KUFA NA KUPONA

SURA YA TATU 

Lo Maisha Magumu

Nilijiona siwezi kufanya lolote. Na kama kweli ningefanya upuzi hapo, nilijua hata mimi ningeyala marisasi. Kwa hiyo nilionelea ninyamaze tu mpaka hapo nitakapopatiwa yangu. Jinsi huyu mtu alivyoingia hata sifahamu maana aliingia kama mchawi bila hata kishindo. Zaidi nilikuwa nataka nimwone ni nani, lakini niliona kwamba ningegeuka uso tu, ningekwisha kazi. Nilijua hata mimi huo ndio mwisho wangu. Mara nyingi huwa katika hatari kama hizi, lakini kwa mwujiza wa Mungu hutokea nikaponyoka. Mara hii mambo yalionekana kuwa tofauti kwani watu hao hawakuweza kufanya kosa hata moja.

"Wewe ni nani, na unafanya nini hapa?" Niliulizwa.

"Mimi naitwa Joe Masanja, na nimekuja hapa kumtazama huyu Fred Kamau ambaye ni mwandishi mwenzangu. Sote tunaandika habari juu ya maonyesho ya mavazi ambayo yameanza hapa. Na nimestaajabu sana kumkuta ameuawa." Nilinyamaza kisha nikasema kwa upole mwingi, "Lakini mbona unanijia kijeshi namna hii, kama kwamba miye nimefanya jambo lolote? Ninashangaa kujiona nimeshikiliwa bunduki mgongoni. Ninaweza kuzimia hivi. Na wewe ni nani? Niliuliza.

"Nyamaza," alijibu "sina muda wa kujibu maswali yako, nimo kazini. Ila nataka kujua uliingiaje humu! Mlango ulikuwa umefungwa. Na kwa nini baada ya kuingia humu ukaonekana kuchunguzachunguza vyumba vilivyo karibu na hiki, kama kwamba ulikuwa ukijua kwamba ulikuwa unafuatwa?"

"Nilifungua mlango kwa kutumia ufunguo niliopewa na huyu rafiki yangu Fred, maana alikuwa na funguo mbili. Nilikuwa nimesahau nambari ya chumba ndiyo sababu ilinibidi nithibitishe ni kipi kati ya hivi vitatu,"nilimjibu. Wakati huo zilikuwa zimepita dakika arobaini na saba, na simu ilikuwa bado haijalia. Hivyo nilizidi kukabiliwa na wasiwasi.

"Wewe ni mwongo - mwongo nambari moja. Hii inaonyesha unafahamu mambo mengi kuliko hivyo unavyotaka kusema. Huyu si Fred ila ni afisa wa upelelezi aitwaye John Mullunga,"  alijibu kwa sauti ya hasira. "Na siye tulikuwa tunajua kwamba atakuja mtu wa aina yake kuangalia. Na wewe lazima ni mmoja wao, ila tu unajidai ni mwandishi. Hivyo lazima na wewe ufe kusudi tuweze kuendelea na mipango yetu."

"Hayo ni maneno yako wala si yangu. Na hata kama ukiniua, siku moja nawe utakamatwa. Miye sikuwa nikijua kuwa huyo ndiye John Mullunga. Na wewe tu ndiye umeniambia maneno haya. Na kama huyu kweli ndiye John Mullunga ambaye nimesikia habari zake, na nyiye mmemwua, basi serikali ikifahamu, itawawinda mpaka watawatia vitanzi." Nilimueleza.

Wakati wote huu nilikuwa nasema kusudi dakika zizidi kwenda ili pengine baadaye nipate mkombozi. Alianza tena kunitisha, "Maiti huwa hazielezi habari. Sitakusikiliza kwa maana wewe ni maiti tayari." Alianza kucheka kisha akaniambia,"Toa sala zako za mwisho. Na kama wewe pia ni afisa wa upelelezi, serikali itatukoma, maana hizi serikali bado hazitutambui. Na 'bosi' wangu nadhani atafurahi sana kusikia John amekufa na kijishenzi kingine."

Wakati huu wote nilikuwa nafikiri namna ya kuweza kujiponyesha. Lakini niliona hakuna. Bastola yangu nilikuwa nayo kwapani lakini nilijua nikijitingisha kidogo tu nitaingia kuzimu! Kwa hasira na uchungu nikasema, "Niue basi sasa unafanya nini? Unapoteza muda wako."

"Fumba macho, usali kwa dini yako, ama vyovyote."

"Naomba nipige magoti basi." nilisema.

Alicheka akasema, "Lo! Nadhani polisi watakaokuja humu watapata tishio, kwani watakukuta wewe umekula risasi sita hali umepiga magoti kitandani unasali. Halafu wataona rafiki yako amelala kifudifudi hapo chini, akiwa kama anaomba msamaha. Naye pia amekula risasi zipatazo sita." Sauti ya huyu mtu ilinionyesha kuwa ni mwuaji, na ni mtu ambaye anafurahia kuua. Pia alionyesha kuwa mtu katili na jambazi.

Nilikuwa wakati wote huu nikifikiria njia ya kujiokoa. Na kule kuomba nipige magoti, ni jaribu la kwanza kama huyo mtu akikubali tu nimtengeneze mara moja. Nikajifanya kuwa nilikuwa natetemeka ovyo. Bastola yake ilikuwa nusu inchi kutoka kwenye mgongo wangu. Nikabaki katika kufikiria jinsi ya kuirusha. Nilijua kuwa mtu huyo alikuwa mwuaji na hatanihurumia.

Mama-Willy alinishauri siku moja kwa kusema. "Mwanangu kama umo hatarini, usife kama kondoo, kufa kama mwanaume ambaye wakati wa kuzaliwa mama yake alishikwa na uchungu wa ajabu."

Tangu siku hiyo sikukubali kufa kikondoo. Basi niliposogea kwenye kitanda, hili jambazi lilipitisha mkono kwenye koti langu. Likatafutatafuta na kukuta bastola yangu ambayo aliichukua. Halafu likacheka. "Yee, eti wewe ni mwandishi. Mwandishi gani anatembea na bastola, automatic '45' katika Afrika ya Mashariki? Mawili, wewe ni jambazi ama afisa wa upelelezi."

Wakati huo akizungumza nilijua nimeishapatikana. Nukta yoyote ningeweza kula risasi. Na kicheko alichocheka kilikuwa cha hasira. Nilisikia akiitupa bastola yangu upande mwingine wa chumba. "Upesi piga magoti. Huwezi kunidanganya mimi ati ni mwandishi. Ingekuwa Marekani ningelikubali, lakini Afrika ya Mashariki usinitanie."

Wakati ninapiga magoti na huku najifanya kama kwamba natetemeka, nilitupa shoto langu kama umeme. Kufumba na kufumbua, bastola ya hilo jambazi iliruka na kwenda kwenye pembe moja ya chumba. Hapo hapo nikamgeukia. Akanitupia ngumi moja, nikaikwepa. Nikatupa shoto langu tena likampata kwenye taya mpaka chini. Ilivyo ni kwamba shoto langu likikupata, ukiwa dhaifu hutaamka tena hadi siku Yesu atakapokuja kwa mara ya pili!

Niliruka mpaka alipo, lakini akanipiga kwa mguu tumboni. Nikaenda kuangukia kitanda! Wakati huo alikuwa ameisha simama. Akanijia wakati nikijaribu kusimama. Akanitia ngumi shingoni na kujikuta niko chini! Halafu akanitia teke la usoni na kuikimbilia hiyo bastola. Kabla hajafika niliruka kama swala na kumchukua 'judo' mpaka kitandani. Katika maisha yangu ya miaka sita katika kazi hii sijaonana na mtu kama huyu. Kweli siku hii, lo, maisha yaliniwia magumu. 

Kabla hajasimama nikamtia ngumi nyingine kwa mkono wangu wa kulia. Na hapo nikaona amedhoofika. nikaondoka kukimbilia bastola. Kabla sijafika nilipata teke la mgongoni na kunifanya nipepesuke. Kabla hajashika hiyo bastola nilimpa tena shoto langu mpaka akaanguka chini. Nilimfuata hapo chini na kumtia teke la tumboni, na jingine ubavuni. Maana majitu kama haya, ukijigamba kuyapiga kichwani tu utacheka. Yanavyo vichwa vigumu kama paka.

Alipodhoofika kabisa niliiendea bastola. Kurudi nikakuta amezimia. Ilikuwa yapata saa tano na robo za usiku sasa. Niliendea chupa ya "whisky" iliyokuwa humu chumbani na kuanza kummwagia na kumnywesha kidogo kidogo. Kisha akaanza kuzindukana. Hapo nikashikilia bastola yangu kwenye taya lake.

"Niambie wewe ni nani, la sivyo utameza risasi zote hizi zilizomo katika hii bastola," nilimwambia.

"Yeeeh, sitaweza kusema hata ufanye nini na afadhali uniue tu," alijibu.

"Sasa kama hutaki kusema jina lako huyu uliyemuita 'bosi' wako ni nani?"

Hakujibu alinyamaza tu. Nikaona nisipokuwa katili hapo sitaweza kupata fununu yoyote. Niliwasha kiberiti changu. "Usiponieleza jina lako nitakuchoma masikio yako ingawa unaonekana kuwa hujali."

Basi nilisogeza moto kwenye sikio lake nikaanza kumchoma. Kwanza alijifanya hajali ingawaje alionyesha kuhisi uchungu wa ajabu. Hii ilinionyesha kuwa yeyote yule ambaye anaitwa 'bosi' wa watu hawa lazima anajua kuchagua watu wake. Kwani kweli ni wanaume. Ni watu wachache sana wanaoweza kuvumilia moto. Lakini maumivu yalipozidi alianza kuguna halafu akaanza kulia.

Mwishowe alisema, "Acha, niachie, nihurumie. Ngoja nitakwambia, hebu niache."

Nilitoa moto penye sikio lake kumpa nafasi aseme.

"Mimi naitwa

Kabla hajasema jina lake alipigwa risasi toka dirishani. Akafa! Niligeuka kutazama aliyemwua, lakini sikuona mtu. Na wala sauti ya bastola au bunduki iliyomwua sikuisikia. Hii ilionyesha kuwa bastola zao zote zina viwambo vya kunyamazisha sauti, ambavyo huitwa "sailensa."

Kupigwa risasi kwa  mtu huyo kulinipa wasiwasi zaidi. Moyo ulipiga mara nyingi mno. Chuki ilinijia maana hawa watu wanaonekana kuwa wameipanga mipango yao kiasi cha kwamba wanahakikisha hawafanyi makosa, hata chembe ya kosa. Nilikata shauri nitoke hapo mahali. Niliangalia zile maiti kwa mara ya mwisho. Nikaamua kwenda kuuchunguza ule mfuko wa John kabla sijaondoka. Lakini kabla sijafika kwenye huo mfuko, nilisikia sauti ikisema, "Simama hapo hapo ulipo, na usijitingishe."

Moyo uliniuma na hofu ilinizidi kwani niliona mara hii hawatafanya makosa kama mara ile.

"Angusha chini bastola yako," mtu huyo nisiyemtambua alisema kwa sauti ya hasira.

"Geuka unitazame."

Niligeuka upande wake na huku nimeinua mikono juu. Huyo mtu alionekana katili zaidi ya yule mwingine. Alikuwa kijana mwenye sura mbaya mbaya. Mweusi na mwenye umri upatao miaka ishirini na minane. Kwa umri tulikuwa tukilingana.

Mimi pia nilikuwa nina umri wa miaka ishirini na minane. Na kuadhimisha sikukuu yangu ya kuzaliwa ilikuwa wiki moja toka siku hiyo. Nilimwacha Della akialika watu kwenye hiyo sikukuu yangu. Lakini huenda badala ya kuadhimisha sikukuu yangu ya kuzaliwa, watakuwa wakiadhimisha matanga yangu, siku hiyo. Maana sasa kila dakika ilinuka kifo kitupu. 

"Mara hii hatutafanya makosa. Huyo mshenzi waahedi hapo chini, alifanya makosa na ndiyo sababu na yeye amepata zawadi yake. Wewe ni nani? Maana unaonekana kuwa tisho kwetu zaidi ya wengine wote. Hakuna aliyewahi kupambana na Kasha akabaki mzima. Hebu nipe maelezo kwa kifupi. Maana utake usitake utakufa tu. Huwa sifanyi makosa mimi."

Nilipomtazama alionekana kuwa mtu ambaye hawezi kufanya makosa. Niliomba Mungu kimoyomoyo na kuanza kutubu makosa yangu.

"Mimi naitwa Joe Masanja. Na ni mwandishi wa habari juu ya 'Maonyesho ya Mavazi," Nimetoka Mwanza. Tanzania," nilisema.

"Pumbavu wee, unadhani unaweza kunidanganya mimi, mwandishi hawezi kuwa jasiri kama wewe hata kuweza kumshinda nguvu Kasha," alisema, kisha akanipiga kofi moja mpaka nikaona jua, ingawaje ilikuwa usiku. Fahamu zikaniruka kwa muda. Ziliporudi nilikuta bado ameshikilia bastola yake na kuniuliza tena mimi nilikuwa nani. Nilimjibu vile vile, "Oke, oke, mimi sitajali kama kesho nitakuona ukila chakula cha mchwa," alisema kwa kiburi sana.

Nilifumba macho maana niliona ndio mwisho wa maisha yangu. Hapo sikuwa na ujanja wowote . Kwani huyu kijana anavyoshikilia bastola, afadhali naye yule, mchezaji wa sinema wa kule Mexico, "Cowboy Cuchilo."

Wakati nilipoona anakaza mkono wake kuachia risasi, kufumba na kufumbua nilishtukia anaanguka chini. Alikuwa amepigwa risasi! Taratibu akakata roho! Niliruka mara moja kuchukua bastola yangu tayari kwa matata mengine yoyote. Mlango ulipofunguliwa nilikuta ni Sammy.

Kwa mara nyingine tena Sammy alikuwa ameponyesha maisha yangu, la sivyo dakika hii ningekuwa mfu.

"Willy - naona walikuwa wamekusakama sana. Sasa, tukimbie tutoke hapa ili ukanieleze jinsi mambo yalivyokuwa, alininong'oneza Sammy.

Kulikuwa na maiti tatu hapo chumbani sasa. Kabla sijatoka hapo chumbani nilienda kwenye mkoba na kuanza kukagua kagua. Nikaona hamna la kutusaidia. Tulipitia dirishani na kutelemkia  kwenye ukuta na kutokea kwenye kijinjia.
Tulikimbia toka hapo mpaka River Road.

"Nilipiga simu baada ya dakika arobaini na tano kama ulivyosema," alisema Sammy," Simu ilionekana kuwa ilikuwa imekatwa, kwa hiyo tukaanza kuingiwa na wasiwasi. Ikabidi tungojee kwa muda wa dakika ishirini tena. Nilipotoka tu baada ya dakika kama tano hivi Lulu naye hakuonekana tena. Pia vijana fulani watatu waliokuwa wakienda lakini tukaona mambo yasingekuwa mazuri sana kwako. Maana usingalijua tumekwenda wapi. Baada ya kungoja kwa dakika ishirini tena, mimi na Robin tulianza kuwa na wasiwasi. Kwa hiyo mimi nikakata shauri nikufuate na kumwacha Robin humo Klabuni kuzidi kuchunguza.

Nilichukua taxi hapo nje mpaka nyuma ya Hilton Hoteli na kuanza kutembea kwa mguu mpaka hapa hotelini. Ndani ya bar watu walionekana kushughulika na ulevi. Kwa hiyo mimi nilienda kwenye kaunta na kuagiza 'bia' moja. Nilianza kumwangalia kila mtu kwa usiri sana. Mwishowe ndipo nikamwona mtu akipenya kwa haraka kati ya mlango mmoja unaotokea nje kwenda mwenye vyumba vya kulala. Huo mlango umeandikwa "HAKUNA KUPITA HAPA."

Nilipoona hivyo nilitoka kwenye 'kaunta' kwa siri na kuingia katika vyumba vya huko juu. Halafu nikangoja. Kwanza mtu huyo aliingia katika chumba cha mkono wa kulia. Baada ya kukaa kidogo alitoka na kuingia humu. Wakati wote huu miye nilikuwa nashindwa kutoka, kwani kulikuwa na wafanyakazi wa humu hotelini wakifanya kazi.

Alipotoka ndipo nikakimbia na kuingia katika chumba cha upande wa kulia. Baada ya kuchungua sana niliona hakikuwemo chochote humo. Ila ukutani katika pembe moja kuna matundu matatu. Haya matundu yanatosha kuingiza mdomo wa bastola. Na ninadhani ndimo huyu mtu wa pili alimomwulia mtu wa kwanza. Na kwa kutumia tundu hilo hilo ndimo mimi nimemwua huyo jamaa. Na nimetumia 'sailensa' hata mimi," alimaliza Sammy.

Na mimi nikamweleza mambo yote yalivyotokea.

Sasa tulijaribu kuunganisha mambo yote yalivyotokea.

Inaonekana hawa watu walijua John amekuja kufanya nini kwa hiyo walitumia kila njia wamwue. Pili wanajua kuwa kuna watu ambao watafanya kazi hii na John, hivyo walikuwa wanavizia mtu yeyote ambaye angekuja katika chumba cha John. Nilipokuwa nimepiga simu mara ya kwanza inawezekana hawa watu walikuwa chumba cha pili. Nilipokata simu, nadhani walionelea wakate waya wa simu, ndiyo sababu wewe uliponipigia haikuweza kulia kengele.

Nilipofika mimi walijua lazima ndiye mwenzake John, hivyo lililokuwepo ni kuniua hata mimi. Nilipoweza kumshinda Kasha. huyu mtu wa pili alikuwa chini ya hoteli akimngojea Kasha. Kasha alipokawia akaona aje aangalie. Alipofika humu hakuja moja kwa moja, akaona aingie mwenye chumba hicho cha pili sababu alijua kuwa wameshatayarisha hayo matundu. Alipochungulia aliona nimeshamshinda nguvu Kasha. Na Kasha alikuwa karibu atoe siri, kwa hiyo ikambidi amwue Kasha kabla hajasema.

"Angeniua na mimi papo hapo lakini alitaka kuwa na hakika mimi ni nani, kwa vile alivyodhani anaweza kunilazimisha kusema. Nilipokataa kumwambia uhakika aliona aniulie mbali, lakini wewe ukamuua kabla. Huyu mtu wa pili alionekana kuwa wa maana zaidi katika huu uhaini kuliko Kasha. Sasa lililopo ni kutaka kujua hawa ni akina nani." Nilinyamaza kumeza mate.

"Maswali ya kujiuliza sasa ni mawili au matatu. Je walimfahamuje John, mapema hivi? Je huyu mwenye hoteli ana uhusiano nao? Sammy alitaka kuzungumza.

"Willy mimi naona kuwa wewe uende tena huko Princess maana sasa ni saa sita kasoro robo. Miye nitarudi Starlight nikamwone Robin. Huenda akawa na jambo. Halafu wewe nenda kazungumze na wafanyakazi wa hapo upate kujua lini chumba hicho kimeacha kutumika. Nadhani vijana wa Robin wamemvia Lulu kwa hiyo huenda Robin anaweza kuwa na jambo juu ya Lulu na watu wake. Hizo maiti hazitatambuliwa huenda mpaka kesho asubuhi. Hii itatupa muda wa kutosha kufanya kazi zetu.

Ukitoka Princess njoo moja kwa moja mpaka Starlight Klabu kabla ya saa saba. Ukichelewa tutajua huenda umesakamwa na siye tutakimbia kuja hapo."

Mawazo ya Sammy niliyaona kuwa ya busara sana. Kwa hiyo tulifanya kama alivyosema. Nilikodisha gari toka River Road kupitia Compos Robeiro mpaka Princess. Sammy naye akakodisha gari kwenda zake Starlight.

Nilipofika Princess nilikuta watu wote bado wanashughulika na kunywa, na kila mtu alijali mambo yake. Wengi walikuwa wakimalizia vinywaji vyao kwani saa za kutoka zilikaribia. Katika pembe moja nilimwona msichana mmoja ambaye hakuonekana mwenye furaha hapo halipoketi. Nilipokuwa nikimfuata hakuonekana kupenda nimfuatie hivyo.

"Habari zako binti," nilimsalimu. Badala ya kunijibu alinitizama tu. Nilikaza roho kiume, nikaenda kukaa kwenye meza moja naye. Uso wake ulionyesha uhasama wa chuki, ingawa sura yake ilikuwa na haiba kiasi cha kutosha .

"Mbona nyiye wanaume hamwezi kujali mambo yenu wenyewe? Huko kuniona hapa unadhani mimi natafuta wanaume?" Alisema kwa dharau.

Si hivyo bibie. Miye mwenzio si mwenyeji sana hapa. Nimekujia ili unisaidie mambo mawili hivi. Na hakika nilistaajabu kuona kisura kama wewe kukaa peke yako hapa pembeni tena ukionekana mwenye kuwa na huzuni. Je, kuna jambo lmekuudhi? Ama ikiwa ni shemeji aliyekuudhi, nitumie nikamsihi," Nilinyamaza nikitabasamu.

"Sema basi unataka nikusaidie nini? Miye hapa napumzika na kawaida yangu huwa sipendelei sana kukaakaa na wanaume wanaokunywa pombe. Ndiyo sababu nimekaa hapa peke yangu. Wewe ni nani?" Aliuliza.

Mimi ni Joe Masanja, mwandishi wa habari juu ya maonyesho ya mavazi. Ninatoka Mwanza. Tanzania. Hii ni mara ya yangu ya kwanza kufika Nairobi. Nina haja ya kujua baa hapa Nairobi zinafungwa saa ngapi siku za jumapili?"

"Nenda uulize huko baa," alijibu kwa hasira.

"Ah binti! Mbona wasichana wa Nairobi wakali hivi? Msichana kama wewe hufai kuwa mkali kwa kijana kama mimi. Uzuri wako unakutaka uwe mkarimu na msikivu ili uweze kuziliwaza nyoyo za watu dhalili kama miye." Nikamjengea tabasamu pana la haiba.

Maneno hayo yalimlainisha kiasi. Ukitaka msichana afurahi, mwambie kuwa midomo yake ni mizuri na mitamu. 

"Wanafunga saa saba, lakini unaweza unafungiwa ndani ukaendelea kunywa mpaka huenda hata saa tisa," alijibu.

"Jee unaitwa nani, na unakaa wapi?"

"Mimi naitwa Lina Samson. Kwetu Nakuru, lakini kwa sasa niko hapa kwa mapumziko kidogo ya mwezi mmoja. Ninaitambua vyema Nairobi sababu nilizaliwa nikakua na kusoma papa hapa mpaka baba alipohamia Nakuru, ambako ndiko masikani hasa," alijibu hali akimwemwesa.

"Sijui kama nitakuona tena Lina. Ningependa kukuona mara nyingi kama hutajali,"

"Ninaishi Guaden Hoteli chumba nambari kumi. Unaweza kupiga simu hapo hotelini, na watakuunganisha na chumba changu. Alamsiki," alimalizia hali akisimaa kujiandaa kuondoka hapo. Akaondoka.

Nilizunguka zunguka kidogo humo ndani kusudi niweze kuona kama naweza kumpata mfanyakazi anayeweza kuaminika kidogo. Nilimuona kijana mdogo hivi, apata umri wa miaka ishirini. Nilitoa noti ya shilingi mia na kumpa. Utafikiria kuwa huenda natumia pesa vibaya, lakini ukitaka cha uvunguni sharti uiname. Kijana kama huyo wakati wa mwambo kama huo ukimpa shilingi mia atakueleza hata yale aliyoyazungumza na mpenzi wake faraghani. Kijana huyo aligutuka sana hata akaniuliza, "He, unataka nini, pombe gani?".

"Hiyo fedha nimekupa, chukua ni yako. Sasa tafadhali naomba unielezee habari fulani fulani, Mbona chumba nambari hamsini hakina kitanda wala mtu?"

"Hicho chumba hakina mtu kwa sababu kinavuja kwa juu siku za mvua. Na siku hizi kuna manyunyu mengi".

"Kimeanza lini kuvuja?"

"Leo kiasi cha saa nne hivi kama unakumbuka kulikuwa na manyunyu,"

"Nambari hamsini na moja kulikuwa na mtu?"

"Ndiyo, mtu mmoja toka Uganda aitwae Fred, ndiye alikuwa amepanga humo kuanzia saa moja asubuhi."

"Kuna mtu yeyote aliyewahi kuingia chumba nambari hamsini kutoka nje wakati wa mchana?".

"Ndiyo, mtu mmoja aitwae Benny, alikuja na watu wengine watatu hivi. Waliingia kukitazama kama wanaweza kukiziba, lakini baada ya kukikagua sana walisema hawawezi, wakaenda zao. Sifahamu wanakaa wapi", alimaliza.

"Basi usimwambie mtu yeyote nilivyokuuliza."

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU