KIKOMO

SEHEMU YA TISA

Mlango ulifunguliwa wakati mimi nikiwa tayari kwa lolote litakalotokea na kwa mshangao wangu Patrick aliingia ndani. Niliruka hapo nilipokuwa. 

"Patrick!".

"Willy". 

Tukakumbatiana. 

"Na nyinyi nanyi! Mnapendana hivyo?" Amanda alisema.

"Usijali," nilimjibu. 

"Yule mdogo wa daktari yuko wapi?" Amanda aliuliza kwa woga.

"Yupo atakuja," Patrick alijibu.

"Patrick nipe habari kwa ufupi maana nimekuwa nje ya hii shughuli kwa masaa kwa hiyo niko nyuma sana na habari." 

"Nafikiri Amanda kishakueleza jinsi tulivyokupata."

"Ndiyo, kanieleza." 

"Huko Dar es Salaam nilipata habari kama saa kumi na moja unusu hivi Chifu alinieleza kwa ufupi juu ya habari zote na maendeleo ya shughuli hii. Mambo mengine yote alimweleza Kamishna Mkuu wa Polisi ashughulikie kama vile kuwatia nguvuni hao majambazi uliokuwa unawakisia. Mimi aliniambia niwe kiwanja cha ndege saa kumi na mbili kamili tayari kwa kuondoka.

"Wakati nikiwa kiwanja cha ndege nikapata habari toka kwa Chifu kuwa Kamishna Mkuu wa Polisi ndugu Oswald Mengi kapata safari ya ghafla. Maana baada ya kuongea na Chifu alipata habari kuwa mkewe aliyekuwa anasafiri toka Arusha alikuwa amepata ajali kati ya Arusha na Moshi na inasemekana kuwa huenda amekufa kwa jinsi hii ameruhusiwa kwenda kumuona mkewe kwa hiyo sasa mambo yote yako mikononi mwa Chifu na Mkurugenzi wa Upelelezi, Mkuu wa Polisi ameitwa arudi haraka maana jambo hili limefikia hatua ya juu haliwezi kushughulikiwa na maafisa wa chini wa polisi.

"Baada ya kupata habari hizi nilipanda ndege ya jeshi na mnamo saa moja unusu nilikuwa Maganzo na ndipo nikaonana na Amanda. Mambo mengine yote nafikiri kesha kueleza."

"Nipe habari za Bantu Bar".

"Baada ya kukuleta hapa nilionelea niwafuate kwa kufuatana na habari nilizopewa na Amanda. Huyo mdogo wake daktari akasema twende naye nami nikaona bora. Tulipofika hapo tulipeleleza uwezekano wa kuwepo huo mkutano lakini hakukuwa na dalili. Tulingoja sana lakini hatukuonana dalili yoyote. Tukajua kwamba lazima kulikuwa na mabadiliko ya mipango."

"Mlingoja mpaka saa ngapi?". 

"Mpaka saa tano unusu hivi. Mimi nilionelea nirudi nikamuacha Wilfed Mbogo ambaye ndiye huyo mdogo wake daktari aendelee na uchunguzi na apatapo habari yoyote aje kutueleza kabla sijaja nikaonelea nimpigie simu Chifu, nimweleze tumefikia wapi na mambo yalivyo. Nilipiga nyumbani kwake nikapata habari kuwa amerudi ofisini. Hii ilinishangaza. Nikampigia ofisini. 

"Nilipompata nikamweleza mambo yalivyo mpaka dakika hii. Kisha nikamuuliza kwanini alikuwa ofisini mpaka dakika hiyo. Akanieleza kuwa alikuwa amepata habari zingine za kusikitisha toka Mwadui leo jioni. Habari hizi ni kuwa umetokea wizi wa ajabu, maana almasi zote zilizokuwa tayari kusafirishwa kwenda kwenye masoko yake zimeibiwa!"

"Zimeibiwa? Saa ngapi?"

"Anasema ni kati ya saa kumi na saa mbili usiku huu!"

"Kwa hiyo inaonekana majambazi hawa wameamua kuchukua kwa mara ya mwisho na kukimbia."

"Hata mimi nafikiri hivyo hivyo."

"Nafikiri ndiyo sababu Khasimu alinieleza kwamba nifungashe vitu." Amanda alinieleza.

"Nadhani walikuwa wamefanya mpango wa kuziiba hizo almas halafu watoroke nchi za nje."

"Hiyo ni kweli kabisa na vile vile Chifu kanieleza kuwa wale watu uliompigia ripoti watiwe ndani chini ya usalama anashangaa kupata habari kuwa wote hawaonekani na wala haijulikani wako wapi. Mbinu za kila aina zimetumiwa na idara ya upelelezi, Polisi lakini hawaonekani kabisa".

"Ahaa. Sasa naanza kupata mwanga mkubwa. Hii ina maana kuwa wote wameondoka kuja Maganzo kugawana hizi almasi halafu kila mtu aangalie usalama wake, baada ya kuona karibu watashikwa. Hii ikiwa ni kweli lazima wataonana mahali fulani hapa mjini au wameshaonana au wanaonana saa hizi".

"Vile vile kumbukeni kuwa Khasimu alisema kwenye simu anamtegemea Mzee leo saa nne." Amanda alitukumbusha.

"Kwa hiyo hii inazidi kudhihirisha kubuni kwetu. Na kama hata Mzee wao yuko hapa hapa bila ya shaka inabidi tujitoe mhanga na tulikamate hili kundi kabla halijasambaa. Au unasemaje Patrick?"

"Itabidi tuwe tayari kupambana na Elungata. Maana nahisi huyu Elungata ambaye ni Joel tu aliyewahi kusikia sauti yake, huenda ndiye wanamwita Mzee. Kwa hiyo ndiye kichwa". 

"Bila shaka, lazima tupambane naye. Lililopo sasa ni kufanya mpango wa namna ya kuwasaka watu hawa",

"Mimi ninavyofikiria, lazima tumkamate Khasimu na Pweke kwanza. Hawa watu wawili ndio watakaotupeleka hata kwenye kichwa".

"Sawa Patrick, Khasimu alikuwa amemchukua Amanda kati ya saa sita sasa ni saa ngapi?"

"Saa saba na nusu." Amanda alijibu.

"Kwa hiyo atakuwa amesharudi nyumbani halafu atakuwa amemkuta Amanda. Hii itamfanya acheleweshe mipango yake kwani hatajua Amanda yuko wapi. Na kwa vile anampenda sana, atajaribu kumtafuta na hii itatupa sisi nafasi ya kuweza kumpata", 

"Milimweleza ndugu Mbogo awe hapa kabla ya saa nane unusu, ikiwa hatakuwa amefika ina maana kuwa jambo fulani limemtokea na itabidi kumfuata kwa hiyo mimi naonelea tujilaze kwa muda huu mchache wa saa moja unaweza kutusaidia kupoteza usingizi mpaka hiyo saa nane unusu"

"Sawa Patrick nafikiri nyinyi watu wawili mnahitaji sana huo usingizi hasa Amanda ambaye hakuzoea kukaa macho hadi saa hizi".

"Na wewe pia lazima ukumbuke bado unaumwa kwa hiyo wote hatuna budi kupata usingizi kabla ya mapambano dhidi ya hawa majambazi hayajaanza" Amanda alisema.

Tulizima taa tukajilaza mimi kichwa kilikuwa bado kinanigonga sana lakini ilinibidi kujitahidi niweze kufanya mapambano ya mwisho kwa hawa majambazo, Mambo haya yalinikera sana kuwa sikuweza kupata usingizi mnamo saa nane na dakika ishirini mlango wa chumba uligongwa, bastola mkononi, Patrick alienda kuufungua.

"Uko salama", aliuliza huku akiwasha taa.

"Salama".

Sisi wote tukaamka na kukaa.

"Itabidi tuondoke hapa mara moja wanatutafuta", alisema Wilfred Mbogo.

"Wamejuaje?" Niliuliza.

"Nitawaeleza njiani watafika hapa wakati wowote". 

Tulichukua vitu vyetu na mara moja tukawa tunaondoka. Patrick alinipa bastola mbili zenye kiwambo cha kunyamazisha sauti.

"Mimi nafikiri tubane tuwasubiri. Tukiwa na bahati ya kushika mmoja wao anaweza kutupeleka mpaka kwa huyo wanaemuita mzee", nilishauri.

"Sawa, lakini kama ni hivyo itabidi Amanda atusubiri mahali fulani kwani panaweza kutokea mapigano makubwa sana", Patrick alishauri.

"Hata kidogo na mimi lazima niwe katika hayo mapambano mpaka nione mwisho wake. Nikifa kwa ajili ya Joel nitakuwa nimekufa kifo cha fahari, Niko nanyi mpaka mwisho mtake msitake".

"Haya mama ni mapenzi yako", nilimjibu.

Kabla hata Wilfred hajaanza kutueleza gari likatokea kwa kasi lakini lilikuwa bado mbali kidogo. Nafikiri ni hao, Wilfred alipiga kelele.

"Wote kwenye majani", niliamrisha.

Karibu na nyumba kando ya barabara kulikuwa na majani marefu basi tulijificha humo gari lilikuja kasi lilipofika karibu na hiyo nyumba likafunga breki na watu wote watano wakatoka na bastola zikiwa mikononi. 

"Ila Willy na Amanda wanahitajiwa kwanza". Mmoja wao aliwaeleza wenzie.

Kila mmoja akachukua sehemu yake tayari kwa mashambulizi, watatu walibaki nje wawili wakaingia ndani. Wote tulikuwa tumelala karibu karibu. "Patrick unaweza kufungua buti ya hiyo gari?" Nilimuuliza kwa sauti ya kunong'ona.

"Naweza bila ya wasiwasi".

"Mimi nataka niingie kwenye buti ndani nikiwa na bahati wanaweza kunifikisha kwenye watu wenyewe ninaowatafuta".

"Wazo zuri," alijibu mwenzangu. "Hata tukisema tuwaue hawa tutakuwa hatujafanya lolote. Naona twende wote ndani ya buti la hilo gari,  Amanda na Wilfred watatusubiri kwa Wilfred".

"Najua mkifanya hivyo safari yenu ni mpaka Shinyanga sasa hivi hakuna muda wa kuelezana niliyosikia. Tuonane Shinyanga Relwe nyumba nambari 13. Mimi na Amanda tutasubiri hapo", Wilfred alitoa rai.

"Oke vizuri," nilikubali.

Gari lilikuwa karibu sana na tulipokuwa, "Nendeni mimi nitawalinda ikiwa watawaona," Wilfred alisema. 

Tulinyata na kwa sababu mawazo yao yote yalikuwa ni ndani ya nyumba, tuliweza kuingia ndani ya buti ya kuwashitua. Buti la gari kama alivyosema Patrick lilikuwa kubwa sana, mlikuwa na taili moja na supana. Hewa iliyokuwamo ilikuwa kidogo lakini ingeweza kututosha.

"Wameisha ondoka ndani ya chumba hamna mtu wala kitu," tulisikia mmoja wao akisema, "Twendeni zetu tukatoe habari mara moja, huenda ana wazo au habari za mahali walipo."

Waliingia ndani ya gari na safari ikaanza. Walielekea barabara ya Maganzo. Mara kwa mara tulifungua mlango wa buti kuingiza hewa na kuangalia wapi tulipokuwa. Walipofika Maganzo hawakusimama bali waliendelea moja kwa moja kwenye barabara inayoelekea Shinyanga. Kwa vile walikuwa wakienda kasi sana. Patrick na mimi niliweza kunong'onezana juu ya mpango wetu na tulimuomba Mungu atusaidie.

Kama tulivyokuwa tumebuni gari liliingia Shinyanga mjinina kuelekea barabara iendayo nyumba za watu wa hali ya juu. Kisha gari likasimama na kuzima injini. Mlango wa geti ulifungwa na dereva aliamurishwa kulisogeza mpaka mbele kidogo. Punde milango ikafungunguliwa wakatoka nje.

""Twendeni ndani, wanawasubiri kwa hamu sana", kiongozi wao alisema.

Tuliwangoja waende kwanza. Hatmaye tukainua buti ili kuona kama hakukuwa na mtu. Tulipohakikisha kuwa ni salama, nikashika kifuniko cha buti ili Patrick atoke kwanza kisha nami nikafuata. Bahati mbaya nikagusa debe, likapiga kelele. Mtu wao mmoja aliyekuwa kwenye mlango wa mbele ya hiyo nyumba akaja kuangalia. Sisi tukabana kwenye sehemu ya seng'enge ya ua. Alipokaribia Patrick alikuwa ameshamzunguka. Akamnyemelea, akamkata 'karate' ya shingo na kufa hapo hapo. Hatmaye akanigeukia na kuniamrisha.

"Nenda sasa, lakini jihadhari sana".

"Hakuna taabu", nilimpa imani. 

Nilipitia mlango wa mbele, nikaingia ndani. Nilisikia sauti zinatoka kwa mbali kwenye chumba cha ndani. Nilipotaka kuingia mlango ukafunguliwa, nikabana. Akatoka mtu mmoja na bastola mkononi. Kwa vile hamkuwa na taa kwenye ukumbi, hakuniona.Nikamlisha risasi na alipoanguka nikamvuta. Nikamtupa kwenye magunia yaliyokuwa karibu na hapo.

Nilifungua mlango wa nyumba taratibu.Taa zilikuwa zinawaka lakini hakukuwemo mtu. Nilisikia sauti zikitokea kwenye chumba cha pili yake. Nikazima taa za chumba hiki cha kwanza nikaenda mpaka kwenye mlango wa chumba cha pili. Nikasikia sauti ya kiaskali ikifoka.

"Kwa nini mlirudi. Nendeni mkawatafute mpaka muwapate. La asivyo msirudi watu kumi na wawili hamuwezi kushindwa na watu wawili"

"Tutajaribu" Mwingine alijibu.

"Hakuna kujaribu" 

Nilihisi hiyo sauti ya Khasimu maana ilikuwa ya kiaskari hasa.

"Khasimu lazima uende nao mumtafute Willy na Umuue pamoja na mwenziwe" sauti hii moja iliamuru.

"Ndiyo Mzee" Khasimu alijibu kwa sauti ya woga.

"Twendeni" walijihimiza.

Mlango wa chumba nilichokuwemo ukafunguliwa 

"Nani alizima taa ?" Khasimu aliuliza.

"Sijui, huenda Saidi" alijibu mmoja wao.

"Washa" 

Taa haikuwaka. Nilikuwa nimetoa globu yake. Wakati huo nilikuwa nimebana nyumba ya mlango.

"Hamna globu" 

"Nini?"

"Hamna globu" 

"Angalieni huenda Willy tayarai yupo hapa" Khasimu alitahadharisha.

Kundi lote lilikuwa humo chumbani na wote walikuwa bado hawajaniona. Vilele hawakuwa wanategemea, hivi hawakuwa tayari. Kwa hiyo nikachukua nafasi ya kumjibu.

"Ndiyo tayari niko hapa Elungata." 

"Nikaachia risasi toka kwenye bastola zangu mbili na kuwaua wote, maana wote walishikwa na bumbuwazi.

"Njooni,njooni ndani tumeingiliwa. Willy ndani, tumeingiliwa Willy yuko ndani, mkamateni." Sauti ya kutisha ilisikika.

Nilirukia chumba cha pili. mlikuwa hamna mtu tena kulikuwa na mlango unaoeleka chumba kingine. Nilirudi nyuma bastola ikiwa mkononi. Nikaruka nikaupiga teke na kuingia ndani huku nikiviringika sakafuni. Hamna mtu! Niliposimama tu. Pweke alikuwa tayari amesimama mlangoni na bastola mkononi. Kwa vyovyote vile angeniwahi.

"Weka bastola chini" alihamru.

"Mpelee sebule ile. Mikono juu" Nikaweka mikono juu

"huna ujanja tena!" 

Nilipofika sebuleni nikashangaa kumuona Patrick naye amekamatwa amefungwa kwenye kiti na huku damu zikimtoka hovyo. nikajua kwamba tumekwisha.

"He, He unashangaa kumuona mwenzio Patrick? Mtanikoma" hiyo sauti ya kutisha ilisema, "Willy Gamba, huu ndiyo mwisho wako. Wengi wamejaribu wameshindwa. Wewe umejaribu sana, na kwa hiyo ninakupongeza."

"Sina haja ya kupongezwa na wewe". 

"Wewe ulijaribu kuingilia himaya ya Elungata, aliyoijenga kwa miaka mingi. Je, Ungeweza?" 

Nikasikia sauti zinajibu "Asingeweza!" nikajua ya kwamba majambazi wenziwe walikuwa tayari wamewasili na wote walikuwa hapa Khasimu tu ndiye alikuwa amekufa.

"Leo, Gamba, ni siku ya furaha sana kwangu na vijana wangu. Siku ambayo nimeweza kuichukulia Serikali kiasi cha Almasi inayotoka kwa mwaka mzima. Ni utajiri ulioje! na wakati huo huo Gamba unauawa mbele ya macho yangu nilifikiri kwamba baada ya leo nitaacha shughuli hii. Lakini sasa nitaendelea, maana baada ya kusikia umekufa hakuna hatakayethubutu tena."

"Una kichaa, hujui kuwa wananchi wa nchi hii hawatakata tamaa bali wataendelea kupambana nawe na kundi lako kwa ujasiri na ari zaidi, ili mradi kulinda uchumi wa nchi yao. Hawatakata tamaa kupambana na mtu juha kama wewe. Wengi wataendelea kujitoa mhanga mpaka siku watakayoweza kukuweka mbaroni. Wamenyonywa na wakoloni na sasa wamekataa kuonewa tena. Wakoloni wenyewe wanawaogopa wananchi wa nchi hii. Hawataki kuonewa wala kunyonywa tena sembuse wewe kibaraka chao. La hasha wananchi watakumaliza, na siku hiyo watakugawanya vipande."

"Ha, ha, ha! wewe ndiye mwenye kichaa nini kizuri kuliko pesa? utajiri. Ha ha ha, pesa inanunua kila kitu. hawa wananchi unaowasema hii pesa itawanunua na himaya yangu itakaa milele."

"Wananchi wa nchi hii wanajali utu na kulinda uhuru wao, hawajali fedha. Hao wanaojali fedha ndiyo majuha kama wewe na hao tutawapiga vita na kuwamaliza kama tulivyommaliza mkoloni"

Mpaka dakika hii nilikuwa nasikia sauti tu yeye alikuwa haonekani.

"Kabla hamjaniua nawahakikishia kwamba Elungata na wenzio akina Johnstone MWita, Mashaka Athumani, Samweli Gichuki na Tom Omondili, Pweke na bibi yako Tausi, hujuma za wananchi zinawasubiri".

"Piga magoti mbwa wee!" Pweke aliamuru.

"Kwa kheri Willy Gamba pamoja na rafikiyo Patric. Tangulieni ahera. Elungata anawatakieni maisha mema huko. Mnalipia matendo yenu ya kuniingilia!" Pweke alitoa upanga mkali. Mara akatokea mtu mwingine naye na upanga mkali. akasimama nyuma ya Patrick.

"Nikisema moja mbili tatu mnawachoma moyoni kwa pamoja mmesikia?" Elungata alisema kwa sauti ya ghadhabu.

"Ndiyo Mzee" walijibu kwa pamoja.

Haya moja mbili ta...

ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. Mkuu nyakasageni, aksante sana. siamini macho yangu, kasi yako ni nzuri sana, natamani uendelee hivihivi hadi iishe. Nakupa hongera mkuu

    ReplyDelete
  2. Tengeneza website ili watu walipie kusoma kitabu chote mtandaoni

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU