KUFA NA KUPONA

SURA YA KWANZA

Karatasi za Siri

Ilivyo ni kwamba mimi siku za Jumapili hulala mpaka saa tatu au saa nne. Na kama huamini hiyo si shida yangu. Ilikuwa Jumapili nyingine. Usiku wa jana, yaani Jumamosi, nilikwenda kwenye dansi na rafiki yangu mmoja msichana. Tulirejea nyumbani mnamo saa tisa na nusu za asubuhi. Kutokana na uchovu mwingi ulionielemea nikafahamu wazi kwamba Jumapili hii nitaamka kama saa tano hivi. Lakini utastaajabu nikikwambia kuwa Jumapili hiyo ilinibidi niamke saa kumi na moja alfajiri!

Kengele ya simu ililia mnamo saa kumi na moja, na miye nilikuwa nimelala saa moja tu hivi. Nilipuuza kuichukua kwani nakueleza nilivyochukia, Mungu ndiye anayejua. Iliendelea kulia na kulia, mwishowe nikaona nisipoijibu pia nisingeweza kulala kwa sababu ingaliendelea kuniudhi. Huyu binti aliyekuwa amelala karibu na hii simu naye aliamka, akaniomba afadhali niijibu. Basi kwa shingo upande, nilimwambia huyu binti anisogezee. Yeyote yule aliyekuwa amepiga hii simu nilikuwa mpaka sasa nimechukia kiasi cha kwamba angalikuwa karibu ningalimwuma.

"Hallo, huyu ni Chifu." Nilisikia sauti ikisema. 

Usingizi ulipotea papo hapo, nikajua kuna jambo, maana, S, anapojifahamisha kwa jina la Chifu jua kuna kazi, na kazi kubwa. "Halo, huyu ni Willy. Chifu mbona unapiga simu wakati kama huu? Nadhani ingefaa uwe kitandani, la sivyo utazidi kuzeeka upesi, kwa mtu wa makamo kama yako, " nilimjibu.

"Sikiliza Gamba, hapa ninapopigia simu ni ofisini, na wala si nyumbani-kitandani kama ambavyo ungalifikiria. Na miye nakuhitaji hapa ofisini mnamo nusu saa bila kuchelewa. Kuna jambo la muhimu na la haraka, hili si ombi ila ni amri, asante sana," alimalizia Chifu.

Nakueleza, hakika kweli, kuna wakati mwingine ninapochukia hii kazi yangu, lakini hata hivyo kwa mtu kama mimi nipendaye visa, nikiwa nasikia kuna jambo kubwa kubwa basi moyo nami huwa unanidundadunda ukiniambia nenda, huenda mara hii kuna visa zaidi. 

Della ambaye ndiye msichana niliyekuwa naye hakupenda kuniona naondoka saa kama zile. Akaniambia, "Willy hii ndiyo sababu nakuchukia. Sasa karibu tena uende kwenye masafari yako ya ovyo ovyo, hasa unapoitwa na hilo lijanaume linaloitwa liChifu. Kweli kama mara hii ukikubali kwenda miye naweza kufa."

Nilimjibu Della nikisema, "Wajua kabisa ya kwamba hii ndiyo kazi yangu, ndiyo inayonipa unga, mboga na starehe za kila aina. Nisipofanya hizi safari, itakuwa kama wewe usipoenda ofisini."

Kwa sababu Della ni msichana mwenye hekima alinyamaza na kuelewa nimesema nini. Kumwacha msichana huyu, na asubuhi kama hii amelala kitandani, na miye nikakimbia ofisini, ati kusudi nikapige ripoti kwa Chifu, moyo wangu ulidunda mara nyingi zaidi. Kama ningehesabu wenda mapigo yangefika tisini kwa dakika moja. "Nitarudi mapema baada ya kumaliza shughuli na Chifu," nilimwambia Della. 

Nilifungua mlango, nikaangaza nje maana kulikuwa bado giza giza. Macho yalipozoea nikafunga mlango kwa nyuma, nikaenda kwenye gari langu. Nikaingia ndani na kuliwasha gari hilo. Kutoka kwangu ambako ni Upanga, mpaka ofisini kwetu ni mwendo wa dakika kumi. Kwa sababu wakati kama huu hakuna magari mengi nilitegemea kuchukua dakika tano hivi. Ingawaje ni kawaida ya Dar es salaam kuwa na joto jingi, asubuhi hii kulikuwa na baridi sana. Nilitia gari moto, nikashika barabara ya United Nations moja kwa moja mpaka Jangwani kwenye taa za 'traffic.' Nikaona hakuna gari ingawaje zilikuwa haziniruhusu kupita. Lakini nilienda tu. Nikaingia barabara ya Morogoro hadi Independence Avenue. 

Nilipoingia Independence Avenue, niliona gari moja inakuja kwa nyuma. Na ilionekana kama kwamba ilikuwa imesimama katika barabara ya Morogoro wakati nikipita, kwa hiyo nikapunguza mwendo, na hiyo pia ikapunguza. Miye nilikuwa sipendi mtu yeyote ajue kuwa nilikuwa nikienda ofisini, saa kama zile. Na kwa nini hilo gari likawa linanifuata? Hiyo ndiyo pia nilikuwa sitaki. Nakwambia, kwa sababu nilishafutwa na magari mengi, mara moja tu naweza kutambua kuwa lile gari linanifuata hata anayenifuata awe mjanja namna gani. Wakati huu nilikuwa nimebakiwa na dakika kumi tu kuripoti kwa Chifu. 

Nilikata shauri kurudi mara moja nikaone nani aliyekuwa ananifuata. Basi nilipiga kona na kuanza kurud. Hilo gari lilipoona nimerudi, likatia moto kuja kwa kasi sana. Likanipita na kwenda mwendo wa kama maili mia moja kwa saa. Dereva wa hiyo gari alikuwa amejifunga shuka. Alikuwa amevaa miwani mweusi ya jua. Nikabahatisha kuwa, huyo alikuwa mtu ninayemfahamu, hivyo alivaa ili kusudi nisiweze kumtambua. Gari lake lilikuwa aina ya Datsun 160 SSS lakini alikuwa ametoa sahani ya namba. 

Nilikata kona tena nikaendelea na safari yangu mpaka ofisini. Niliendelea mbele kidogo ya ofisi kusudi nione kama hilo gari lilikuwa karibu hapo. Ilionekana huyo jamaa alikata shauri kwenda zake. Nilianza kupanda juu ya jumba ambalo ndimo zilimo ofisi zetu hapo Independence  Avenue karibu na jengo la Bima ya Taifa. Ilikuwa tayari saa kumi na moja na nusu. Niligonga kwenye mlango wa ofisi ya karani wa Chifu. Nilisikia sauti ya Maselina ikinikaribisha. 

Nilifungua mlango na kuingia ndani. Nilimuhurumia sana Maselina maana naye alionekana mwenye usingizi mwingi. Nilipomuuliza alifika saa ngapi ofisini alinieleza kuwa Chifu alikuwa amempitia nyumbani kwake huko Magomeni Mikumi, yapata saa kumi hivi, wakati yeye alipokuwa amefika kutoka 'Afrikana Hoteli' ambako alikuwa ameenda kustarehe na rafiki zake. Akazidi kunieleza kuwa lazima kulikuwa na jambo kubwa sana kwani Chifu alionekana hana furaha kabisa. 

Kweli Maselina alifaa sana kuwa karani wa Chifu, maana alikuwa msichana mwenye bidii sana ya kazi. Hata mimi nilimpenda kwa ajili ya bidii zake na pili alikuwa na umbo la kupendeza. Alizidi kunieleza kuwa Chifu alikuwamo ndani akiningojea. Maselina alimpigia simu Chifu na Chifu akamwambia aniambie niingie. Basi niligonga kwenye mlango ulioandikwa "MKURUGENZI WA UPELELEZI." Nilisikia sauti ya Chifu ikisema, "Ingia ndani Gamba." 

Nilipoingia ndani nilimkuta Chifu anavuta mtemba. "kaa chini," aliniambia. Sura yake ilionyesha kama kwamba kulikuwa na jambo ambalo hakulipenda. Alikaa kama dakika kumi hivi akiniangalia tu bila kunieleza neno. Hata miye mwenyewe nilijisikia sina furaha hata chembe. Kisha Chifu alitoa mtemba wake kwenye mdomo, akakung'utia majivu ya tumbaku katika sahani la majivu. Akaanza kutia tumbaku mpya. Halafu akainua macho yake na kuanza kusema, 
"sikiliza kwa makini sana tafadhali maana sitaki kuwepo makosa yeyote ambayo yanaweza kuleta hatari. Habari niliyonayo ni muhimu sana, hivyo kwamba, kosa la mtu mmoja tu, linaweza kuleta maangamizi ya Afrika nzima."

"Mnamo usiku wa manane, nimepokea simu nyumbani kwangu ikitoka kwa mkubwa wa Polisi. Mkubwa wa Polisi alinieleza ya kwamba, ofisi moja ya wapigania uhuru imebomolewa. Na kwamba karatasi fulani za siri zimechukuliwa." Alipofika hapo Chifu alionekana hana furaha katika kutaja neno hili 'zimechukuliwa.' Aliendelea kusema, "Na polisi wanafikiri kwamba jambo hili limefanyika kati ya saa nne usiku na saa tano. Askari Polisi aliyekuwa akilinda amekutwa amekufa kwa kupigwa risasi tatu kifuani. Polisi walifika hapo ofisini yapata saa tano kamili, baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja aliyeiona hiyo maiti ambayo ilitupwa barabarani. Mtu huyo alikuwa akitoka dansini akielekea nyumbani kupitia mtaa wa Nkurumah. 

"Polisi walifika na Dakitari. Daktari alieleza kwamba huyo askari alikuwa amekufa yapata saa moja iliyopita, ambayo ilionekana ilikuwa saa nne. Mkubwa wa wapigania uhuru alifika baada ya kupigiwa simu na akachunguza vitu vilivyopotea. Ilionekana kwamba kila kitu kilikuwemo ila kabati moja la chuma ambamo mlikuwa na karatasi za siri, kufuli la kabati hilo lilifunguliwa kwa kutumia bastola .45. Karatasi hizo zilizochukuliwa ni za maana sana kwamba lazima 'kwa njia nzuri ama mbaya' zipatikane. Maana zisipopatikana, zinaweza kuleta maangamizi kwa wapigania uhuru na kwa nchi huru zote za Afrika." 

Alipofika hapa mimi nilisema, "ingefaa unieleze jinsi ninavyohusika katika mambo haya, maana mpaka sasa bado inaonekana hakuna jambo au kiini cha kuweza kuzipata iwapo hawamjui mtu yeyote aliyehusika na mambo haya."

Chifu hakusita kupanua midomo kunieleza, "baada ya kuelezwa yote haya, imeonekana kwamba. Na pia wakuu wa serikali wanafikiri kuwa wizi wa karatasi hizi, Ureno na Afrika ya Kusini ndiyo wako nyuma ya mambo yote haya, pia Indonessia. Lakini watu waliofanya au waliozichukua hizo karatasi ni watu au majambazi wa papa hapa Afrika ya Mashariki. Maana kutokana na wizi wenyewe ulivyotokea, imeonyesha kwamba ni watu wenyeji wa Afrika ya Mashariki tu wanaweza kuendesha wizi huu. 

"Mimi sasa ninavyofikiria ni kwamba hizo karatasi zina mambo yote jinsi wapigania uhuru wanavyoweza kufaulu katika mambo yao. Kwa hiyo wakafanya jitihada wazipate, lakini hawakuweza, maana wapelelezi hao wote wamekamatwa kama unavyojua. Hivyo wakaona jambo wanaloweza kufanya ni kuwafuata majambazi katika Afrika Mashariki ambao haja yao kubwa ni pesa. Sasa basi, hao watu wakafuata hao majambazi na kuwambia kuwa watalipwa pesa kiasi kikubwa. Na hapo ninavyofikiriwa. Majambazi wakakubali kufanya hivyo.

"Zaidi ya hayo," aliendelea Chifu, "hao majambazi hawajali kama wapigania uhuru wanashindwa ama wanashinda. Na wala hawaoni hatari za mbele kwa nchi zote za Bara la Afrika. Kweli, hao majambazi ninavyofikiria kuwa ndiyo wamefaulu. 

"Sasa hapo ndipo sisi tunaingia katika habari hii. Na sasa sikiliza kwa makini. Wakuu wa Serikali wamekaa na kufikiri usiku huu huu na kuona watupe sisi kazi hii, na ni lazima tufaulu ama sivyo bara zima la Afrika litaumia si Tanzania wala Zambia wala Ethiopia wala Kenya zitakazoumia pekee. Wala si Msumbiji na Rhodessia na Angola peke yake. Kwa hiyo nimekuita wewe na utaondoka leo hii kwenda kwenye tume hii. Ninavyofikiria ni kwamba karatasi hizo hazijatoka katika Afrika Mashariki, maana Polisi katika nchi zote wameishafahamishwa na kuna ulinzi mkuu katika mipaka, viwanja vya ndege na mahali penginepo. 

"Hao majambazi wanajua kwamba Serikali itachukua hatua kuzitafuta hizo karatasi kwa njia nzuri ama mbaya watajaribu kuwapa wanaohusika upesi iwezekanavyo. Lakini nadhani hawatazitoa mpaka wamepokea fedha yao. Lakini lazima ujue kuwa makundi ya majambazi yana akili sana wanangojea sisi tuanze kushughulika kusudi wajue kama kweli tunaweza kuwafikiria wao. Watakapoona kuwa tunawashutumu, mara moja na wao, wataanza kupambana nasi, maana hawatakubali kupoteza hiyo fedha. Hapo ndipo maisha yatakuwa magumu maana itakuwa ua au uawa. Na huenda wakasaidiwa na majasusi toka Ureno, Afrika Kusini na Rhodesia. 

 "Na pia nilifikilia kuwa, hao majambazi watapanga mahali pa kuonana na hao watu ili wabadilishane hivi vitu. Na lazima wapelelezi wa nchi hizi ndiyo watatumwa na Serikali zao kuja kuonana na hao majambazi. Hatari nyingine ni kuwa hao majambazi lazima wawe na majina ya wapelelezi wetu maarufu, na wewe ukiwa nambari moja kwenye orodha hiyo. Sasa ninafikiria kuwa ofisi kuu ya majambazi hao iko Nairobi. Kwa hiyo utaondoka hapa kwenda Nairobi, leo hii saa tatu unusu na ndege ya shirika la ndege la Afrika Mashariki. 

"Vyeti vyote vya kusafiria viko tayari. Huenda itakubidi usafili mpaka Afrika Kusini au Ureno au Rhodesia ikiwa lazima. Mambo ya safari katika nchi hizo pia yako tayari. Ukiona ni lazima kusafiri katika nchi hizo usisite. Jina lako tangu sasa ni "Joe Masanja," na kazi yako ni uandishi wa habari juu ya maonyesho ya mavazi. Maana tangu kesho maonyesho ya mavazi yataanza kote ulimwenguni. Upashanaji wote wa habari kati yetu katika kazi hii, utajulikana kama "Kufa na Kupona." Na pia nakupa hiki cheti ambacho kimetolewa na Serikali, kikikuruhusu kuua kama ni lazima. Nakutakia mafanikio mema. Mungu akusaidie ila nakuonya usihusiane sana na mwanamke, na katika hii safari usimwamini mwanamke yeyote." 

Chifu alimalizia kunieleza, lakini bado niliona mambo yote hayo ni kama muujiza. Kwani hakukuwa hata na chambo cha kuanzia. Ilikuwa kwamba nitaenda Nairobi bila hata kuwa na fununu ya mtu ambaye anaweza kuhusika habari yote niliona kama ya mwendawazimu. Kweli ilikuwa uendawazimu mtupu. Kisha nikamuomba Chifu kama angaliweza kuniruhusu kuuliza swali, naye akakubali.

Nilimuuliza, "kuna mtu yeyote ambaye anaweza kunisaidia huko Nairobi?" 

"Nitapata jina la huyo mtu mnamo saa mbili na nusu asubuhi hii, na kama pia kutakuwa na maelezo yoyote zaidi nitakupa wakati huu." 

Nilitoka ofisini kwa mkurugenzi wa upelelezi, na kufungua mlango. Nilimkuta Maselina amelala kwenye meza: Nikamgusa hakaamka. Akaniuliza ilikuwa ni saa ngapi. Nikamweleza ilikuwa saa kumi na mbili unusu. Akaniomba nimweleze kwa kirefu palikuwa na nini. Lakini sikuwa na muda, kwani ilikuwa inanibidi nijitayarishe upesi iwezekanavyo, nipate ondoka saa tatu.

Nilimweleza kwa kifupi tu mambo yalivyokuwa. Maselina akaniambia, "Willy, kweli safari hii mambo ni mengine, na kesi hii inaonekana imejisokota vibaya sana. Lakini naamini unaweza ukaisokotoa na kurudi salama Mungu awe nawe." 

Nakwambia kama mtoto huyu angalikuwa anakuaga wewe, walahi usingefanya safari, maana utadhani badala ya kukuombea usalama, anakuombea maafa! Maana hiyo sauti yake ilikuwa mno mbichi mbichi. Nilimwaga Maselina. 

Nilitoka nje nikakuta kulikuwa kumeishapambazuka. Nikaingia katika gari langu, huyoo Upanga. Mitaani bado hakukuwa na watu maana kumbuka kuwa hii ni Jumapili. Nilipofika nyumbani kwangu nilimkuta Della bado amelala. Lakini baadae aliponiona tu, jambo la kwanza kuniuliza ni kama nitaondoka. "Naondoka mnamo saa mbili zijazo."

Della alianza kulia, na huyo mtoto anapolia, ndipo anakuwa mzuri kiasi cha ajabu. Utadhani mwelekevu ambaye Shaaban Robert anamzungumza katika kitabu chake cha 'Adili na Nduguze. Kama hujakisoma miye Willy nakuomba ukakisome ndipo utajua Della ni msichana mzuri wa kiasi gani. 

Nilimbembeleza Della na kumwambia, "Usijali sana. Safari si mbaya sana, na nitarudi muda si mrefu." Lakini moyoni nilijua hii safari ilikuwa "HATARI TUPU!"

Della aliamka akaanza kutengeneza kahawa, wakati mimi nikifungasha vitu vyangu vya lazima. Muda mchache kijana mmoja alibisha hodi mlangoni. Nilipomuona nikafahamu kuwa alikuwa mfanyakazi ofisini kwetu. Daudi alikuwa ametumwa na Chifu kuniletea kamera moja ya gharama sana, ambayo ningetumia kama mwandishi wa habari na mchukua picha za maonyesho ya mavazi. Pia alibeba bastola mbili zote " automatic .45." Visu sita na vitu vingine ambavyo ningeweza kuvitumia safarini. 

Pia alinieleza kuwa Chifu alikuwa amekata shauri niende pamoja na ofisa mwingine wa upelelezi, kwa jina la Sammy Rashidi. Huyu kijana nawambieni nyie kuwa ni mwamba, maana katika kazi yetu hii kila siku ni nambari mbili akinifuata mimi. Na mara nyingi ameponyesha maisha yangu. Alishawahi kushinda mashindano ya kutupa visu katika mashindano ya Jumuia ya Madola. Ukiwa na bastola na Sammy akiwa na visu, jua umekwisha kazi! 

Kusikia Sammy anakwenda na mimi, Moyo wangu ulipata furaha kidogo. Daudi alinieleza kuwa Sammy atakwenda akitumia jina la Athumani Hassani. Kazi yake itakuwa msaidizi wangu katika mambo ya kuchukua picha, na yeye ndiye atakayekuwa mchukuaji picha, na kwamba tutaonana naye kiwanja cha ndege cha hapa Dar es Salaam saa tatu.

Sasa ilikuwa saa moja na nusu, Della alikuwa tayari ameweka kahawa, mayai na mkate. Miye nilikuwa nimemaliza kufungasha vitu vyangu. Nilikuwa nangojea tu habari zaidi kutoka kwa Chifu. Tulikaa mezani na Della na kuanza kunywa kahawa. Nilizidi kumbembeleza Della, "Usijali sana juu ya safari yangu. Na kama mola akipenda tutaonana tena." 

Ilipofika saa mbili kamili, simu ilisikika. Nikaenda kuijibu, na kama ilivyotegemea, ilikuwa inatoka kwa Chifu. Chifu alisema, "Gamba sikiliza. Nairobi mtaonana na Ofisa mwingine wa Upelelezi aitwaye John Mlunga. Huyu ni kijana tunayemuamini sana. Nadhani mlishawahi kuonana. Yeye aliishafika Nairobi toka Kampala asubuhi hii. Atakungojea saa nne asubuhi katika Hoteli ya Fransae huko Nairobi. Inaonekana yeye anafununu kidogo kuhusu hii habari mpaka wakati huu. Maana anajua mambo mengi sana ya hapo Nairobi baada ya kufanya kazi hapo kwa siku nyingi akipambana na majambazi wa hapo kwa muda mrefu. Sasa tayarisha kila kitu uondoke. Nakuombea safari njema."

Baada ya kupata habari zote hizi kwa Chifu nilionelea sasa niondoke kwenda zangu kwenye kiwanja cha ndege. Ilibidi Della anisindikize mpaka kwenye kiwanja ili apate kurudi na gari. Sikuwa na mzigo mkubwa sana, kwani huwa nina mfuko mmoja wa ngozi ambao nikiufunga unaonekana mdogo sana lakini ndani yake unaweza kubeba hata ngamia! Della alitia gari moto tukaondoka. Niliangalia nyuma kuiangalia nyumba yangu na sehemu ya Upanga kwa makini sana. Sijui ilikuwa mara ya mwisho kuiona ama nitaiona tena, huo ulikuwa ndiyo wasiwasi wangu.

Nilionelea nipite kwanza mtaa wa Nkurumah nikaone hilo jengo lililobomolewa, kwa sababu nilikuwa bado na dakika ishirini za kupoteza kabla sijafika kwenye kiwanja cha ndege. Na mwendo wa kutoka mjini mpaka kiwanja cha ndege. Ikiwa Della anaendesha ni dakik tano, kwani huyu msichana anafahamu kuvuta gari. 

Nilipofika kwenye hilo jengo, nilimwacha Della ndani ya gari nikamwambia, "usitoke garini humu ila uwe ukiangalia ikiwa kuna mtu yeyote anayeonekana na wasiwasi wa kuiona hii gari hapa."

Wakati huu watu wengi walikuwa wamekusanyika kwenye hilo jengo, kwa hiyo ilikuwa rahisi sana kuchunguza mambo fulani fulani bila mtu kuwa na wazo lolote juu yako. Polisi walikuwa wanasukumasukuma watu wasikaribie sana, hata mimi nilianza kusukumwa lakini polisi Inspekta mmoja alivyoniona alinichukua na kunionyesha kila kitu. Jambo moja nililofikiria ni kwamba hao watu waliobomoa hili jengo walikuwa wakifahamu kabisa kuwa hizo karatasi za siri zilikuwa kwenye hili kabati la chuma, maana la sivyo, wangalikuwa wamejaribu kupinduapindua na kutafuta tafuta kila mahali. Lakini vitu vyote hata wino katika vidau, haukuwa umemwagika japo tone moja hii inaonyesha kuwa walikuja moja kwa moja bila kugusa kitu kingine chochote, na kupiga kufuli la kabati kwa risasi na kuchukua karatasi na kwenda zao. Pia inaonekana haikuwachukua muda mrefu. 

Hili jambo ambalo nimekueleza hapo juu, linanipa wazo. Na kama wewe pia ni mtu mwenye kufikirlia kama miye Willy nadhani tayari umepata wazo ni kwamba hizi karatasi zilikuwa zikifahamika kwa watu wachache sana. Na kama hata zilijulikana kwa wapigania uhuru kuwa zipo, wachache walijua zipo wapi. Kwa hiyo ingawaje hao majambazi walijua zipo, wasingeweza kujua mahali gani zilipo, mpaka wameambiwa na mtu anayejua zaidi juu ya karatasi hizo. La sivyo wangalitafuta kila mahali kabla ya kuzipata. Hivyo tungalikuta vitu vimevurugwa vibaya sana. Kama una kichwa cha kufikiria nadhani umejua nina maana gani.

Baada ya kupata fununu fununu, na kufikiria mambo mawili matatu, niliondoka hapo mahali na kurudi kwenye gari ambamo Della alikuwa akiningojea. Della aliniambia, "Sikumuona mtu yeyote ambaye alionekana kuwa na wasiwasi juu ya gari hii. Ila tu niliona gari moja aina ya Dutsun 1600 SSS, dereva wake alikuwa amevaa shuka na miwani myeusi. Dereva huyo alinitupia macho kidogo tu."

Nadhani hiyo habari ya Della inakupa wazo jingine kwani hilo gari ndilo lililokuwa likinifuata wakati nikienda ofisini kwa Chifu. Della alivuta gari moja kwa moja mpaka kiwanja cha ndege ambako tulimkuta Sammy akiningojea kwa hamu. Nilimwaga Della kwa kumbusu kisha akarudi zake hali machozi yakimtoka.

Comments

  1. Mwanzo mzuri Mkuu Nyakasageni. Nashika nafasi ya kwanza daima kuhakikisha sipitwi na tukio hapa. Niahidi tu vitu mfululizo,maana ndipo raha ya riwaya inaonekana.

    Pia kama hutojali, kwenye utangulizi, edit utuwekee jina la mwandishi, mwaka wa publication, na taarifa muhimu kuhusu kitabu, zinasaidia sana kufurahia au kujifunza mambo mbalimbali

    ReplyDelete
  2. Mkuu,utatuua kila saa kuchungulia humu ndani

    ReplyDelete
  3. Dalili za awali kabisa hii story tutaonja joto lajiwe. Cha moto tuttakipata

    ReplyDelete
  4. Mkuu usijali, sisi twasubiri!
    Tuko pamoja!

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU