KIKOSI CHA KISASI

SURA YA KUMI NA MOJA 

USHINDI NI DHAHIRI 

II

Willy na Robert ambao walikuwa wameondoka jioni ile na kuelekea mjini walirudi kiasi cha saa tatu na kumkuta Tete na Ozu wakiwa wameishatengeneza chakula. Willy alikuwa amepitia hotelini kwake ambako alichukua vifaa fulani fulani ambavyo vilikuwa vya lazima katika shughuli ya usiku huo. Pamoja na silaha zaidi alizokuwa amechukua, alichukua na fulana mbili ambazo zilikuwa haziingiwi na risasi. Fulana hizi Willy alikuwa mara kwa mara anazitumia alipokuwa karibu kukabili pambano kali sana. Na mara nyingi zilikuwa zimemsaidia, hivi alikuwa akisafiri nazo mara kwa mara. Fulana hizi zilikuwa ni zawadi alizokuwa amepewa na Mkuu wa kikosi cha Scotland Yard wa huko Uingereza alikokuwa amepelekwa kwa mafunzo ya miezi sita na kujitokeza kuwa mtu aliyefuzu vizuri kuliko watu wote waliokuwa wamepitia kwenye kikosi hicho cha mafunzo. Kwa furaha ya Mkuu wa kikosi hicho alimpa fulana hizo kama zawadi.

Robert alikuwa amemwacha Willy Hoteli kwake akijitayarisha, na yeye akaenda nyumbani kwa rafiki yake yule aliyekuwa Afisa wa juu katika Shirika la Upelelezi la Zaire C.N.D. Alimkuta huyu rafiki yake na wakazungumza vitu vya manufaa kati yao. Akiwa na furaha kubwa baada ya kuwa na mazungumzo yaliyofanikiwa kati yake na huyu rafiki yake alirudi hoteli Memling akampitia Willy na bila kumueleza Willy wapi alikuwa ameenda, walirudi nyumbani. 

"Chakula tayari", Tete aliwaeleza.

"Ooh, safi sana mimi nina njaa sana", Robert alidai.

"Vipi Bwana Kadima mmempa chakula?" Willy aliuliza.

"Tayari kabisa", Ozu alijibu. Walikaa kwenye meza wakala chakula cha jioni ambacho kilikuwa kimepikwa vizuri sana. Wakati wakila Tete alieleza."

"Wakati mmeondoka alikuja msichana mmoja hapa anaitwa Ebebe, alikuwa anamtafuta Robert. Tulimwambia Robert ametoka amsubiri lakini hakutaka, akaondoka akaenda zake. Alionekana amechukia".

..."Shauri yake nitamwona kesho. Rafiki yangu sana, lakini ana wivu mwingi." Robert alieleza.

"Nafikiri alipomkuta Tete anapika alifikiri kuwa amepinduliwa serikali yake ya hapa nyumbani," Willy alitania wote wakacheka. 

"Hasa alipoona mapinduzi yenyewe yamefanywa na msichana chuma namna hii", aliongeza Ozu. Walipomaliza kula walianza kujiandaa. 

"Tunasubiri tukashambulie sehemu hii usiku, ili kama watakuwa wanatusubiri wawe wameshakata tamaa na kuchoka. Unajua mtu wa kawaida tu kuwa katika hali ya tahadhari kwa muda usiopungua masaa manne ni vigumu sana", Willy aliwaeleza.

"Hizo ndiyo saa zenyewe, wengine watakuwa wameanza kusinziasinzia. Hata mimi zamani kabla sijazoea, nilikuwa na ubovu huo", alieleza Ozu.

Willy alitoa fulana zake ndani ya mfuko akaeleza. "Hapa ninazo fulana hizi mbili ambazo haziingiwi risasi. Sasa kati yenu sijui nani atachukua moja,"

"Mpe Robert mimi sina taabu," Ozu aliamua.

"Hapana mpe Ozu. Mimi nina ujuzi wa hali ya juu sana katika karate na kung fu, sitahitaji kabisa fulana hiyo. Na kwa taarifa yenu ni mara chache, natumia silaha, mpaka iwe lazima sana," Robert alieleza. Willy alikubaliana na Robert kwani alikuwa amemuona siku ile walipopambana na akina Mulumba. 

"Ozu chukua hii. Wewe una ujuzi mwingi katika kutumia bunduki hasa hizi kubwa kubwa hivyo naamini utahitaji". Willy alimshauri. 

"Huenda tumpatie dereva wetu." Ozu alisema huku anamwangalia Tete.

"Wacha matani, mimi sina haja nayo", Tete alijibu kwa ukali. 

"Wengi wape," alijibu Ozu na kuichukua ile fulana.

"Sasa ni saa nne twendani tukapumzike lakini saa nane tuwe tumejiweka tayari kwa kuondoka hapa." Willy alishauri. Kila mmoja alienda chumbani kwake, Willy na Tete wakaandamana chumbani kwa Willy. "Tete unajua unachukua mzigo mzito sana usiokuwa kiasi chako," Willy alimweleza Tete.

"Wewe niache, mimi mwenyewe ndiye nimekata shauri na wala sikushawishiwa na mtu yeyote. Tuzungumzie jambo jingine Willy, jambo hili tuliache hivyo lilivyo, mimi nitakwenda pamoja nanyi," Tete alijibu kwa ukali, Willy bado alikuwa hajakuwa na imani kabisa na msichana huyu. Maana yeye Willy huwa hawaamini sana wasichana wenye sura nzuri kwani kila wakati mambo yao hayaeleweki. Lakini hata hivyo aliamua kuyaacha mambo yalivyo aangalie huko mbele ya safari.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU