KIKOSI CHA KISASI

SURA YA KUMI NAMOJA

USHINDI NI DHAHIRI

V

Huko sehemu za Nsele ambayo ni sehemu inayotumiwa na wakazi wa Kinshasa kwenda kupumzika wakati wa siku za mapumziko, na ambayo iko kando kando ya mto Congo. Jumapili hii palijaa watu. Sehemu hii ambayo iko kilomita 60 kutoka Kinshasa ni sehemu nzuri sana. Katika watu waliokuwa wamefika hapa kulikuwa na kundi la wavulana watatu na wasichana watatu ambao walivutia sana watu wengine kwa jinsi walivyokuwa.

Siku tatu baada ya kusafisha kikundi cha 'WP' Willy na wenzake walikuwa wanapumzika hapa Nsele. Willy akiwa katika nguo za kuogelea alilala kando kando ya bwawa la kuogelea lililoko sehemu hii linaloitwa 'Bassin Olympic' na huku Tete ambaye naye alikuwa katika nguo za kuogelea, alijilaza ubavuni mwake huku akimpapasa kifuani kwa mkono laini wakiota jua. Mara Ozi akiwa ameshikana mikono na Ntumba na Robert akiwa amemshikilia Ebebe kiunoni na wote wakiwa katika nguo za kuogelea walikuja mpaka pale Willy na Tete walipokuwa wamelala. Ozu akiwa amebeba gazeti mkononi. 

"Willy umeshaona gazeti la 'Salongo' leo" Ozu alimuuliza.

"Bado", Willy alijibu. 

"Haya soma habari hizi hapa", Ozu alimuonyesha. Willy alichukua gazeti, yeye na Tete wakaanza kulisoma. Lilikuwa limeandikwa kama ifuatavyo.

"Wapelelezi wa OAU juzi usiku waligundua na kuteketeza maofisi yaliyokuwa yanatumiwa na majasusi wa Shirika la Ujasusi la Afrika Kusini 'BOSS'. Ofisi hizi ambazo zilikuwa mjini hapa zilijidai ni za biashara na kumbe za majasusi zimeteketezwa kabisa na wapelelezi hao. Hili limekuwa onyo kali sana kwa Afrika Kusini kuacha mbinu zake za kishenzi inazotumia katika Afrika huru.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi ya OAU, ambaye naye yuko mjini hapa tokea juzi amezitaka serikali zote za Kiafrika zenye mikataba na uhusiano wowote na Afrika Kusini kuvunja mara moja mikataba hiyo vinginevyo afadhali zijitoe katika umoja wa nchi huru za Kiafrika, ili harakati za Ukombozi wa Kusini mwa Afrika ziweze kupata nguvu kamili. Na huko Algiers Algeria. Umoja wa Chama cha umoja wa vijana wa Afrika (PAYM) ambacho kina makao yake makuu nchini humo, kimeitisha maandamano kwenye ofisi zake zote zilizoko katika nchi mbali mbali za Kiafrika ya kuzitaka nchi za Kiafrika zenye uhusiano wa kiuchumi na Afrika Kusini kuvunja uhusiano na nchi hiyo baada ya kugundulika mbinu zake", gazeti hilo lilieleza. Willy aliweka gazeti kando. 

"Tutaenda wote Dar es Salaam?" Tete alimuulza Willy alipomuona amemaliza kusoma gazeti. Willy aliwaangalia wenzake waliokuwa wamesimama kando wakingojea atoe maelezo yake juu ya habari zilizoandikwa kwenye gazeti hilo lakini akainuka na kumlalia Tete kifuani akamjibu. "Tutaangalia", huku akimbusu.


MWISHO  0784296253

Comments

  1. Asante sana kiongozi kwa hadithi hii.
    Shukrani sana.

    ReplyDelete
  2. Aksante sana Mpiganaji. Tutarajie story gani nyingine?

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU