KIKOMO

SEHEMU YA KWANZA

Nilifika ofisini kwangu yapata saa mbili unusu. Gari langu lilikuwa limeniletea matatizo kidogo njiani. Katibu wangu nilimkuta tayari keshafika saa nyingi kama kawaida yake.

"Habari ya leo. Mbona umechelewa hivi?"

"Salama tu. Gari langu binti nafikiri niliuze maana siku hizi linanihunia sana".

"Lazima likuhunie, nalo unafikiri halichoki, maana linakata mitaa ya Dar es Salaam yote kila siku". Tukacheka.

"Kuna habari zozote?"

"Katibu wa Chifu alipiga simu na kuacha maagizo kuwa uende ukamuone Chifu mnamo saa tano na nusu, habari nyingine ndiyo mpigie Didi simu".

"Asante Luiza", nikaingia ofisi kwangu. Niliangalia majalada yaliyokuwa yakisubiri niyashughulikie kabla sijaenda kumuona Chifu hapo saa tano na nusu. Kufika saa nne nilikuwa nimeishayapitia majalada yote muhimu na kulikuwa na mawili kati yake ambayo ilinibidi niende nayo kwa Chifu kusudi niweze kuyazungumzia kabla sijaendelea mbele na matatizo yake.

Nilikumbuka kuwa ilikuwa inanibidi nimpigie simu Didi. Nilibonyeza simu kumuita Katibu wangu.

"Luiza nipigie simu kwa Didi".

"Sawa".

Muda si mrefu simu yangu ikalia.

"Huyo yuko kwenye simu".

"Halo, habari?"

"Nzuri, hujambo?"

"Sijambo".

"Nimekupigia simu asubuhi lakini ulikuwa bado hujafika, maana nyiye wazee hamchelewi".

"We, acha kunikoga nchi hii haina wazee wanaofanya hivyo. Ukifanya hivyo utaachishwa kazi".

Alicheka nami nikacheka.

"Je wasemaje?"

"Nina shida kidogo nilitaka kukueleza kuwa utokapo ofisini saa nane na nusu nipitie. Kuna jambo la maana sana ninalotaka kukueleza na kulifanya".

"Sawa mama. Hapana taabu. Mimi saa nane na dakika thelathini na tano juu ya alama napiga breki hapo".

"Nitashukru sana, kwaheri".

Nikakata simu. Nilikaa nikifikiria jinsi ya kumwelezea Chifu matatizo yaliyokuwa katika majalada haya mawili niliyokuwa nimeyaweka pembeni. Niliona nichukue notisi kidogo maana Chifu yeye huhitaji maelezo kamili. Saa tano na dakika ishirini na tano nilimwendea katibu wangu.

"Naenda kwa Chifu, chukua habari yoyote".

"saa sita na nusu naomba kwenda kumpeleka mdogo wangu hospitali, anaumwa".

"Kama nitakuwa nimerudi, lakini kama sijarudi usiondoke, kama kawaida Luiza". 

"Najua bosi, usiwe na wasiwasi".

Ofisi ya Chifu haikuwa mbali sana na yangu kwani tulikuwa kwenye ghorofa moja. Nilipofika nilifungua mlango wa chumba cha Katibu wa Mkurugenzi wa upelelezi.

"Halo Maselina, hujambo".

"Sijambo, Willy siku hizi hatugongani?"

"Kazi nyingi, na vile vile wewe unaadimika kama shilingi ya mwambo!"

"Nhuu, usinitanie wewe ndiwe..." Kabla hajamaliza hiyo sentesi yake mlango wa Chifu ulifunguliwa na Chifu mwenyewe akatoa uso ulioonekana wa ukali sana.

"Waheshimiwa wamo ndani wanakusubiri wewe, na wewe unacheza hapa".

"Samahani Chifu", nilijibu kwa aibu.

"Maselina, hatutaki simu mpaka iwe ya lazima sana. Chifu alisema kwa sauti nzito.

Nilipoingia kwenye ofisi ya Chifu nilishangaa sana. Mimi nilitegemea huu kuwa moja ya mikutano yetu ya kawaida, lakini nilishangaa kuwaona Mkuu wa Polisi na maafisa wa kizungu ambao sikuwafahamu. Pamoja na hao walikuwepo maofisa kadhaa wa polisi. Kwenye meza ya mkutano kulikuwa kumebaki kiti kimoja ambacho nilihisi ni changu. Baada ya kuwasalimia wote nilienda nikaa kwenye kiti hicho.

"Nafikiri wote tunafahamiana?" Chifu aliuliza.

Wote tulitingisha vichwa.

"Nasikitika kukueleza kuwa huu si kama mikutano yetu ya kawaida, mkutano huu una jambo lake la pekee na ndiyo sababu unawaona maafisa hawa wageni wanaotoka katika Shirika la polisi Duniani (Interpol) Wote wamekuja kutusaidia kutatua matatizo ya uhalifu ambayo yanatushinda na ambayo kwa kweli yanahusu dunia nzima".

Nikaweka majalada yangu pembeni.

"Unamkumbuka Jack Mbwile?"

"Ndiyo namkumbuka. Nimewahi kufanya naye kazi, wakati nilipokuwa nimetumwa kwenye kazi moja huko Ziwa Tanganyika. Katika Idara yetu ya upelelezi ndiye alikuwa nambari moja katika kuogelea. Aliweza kuogelea kutoka Visiwa vya Unguja hadi pwani ya Tanzania Bara".

"Basi Jack amekutwa amekufa huko Mwanza kando kando ya Ziwa Victoria mahali paitwapo Mwanza South", Chifu alieleza.

"Loo! Alikuwa anafanya nini huko?" Nilimuuliza haraka.

"Marehemu miezi miwili iliyopita tulimshirikisha katika Idara ya Polisi kusaidia upelelezi wa wizi na uuzaji wa magendo ya almasi. Yapata miezi kama minne hivi tuliombwa na polisi kushughulikia jambo hili ambalo sasa lilikuwa limefikia kiwango kibaya, kwani ripoti iliyotoka kwenye machimbo ya almasi ya Mwadui inasema ya kwamba kwa muda wa miezi sita iliyopita madini yaliyo tayari kusafirishwa yamepungua kwa asilimia arobaini na tano kuliko kawaida. Hii haitokani na kupungua kwa madini, ila inatokana na wizi.

"Idara ya polisi imejishughulisha sana na upelelezi wa wizi huu, lakini wameweza kushika wezi wadogo wadogo ambao hawawezi kuleta tofauti yote hii. Kwa hiyo wametuomba msaada juu ya jambo hili. Papo hapo tulimtaka Jack akiwa huko Mwanza atusaidie. Kwa bahati mbaya habari nilizozipata asubuhi hii ni kwamba Jack amekutwa amekufa. Polisi wameeleza kwamba amekufa maji. Upelelezi zaidi bado unaendelea juu ya kifo hiki. Mimi naamini kuwa Jack hakufa maji, atakuwa ameuawa na pengine amehusika na habari hizi za wizi wa almasi."

"Tokea aende Mwanza ni muda gani sasa?" Nilihoji.

"Yapata mwezi unusu".

"Alikuwa bado hajatoa ripoti yoyote?"

"Bado. Kwa jinsi mambo yalivyo ndiyo sababu Waziri pamoja na maafisa hawa wa Usalama wamefika hapa. Wamekuja kutafuta mbinu zaidi za kulitatua jambo hili. Waziri anaitaka Idara hii itoe msaada wa hali ya juu ili kulitatua jambo hili ambalo linagusa uchumi wa Taifa letu. Nimekuita hapa uelewe uzito wa jambo hili na uchukue dhima ya Taifa katika kupeleleza.

"Idara yetu imelipa tatizo hili nafasi ya mbele katika kazi zote na wewe utaziacha kazi zako zote zingine na kuchukua kazi hii. Utafanya kazi bega kwa bega na Polisi na kwa sababu wao wamekuwa wakishughulika na jambo hili kwa muda mrefu watakupa kila msaada wa maelezo yatakayokusaidia katika jambo hili. Tumekata shauri kukomesha kabisa wizi huu.

"Mpaka sasa kuna fununu ya watu fulani fulani ambao wamesambaa Afrika Mashariki nzima ambao wanaweza kuwa shina la tatizo hili. Lakini namna ya kuweza kuhakikisha na kuwatia mbaroni imekuwa inatushinda. Jambo ninalotaka kuongeza kidogo tu ni kwamba serikali inaamua kila njia ifanyike jambo hili likomeshwe. Kwa wakati huu ambao nchi yetu inahitaji pesa za kigeni sana, ni dhahiri kuwa serikali hairidhiki kuona jambo hili linaendelea. Kwa hiyo, kijana, umetwishwa mzigo mkubwa na nchi yako na ni imani yangu kuwa utafanikiwa. Hatutavumilia kuona watu wachache wanadhoofisha uchumi wa nchi nzima. Mungu akusaidie".

Maneno haya yalinichoma mno maini. Neno moja tu ndilo niliweza kujibu.

"Amina".

"Habari za maendeleo yako nitazipata kutoka kwa Mkurugenzi wako", Waziri alimalizia.

"Kama nikirudi hai", nilijibu huku nikitabasamu.

Tuliagana naye kisha mie nikaondoka.

Ofisini kwa katibu wa Chifu nilimkuta katibu wangu.

"Unafanya nini huku nami nimekwambia ukae ofisini?"

"Kuna mtu anakuhitaji kwa haraka eti ni mvuvi kutoka Mwanza".

"Mvuvi ananitafutia nini mimi?"

"Nitajuaje, yeye anasema ni lazima akuone".

Twende basi."

"Ndiyo hata kwaheri hamna?" Maselina alilalamika.

"Loo, kichwa changu kimevurugika, kwaheri, ngoja nikimbie. Chifu akifungua mlango na kuniona hapa tena atanifukuza kazi. Wote tulicheka na kuondoka. Tulipofika ofisini kwangu nilimkuta huyo aliyeitwa mvuvi amekaa kwenye viti vya wageni.

"Karibu ndani".

Akaingia.

"Keti chini".

"Asante".

"Habari za Mwanza".

"Nzuri tu".

"Nikusaidie nini?"

"Mimi naitwa Matayo Buluba, kazi yangu ni mvuvi". Kisha akatoa picha mfukoni mwake akanipa. Katika picha hiyoalionekana yeye akiwa na marehemu Jack Mbwile.

"Unamfahamu huyo?"

"Ndiyo, ni Jack Mbwile".

"Sawa, wewe ni Willy Gamba, siyo?"     

"Ndiyo, umenifahamu wapi?"

"Ndugu huyu nasikitika kusema sasa ni marehemu!"

"Nimesikia".

Nilipojibu tu hivi akaonyesha sura ya kushangaa!. 

"Nimepata habari, usijali nimejuaje, wewe endelea na maelezo yako.

"Marehemu tulionana yapata kama mwezi hivi, na alikuwa mtu mzuri sijapata kuona. Nilikuwa nakaa naye huko Kirumba. Tulionana siku moja Ziwani, na katika mazungumzo tukaelewana. Yeye alikuwa anapenda sana kuogelea na mimi ni mwogeleaji mashuhuri Mwanza . Tumewahi kufanya mashindano ya kuogelea na kwa mara mbili hivi ameshinda. Kisha katika mazungumzo na kutaka kujua anakaa wapi ndipo aliponieleza kuwa alikuwa amefika siku chache tu zilizopita na kwamba alifikia Hoteli ya Mwanza. Mwanza alijia shughuli za kibiashara.

"Wewe wakati huo ulikuwa unaishi wapi?"

"Nilikuwa naishi Kirumba, na nilikuwa naishi katika nyumba yangu mwenyewe, yenye vyumba vinne".

"Ulikuwa umeoa wakati huo?"

"Nilikuwa nimetaliki na nilikuwa bado sijazaa na huyo mke. Na kwa vile nilikuwa sina mpangaji nyumbani mwangu nikakata shauri Jack Mbwile aje tuketi wote, naye akakubali. Alikuwa mtu ambaye unaweza kumzoea mara moja tu".

Alinyamaza kidogo na kuniangalia. Alipoona sina la kusema akaendelea.

"Kila siku alikuwa anaodoka kufanya shughuli zake na miye nikienda zangu kwenye shghuli za uvuvi. Tukionana jioni alikuwa akinichukua na kwenda kutembea kidogo kwenye moja baridi moja moto". Alitabasamu kidogo kisha akaendelea. "Ila siku zingine alikuwa harudi mpaka asubuhi. Leo ni Ijumaa siyo?"

"Ndiyo".

"Sasa. Jumatatu tangu atoke asubuhi hakurudi mpaka tulipoonana Jumanne saa kumi wakati aliponifuata ziwani nilipokuwa nikisuka mitego yangu. Baada ya kusalimiana aliniomba niache kazi hiyo kidogo twende nyumbani. Tulipofika nyumbani aliniambia kuwa usiku wa Jumane hiyo alikuwa na mkutano mkubwa sana ila ulikuwa na hatari. Pia akanieleza kuwa jambo lolote likimpata nije Dar es Salaam. Aliniandikia jina la mtaa na jengo na nije nimuone mtu aitwaye Willy Gamba. Alisema kuwa nikimuonyesha huyo mtu picha tuliyopiga wote atanipokea vizuri kwani ni ndugu yake. Kisha alinipa na bahasha hii".

Alitoa hiyo bahasha na kunipa. Kisha akaendelea.

"Bahasha hii ilikuwa nikupe kama jambo limemtokea, kama angerudi angeichukua mwenyewe. aliniachia shilingi elfu moja za kusafiria ikibidi",

"Wewe ulimshauri nini?"

"Mimi nilimshauri asiende ikiwa ameona kuna hatari katika mkutano huo. Lakini aliniambia ni lazima aende kulikuwa na jambo la lazima sana katika mkutano huo. Nilimweleza kuwa ingefaa twende wote, lakini vile vile alikataa. Kisha tuliagana akaondoka. Usiku mzima sikulala kwa kumsubiri na hakurudi Jumatano yote hakuonekana, Usiku wa Jumatano pia sikuweza kulala.

"Jana mnamo saa nne hivi nilikwenda ziwani kuwangoja wavuvi wenzangu waliokuwa wamekwenda kuvua. Huko ndiko nilikopata habari hizi za huzuni. Wavuvi wa huko Mwanza South walinieleza kuwa wamemkuta rafiki yangu amekufa maji mnamo saa kumi na mbili na nusu asubuhi. Nilishangazwa sana nikakumbuka maneno yake. Badala ya kwenda polisi nikakata shauri kuja kwako moja kwa moja".

"Wavuvi walinieleza kuwa polisi walikuwa wameishachukua mwili na kuupeleka hospitali na upelelezi wa kifo umeanza. Saa nane nikakodi taksi na kuja huku, nimefika leo asubuhi." Alinyamaza huku machozi yakimtoka.

"Loo, jambo la kuhuzunisha sana! Huyu ni rafiki yangu sana. Asante sana kwa habari zote, mimi nitakuja Mwanza na nitakuja kukuona".

Niliandika taarifa yote na nikamshukru sana. Nilimpa kiasi cha fedha kumsaidia nauli na masumbufu ya njiani.

"Sawa, unatarajia kurudi lini?" nilimuuliza.

"Narudi leo kwa basi".

"Mimi nitafika kesho".

"Njoo kesho kutwa Kirumba Na. 32 ndiko nyumbani kwangu. Haya kwaheri, nataka nirudi mapema huenda Polisi wananitafuta".

"Wakati unafika Mwanza na mimi nitakuwa nimefika, usiseme lolote kwa polisi mpaka tumeonana. Vitu vyake unavyo?"

"Nimeviacha Mwanza. Akili yangu ilikuwa imevurugika kwa hiyo nilikuwa tu nataka nikuone kwanza ndipo roho yangu itulie".

"Basi viweke mpaka nifike. Kwaheri".

Tulishikana mikono tukaagana. Alipoondoka nikafungua hiyo bahasha, na ndani mlikuwa na karatasi kubwa lakini imeandikwa neno moja tu. ELUNGATA.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. Aksante sana Nyakasageni. Nakushauri ilikuweka taarifa sawa, uwe unaanza kwa kutambuisha kitabu na mtunzina ikibidi mwaka wa kuandika kitabu hicho.mfano:-

    jina la kitabu:KIKOMO
    Jina la Mwandishi: ELVIS MUSIBA ni mfanotu
    Mwka wa uandishi:

    Hii itasaidia hata wasoma ambao hawajui kazi za willy gamba na joramu kiango kuwatambua waandishi halisi wa fasihi hizo na kuwaenzi.

    Ila aksante kwa simulizi, usituache hewani sana

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU