KIKOMO

SEHEMU YA KUMI

Kabla hajamaliza hiyo tatu taa zikazimika. Kufumba na kufumbua nikamrukia huyo aliyekuwa tayari kumchoma Patrick, Pweke alikuwa amenikosa, maana baada ya kuruka tu nikasikia Pweke akiguna.

"Aaa nakufa!"

"Washenzi" Sauti ya Elungata ilisikika.

Huyu mtu niliyekuwa nimemrukia kwa woga aliangukia Upanga huku akitoa kelele.

"Mama wee"

Taa ziliwaka, nikamuona Wilfred Mbogo aliyekuwa sasa ameshaingia chumbani akanitupia bastola, yeye akabaki na bunduki.

"Nilinde nimfungue Patrick," nilimwamrisha.

"Hamna tabu" nilichukua upanga wa Pweke nikakatakata kamba alizokuwa amefungwa Patrick.

"Asante sana Wilfred."

Patrick alishukuru huku bado hana maumivu mengi.

"Amanda yupo nje tumuwahi" Wilfred alinong'oneza kila mtu bastola mkononi, tukatoka nje kwa mapambano na kundi la Elungata.

"Nyumba hii ina milango mitano ya kutokea nje sasa sijui Elungata na wenziwe watatokea mlango gani." alieleza Patric huku akituonyesha mahali ilipo.

"Wewe Wilfred tokea mlango wa uani. Patrick mlango wa pembeni na mimi nitatokea mlango wa mbele" 

Wilfred alipiga risasi mbili. na hapo hapo tukaona taa zinazimika kwa upande niliotokea niliruka chini na kujivingilisha, risasi zilipigwa lakini zilinikosa. Nilisikia mlio wa bunduki ya Wilfred tena.

Taa zikawaka. Nikawaona watu wawili kabla hawajafyatua risasi zao, mimi nikawawahi. Upande wa Patrick nikasikia bastola inalia. Baada ya muda kidogo gari likatoka mbio.

"Wanakimbia hao" nilisikia sauti ya Amanda.

niliachia risasi lakini gari likawa linaenda tu.

"Elungata na wenziwe wawili wamekimbia" PatricK alieleza.

"Kwa hiyo watatu wamekufa yule msichana yuko wapi?" niliuliza.

"Hata mimi sijui"

"Mtazame ndani" 

"Ok" 

Nilisikia mlio wa bunduki upande wa Wilfred na nikasikia msichana akilia.

"Niache. Niache haa haa usiniue" 

"Usimuue" nilipiga kelele nikijua ni tausi.

Wilfred. Amanda na Tausi walijitokeza na kisha Patrick.

"Elungata na wenziwe wamekimbia na almasi zote" Tausi alipiga kelele.

"Huna haja nazo sasa.Uhalifu wako leo umefika kikomo"

"Mimi ndiye niliyekuwa opareta wa umeme. Unaonaje?" Amanda alijidai.

"Alaa mimi nilikuwa nashangaa sana, hizi taa zilikuwa zinazimishwa na kuwashwa na nani. Binti umefanya kazi nzuri sana na kweli una nidhamu."

"Mara tukasikia mlio wa gari za polisi 999"

"Tumeegesha gari mbele ya pale barabarani" Amanda alisema.

Haya twendeni tusije tukakutwa na Polisi. Muda wa kuonana na polisi bado.

Tuliingia ndani ya gari, Amanda akanipa ufunguo wote watano tukaingia ndani. Safari kituo cha polisi.

"Mmejuaje huku?" nilimuuliza Wilfred.

"Mlipotoka tu walikuwa wamemwacha mmoja wao basi nikamvizia nikamtwanga halafu tukamlazimisha atulete huku nikamtuma Amanda akachukue hilo gari ambalo ni la kaka yangu tukawafuata. Tulijua tu kuwa mtakuwa katika taabu maana yule mtu alitueleza jinsi hapo mahali panavyolindwa. Basi tukaja pamoja na msaada na robo ya ushujaa wa Amanda ambaye aliweza kupenya mpaka kwenye swichi kuu ya mtambo mkubwa wa kuwasha na kuzimisha umeme".

"Mungu si Athuman", Patrick alisema. Tukawa tumeingia kituo cha polisi. Tulimnyanyua Tausi na kumpeleka kaunta.

"Ofisa wa zamu yuko wapi?"

"Yuko ndani", alijibu Koplo mmoja wa kaunta.

Tulipofika ndani nikamkuta Inspekta wa zamu. Nikatoa kitambulisho changu.

"Mweke huyu mama ndani mpaka utakapopata amri nyingine, Nkuu wa mkoa wa Polisi yuko hapa Shinyanga?"

"Ndiyo yupo."

"Mpigie nyumbani kwake". 

Ilikuwa sasa yapata saa kumi na moja asubuhi.

"Hallo", aliita Inspekta.

"Kuna ndugu wa Idara ya Upelelezi, Ndugu Willy Gamba anataka kuzungumza nawe".

"Hallo, Willy Gamba hapa".

"Habari gani?" aliamkia huku sauti ikitetemeka.

"Jambo la kwanza funga barabara zote gari lolote lisiweze kuingia wala kutoka Shinyanga sasa hivi, usichelewe hata dakika moja, na uwaeleze Mwanza na Geita washike kila gari linaloingia toka Shinyanga sasa hivi na wangoje amri nyingine".

"Sawa, asante sana".

"Pili kuna nyumba moja huko Ushirika, Polisi wa 999 wameenda huko, tafadhali wakae hapo hapo mpaka amri nyingine itakapotoka. Wewe tuonane saa moja hapa Kituo cha Polisi".

"Sawa ndugu".

Kisha nilichukua simu nikapiga kwa Chifu. Wakati nangojea simu nikashauri Amanda akapumzike.

"Hata mimi naona hivyo", Patrick alisema.

"Kazi uliyoifanya inatosha, Amanda", niliongezea.

Aliniangalia kwa jicho la mahaba sana.

"Nitakuona tena Willy?".

"Bila ya shaka. Si uko likizo? Basi nenda kashike chumba Shinyanga Hoteli, pumzika mimi nitakukuta hapo".

"Sema sisi", Patrick alitania.

Wote tukacheka.

"Haya, nitasubiri kwa hamu kubwa. Mungu awasaidieni mumkamate Elungata".

"Siku za mwizi ni arobani, nafikiri karibu siku zake zitatimia", Wilfred alisema.

"Nafikiri Wilfred ampeleke halafu aturudie sisi hapa", Patrick alishauri.

"Sawa, Wilfred mpeleke".

Wilfred na Amanda wakaondoka. Inspekta akamshika Tausi mkono ili kumpeleka rumande.

"Mimi mtanifanya nini?" Tausi aliuliza.

"Sisi hatutakufanya lolote, ila wananchi ambao umekuwa unawadhulumu watajua la kukufanya. Sisi tutakupeleka mikononi mwao. Lazima ujuwe kuwa uhalifu haulipi", nilimjibu.

Niliinua simu. Inspekta akamvuta Tausi na kumpeleka rumande.

"Halo Willy hapa".

"Unasemaje?" Chifu aliuliza.

Nilimweleza maendeleo yote mpaka dakika hiyo.

"Kazi nzuri sana", alijibu.

"Tunakuomba uchukue ndege na ufikie haraka hapa Shinyanga bila kuchelewa".

"Kwanini?".

"Njoo kuna mambo mengine ambayo sitaweza kukueleza. Nataka uje uyaone mwenyewe kwa macho".

"Sasa ni saa kumi na mbili kasoro robo. Saa tatu nitakuwa hapo. Tuonane Tanganyika Hoteli."

"Asante sana".

Nikaweka simu.

"Anakuja?" Patrick aliuliza.

"Ndiyo, anakuja".

"Kwanini umemwita?" Patrick aliuliza zaidi kwa kushangaa.

"Na yeye aje apambane na Elungata, tumechoka na sisi".

Wote tukacheka lakini nikajua jibu langu halikumridhisha Patrick.

"Sasa tufanye nini?"

"Tumungoje Wilfred. Yeye ana rafiki hapa na tunaweza, sasa tunaweza kwenda kuoga, tukapumzika kidogo, saa moja tuwe hapa kuonana na Mkuu wa Polisi wa Mkoa".

Mara Wilfred akatokea huku jasho likimtoka.

"Mbona jasho linakutoka hivi?" nilimuuliza.

"Hee bwana, kuna makubwa tena, watu watatu wamekutwa wamekufa ndani ya lile gari alilotoroka nalo Elungata!".

"Upande gani?"

"Karibu na kituo cha mabasi. Ina maana watu wamekufa?"

"Si waliotoroka na Elungata walikuwa wawili na yeye wa tatu?" Patrick alihoji.

"Si kitu cha kushangaza. Polisi wametambua moja wapo za maiti kuwa ni maiti ya Mkuu wa Polisi wa Mwadui."
Hii haikunishangaza sana ingawaje Patrick alionekana na mshangao.

"Tena wameuawa kwa kupigwa risasi kifuani", alimalizia.

"Hii ina maana Elungata amekata shauri kuwarusha wenziwe. Sasa kabaki peke yake na mali yote", nilisema.

Niliingia ndani mpaka ofisini kwa Inspekta.

"Tafuta kama kuna gari lolote lililoibiwa mjini hapa yaani kama kuna mtu amepotelewa na gari lake".

"Sawa ndugu".

"Sisi tunatoka tutarudi hapa saa moja."

Tuliondoka kuelekea kwa rafiki yake Wilfred. Tulioga na kupata chai. Ilipofika saa moja tukaanza safari ya kurudi Polisi. Tulipofika huko nikaenda moja kwa moja mpaka ofisini kwa Inspekta.

"Umepata habari yoyote?" Nilimuuliza.

"Ulipoondoka tu nilituma magari ya polisi 999 matatu lakini sikupata taarifa yoyote ya kuibiwa gari".

"Vizuri".

Nilitoka na kuwafuata akina Patrick ambao walikuwa ndani ya gari.

"Inspekta anasema hakuna gari lolote lililoibiwa".

"Ina maana kuwa Elungata bado yuko Shinyanga kama hakuondoka kwa miguu, jambo ambalo haliwezekani", alisema Patrick.

"Sawa kabisa, hata mimi nafikiri Elungata yuko hapa hapa mjini.

Mara likanijia wazo, moyo wangu ukapiga upesi upesi. Nikaona nifanye kama mawazo yangu yanavyonituma.

"Vipi mbona umeduwaa?", Wilfred aliniuliza.

"Nilikuwa nafikiri Wilfred, asante sana kwa shughuli yote uliyofanya".

Nilitoa kibeti changu, nikatoa fedha.

"Chukua hizi shilingi elfu tatu, iwe nauli yako ya kwenda Dar es Salaam".

"Niende Dar es Salaam kufanya nini?" alidakia kwa kushangaa.

"Fika Dar es salaam. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Umwone Mkuu wa Polisi wa Tanzania, tarehe kumi na tano mwezi huu. Utakuta habari zako zote huko".

"Habari gani?".

"Utazijua wakati huo. Ni lazima ujivune, maana jina lako litakuwa kwenye vitabu vya mashujaa wa Tanzania kwa sababu umepigana kiume, kuyaangusha haya majambazi".

"Lakini mbona bado hatujamkamata Elungata?".

"Hiyo tuachie sisi. Kazi iliyobaki ni ndogo sana, kwa kusema ukweli imekwisha. Soma gazeti la keshokutwa na utashangaa".

"Haya kwaheri. Mungu akipenda tutaonana".

Tuliagana huku machozi yakitulengalenga. Wilfred aliondoka na gari.

"Ulishafanya mipango au vipi?" Patrick aliuliza.

"Nikirudi tu Dar es salaam sina budi kufanya mpango, kazi aliyofanya lazima impatie maslahi fulani.

"Sawa, hakika huyu kijana kafanya kazi kama mmoja wetu. Kusema kweli anastahili sifa na tuzo. Twende zetu tukatafute hoteli ya kulala". 

"Itabidi tukae hoteli mbali mbali".

"Tupite Shinya Hoteli tuone kana kuna nafasi, halafu twende Butiama. Tukipata nafasi Shinyanga wewe utalala hapo", Patrick alisema huku akitabasamu.

"Kwanini?"

"Amanda yuko huko".

Wote tukacheka.

"Si lazima".

Tukacheka tena.

"Hapana iko sababu, kama nafasi ipo Shinyanga Hoteli wewe utakaa hapo. Utajua baadaye kwa nini".

"Sawa, wewe ndiye bosi".

Wakati tunataka kuondoka tu Mkuu wa Polisi wa Mkoa akafika na gari.

"Umechelewa sana, sasa karibu saa mbili kasorobo", nilimwambia.

"Nilikuwa nachunguza mambo yalivyokwenda. Toka saa zile hakuna gari lililotoka Shinyanga. Magari yote yaliyoingia yamekaguliwa vizuri kabisa. Jambo la kusikitisha tu ni kwamba nimepata habari za mauaji ya Mkuu wa Polisi wa Mwadui".

"Hata sisi tumesikitishwa sana".

"Tunajaribu hivi sasa kutambua maiti zingine zilizokuwemo ndani ya gari".

"Fanyeni hivyo".

"Nimepata simu toka Dar es Salaam kuwa Mkuu wa Polisi atafika hapa mnamo saa tatu".

"Vizuri, lakini sasa tunaomba gari moja", nilimwambia.

"Bila ya wasiwasi chukueni".

"Ukipata habari zozote tuwekee, tutakuja kuulizia".

"Mimi sitatoka, niko hapa hapa namsubiri Mkuu wa Polisi".

Tukaondoka mpaka Shinyanga Hoteli.

"Vyumba vipo?" niliuliza.

"Vipo".

"Hebu nipe kitabu cha wageni niandike".

Nilipewa kitabu. Nikaangalia majina yote yaliyokuwemo. Jina la Amanda lilikuwa chini kabisa, chumba nambari tisa. "Patrick njoo uchague chumba".

Akaangalia majina yote.

"Nachagua chumba nambari kumi, lakini usilie wivu, wewe mwenyewe unayataka".

Tukacheka. Baada ya hapo tukaelekea Butiama Hoteli.

"Kuna vyumba vya kulala?| 

"Kimebaki kimoja tu chenye vitanda viwili".

"Sawa, nipe kitabu".

Alinipa kitabu, nikaanza kuangalia. Mara moyo wangu ukaruka kidogo. Jasho likanitoka, nikajikaza mshangao wangu usionekane. Kisha nikajaza kitabu kama ilivyohitajika.

"Mna mizigo?" aliuliza mpokezi wageni.

"Tutaleta".

"Haya, vizuri".

Ilikuwa yapata saa mbili na nusu sasa.

"Twende tukapate chakula cha asubuhi Tanganyika Hoteli wakati tunangoja Chifu afike," nilimwambia Patrick.

"Sawa, hata mimi nasikia njaa sana. umesema jambo la maana sana.

Tulienda zetu Tanganyika Hoteli tukaagiza chakula. Chakula kikaja, tukala kimya kimya, maana kila mtu alikuwa na njaa.

"Lo, mnakula kama kwamba mnangombana na chakula", Chifu alitushtua.

Chifu na Mkuu wa Polisi walikuwa wameingia bila ya kuwaona kwa jinsi tulivyokuwa tunakishughulikia chakula kikamilifu.

"Lo, nyuso zenu vipi, mbona kama mmeraruriwa na chui", Chifu alitania kama kawaida yake.

"Kuna binti mmoja ana kucha huyo, afadhali ya Chui," nilitania.

Tuliinuka na kuwavutia viti.

"Shikamoo", tulisalimu kwa pamoja.

"Marahaba", wote wakajibu kwa pamoja.

Nilimwita mhudumu wa hoteli awahudumie. 

"Nasikia mliweka ulinzi gari lisiingie wala kutoka, mbona kiwanja cha ndege mlisahau? Hamfikirii kuwa mtu angeweza kutoroka kwa kupitia njia hiyo?". aliuliza Mkuu wa Polisi.

"Sijui", Mkuu wa Polisi wa Mkoa", nilimjibu.

"willy, huwezi kumjibu Inspekta Mkuu hivyo!" Chifu alinikanya.

"Samahani mzee, nafikiri akili yangu imevurugika sana.

"Kuna zaidi mpaka sasa, kuliko kifo cha Mkuu wa Polisi wa Mwadui?" Mkuu wa Polisi aliuliza.

"Hapana zaidi", nilijibu.

"Sasa mmetuitia nini? Elungata mmeshamshika?" Chifu alifoka kwa sauti ya chini chini.

"Kukujibu maswali yako mawili kwa pamoja bado hatujamshika, tumekuita uje kutusaidia.

"Willy, tusitaniane. Unadhani".

"Basi Chifu, sidhani kama kawaitia hilo. Hata mimi hajaniambia. Nafikiri tungoje, atatueleza anavyofikiri yeye", Patrick aliingilia.

Chifu alisonya kwa hasira, lakini hakunishtusha, maana ndivyo alivyo. Hujiwa na hasira mara moja na kupoa hasa afikiriapo kwamba unajaribu kutaniana na huku yeye akiwa na maana kazi. Tulimalizia kula chakula tukiwa kimya. Tulipomaliza kula na kulipa, nikasimama.

"Sasa twende kwanza hotelini tukazungumze vizuri, hapa si mahali pa kuzungumzia kazi ila mahali pa kula".

"Ndiyo sababu ukawa matata?" Chifu alisema akitabasamu.

Tulipofika Mkuu wa Polisi akasema. "Mimi nafikiria twende tukaelezane kwenye Kituo cha Polisi". 

"Sisi siyo Polisi, kama unataka kuchukua maelezo kwenye karatasi za polisi ni..."

"Willy, nilikwambia nini? Mbona unakosa nidhamu!" Chifu alionya tena.

"Kweli, samahani nasikitika sana. Nafikiri sijalala vizuri siku nyingi. Kichwa changu bado hakifanyi kazi sawaswa".

"Basi twende zetu huko hotelini kwake anakokusema." Mkuu wa Polisi alisema.

"Mna gari?" niliwauliza.

"Tulikuja na taksi kutoka kiwanja cha ndege, tukairuhusu iondoke baada ya kufika hapa".

Patrick aliwafungulia milango ya gari. Niliendesha mpaka Butiama Hoteli. Tulitelemka tukaingia hotelini. Kufika tu mapokezi akanidakia.

"Mizigo iko wapo, kama huna mizigo hupandi juu!".

Nikatoa kitambulisho changu. 

Akanipa funguo huku akitetemeka.

"Orofa ya kwanza kiko mkono wa kulia".

Tulipoanza kupanda ngazi tu nikatoa bastola yangu na Patrick naye bila ya kuchelewa akatoa bastola yake, Chifu na Inspekta Mkuu wakatazamana bila ya kusema lolote na kumeza mate.

Tulipofika orofa ya kwanza nikaangalia vyumba. Chumba nilichokuwa nakitafuta kilikuwa upande wa kushoto. Nilielekea upande huo nao wakanifuata. Nilipofika karibu na chumba nilichokuwa nakitafuta, nikamuonyesha Patrick ishara ya kuwakinga Chifu na Inspekta Mkuu iwapo kutatokea taabu yoyote. Nilipowaangalia Inspekta Mkuu akatoa kitambaa na kuanza kufuta jasho. Nilipokuwa sawasawa na mlango nikarudi nyuma kwenye ukuta bastola mkononi. Nikaruka na kuupiga mlango kwa magoti yote mawili. Mlango ukafunguka nikaangukia ndani.

"Usisogee popote, kaa kama ulivyo," nilimwamrisha na huku nimemlenga bastola, "Patrick walete wazee ndani".

Patrick akiwa na bastola mkononi aliwangiza Chifu na Inspekta Mkuu ndani. Wote walipoingia wakashtuka, wakashikwa na bumbuwazi.

"Oswald Mengi umefika huku lini?" Inspekta Mkuu aliuliza kwa mshangao. 

Kabla hajajibu nikasema, "Onaneni na Oswald Mengi Elius Elungata Kamishna Mkuu wa Polisi na mkuu wa Majambazi wa wizi wa almasi".

"Mwongo, mwongo ananisingizia ," alipiga kelele huku akitetemeka kwa woga.

Chifu, Patrick na Inspekta Mkuu walikuwa bado katika mshangao.

"Chifu, nilikuita kusudi uje ujionee mwenyewe jinsi baadhi ya viongozi wetu walivyo waovu. Ni jambo la kusikitisha sana kufahamu kuwa Kamishna Mkuu wa Polisi ambaye anapaswa kuupiga vita ujambazi ndiye Mkuu wa majambazi".

"Mimi sielewi hata kidogo", Patrick alidai.

Chifu na Inspekta Mkuu wote walionyesha mshangao!

"Ni mwongo ni mwongo mkubwa. Anataka kunisingizia tu. Kashindwa kumtafuta Mkuu wa majambazi. Ananisingizia mimi. Nimekuja kwa ajili ya kazi hii hii huku nikiwa nimemwacha mke wangu mahututi. halafu unakuja kunisingizia kiasi hiki. Mimi niwe Mkuu wa majambazi. Wewe Willy una kichaa? Kichaa", Oswald Mengi alisema kwa ukali.

"Kama tungechelewa kidogo, Elungata angepotea kabisa na tungeonana na Oswald Mengi peke yake, akidai kuwa baada ya kupata habari kuwa Inspekta Mkuu na Chifu wako hapa na yeye akaja. Wote tungeamini na Elungata asingepatikana kamwe kwa sababu Elungata ndiye Oswald Mengi!" 

"Kweli kabisa nimekuja kupigana nanyi bega kwa bega dhidi ya majambazi," alipiga tena kelele.

Wote walikuwa wapo na mshangao.

"Chifu kaeni kwenye viti"

Mlikuwa na viti viwili Patrick akaegemea kwenye mlango huku bastola yake ikimlenga Mengi. Mimi nikakaa juu ya meza, bastola yangu ikimlenga vile vile.

"Nitawaeleza mambo yote toka mwanzo mpaka mwisho"

Wote wakaa chini wakiwa bado wameshangaa la kusema hawana!

"Katika mashimo ya almasi ya Mwadui kumekuwa na wizi mdogo mdogo wa almasi, ambao ulianza miaka mingi toka hata wakati wa ukoloni na nyote mnajua. Wizi ambao ulianza kushtusha serikali umetokea miaka miwili tu hivi iliyopita. Na kama mnakumbuka, Mengi alikuwa mkuu wa Polisi wa Mwadui kwa miaka mitano na wakati wote huu wizi ulikuwa ni mdogo mdogo tu.

Miaka miwili na nusu iliyopita, Mengi alipandishwa cheo na kuwa kamishna Mwandamizi wa Polisi na kuhamishiwa Dar es Salaam, Miaka yote hii alipokuwa Mwadui alikuwa anapanga jinsi gani anaweza kuanzisha wizi wa almasi, lakini akaona kuna hatari ya kuweza kugunduliwa. Wakati amepanda cheo na kuhamishwa ndipo akapata nafasi. Na kama mnakumbuka yapata miaka miwili na nusu sasa toka atoke Mwadui na ni baada ya miezi sita tu ndipo wizi kabambe ulipoanza.

"Mkuu wa Polisi wa Mwadui, ambaye sasa hivi ni marehemu alihamishiwa Mwadui miaka miwili iliyopita na kama sitakosea Mengi ndiye aliyependekeza jina lake na akapendekeza kuhamishwa kwa Mkuu wa Polisi aliyekuwa amekaa hapo muda mfupi tu Mengi alimpa huyu marehemu mipango yake na jinsi ya kuitekeleza.

"Na huko Mwadui alikuwa na kijana wake Khasimu Omari ambaye alikuwa Inspekta Mwandamizi na alimwelekeza akafanya naye kazi bega kwa bega chini ya mwongozo wake. Kwa hiyo hii iliwapa nafasi nzuri sana ya kuweza kuendesha wizi bila wasiwasi. Na kwa upande wa Mengi ingekuwa vigumu sana mtu yeyote kumfikiria. Vile vile ingekuwa vigumu kuwashika, maana mara utokeapo uchunguzi ilibidi yeye Mengi ahusike katika kuutekeleza na hivyo aliweza kujua mbinu za kuangamiza uchunguzi wa hali yoyote kabla haujafika mbali.

Khasimu Omari alikuwa anajuana na Pweke ambaye kwa mara nyingi alikuwa anaendesha wizi mdogo mdogo na kwa jinsi ile yeye ndiye aliyekuwa akijua masoko ya wizi wa almasi za wizi. Kwa hiyo upande wa soko ilikuwa kazi ya Pweke ambaye alijuana na wale watu niliowapa majina muwakamate ma kuwaweka chini ya ulinzi, maana hao ndio waliokuwa wakala wa almasi kwa wafanya magendo kwa nchi za nje. Kwa jinsi ile mambo yalienda vizuri bila ya wasiwasi maana kila upande ulikuwa na mpango thabiti.

"Kwa hivi, Chifu kila alipokuwa akituma wapelelezi, walikuwa hawawezi kufua dafu, maana habari zilijulikana tu baada ya kuondoka hapa. Wote akina Jack Mwile, Makungu Majula na wengineo waliweza kuuawa kwa urahisi kwa sababu hiyo hiyo. Mbile katika uchunguzi wake alifika mbali kiasi cha kujua kuwa mtu aitwae Elungata ndiye aliyekuwa Mkuu wa majambazi, lakini aliuawa kabla hajaweza kuleta ripoti kamili. Kwa bahati aliweza kunifikishia ujumbe juu ya hili jina.

"Kila uhalifu una kikomo chake, maana itajatokea siku moja atafanya kosa kidogo na ndipo atajisaliti.

"Wakati mimi naondoka, watu waliojua juu ya kuondoka kwangu, ni wewe Chifu, Inspekta Mkuu, Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, na bila ya shaka, Mengi ambaye Inspekta Mkuu alienda kumweleza akiwa kama msaidizi wake mkuu.

"Kosa la kwanza alilofanya Mengi ni kuwa mimi nilipofika tu Mwanza, habari zangu zilikuwa tayari zimefika, maana sikukaa hata masaa mawili kabla ya chumba changu hakijakaguliwa na hali nilikuwa nimebadilisha sura na jina. Ingekuwa vigumu mtu yeyote nje ya hao niliowataja kunitambua. Kwa hivi mara moja nikaanza kuhisi kuwa kuna mtu miongoni mwetu aliyekuwa na uhusiano na haya majambazi. Kwa hiyo nikaanza kujihadhari sana huku nikijaribu kumtafuta huyu mtu kati yatu.

"Jambo lilonidhihirishia kabisa kuwa huyu mtu yu miongoni mwetu ni wakati George alipokuja, kwani na yeye kabla hajafika habari zake zilikuwa zimefika. Na wakati huu watu walikuwa wanajua habari za safari ya George ya Mwanza, Ni wewe Chifu na Mengi, maana Waziri pamoja na Inspekta Mkuu walikuwa wamekwenda Lusaka. Kwa hivi ikabidi nichunguze zaidi kati yenu ni nani.

"Mambo yalipozidi kwenda vibaya kwa upande wake Mengi akatoa amri ufanyike wizi wa hali ya juu kabisa na kumweleza Khasimu na Mkuu wa Polisi wa Mwadui kuwa anawasili Maganzo kitu kilichonifanya sasa nimtuhumu Mengi peke yake ni wakati Patrick alipokuja, Habari zake hazikuwa zimefika kwa kuwa Mengi hakujua kuwa Patrick alikuwa akija maana yeye alikuwa wakati huo ameisha omba ruhusa ya kwenda kumuona mkewe aliyepatwa na ajali. Kwa hivi Patrick alipofika hakuna aliyejua.

"Habari kuwa mkewe alikuwa amepatwa na ajali ilikuwa ni uongo. Hii ilikuwa njia ya kutafuta namna ya kuja Maganzo. Kwa hiyo badala ya kwenda Arusha, ambako kweli ndiko mke wake aliko, amekodi ndege ya Tim Air na kuja Shinyanga. Ukitaka kuthibitisha utakuta mtu kwa jina la Ochald Mengi amekodi ndege kuja Shinyanga jana jioni kwani walimtegemea kufika Maganzo mnamo saa nne.

"Alipofika Maganzo na kukuta mambo yameharibika zaidi, akawachukua wenzie mpaka Shinyanga, ambako wangegawana almasi zilizoibiwa jana, halafu kila mtu aende zake. Kwa bahati sisi tukaweza kuwagundua. Kitu kingine kilichofanya nijue kwamba lazima huyu mtu tunamfahamu ni wakati tumeshikwa mimi na Patrick Elungata alikuwa akizungumzia kwenye chumba akiwa amejificha na sauti aliyokuwa anaitoa ungejua kuwa ni ya kuiga. Hii ilizidi kunidhihirishia kuwa huenda hisia zangu ni sahihi.

"Watu waliokuwa wakifahamu kuwa Elungata ndiye Oswald Mengi, walikuwa watu wawili tu, Khasimu Omari na Mkuu wa Polisi wa Mwadui kwa hiyo kuuawa kwa Khasimu Omari kwenye hiyo nyumba huko Ushirika ilimpa Mengi wazo la kutoroka na hao wengine, sisi tubaki tuwamalize wale waliobaki ndani ya ile nyumba. Lakini yeye akawamaliza hao alioondoka nao akiwemo Mkuu wa Polisi wa Mwadui, ambaye ndiye peke yake aliyebaki akimjua yeye ni nani.

"Alijua kwamba kaisha waua hao atakuwa amebaki na almasi zote na angeweza kujitokeza kama vile anavyosema sasa kuwa naye amekuja kuona mambo yanakwendaje. Lakini kwa vile nilikuwa nimeisha muhisi, nilipata habari za kuuawa kwa hawa watu ndani ya gari akiwemo huyo Afisa wa Polisi. Nikajua karibu tunapata mzizi wa tatizo letu ndipo nikaomba ufike ujionee mwenyewe.

"Kwanza nilifikiria kwamba atatoroka. Lakini nilipoambiwa kwamba hakuna gari lililotoka, nikajua dhahiri kuwa bado Elungata yumo Shinyanga. Kusudi niweze kuthihirisha mambo yote niliyokuwa nimekisia, nilienda kila hoteli nitafuta jina linalofanana kidogo na Oswald Mengi. Kwa bahati nilipofika hapa Butiama Hoteli kuangalia katika rejista. Nikakuta jina la Ochard Mengi. Hii ikanidhihirishia kuwa makisio yangu yalikuwa sawa. Maana jina la Ochard Mengi ni kidogo sawa na Oswald Mengi.

"Chifu, hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa. Sasa kutaka kukudhihirishia asilimia mia moja kuwa yote niliyosema ni kweli bila ya kumsingizia mtu unayemtafuta ni yeye, subiri. Patrick mwangalie, akileta ujanja wowote piga risasi".

Nilifungua kabati la nguo la humo chumbani. Nikakuta hicho nilichokitaka, kisanduki kidogo cheusi.

"Wewe mshinzi sana. Willy, umenimaliza", Mengi alisema.

Nilifungua hicho kisanduku, ambacho ni cha gharama sana, kikiwa na mifuko ya siri mingi ndani. Katika mfuko mmoja wa siri nikakuta nilichokuwa nikitafuta. Nilitoa mkoba uliojaa almassi tele, zilizokwishapigwa muhuri tayari kwa kusafirishwa ng'ambo.

"Kweli kikulacho ki nguoni mwako". Chifu alisema kwa masikitiko makubwa.

"Piga simu hapo chini ita polisi 999," Inspekta Mkuu alimweleza Patrick.

Patrick akaondoka kwenda kuita 999.

"Kikulacho ki nguoni mwako ni kweli Chifu. Mtu kama huyu anayestahili kulinda uchumi wa wananchi, yeye mwenyewe anakata shauri kuwanyonya na kuwatesa. Ningekuwa na madaraka mtu kama huyu ningemweka hadharani wananchi wenyewe watoe hukumu", alimalizia. 

"Mimi nafikiri kuna haja ya kufanya marekebisho katika ngazi zote za uongozi. Kila kiongozi amulikwe maana ni afadhali kuwa na watu wa kawaida elfu moja waovu kuliko viongozi au hata kiongozi mmoja mwovu", alisema Inspekta Mkuu.

"Lililopo sasa ni kuishauri serikali ifanye uchunguzi na iwapo kuna kiongozi anayeonekana msimamo wake ni wasiwasi basi aachishwe uongozi. Wale wanaobaki wapigwe msasa, waweze kuelewa wajibu wao kwa wananchi ni nini, wajibu kwa kazi waliyokabidhiwa na wananchi ni nini. Watoe tamaa ya kujinufaisha wenyewe bali wajitoe mhanga kwa faida ya taifa zima. Jambo la huyu Mengi litasikitisha wengi lakini imekuwa fundisho kwa serikali na wananchi kwa ujumla, kuwa kati ya viongozi wenyewe wa nchi hii, yamo majambazi nambari moja. Mara kwa mara watu hufikiria watu wadogo. Lakini tokea sasa tutakaza macho kwa watu wakubwa, maana hawa ndiyo rahisi sana kuangusha taifa hili kiuchumi. Ni aibu kwa mtu kama huyu", Chifu alisisitiza huku machozi yakimlengalenga.

"Nitahakikisha kuimarishwa kwa Jeshi la Polisi kikamilifu, na naomba iwe hivyo katika sehemu zingine kwa manufaa ya wananchi. Ni jambo la kusikitisha sana, maana nilimwamini sana Mengi, ni sikitiko lililoje!".

Wakati huo huo polisi wakafika pamoja na Patrick.

"Mnaweza kuchukua wiki moja na kupumzika", Chifu alituambia.

"Asante sana", tulishukuru.


MWISHO

Comments

  1. Mkuu, nakushukuru kwa kutupa burudani kwa stayle ya aina yake. Umeitendea haki riwaya hii, maana imekuja angalau kwa mfumo wa non stop. Hongera na pongezi.

    Mimi nishamaliza,kila siku kodo kuangalia kitu kipya

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU