KIKOMO

SEHEMU YA TATU

Safari yangu ilikuwa safi sana. Nilitumia saa kumi na mbili tu mpaka Mwanza. Ilikuwa saa tano asubuhi nilipoingia Mwanza. Nilikwenda moja kwa moja hadi Hoteli ya Mwanza katika mtaa wa Posta. Niliegesha gari nje na kuchukua mizigo yangu madi Mapokezi ya wageni.

"Habari ya leo ndugu!" 

"Nzuri, tukusaidie nini?"

"Naweza kupata chumba?"

"Bila shaka, vyumba vipo chungu nzima".

Alileta kitabu na kunipa.

"Jaza humo ndani".

Nikajaza Jina Mark Buhulula. Kazi Mfanyabiashara. Anuani S.L.P 3300 Shinyanga: muda wa kukaa siku kama kumi hivi. Nitokako Shinyanga, kwenda Mwanza, nikamaliza kujaza yote haya.

"Nitakupa chumba namba 230 ghorofa ya pili". 

Kisha akamwita mtumishi mmoja.

"Juma njoo hapa".

Juma akafika.

"Mpeleke huyu ndugu chumba namba 230".

Juma akabeba mzigo wangu tukafuatana. Chumba kilikuwa kizuri sana.

"Unataka nini? Aliuliza.

"Hiyo ni asante yako".

"Loo asante sana ndugu. Ukitaka msaada wa aina yoyote ile niambie nitakusaidia".

"Ikibidi nitafanya hivyo".

Nilifungua mizigo yangu na kuiweka vizuri. Chupa aliyonipa Chifu niliifungua. Loo Mlikuwa na vipande vya almasi vinne vizuri sijapata kuona. Hata miye mwenyewe moyo wangu ulipiga haraka haraka. Hivi vipande vinne tu vingeweza kunifanya tajiri maisha yangu yote. Kisha nikapunguza mawazo yangu, nikavirudisha ndani ya chupa na kuviweka mahali pa usalama nikainua simu ya humo chumbani.

"Naweza kupata Dar es Salaam?"

"Namba gani?" Aliuliza Opereta wa kike kwenye simu.

"Dar es Salaam 08381".

"Nitakwita".

Nilijilaza kidogo kitandani. Zilipita dakika kama kumi hivi, kisha simu ikalia. Nikainyanyua haraka.

"09351 Dar es Salaam hapa, nikusaidie nini?"

"Willy hapa, hujambo Maselina?"

"Sijambo, vipi huko?"

"Niko MWanza Hoteli".

"Vizuri, nitakupigia simu baadae ndugu", akakata simu.

Nilionelea nioge kisha nipate chakula cha mchana, halafu nije nilale kidogo, maana nilikuwa bado sijalala. Baada ya chakula nilirudi chumbani na kulala. Niliamshwa na simu mnamo saa kumi hivi.

"Hallo nani?"

"Simu yako", alijibu opereta.

"Hallo Mark hapa".

"Subiri, zungumza na Chifu".

"Mark habari za saa hizi?"

"Nzuri, nilikuwa nimelala".

Mnamo saa moja hivi nenda forodhani, kuna boti moja inawasili toka Ukerewe. Ndani ya boti hiyo kuna mtu mmoja aitwaye Makungu Majula ana habari za maana sana ambazo huenda zikafumbua tatizo letu bila matatizo makubwa. Atakuwa amevaa jamba-koti moja la kaki na kofia nyeusi. Umwonapo nenda mpokee halafu taja neno Inter na yeye atajibu Inter halafu mtazungumza.

"Nitafanya hivyo, asante", nilijibu.

Nilipiga simu mapokezi kuwaomba waniletee chupa moja ya Dimple pamoja na sprite kama tano hivi na barafu. Hiki kinywaji kingeweza kunisukuma hadi wakati wa kwenda forodhani kumpokea Makungu.

Mnamo saa kumi na mbili unusu niliondoka kuelekea ziwani. Mwendo wa kutoka Mwanza Hoteli mpaka forodhani ni kama dakika kumi tu hivi. Saa moja kasorobo ilinikuta tayari niko forodhani, kulikuwa na watu wengi ambao nao walikuwa wamekuja kuwalaki wageni wao. Nilipoangalia ziwani niliona boti ikija kwa mbali kidogo.

"Bana jambo?" Mhindi mmoja alinisalimia.

"Sijambo ndugu".

"Hii boti toka Kerewe? Mimi iko kuja goja toto yangu, toka kwa rafiki yake Nansio."

"Na mimi nasubiri rafiki yangu kutoka huko huko".

Boti sasa ilikuwa imekaribia mita mia tano hivi. Mara tu tukashtukia kishindo kikubwa mno, na watu wote kuanza kukimbia huku na huku. Mara hiyo boti ikashika moto na vipande kurushwa huku na huku. Watu wengi walikuwa bado na mshtuko na walikuwa hata bado hawajaelewa nini kimetokea. Polisi wanamaji waliingia mara moja ndani ya boti yao na kuelekea huko kwenye boti kuokoa maisha ya wote ambao walikuwa wangali hai. Mimi nilikata shauri kutulia na kuangalia mwisho wake.

"Toto yangu, toto yangu", huyo Mhindi aliyekuwa anazungumza nami alilia. Kisha akachomoka kuelekea ziwani. Bahati nilimwahi nikamshika.

"Tulia kwanza huoni watu wanashughulika kuokoa abiria waliopata ajali? Ukijitosa na wewe majini utakuwa umefanya nini".

"Toto yangu peke yake, kama iko kufa na mimi iko kufa tu potelea mbali Mungu iko".

Wakati huo Polisi wengi walikuwa wamefika na kusaidia kutuliza watu waliokuwa wamekuja kupokea wageni wao kwani vilio vilikuwa vimevuma kote forodhani-kwa jinsi boti ilivyokuwa imeteketea hata mimi niliamini kwamba hakuna mtu hata mmoja aliyekuwa amepona.

Mara moyo wangu ukashituka na kuanza kuhisi kuwa hii hakikuwa ajali. Ajali imetokea kwa sababu Majula alikuwa ndani ya boti na alikuwa na habari za maana za kunieleza mdomo kwa mdomo. Kama mambo ni hayo basi tayari walikuwa wameishanijua.

Niliangaza macho huku na huku ili niweze kuona kama kuna mtu yeyote anayeniangalia. Nikakuta hakuna nilimtoroka huyo Mhindi aliyekuwa sasa amekaa chini huku akilia na kujiingiza katika kundi kubwa, ambalo lilikuwa limeshafika kushuhudia ajali hii mbaya.

Boti za polisi na mashua za wananchi zilikuwa bado zinaokota Maiti za abiria. Mara tuliona boti ya polisi ikija na mtu mmoja, ambaye walikuwa wamemlaza ndani ya boti. Walipofika ufukoni nilisogea kuangalia na nikaona ni msichana ambaye naye alikuwa abiria ndani ya boti ya ajali. Alikuwa bado hai. Polisi Inspekta aliyekuwa karibu yangu aliwauliza ndani ya boti, "Wangapi wamepona?"

"Mpaka sasa nafikiri ni huyu tu".

"Mfanyieni huduma ya kwanza".

"Ndiyo, Afande".

"Sajenti Kibonye?" Inspekta aliita.

"Afande".

"Rudisha watu nyuma, huyu mtu aweze kufanyiwa huduma. Tulianza kusukumwa huku na huku. Sura ya huyu msichana ilikuwa tayari kichwani mwangu. Sikuwa na haja ya kukaa zaidi, nikaonelea niondoke maana giza lilikuwa linazidi. Nilikata shauri kurudi moja kwa moja mpaka hotelini kwangu. Niliingia ndani ya chumba cha chakula kwa ajili ya mlo wa jioni.

"Habari za jioni?" nilimsalimia mmoja wa watumishi wa hapo ndani.

"Nzuri tu, sijui utakula nini?"

"Samaki wapo?"

"Wapo ngege, ningu na hata kambale wapo ukiwataka".

"Nipe ngege na viazi".

"Asante".

"Niletee na CocaCola".

Wakati nangoja chakula nikaanza kuwa na mawazo chungu nzima. Majula alikuwa ameishauawa. Bila shaka alifahamika kuwa angekuja kuleta habari ambazo ningemtia mtu hatiani. Nilikua sijaelewa huyu Majula alikuwa anafanya kazi gani na wala uhusiano wake na kazi yetu nilikuwa sijui. Nikakata shauri kumuuliza Chifu.

"Mtu mmoja kafanya watu chungu nzima kufa, kweli binadamu ni katili, nilifikiri sana. Hawa watu walikuwa wameamua kuzima wasifahamike ili waweze kuendelea na shughuli zao za kudhorotesha uchumi wa nchi. Lakini siku za mwizi ni arobaini. Waswahili husema.

Bado nikiwa na mawazo mengi nililetewa chakula. Nilikula kwa kujilazimisha, maana chakula kilikuwa hakiendi kabisa. baada ya hapo nilipanda chumbani kwangu. Nilipofungua mlango na kuwasha taa, mara nikajua mliwahi kuwa na mtu. Sehemu yote ilikuwa imechunguzwa kifundi sana. Hakuna kitu hata kimoja kilichokuwa kimechukuliwa: Hii inathibitisha kuwa tayari waliwakuwa wameshanifahamu, kwa hiyo ilikuwa hatari kubwa sana kwangu. Nilifungua chumba changu nikatelemka chini. Nilienda moja kwa moja mpaka Posta ambako niliingia katika kibanda cha simu.

"Halo, Opereta, naomba Dar es Salaam nambari 07911."

"Nambari yako ngapi?"

"Nambari yangu ni Mwanza 0233".

"Subiri nitakuita".

Nilisubiri kiasi cha dakika tano hivi halafu simu ikaita.

"Halo, wewe ndiye uliyeita Dar es Salaam?"

"Ndiyo".

"Haya weka shilingi sita".

Nikaweka shilingi sita.

"Sasa zungumza".

"Halo, mzee yupo?"

"Ndiyo, yupo nani wewe?" Sauti nyororo ya kisichana iliuliza.

"Mwambie Mark"

"Halo kijana vipi?"

Sauti ya Chifu ilikuwa na mshtuko kidogo.

"Mambo si mazuri. Yule mtu wetu kapata ajali kabla sijaonana naye. Boti aliyokuwa akisafiri nayo nafikiri imetegewa bomu imelipuka na kupasuka ovyo ovyo. Watu wote wamekufa ila msichana mmoja tu. Mambo naona sasa yanaanza kufurahisha".

"Sasa unasemaje?"

Nilihisi kwamba yote niliyomwelezea hakuyajali.

"Mipango ya operesheni yote naigeuza. Nikijipeleka kama nilivyopanga basi najichimbia kaburi. Inanibidi sasa nijihadhari. Nitahitaji msaada fulani fulani zaidi kutoka ofisi kuu.

"Vizuri, endelea unavyoona ni sawa, maana opereshani yote iko mikononi mwako. Kila unachohitaji utapata, kwaheri".

"Kwaheri, asante".

Nilipomaliza kupiga simu nilionelea huu ndiyo muda wa kwenda kumuona Buluba. Nambari ya nyumba ilikuwa 32 Kirumba. Niliondoka moja kwa moja kwa miguu kuelekea Kirumba na huku mawazo yangu yakinizunguka sana. Nilitafuta hiyo nyumba kwa bidii sana lakini kwa sababu nambari zenyewe hazikuwa na mpango ilinibidi niulize. Nilikwenda kwenye duka moja la Mwarabu kuuliza.

"Habari ndugu".

"Nzuri".

"Nyumba nambari 32 inaweza kuwa wapi?"

"Nasunguka pande ile takuta nambari 32".

"Asante".

Nilifuata maelezo ya Mwarabu na mara moja nikaiona. Nilibisha hodi mlangoni lakini hakukuwa na jibu. Taa ilikuwa ikiwaka ndani. Nilizungusha kitasa mlango ukafunguka, kumbe ulikuwa wazi. Huenda alikuwa ameenda dukani, nikaingia nimsubiri.

Nyumba ilikuwa na sebule nzuri yenye saa kubwa sana ukutani. Nayo ilionyesha saa moja usiku, wakati nilipokuwa naingia. Taa ya chumba cha karibu nayo ilikuwa inawaka. Katika hali hii nikafikiria huenda amejilaza kitandani na usingizi ukamzidi. Nikaamua nimwangalie humo chumbani.

Lo! Nilipofungua chumba nilipata tishio jingine Matayo Buluba alikuwa ananing'inia darini amekufa! Jasho lilinitoka. nikashikwa na bumbuwazi kubwa. Jack Mbwileamekufa, Majulanaye! Sasa Buluba.

Wakati nakata shauri kuondoka nikasikia mtu anafungua mlango wa sebuleni. Nilijibanza kwenye ukuta karibu na mlango wa chumba cha kulala.

"Lazima utakuwa umeangusha humo chumbani", sauti moja ilisema.

"Huenda, lakini sidhani", alijibu mwingine.

"Fanya haraka, tafuta haraka haraka, anaweza akaja mtu akatukuta humu," sauti ya kwanza ilionya.

"Hapa sebuleni hakuna. Lo, sijui nisipoiona hiyo karatasi nitakwenda wapi!"

Kumbe walikuwa wanatafuta karatasi. Mara moja nami nikatazama huku na huku nikakiona kijikaratasi chini ya uvungu wa kitanda. Mara mlango wa sebuleni ukafunguliwa. Pandikizi la mtu likaingia, lakini bado lilikuwa halijaniona. Macho yake yalienda moja kwa moja kwenye hicho kikaratasi chini ya uvungu. Alipotaka kuinama ili akiokote kufumba na kufumbua alikuwa amelala chini kwa vile nilimpiga teke la uso bila ya yeye kutegemea.

Bastola aliyokuwa ameshika ilimtoka mikononi nami nikaruka kasi kuikota na kumwelekezea mwenzake ambaye alikuwa amepigwa butwaa. Kwa wepesi wangu nilifyatua risasi na kumpiga mwenziwe mkono wa kulia ambao ulikuwa umeshikilia bastola. Nayo ikadondoka bila ya yeye kutaka. Mwenziwe alipojaribu kujitahidi kunyanyuka hakua na la kufanya isipokuwa kusalimu amri yangu sasa. 

"Kwanini mmemuua Matayo?" Niliwauliza.

"Sijui", hilo pandikizi lilijibu kwa hofu.

Hasira zikanipanda huku nimeshikilia bastola.

"Naona tunataniana. Mumemuua rafiki yangu na halafu mnafanya masihara, mtanitambua sasa". 

Kabla sijafanya chochote nikakikumbuka kile kikaratasi ambacho nilikuwa nacho mikononi. Huku nimeshikilia bastola tayari, nilikisoma hicho kikaratasi. Kiliandikwa.

Ndugu Busy, fika Songwe klabu kabla ya saa sita usiku bila ya kukosa. Ukikosa usije ukanilaumu. Lonely.

"Huyu Busy ni nani?" Nilimuuliza yule pandikizi.

"Simjui, Tom ndiye alikuwa akimjua. Mimi huwa namsikia tu".

"Mwongo, sema ukweli la sivyo utamfuata mwenzio sasa hivi". 

Wakati huo mwenzake niliyempiga risasi alikuwa akitapatapa kwa maumivu ya mkono.

"Kweli mimi simjui ila namsikia tu, ndiye anafanya mipango yote ya magendo ya almasi yeye ni kama wakala na.

Kabla hajamaliza mlango ulifunguliwa. Mimi mara moja nikaruka upande kama umeme. Kisu kilichokuwa kimetumwa kuniua kwa bahati nikamwingia pandikizi kifuani na mtu aliyekitupa akakimbia. Nilipomwangalia pandikizi alikuwa ameanguka chini huku damu ikimtoka kasi kifuani. Hakuonyesha matumaini ya kuepa kifo iwapo angebakia muda mfupi ufuatao. 

Ingawa nilijikaza sana lakini nilianza kuona mahali pale hapakuwa na usalama wowotw kwangu. niliamua mara moja kuwapiga wote risasi mbili na kuondoka upesi iwezenavyo kabla jeshi la maharamia halijanivamia. Kisha nikakimbilia nje ili nirudi hotelini nilikofikia.

Sijui ni muda gani nilitumia lakini nilikuwa nikienda kasi mno. Sikuwa na haja yoyote ya kutafuta gari. Nilifika hotelini huku nikitweta na kutoa jasho jingi. Nilipotulia kidogo nikaoga na kubadilisha mavazi. Niliongeza risasi zaidi za bastola yangu kwa vile nilijua sasa maadui zangu ni wengi mno na itanilazimu mara kwa mara kupambana bila ya kutegemea. Funguo za chumba nilizichukua kwani nilikuwa wasije wakajua ni wapi nalala.

Sehemu hii ya mji wa Mwanza kuna kampuni ambayo unaweza muda wowote kukodi gari na ukaliendesha mwenyewe. Nikafanya hivyo na nikaamua kwenda Songwa Club kadri ya hicho kikaratasi kilivyosema. 

Songwa Club iko kilomita kama kumi kutoka Maganzo, ama ni kama kilomita nne kutoka njiapanda iendayo Mwadui.

ITAENDELEA 0784296253


Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU