KIKOSI CHA KISASI

SURA YA KUMI

MAPAMBANO BADO YANAENDELEA

II

Katika ofisi za Pierre huko gereji Du Peuple, viongozi wa 'WP' walikuwa wamekusanyika tena saa nne hii kuelezana nini wafanye baada ya tukio la jana usiku. "Mmemaliza kuandika maelezo yenu polisi?" Pierre aliwauliza wenzake.

"Ndiyo tumemaliza, wote tumeandika maelezo mafupi tu kama tulivyozungumza. Tumeeleza tu kuwa sisi tunafikiria ni washindani wetu ambao wanaweza kuwa wamefanya maafa haya. Polisi hawakuonekana kuridhika lakini walichukua tu hivyo hivyo sababu Max alikuja akiwa ametumwa na Mkurugenzi, wewe mwenyewe unawajua polisi wanavyomuogopa Mkurugenzi," alijibu Jean kwa niaba ya wenzake.

"Vizuri. Habari tulizozipata kutoka Boss kuhusu huyu Willy Chitalu ni kwamba mtu huyu ni Willy Gamba ambaye ni mpelelezi nambari moja Afrika. Mimi niliwahi kumsikia na kuna jarada lake katika makao makuu ya BOSS. Niliwahi kusoma jarada hili wakati wakiwa Johannesburg. Mtu huyu ni hatari sana. Ni mpelelezi mjanja sana na jasiri sana. Kwa hivi mambo yalivyofanyika jana usiku yanadhihirisha kabisa ni yeye. Kwa hivi jamani tujue tuko katika upinzani wa hali ya juu", Pierre aliwajulisha wenzake.

"Kijana huyo hata mimi nimekwisha wahi kumsikia. Jamaa mmoja wa CIA aliwahi kunieleza juu ya kijana huyu na kunieleza kuwa aliwahi kupambana huko Uganda na akanihakikishia kuwa hajawahi kuonana na mpelelezi kama huyu. Aliniambia kuwa kijana huyo angelimuua lakini alimuonea huruma na kumpeleka mikononi mwa serikali ya Uganda ambao walimfukuza nchini na kurudi Maerekani", Papa alieleza.

Jean naye alieleza kuwa alikuwa amewahi kumsikia na kwamba hata yeye alisikia kwamba huyu mtu ni hatari sana.

"Lo, mimi tu ndiye sijawahi kumsikia. Itakuwa vizuri kupambana naye, maana na mimi siku moja nitakuwa na kitu cha kusimulia juu yake," Muteba alisema.

"Si mtu wa kuomba kuonana naye", alimjibu Papa.

"Kwa hiyo jamani nyinyi wenyewe mnajua ni upinzani gani tulionao kwa sasa hivi; Hawa watu watatu wakiwa sasa pamoja ni hatari kabisa.Mpaka sasa hivi agizo kutoka BOSS ni kwamba tuwakabili watu hawa mpaka hapo watakapoamua vinginevyo," Pierre aliwajulisha.

"Lakini watu hawa wamejificha wapi? Maana hotelini kwao hawalali, na jana tulipowafuata walihakikisha kuwa wanatupoteza huenda tukipata wanakojificha mchana kutwa tunaweza kuwashambulia kwa urahisi", Muteba alishauri.

"Kwa sasa hivi itakuwa vigumu maana watu wengi wameuawa. Kitu ambacho mimi nakifirikiria ni kwamba leo lazima watashambulia gereji hii. Kama wameweza kuyajua magereji mengine yote lazima na hili wanalijua. Kwa hiyo sisi itatubidi tujitayarishe kuwakabiri; naamini watu hawa hawawezi kutushinda hata kama wana ujuzi wa namna gani. Nimezungumza na Mkurugenzi amesema atatuongezea ulinzi kwa kutupa watu na silaha za kutosha. Sisi wenyewe tukiwa tunaongoza kikosi hiki naamini wakithubutu kushambulia leo ndiyo mwisho wao..." Simu ililia ikamkata Pierre kauli, "Samahani," aliwaeleza akaiendela simu. Alizungumza mara moja akakata simu akasema. "Jamani naitwa wakala haraka sana, kwa hiyo inatubidi tuvunja mkutano huu ili tuonane hapa kiasi cha saa tisa mchana wakati tutakapopanga mambo ya jioni. Kwa sasa hivi kajitayarisheni tayari kwa pambano la jioni maana leo ndiyo leo". Walikubaliana kuwa wataonana saa tisa za mchana halafu wakatawanyika.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU