nguo zake. Ilikuwa saa kumi kasoro dakika kumi Kofi alipompitia Ozu kwenye bar. "Niko tayari kabisa, twende zetu tukawawahi Willy na Robert wasije wakatungoja sana. Maana tulikubaliana kuonana saa kumi", Kofi alimweleza Ozu.

"Twende zetu," alijibu Ozu. Ozu alilipa bia yake na wakaondoka. 

Nje ya Hoteli Intercontinental kundi la 'WP' lilikuwa limekaa tayari likiwasubiri, Pierre na Jean pamoja na vijana wao wawili walingojea kwenye mlango unaotokea pembeni mwa hoteli upande wa barabara ya 8E Armie. Papa na Muteba pamoja na vijana watatu walingojea kwenye mlango wa mbele, Makundi haya mawili yalikuwa kila moja likiwa linajifanya linashughulikia gari lililoharibika na kwa jinsi hii hakuna mtu aliyewajali. Pierre, Jean, Papa na Muteba walibaki wamekaa ndani ya gari tayari tayari huku vijana wao wakijifanya kushughulika.
  
Kofi na Ozu walikata shauri kutokea mlango wa mbele bila kujua kuwa wanangojewa, walitembea katika tahadhari yao ya kawaida tu. Walipotokea mlangoni waliangaza kwa mara moja. Na wakati huo huo Papa na Muteba walibonyezwa kuwa tayari walikuwa wameshatoka nje. Papa na Muteba waliruka mara moja na kupiga risasi. Ozu aliwaona mara moja wakati Kofi aliangaza sehemu nyingine, hivi Ozu akapiga kelele "Kofi" yeye akajitupa nyuma ya gari wakati ule ule risasi zikamiminika pale alipokuwa amesimama. Kofi aliposhituliwa na Ozu aliruka kama umeme kwa bahati mbaya risasi zikampata kifuani na kuanguka ndani ya mlango wa hoteli na kujiviringisha mle ndani. Ozu alipiga risasi kuwazuia wale watu, lakini waliruka ndani ya gari na kuondoka mwendo mkali sana. Ozu alisimama akakimbia ndani ya hoteli ambako watu wote walikuwa wamelala chini kwa kuogopa risasi na huku kelele za vilio zikisikika huku na huko. Alienda akamwangalia Kofi akakuta tayari ameishakata roho. Alikuwa amechanwa na risasi kifuani kwani watu wale walikuwa wametumia 'Sub Machine Gun' 

"Kofi Kofi," Ozu aliita huku machozi yanamtoka. Watu walikusanyika na simu ikapigwa polisi.

"Sijaona kitu kama hiki kwa muda mrefu sana hapa Kinshasa. Kumshambulia mtu mchana mchana mbele ya watu wengi namna hii na mbele ya hoteli kubwa namna hii," mtu mmoja katika hilo kundi alilalamika.

"Tena aliyekuwa na bunduki ile kubwa alikuwa Mhindi", mtoto mmoja mdogo alisema, lakini mama yake akamfinya na kumvuta kutoka hapo. Kwa sababu ya uchungu mwingi. Ozu hakujua la kufanya ila alijua hawezi kufanya jambo lolote kwa sasa ila kwenda kuwaarifu akina Willy tayari kwa mapambano na watu hawa. Vile vile kama polisi watamkuta hapo wangepoteza muda mwingi wa kumuuliza maswali. Hivi aliangalia mwili wa Kofi akasema moyoni. "Kofi umekuwa kama mdogo wangu tangu tulipofahamiana, Mungu yupo damu yako haitamwagika bure. Nitahakikisha," kisha akapotea ndani ya kundi lililokuwa pale kama umeme. Pierre na kundi lake walirudi gerji Du Peuple na furaha kubwa sana kwa sababu walijua wamepunguza adui mmoja hivyo upinzani jioni yake ungekuwa kidogo sana.

"Watu wawili kwa watu thelathini, hawatuwezi" Papa alidiriki kusema. 

ITAENDELEA 0784296253 

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU