KIKOSI CHA KISASI

SURA YA KUMI NA MOJA 

USHINDI NI DHAHIRI

III

Ilipotimia saa nane simu ililia ofisi kwa Pierre. "Hallo", aliitikia alipoinua simu.

"Fernand hapa, vipi mambo bado?" Aliuliza Mkurugenzi.

"Bado, huenda hawatakuja na kama hawatakuja watakuwa wamvuruga mambo maana mimi nimechoka. Kama tutamaliza shughuli hii mimi kesho nitaondoka." Pierre alieleza kwa unyonge. 

"Usiwe na wasiwasi mambo yote yako tayari, ukimaliza shughuli za hapo tu njoo moja kwa moja hapa ofisini, mimi nipo tu mpaka mwisho", alijibu Fernand na kukata simu.

Pierre aliangalia tena saa yake, akiwa na mashaka makubwa kama mambo yangekwenda kama walivyopanga. Wenzake nao ambao walikuwa nje na vijana wao walikuwa nao wamechoka. Kwani walikuwa sasa wamesimama wakisubiri zaidi ya masaa manne. Wale vijana wengi walikuwa wameanza kusinzia sinzia. Kwa ujumla jeshi zima lilikuwa limeshikwa na uchovu, na mawazo ya kwamba "Hakuna kitu" ndiyo yalikuwa yamewajaa wote.


IV

Ilikuwa saa tisa kasoro robo wakati KIKOSI CHA KISASI kilipokuwa tayari kuondoka nyumbani kwa Robert ili kuelekea Limete. Kila mtu alivaa mvao wa kazi. Tete naye alivaa dingirizi na T'shati, na akaweka jaketi juu. Miguuni alivaa raba na nywele zake akawa amezifunga, kwa ujumla alionenana mmoja wao kabisa. "Loo utafikiri tunaenda kuteka ndege nyara. Kwa kawaida wateka nyara wasichana wa Kipalestina huwa ni wazuri sana kama Tete" Ozu alitania. 

"Na wewe na maneno yako". Robert alijibu na kuingia stoo. Aliporudi alikuwa na kamba akampatia Willy. Ilikuwa kamba ndefu. Willy akaikata akampa Robert kipande akamwambia aiweke wataondoka nayo. Willy alienda akafungua mlango wa chumba ambamo Kadima alikuwa amelala. Alimkuta Kadima amelala akamwamsha. 

"Samahani Bwana Kadima itabidi nikufunge kwa usalama wako," Willy alimwambia. Kadima alimwangalia tu bila kumjibu, Willy akamfungia kwenye kitanda. Alimfunga miguu na mikono kwa ustadi kabisa, "Samahani sana", Willy alimwambia tena Kadima na kuondoka, na kuufunga mlango vizuri kabisa. "Sasa twende zetu," Willy aliwaambia wenzake. Wakiwa wameweka silaha zao tayari walipanda ndani ya gari Willy alilokuwa akitumia. Tete akapiga moto na kuondoka pale nyumbani kwa Robert kama risasi.

"Tete ukifika Limete kwenye barabara ya P.E Lumumba ingia barabara ya tisa inayoingia viwandani, nenda moja kwa moja na usimamishe gari mbele kidogo na Kampuni ya BISCO, sisi tutatelemka hapo. Wewe utarudi mpaka kwenye njia ndogo inayounganisha mabarabara yanayoingia viwandani, na egesha gari mbele ya nyumba ya pili kutoka barabara ya nane. Nyumba hii wenyewe wamekwenda Brazzaville na haina mlinzi bali lango lake limefungwa. Wewe utaegesha gari mbele ya lango la nyumba hiyo na nina imani hakuna mtu atakutilia mashaka yoyote. Utatungoja hapo ukiwa tayari tayari, kama itapita zaidi ya saa moja na nusu hujaona hata mmoja wetu, jua mambo yameharibika ondoa gari uende zako. Lakini nina imani nusu saa itatutosha. Umenielewa?" Willy aliuliza.

"Nimeelewa hamna wasiwasi kabisa" Tete alimjibu kwa sauti kavu kabisa.

Kutokana na taarifa Ozu aliyokuwa ameleta, kampuni ya Bisco ambayo hutengeneza biscuti inafanya kazi masaa ishirini na nne. Na inafanyakazi kwa zamu na kwa bahati kulikuwa na zamu iliyokuwa inaingia saa tisa za usiku. Kufuatana na taarifa hii ndiyo sababu walikuwa wameamua kushukia mbele ya Kampuni hii ili ionekane kama kwamba gari ile ilikuwa imeleta watu wa zamu. Jengo la gereji Du Peuple likuwa jengo la tatu mkono wa kushoto kwenye barabara ya tisa kama unatoka barabara ya Patrice Emiry Lumumba. Kulikuwa na majengo mengine matatu makubwa kabla hujafika kwenye jengo la kampuni ya BISCO kutoka gereji Du Peuple. 

Tete ambaye aliwadhihirishia abiria wake kuwa alikuwa dereva stadi sana aliongoza gari kama alivyokuwa ameelezwa. Alipofika kwenye kona ya P.E. Lumumba na barabara ya tisa. alionyesha taa na kuingia barabara ya tisa. Alivuta gari katika mwendo mkali sana na kusimama mbele kidodo ya Kampuni ya BISCO. Alimvuta kidogo Willy aliyekuwa amekaa naye kwenye viti vya mbele ya gari na kumbusu haraka haraka. "Bahati njema aliwaambia kwa ujumla huku akiwarushia busu".

"Na wewe vile vile," Ozu alijibu kwa niaba ya wenzake. Vijana wa Kikosi cha Kisasi wakatelemka kuelekea kwenye mapambano ambayo yangeamua mwisho wa kazi yao unakuwa vipi. Tete aliondoa gari lake, huku watu wote walioona mwendo wake wakahisi kuwa alikuwa taksi dereva aliyekuwa ameleta wafanyakazi wa BISCO waliokuwa wamechelewa zamu. Wazo hili ndilo lilimpata hata Papa aliyeliona gari hili na kulishuku lakini baada ya kusimama mbele ya kampuni ya 
Bisco akaondoa wasiwasi wake.

Baada ya kutelemka tu Willy na wenzake walipotelea ndani ya uchochoro uliokuwa ukipita kati ya BISCO na jengo lililokuwa linafuata. Kulikuwa na giza katika uchochoro huu lakini kwa vile Ozu alikuwa amepita aliwaongoza. Walienda mpaka wakatokea kwenye uchochoro uliokuwa nyuma ya majengo haya yaliyokuwa yanatazama barabara ya nane. Walipokaribia jengo la gereji Du Peuple kwa nyuma, walianza kutembea kwa kunyata na katika tahadhari kubwa. 

"Sii" Robert aliyekuwa mbele aliwasimamisha wenzake, "Nimeona mtu amepita", aliwanong'oneza, "Nisubirini" Robert alienda akinjongwajongwa, na alipofika kwenye pembe ya mwisho ya jengo jirani na gereji Du Peuple alisimama. Alianganza akaona kuna walinzi watatu kwenye ukuta uliokuwa umepakana na jengo hili jingine na walikuwa wanazungumza. Walikuwa hatua chache tuu na alipokuwa. Alipoangalia juu ya ngome ya ukuta uliozunguka gereji Du Peuple aliona kulikuwa na walinzi wanatembea kwa juu. Mmoja alitembea juu ya ukuta wa nyuma na mmoja kwenye ukuta wa pembe ya upande waliyokuwa. Alipokwisha kuona mambo haya alirudi pale wenzake walipokuwa akawaeleza.

"Kwa hiyo hawa wanaozungumza nafikiri ndiyo walinzi wa nje". Willy alisema.

"Sawa kabisa", Robert alikubaliana, "Na ninafikiria kuna mlinzi mwingine juu ya ukuta wa upande mwingine lakini amezuiwa na paa la nyumba hatuwezi kumuona", aliongeza wote watatu wakiwa wamefichwa na kivuli cha majengo haya walinyata mpaka kwenye pembe ya mwisho ya kutokea gereji Du Peuple. Wale walinzi waliokuwa wanazungumza walimaliza na wakamuacha mmoja wao anaelekea mbele ya jengo. Watu hawa walipitia karibu kabisa na pale akina Robert walipokuwa wamejibanza. 

"Hawa watu hawaji tunasumbuka bure, mle ndani watu wameishachoka wanasinzia ovyo", mmoja wao alisema.

"Hata mimi najisikia kuchoka kabisa katika siku hizi tatu sijalala vizuri", yule mwenzake alijibu na wakaendelea. Walipoenda hatua chache kidogo Robert alinyata mpaka kwenye ukuta wa ngome bila kuwagutua walinzi hawa. Aliangalia juu akamuona yule mlinzi aliyekuwa juu ya ukuta alikuwa amekwenda upande mwingine, hivyo hakuwa na wasiwasi wa kuonekana.

Wale walinzi wawili walisimama, mmoja wao akamuomba mwenzake sigara Robert alichukua hii nafasi wakati mawazo yao yako kwenye sigara akawanyatia. Yule mmoja alitoa sigara akampa mwenzake na akatoa kiberiti ili kumwashia sigara. Robert alikuwa ameishafika bila wao kujua, akatoa kiberiti chake haraka akamwashia yule mlinzi aliyekuwa tayari ameweka sigara yake mdomoni akingojea moto. Yule mlinzi mwingine aliyekuwa amewasha kiberiti akagutuka, moto mwingine unatoka wapi. Walipotaka kugeuka tu Robert akawapiga karate wote wawili kwa mara moja na pigo alilokuwa ametoa lilikuwa kali sana akiwa amewapiga shingoni, wote walianguka chini na kufa pale pale bila kelele.

Aliangalia tena juu ya ukuta yule mlinzi wa juu alikuwa haonekani. Akawafanyia ishara wenzake wamfuate. Wakiwa wamezuiwa na kivuli cha majengo waliruka mpaka nyuma ya majengo ya gereji Du Peuple ambako Robert alikuwa bila kuonwa na walinzi wa pembeni kwao. Waliwavuta hawa watu wakawalaza chini ya ua wa michongoma mtu asiweze kuwaona kwa urahisi. Willy alimuona yule mlinzi wa juu ya ukuta wa upande ule wa nyuma akirudi akiwabonyeza wenzake ambao walijibanza. Ozu alijificha chini ya michongoma. Robert na Willy wakajifanya kama kwamba wao ndio wale walinzi waliokuwa wameuawa. Kwa vile wote walivaa nguo nyeusi nyeusi ilikuwa vigumu kutambuana usiku namna hii. Yule mlinzi wa juu hakuweza kuwatilia mashaka kwani aliamini ni wenzake.

Yule mlinzi alipokaribia Robert alimwita kwa kumfanyia, "Sii" yule mlinzi alikuja akauliza, "Unasemaje?"

"Inama nikueleze", Robert alimwambia akawa anajua ni mwenzake akadanganyika akainama. Robert aliruka kama umeme akampiga karate ya katikati ya paji la uso na kumpasua kabisa. na wakati huo huo alimvuta wakamdaka na kumlaza chini akiwa ameisha kufa. Naye alikufa bila kelele. Upesi upesi wakampandisha Ozu akachukua nafasi ya yule mlinzi, akaanza kulinda sehemu hii ya nyuma. Kitendo hiki kilifanyika bila kufahamika ndani ya ngome.

Willy alizunguka mpaka pembe nyingine akakuta hakuna mlinzi wa chini ila yule wa juu ya ukuta alikuwepo. Willy alikohoa yule mlinzi wa juu aliyekuwa anaangalia upande mwingine akageuka, akampungia mkono. Akiwa anafikiri kuwa ni yule mwenzake alikuja. Ozu aliyekuwa tayari akijifanya kulinda sehemu hii ya nyuma aliona ishara ya Willy akajua Willy alikuwa anataka kufanya nini, hivi naye akasogea upande ule. Yule mlinzi akiwa na uhakika na uhakika kuwa wote walikuwa walinzi wenzake alikuja mbio mbio. Alipofika pale Willy alipokuwa amesimama Ozu naye akawa amefika. "Huyu anasemaje", yule mlinzi alimuuliza Ozu.

"Inama msikilize," Ozu alimweleza kwa sauti ya chini chini. Alipoinama tuu Ozu alimkata mkono wa shingo na kumtua chini. Robert alikuja wakamficha. Robert akampandisha Willy kwenye ukuta akachukua nafasi ya huyu mtu.

Ozu alimfuata yule mlinzi wa chini wa upande ule waliokuwa wametokea. Mlinzi huyu alikuwa amesimama tu karibu na kona ya kwenda upande wa nyuma. "Hallo" Ozu alimwita kwa sauti ya chini chini, yule mlinzi akaangalia juu. Ozu akamuonyesha ishara kuwa anaitwa kule nyuma. Robert alikuwa amebana kabisa kwenye kona akiwa anaona mambo yote yaliyokuwa yanafanyika. Yule mlinzi naye akiwa hana wasiwasi wowote akijua kuwa hawa ni walinzi wenzake alienda haraka haraka. Alipojitokeza tu kwenye kona Robert alimrukia akamkaba kabari mpaka akamuua na kumvuta mpaka pale wenzake walipokuwa wamelazwa. 

Ozu akamuonyesha ishara Willy kuwa amebaki mmoja. Bila kujua nini kinatokea yule mlinzi wa juu ya ukuta wa upande ule waliotokea alikuwa anaendelea na shughuli zake za ulinzi bila wasiwasi. Robert alijifanya kuwa yeye ni mlinzi wa chini wa upande ule alimwendea akamwita, "Sii" Yule mlinzi alipogeuka kumwangalia alimuonyesha ishara amfuate nyuma. Yule mlinzi akiwa hana wasiwasi naye alimfuata. Alipofika kule kwenye ukuta wa nyuma Ozu naye alikuwa yuko tayari. "Inameni niwaeleze". Robert aliwaambia wote. Ozu alijifanya anainama na yule mlinzi naye akadanganyika akainama. Ozu akamkata mkono wa shingo na kulivunja, akamsukumia Robert akamdaka na kumvuta chini. Kisha Ozu akainama akampa Robert mkono akapanda na yeye juu ya ngome.

Willy ambaye alikuwa ameishazunguka na kuona jinsi ulinzi ndani ya gereji ulivyokuwa alipita kwa wenzake akiwaeleza huku wakijifanya kama kwamba wanabadilishana sehemu, "Sehemu ambayo bado wako macho ni kule mbele, sehemu hizi zote wengine wamelala na wengine wanasinziasinzia." Willy alimnong'oneza Robert.

"Basi mimi ninatelemka kwa huku nyuma. Nitajaribu kushambulia kwa kadri niwezavyo nikitumia mikono yangu, nyinyi muwe tayari kunichunga kama watagutuka," Robert alisema.

"Kuna walinzi karibu ishirini humu ndani," Willy alimweleza. Kisha Willy aliendelea akamweleza Ozu. Walipokuwa wameshika nafasi sawa sawa na kuweza kumchunga. Robert kama nyani alitumbukia ndani ya gereji kwa nyuma bila kishindo. Jean ambaye alikuwa analinda sehemu ya nyuma pamoja na vijana wapatao sita alikuwa amelala ndani ya gari moja bovu, na akiwa amewaamrisha vijana wake kumwamsha kukitokea tatizo lolote. Alikuwa amekaa macho, mpaka saa tisa lakini akawa amekata tamaa kuwa hawa watu hawawezi kuja tena. Na kwa vile alikuwa hajalala vizuri kwa muda wa siku tatu alisikia usingizi mzito sana.

Ilikuwa sasa imepita miaka mingi bila Jean kujiweka katika hali ya kuweza kukabili hali ya namna hii. Zamani alipokuwa hajaletwa Zaire angeweza kukaa hata juma moja bila kulala asichoke kama alivyokuwa amechoka siku hii, Hivto Robert alipotumbukia ndani Jean alikuwa amelala kabisa. 

Baada ya Robert kutumbukia ndani aliwanyatia walinzi wawili waliokuwa wameegemea kwenye gari, aliwatokea nyuma akawapiga karate za katikati ya vichwa vyao wakafa pale pale kwani alivipasua kabisa. Akatoa ishara kwa Willy kuwa ameua wawili. Kisha akamuona mlinzi mmoja anatokea sehemu ya kushoto kwake akajiegemeza kwenye gari kama mmoja wao, na kutoa sigara. Yule mlinzi alipomuana alimfuata akidhani ni mwenzake akamwomba sigara. Robert akampa halafu akatoa kiberiti kumwashia, na akatelemsha kiberiti chini. Yule mlinzi alipotelemsha mdomo chini ili kuwasha sigara. Robert alimkata mkono wa shingo na kulivunja. Akamchukua taratibu akamuegemeza kwenye gari. Alipozunguka kutokea ule upande wa kushoto, Willy alimfanyia ishara kkumuonyesha kuwa kuna watu ndani ya gari alilokuwa karibu kulipita. Alichungulia ndani akakuta kuna walinzi wawili wamelala, alifungua malngo taratibu kabisa akatoa bastola yake yenye sailensa akawapiga risasi kimya kimya.

Ni wakati alipokuwa amemaliza kuwaua hawa ndipo mlinzi mwingine aliyekuwa amelala ndani ya gari ambapo Robert alikuwa amewaegemeza wale watu wawili aliokuwa amewaua kwanza alipoamka. Kufungua mlango, alipojitokeza na kuwagusa wale wenzake aliokuwa anafikiri wamelala akakuta wamekufa. Kwa hifu akafyatua risasi ovyo. Gereji nzima ikawa katika vurugu, Walinzi waliokuwa wamelala wakaanza kukimbia ovyo, hii iliwapa nafasi nzuri Willy na Ozu kujua ni wapi washambulie. Ozu alirukia ndani katikati ya kikundi kilichokuwa kinaongozwa na Papa na akaanza kushambulia. Willy naye alirukia katikati ya gereji ambako Muteba ndiko alikuwa akiongoza. Robert akabaki kule kule kwenye kikundi cha Jean.

Jean aligutushwa na mlio wa bunduki, akaamka na kupiga kelele, "Shambulia shambulia", Robert aliwahi kumpiga risasi yule kijana aliyekuwa anapiga risasi na kutahadharisha gereji nzima. Jean alijikuta hana mtu ila yeye peke yake kwa upande huu. Robert alimuona, akamsubiri kwani alikuwa anakwenda ovyo katika woga mkuu. Kisha akakata shauri kurukia kwenye ukuta na kujitupa nje. Robert alihisi mawazo yake, na kwa vile alikuwa ameelekeza mgongo wake kwa Robert, Robert alimnyemelea akapiga bastoka kutoka mikononi mwa Jean, Jean kwa hofu aligeuka akajikuta uso kwa uso na Robert.

"Nitakuua kwa mikono yangu kulipiza vifo vya wazalendo wa Afrika ambao umewaua". Robert alimtishia Jean naye alikuwa mjuzi sana wa karate, hivi hakusita kuzianzisha moja kwa moja akifikiri Robert hakuwa na ujuzi kiasi chake. Jean alipeleka pigo la kwanza akapoteza la pili akapoteza la tatu akapoteza, akabadilisha. Robert alikuwa anatabasamu. Jean alipobadilisha alikuja na ufundi wa hali ya juu sana. Mapigo haya yalimpata Robert na kumpandisha mori. Robert alimwingilia Jean kwa Kung fu ya hali ya juu kabisa ambayo Jean alikuwa hajawahi kuona. Robert alimpiga Jean mapigo matatu mfululizo. Jean akaona hamwezi akageuka kutaka kukimbia. Robert akamvuta shati, akamgeuza na kumpiga mapigo mengine matatu ya haraka haraka. Jean alijaribu kwa kadri ya ujuzi wake lakini wapi. Jean aliruka juu ya gari, halafu akamrukia Robert. Robert akamkwepa halafu yeye Robert akamrukia Jean akampiga teke kali kali ajabu kifuani, likamuua Jean pale pale.

Willy aliporukia ndani ya gereji alikuwa ameshikiria 'machine gun'. Aliwaua walinzi kama mchezo maana walikuwa wanapigana bila mpango, Muteba alipoona walinzi wake wanakwisha alichukua 'machine gun' akaanza kushambulia yeye mwenyewe. Alikumbuka ujuzi wake aliokuwa ameupata vitani na katika makambi ya mafunzo ya BOSS, Willy akiwa anadonga huku anaruka hapa na pale aliwaua walinzi wa Muteba wote. Ikawa wamebaki yeye na Muteba. 

Ozu naye alishambulia vibaya sana kundi la Papa. Hili ndilo kundi lililokuwa kali sana. Lakini Ozu alipigana kwa ujuzi wa hali ya juu, Akitumia magari kama ngao yake aliua mmoja mmoja akitumia bastola. Walipoanza kutumia bunduki kubwa na yeye akakamata 'machine gun' na hapa ndipo hakuwakawiza, akawa amebaki yeye na Papa. Pierre aliyekuwa anachungulia mapigano yalivyokuwa yanakwenda, aliogopa alipoona walinzi wake walivyokuwa wameteketezwa. Hivyo akatambua kuwa mwisho wa mapigano haya ungekuwa mbaya.

Alirudi ofisini kwake haraka haraka akachukua mkoba wake aliokuwa ametayarisha, akachukua bastola yake akaijaza risasi aoaktoka ndani ya ile ofisi. Alipofika nje ya ofisi alikuta mapambano kati ya Muteba na Willy. Ozu na Papa yanaendelea, Robert alikuwa naye ndiyo anaondoka nyuma ya ofisi baada ya pambanp lake na Jean. Hivi Pierre aliweza kukimbia bila upinzani mkubwa. Wote waliokuwa wanapambana walimuona lakini hawakuwa na nafasi ya kumfanyia lolote. Hivyo alipata nafasi ya kuondoka gereji Du Peuple salama. Ozu alipokumbuka sura ya Papa wakati anampiga Kofi risasi alijawa na hasira na uchungu mpya hasa ALIPOTAMBUA KUWA MTU HUYU NDIYE ALIYEKUWA ANAPIGANA naye sasa.

"Papadimitriu?" Ozu aliita. Papa hakujibu ila alitupa risasi nyingi pale sauti ilipokuwa inatokea. "Mchana umemuua ndugu yangu Kofi nikikuona sasa utalipa, utalipa madeni yote". Ozu alimpigia kelele. Ghafla Ozu aliruka juu ya gari, Papa akamimina pale risasi nyingi. Ozu aliruka tena kabla na kumuwahi na kuupiga mkono wake risasi, bunduki ikaanguka upande. Papa aliinuka na kujaribu kuirukia tena bunduki yake Ozu akampiga risasi ya kiuno akaanguka chini na kupiga kelele. Ozu alimfuata mpaka pale chini. "Umeua watu wengi sana katika maisha yako, watu wasio na makosa. sasa mimi ninawalipizia wote. Nitakupiga risasi tatu kifuani, kumlipizia ndugu yangu Kofi, na zile zitakazofuata ni kuwalipizia ndugu zangu wana mapinduzi wa Afrika uliowaua", Ozu alimsomea risala. 

"Nisamehe...," kabla hajamaliza Ozu alimpiga risasi zaidi ya kumi. 

Willy na Muteba walipambana vikali sana. Muteba alitumia ujuzi wake wote aliokuwa nao, lakini alimkuta Willy yuko tayari kabisa. Willy alitupa 'machine gun' akachukua bastola. Muteba aling'ang'ania 'machine gun' lakini Willy aliruka hapa na pale kumhangaisha mpaka risasi zikamuishia, hapo ndipo Willy aliporuka mpaka pale Muteba alipokuwa kabla hajachukua silaha nyingine, Muteba alisimama wakaangalia na Willy ana kwa ana. "Wewe ndiye Willy Gamba?" Muteba alimuuliza.

"Ndiyo mimi, na wewe ndiye Muteba Kalonzo?" Willy naye alimuuliza.

"Tete yuko wapi?" Muteba alimuuliza Willy.

"Yupo hapo nje ndani ya gari langu". Willy alimjibu taratibu huku bastola imemlenga Muteba kifuani.

"Umemkamata kwa nguvu?" Muteba alisema.

"Amenitafuta kwa hiari yake. Hana nafasi na watu waovu kama wewe" Willy alimtibua Muteba, jambo hili lilimtia uchungu akapandisha mori. Kama umeme aliruka na kupiga teke bastola ikatoka mikononi mwa Willy. 

"Mwongo..." alipiga kelele. Hapo hapo alichomoa bastola yake nyingine kwa upesi sana na kupiga risasi pale Willy alipokuwa lakini Willy naye alikuwa ameisharuka kabla risasi hazijatua pale. Akiwa ameruka kabla hajatua chini alichomoa bastola yake nyingine akampiga Muteba risasi iliyompata katikati ya paji la uso na kumuua. Willy aliangalia chini akajiviringisha aliposimama akamuona Robert amesimama karibu naye akiwa ameshikilia bastola. 
"Umemuwahi vizuri sana, sikutegemea, mimi nilikuwa tayari tayari", Robert alimweleza Willy.

"Asante sana, mtu huyu alikuwa hatari sana," Willy alijibu. Ozu alikuja anakimbia. 

"Tayari?" aliuliza. Wenzake walimjibu tayari. Wote walitoka pale mbio kwani walitegemea polisi kufika wakati wowote. Walipofika pale Tete alipokuwa ameegesha gari walipanda Willy akasema. "Moja kwa moja SOZIDIME".

Tete ambaye alikuwa anawasubiri kwa wasiwasi sana alifurahi kuwaona wote wamerudi salama. Alitia gari moto na kuondoka kuelekea sehemu za Gombe. "Nimeona gari la Pierre linaelekea mjini", Tete aliwaeleza. 

"Ndiyo hata sisi tumemuona", Willy alimjibu. Tete alienda na kusimamisha gari pale "CINE RAC' "Sasa utatusubiri hapa," Willy alimweleza Tete, wakatelemka wote watatu.

"Robert utatupandisha sisi turuke juu ya michongoma tukiisha ingia ndani tutakufungulia wewe lango", Willy alimweleza Robert. Walienda kwenye uchochoro uliokuwa unatenganisha Cine Rac na ua wa Sozidime. Walipofika pembeni mwa ua huu wa michongoma Robert alimpandisha kwanza Willy ambaye alirukia ndani ya ua wa ofisi hii na kuwa tayari kwa pambano lolote. Kisha Robert alimpandisha Ozu na wote wawili wakawa wametumbukia ndani. Kwa mshangao wao walikuta ile ofisi shwari kabisa na hakukuwa na dalili ya kuwepo mtu. Lakini hata hivyo walikaa tayari tayari na walitembea katika tahadhari kubwa. Robert alizungukia kwenye lango Willy akamfungulia, 

"Inaonekana hakuna mtu hapa lakini wanaweza kuwa wamefanya mtego, hivyo wewe Robert utabaki umejibanza nje, wakati sisi tutakapoingia ndani, kama lolote likitokea unajua la kufanya", Willy alimweleza Robert.

"Sawa", Robert alijibu. Robert alinjongwajongwa na kubana kwenye ukuta wa ile. Willy na Ozu walenda kwenye mlango wa mbele. Willy akatoa funguo zake malaya na kuanza kufungua huku Ozu akiwa tayari tayari analinda kwa lolote. Lakini kinyume na walivyotegemea, walifungua mlango ule bila kupambana na kitu chochote. Waliingia ndani wakarudisha mlango na wakajikuta wako mapokezi ya ile ofisi mahali ambapo Willy alipokuwa amefika.
Ghafla taa zikawaka, na wakajikuta wote wanaangalia ndani ya midomo ya bunduki ya watu wanne waliokuwa wamewalenga huku wamelala chini. 

"Tupeni silaha zenu", walielezwa. Kuona walivyokuwa wamesakamwa walitupa silaha zao. Mmoja wa wale watu alisimama akaanza kuwapekua na kuwanyang'anya silaha zilizobaki. Mara Max akatokea.

"Oh Willy, mbona umekuja namna hii, wafanyabiashara hawavuji ndani ya maofisi ya watu, karibuni", Max alisema huku akitabasamu. "Haya tembeeni", waliamrishwa na mlinzi mmoja aliyekuwa ameshikilia 'machine gun'. Willy na Ozu walijua hapa wasingeweza kuanza lolote ila kufuata amri ili waweze kununua muda, kwani walikuwa wamejiingiza ndani ya mtego wao wenyewe kama wajinga. 

"Lukamba, nenda ukafunge lile lango na kufuli na fikiri watu tulio kuwa tunawangojea wamefika," Maxx alimwamru Lukambo akiwa ameshika silaha yake sawa sawa alifungua mlango na kutoka nje. Willy na Ozu waliongozwa huku wanamfuata Max.

Robert aliona mambo yote yalivyotokea. Hivyo Lukamba alipotoka nje Robert alimvizia. Lukamba akiwa anaenda bila wasiwasi Robert alimnyemelea na alipofika pale langoni Robert alimkaba kabali kwa nyuma na kumuua halafu akamlaza chini. Robert alifungua lile lango akakimbia mpaka pale Tete alipokuwa ameegesha gari. Alitoa kikaratasi kilichokuwa na jina na anuani akampa Tete halafu akamweleza. "Nenda pale kwenye kibanda cha simu kiko hapo kwenye kona ya upande ule wa Cine Rac. Mpigie huyu Umba Kitete ni rafiki yangu, na ni afisa wa C.N.D. mwambie Robert anasema mambo tayari, aje hapa Sozidime na atakukuta wewe na wewe utaingia naye ndani, afanye haraka maana mambo tayari. Yeye anaelewa nilikuwa nimezungumza naye wakati tulipokuacha na Ozu, tukaondoka na Willy saa zile zajioni. Hivi utamkuta yuko tayari, fanya haraka".

"Usiwe na wasiwasi", Tete alijibu, Robert aliweka bastola yake sawa sawa haraka haraka akarudi ndani ya ua wa Sozidime akajifanya yeye ndiye Lukomba. Kwa vile Max na watu wake walikuwa wanajua kuna Willy na Ozu tu, hivyo walipowakamata wale wawili walijua hakuna mtu mwingine. Jambo hili lilimpa faida sana Robert kuingilia ofisi za Sozidime bila kipingamizi kikubwa.

Willy na Ozu waliongozwa mpaka ofisini kwa Fernand ambako Max alifungua ule mlango wa siri, na kuwatelemsha kuelekea chumba cha siri. Jambo hili halikuwashangaza sababu walikuwa na habari nalo kabla. Max aliwaongoza mpaka katika chumba cha siri ambako walimkuta Pierre na Fernand wamekaa wanakunywa kahawa.

"Nimewaleta hawa watu ambao wametupa taabu nyingi sana." Max aliwaambia Fernand na Pierre.

"Ohooo, karibu Willy Gamba pamoja na Kapteni Petit Osei, nashukuru sana kuwaona. Lazima nitoe heko zangu kwenu kwani kazi yenu mmeitekeleza vizuri sana ingawaje hamtaweza kuimaliza kabisa. Kwani hapa ndipo mmefika mwisho wenu," alijigamba Fernand halafu akatoa kicheko cha dharau kisha akaendelea; "Nchi huru za Kiafrika, nchi huru za Kiafrika... zitaweza nini?"

"Haziwezi kamwe," alijibu Pierre.

"Unajua bwana Gamba mimi nasikitika sana kuwaueni vijana shupavu na jasiri kama nyinyi, lakini itabidi nifanye hivyo maana hiyo ni amri kutoka kwa wakubwa zangu. Lakini kabla sijawaueni nitawaeleza kwanini nchi za Kiafrika hazitaweza kamwe kuishinda Afrika Kusini", alinyamaza kidogo kupitisha mate halafu akaendelea.

"Nchi za Kiafrika hazina umoja. Nchi za Kiafrika viongozi wake wengi ni watu wapenda pesa wala siyo viongozi wanaopenda nchi zao kwa dhati, OAU ikipiga kelele Afrika Kusini iwekewe vikwazo vya uchumi na jambo hili likipitishwa kwenye kikao cha viongozi wa nchi huru za Kiafrika, kesho yake viongozi wengine wanatupigia simu na kutuambia tusijali hayo yaliyopitishwa, hiyo ilikuwa ni siasa tu. Uhusiano wetu utaendelea hapo hapo ulipokuwa. Kwa hivyo nchi za Kiafrika zinakosa umoja na hili ndilo tatizo lake kubwa. Kwa mfano utakuta BOSS inasaidia viongozi wengi wa nchi huru za Kiafrika wasiweze kuangushwa. Wewe unafikiri mtu uliyemsaidia namna hiyo ukimuomba msaada wa kukupa siri za OAU atakataa. Kwa taarifa yenu BOSS itasonga milele, na itaendeleza shughuli zake bila shida katika Afrika. Hao wapigania uhuru tutahakikisha tutawateketeza, kiasi mlichotuchafulia sisi hatukijali ni kama mtu aliyejikwaa tu na kuumiza kidole. Lakini akishakiangalia na kukifunga anaendelea na safari yake." Fernand aliangua tena kicheko.

"Lakini ujuwe siku zaja, wapo vijana wanamapinduzi wa Kiafrika ambao watateketeza kabisa udhalimu wa makaburu na Afrika nzima itakuwa huru. Kitu ambacho lazima ujuwe ni kwamba utafika wakati vijana wa Afrika watakuwa wamekandamizwa sana na hawatakubali lazima watafanya mapinduzi makubwa ambayo yataangusha serikali zote za vibaraka, na kuua ukoloni mamboleo na kujenga serikali za kizalendo. Mapambano bado yanaendelea, ushindi ni dhahiri", Willy alizungumza kishujaa kabisa.

"Wapige risasi hawa, wananieleza siasa inayonuka, ambayo sitaki kui..." kabla Fernand hajamaliza kusema, mlango wa hiki chumba ulifunguliwa ghafla na Robert akajitupa ndani bastola mbili mkononi na kuwashambulia walinzi wa Fernand ambao walishituliwa bila kutegemea, hivi hawakuwa tayari kwa tukio. Kule kufunguliwa tu mlango Willy na Ozu waliruka upande mwingine, na kumpa Robert nafasi ya kuwapiga risasi wale walinzi. Bastola za hawa walinzi zilidondoka na moja ikarukia karibu na Willy alipokuwa akaidaka na kumsaidia Robert katika mashambulizi ambayo yalichukua chini ya nusu dakika na kuweza kuwa wameua walinzi wote pamoja na Max. Pierre alikuwa amejeruhiwa sana, Fernand ndiye alikuwa mzima akiwa anatetemeka ovyo. 

"Vijana wa C.N.D. watafika sasa hivi. Tete atakuja nao", Robert alisema huku Willy na Ozu wanamwangalia kwa mshangao mkubwa. Willy alimwendea Fernand akamfunga mikono na miguu na akamweleza, "Huu ndio mwanzo wa kuwasafisha majasusi wa nchi zinazopinga maendeleo ya Muafrika, wewe ndiwe utakuwa mfano". Ozu alimwendea Pierre lakini alikuwa mahututi sana lakini akatambua kuwa angeweza kufa dakika yoyote.

"Muteba, Jean na Papa wamekufa sasa wewe", alimweleza. Willy alifungua mkoba wa Fernand uliokuwa pale kwenye meza, na ndani yake akakuta makaratasi yenye habari za kijasusi zilizonaswa katika nchi nyingi za Kiafrika. "Karatasi hizi ndizo zitakuwa kielelezo", Willy alisema. Mara wakasikia nyayo zinateremka ndazi. Haraka haraka Tete akiwa anaongoza msafara wa watu sita aliingia.

"Oh Willy nilifikiri tutakuta mambo yameshaharibika", Tete alisema akamrukia Willy, akaning'inia shingoni mwake na kumbusu. 

"Kazi na dawa", Ozu aliwatania.


"Kazi imekwisha. Bwana Umba huyu mtu wako. Mfuko huu umejaa karatasi ambazo ni vielelezo. Nyumbani kwangu kuna shahidi mwingine twende ukamchukue. Hadithi kamili nitakueleza baadaye", Robert alimweleza Umba afisa wa juu wa C.N.D.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. Mkuu,aksante sana, Leo umetupa kazi nzuri, umetupa uhondo wa nguvu, aksante sana. Ubarikiwe mkuuuuuuu

    ReplyDelete
  2. Naombeni dhamira na zinazopatikana
    Katika kitabu cha kikosi cha kisasi

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU