KUFA NA KUPONA

SURA YA SITA.

Benny Aja juu.

Alipofungua mlango tu nikaupiga teke mkono wake uliokuwa umeshikilia bastola. Bastola hiyo ikaanguka kama hatua tatu hivi upande mwingine wa chumba. Nilikuwa nimeishatoa bastola yangu na kuiweka tayari mkononi. Alitaka kupiga kelele, lakini nikamuonyesha bastola, kwa hiyo akafunga akanyamaza.

"Funga hilo domo lako, la sivyo ukilipanua tu, risasi zote zitamalizikia ndani yako."

"Jina lako nani?" Wakati huo nikimuuliza tumeishaingia ndani na huku nimefunga mlango. Nilipomuuliza hakujibu. Kufumba na kufumbua wakati nikigeuza kidogo macho yangu upande mwingine akaipiga teke bastola yangu. Nayo ikaanguka mahala pengine. Hapo hapo akanitia ngumi moja mpaka nikaanguka chini. 

Nilipokuwa nikiribu kusimama, akanitia nyingine, mpaka chini. Kweli huyu kijana, anajua kuzipiga, maana ngumi zake zinatoka mfululizo kama nini. Alipogeuka kuchukua bastola nilijikunja na kumpiga 'Farasi teke' mgongoni mpaka akaanguka chini. Nilisimama upesi upesi, na kabla yeye hajasimama nilimtia teke moja la usoni mpaka akaona nyota na kuzirai.

Nilimwendea hapo chini na kumsukumasukuma. Kisha nikaiendea bastola yangu na kumsogelea. Alipoanza kupata fahamu nilianza kumuuliza tena. "Jina lako ni nani?" 

"Naitwa James, na wapenzi wangu huniita Jim, lakini wewe sitaki uniite Jim maana ni adui yangu. Tangu nizaliwe sijapigwa na mtu namna ulivyonipiga wewe kwa hivyo niite James, koroboi we." 

"Unamfahamu Benny?"

"Ndiyo"

"Tangu lini"

"Kwa muda wa mwezi hivi."

"Kwani umekaa hapa Nairobi kwa muda gani?"

"Yapata miaka kumi sasa."

"Na kama Benny pia anakaa humu humu mjini mbona mlikuwa muda wote hamjafahamiana?"

"Kwani wewe unajua watu wote wa Mwanza?" alinijibu kwa jeuri sana.

"Nani amekuambia natoka Mwanza?"

"Lulu na Benny"

"Kwa nini ulimbadilisha Lulu kutoka kwenye jukwaa kabla ya zamu yake?"

"Hiyo ni kazi yangu si yako. Unataka nini?" alisema kwa wasiwasi hali akitazama dirishani."

"Nilipotupa macho nyuma kuangalia mlango ulifunguliwa na kijana mwingine akaingia ndani huku ameshikilia bastola mkononi. Nilijipindua mara moja na kumweka James juu yangu. Kisha nikasimama naye huku nimemfanya ngao yangu. 

"Eh, kumbe una akili za kutosha." alisema huku sauti yake ikigundagunda. 

"Jaribu, na kabla ujaniua mimi utakuwa umemuua James kwanza. Si ajabu hiyo?"

"James hana thamani sana akifa zaidi ya kifo chako. Kilivyo na thamani!" alijibu huku uso wake umekunjamana.

Ghafla nilimsukuma James na kumwangukia mwenzake na hapo wote wakaanguka chini. Kabla hawajasimama nilipiga teke mkono ulioshikilia bastola. Kisha nikaanza kuwapa kazi. Kijana huyo aliposimama nilimpiga kichwa mpaka chini. James akatupa ngumi lakini nikaepa. Nilimtia kichwa mpaka akatabawali. Maana alikuwa bado na maumivu ya magigano ya kwanza. Huyo kijana akabeba kiti na kunitupia lakini nikawahi kukidaka. Nilimtwanga kwa kiti hicho kichwani na kumfanya apepeseke mpaka ukutani. James alikuwa hawezi kusimama sasa ila kubaki akikoroma tu. Kijana huyo mwingine akaniwahi kwa ngumi moja kwenye shavu. Loo! mikono yake ni kama chuma, jino langu moja likanitoka. Hasira zilivyonipanda Mungu ndiye ajuaye. Maana sijawahi kupingwa ngumi mpaka jino likatoka. Kutokana na hiyo hasira nikamtia ngumi tatu mfululizo. naye akawa kama James.

Kwa bahati nikaiona kamba hapo ndani. Kabla hawajapata fahamu, niliwafunga pamoja kwa ustadi sana kisha nikafuata maji ya barafu na kuwamwagia. Walipopata fahamu nilivuta kiti nikakaa huku nimeshikilia bastola yangu mkononi.

Tuue basi unangoja nini?" alisema huyo kijana mwingine.

"Nitauaje watu waliokwisha kufa wenyewe?" nilijibu.

"Maana ya kutufunga hivi kama magunia ya kauzu ni nini?" aliuliza James.

"Maana nimeona nyinyi ni watu hatari sana." 

"Sasa nadhani utajibu maswali yangu James maana utani sasa umekwisha. Jina langu ni Willy, Willy Gamba, wa Idara ya upelelezi ya Tanzania lakini ambayo inafanya kazi bega kwa bega na Idara za namna hii katika Afrika nzima." niliposema jina langu, kila mtu alitoa macho ya woga. 

"Kama ni Willy Gamba, nitajibu maswali yako yote, sina njia nyingine. Lo! Kunaonekana kuna makubwa hapa mjini mpaka wakakuleta wewe. Maana nimeishasoma habari nyingi juu yako na vituko vyako vyote. Sina njia, uliza tu. Niko chini ya miguu yako," alijibu James.

"Mimi sikujua kama ni Willy na kama ningalijua nisingethubutu kukufuata." alisema huyo kijana mwingine.

"Nani alikutuma kunifuata?" nilimuuliza.

"Benny, ndiye alinituma."

"Kwa nini alikutuma kunivizia?"

"Alisema kuwa wewe unaonekana mwenye kuingilia mipango yake na hivyo lazima uuwawe mapema, kusudi mipange iweze kufanyika kesho usiku."

"Mipango gani hiyo?"

"Sijui, na hakunieleza zaidi."

"Wewe ni nani wake mpaka akutume kuniua.?" 

"Mimi nimeanza kumfanyia kazi tangu juma lililopita, sababu najua kutumia bastola. Nimewahi kuwa jeshini kwa muda."

"Alikwambia kwa nini anataka mtu kama wewe?" 

"Ati kwa sababu yeye ana pesa nyingi."

"Unamfahamu Lulu?"

"Ndiyo."

"Ni nani?"

"Ni mpenzi wa Benny."

"Tangu lini?"

"Sijui"

"Benny alipokuwa akikutuma Lulu alikuwepo?"

"Ndiyo"

"Lulu alisema nini juu yangu?"

"Naye alisema kama Benny tu, ila aliongezea kuwa lazima nikuendee vizuri maana unaonekana kuwa mtu mbaya sana." 

Kisha nilimgeukia James, "Jim mpenzi, jibu swali langu ambalo nilikuuliza kabla kikaragosi cha Benny akijatuingilia."

"Hebu uliza tena"

"Kwa nini ulibadilisha wakati wa Lulu kuja kwenye jukwaa?"

"Kwa sababu niliona ishara toka kwa Benny."

"Ishara gani uliona?"

"Alishika na kurekebisha tai yake."

"Ulijuaje kuwa hiyo ni ishara ya kukuambia ubadilishe wakati wa Lulu kutoka?"

"Benny alikuwa ameniambia kuwa kuna watu wanaomtafuta, na yeye ni lazima awafutilie mbali kabla wao hawajafanya hivyo, na tena alisema kwamba anashughuli zake ambazo anataka ziishe kabla ya kesho kutwa asubuhi. Hivyo akanipa pesa ili nimfanyie kama alivyokuwa akitaka. Ati kwa sababu Lulu alikuwa akichukua mawazo ya watu, aliona kuwa akitaka wauwawe wangeweza kuuawa bila watu kujua nani amewaua."

"Kwa nini hukukataa?"

"Kwa sababu angeweza kuniua hata mimi, ndiyo alinitisha."

"Ulimuona mtu aliyemuua yule mtu aliyekufa pale ukumbini." 

"Hapana sikumuona, lakini nilifikiria wewe unajua." 

"Kwa nini ulichukua bastola nilipogonga mlangoni."

"Kwa sababu nilikuwa na wasiwasi juu ya mambo niliyokuwa nimeambiwa na Benny."

"Huwa unakaa na bastola hapa kwako, ama umepewa leo tu kuitumia.?"

"Nilipewa na Benny niitumie iwapo nitafuatwa na mtu yeyote."

"Kuna mtu mwingine yeyote anayeshirikiana na Benny?"

"Sijui hajaniambia lakini nafikilia huenda yupo, maana baada ya Lulu kuingia kwenye jukwaa leo, Benny alienda kupiga simu."

"Kuna watu wangapi waliotumia hiyo simu leo tulipokuwa kwenye maonyesho?"

"Ni Benny tu niliyemuona"

"Nambari ya simu aliyotumia Benny ni ngapi?"

"Una maana alikokuwa akipiga ama ile aliyokuwa anatumia?"

"Nina maana zote."

"Alikokuwa akipiga sijui, lakini ya mle mwenye 'hall' ni 21899."

Niliwambia wafunge midomo yao, mpaka baada ya siku mbili hivi. Nilionelea niwaache hivyo ningemwambia Robin aje awachukue awaweke ndani kwa siku mbili hivi." 

"Haya wajomba, kama mnataka usalama fanyeni kama nilivyowaambia, na ujanja wowote, mnaweza kujikuta mko ndani zaidi. Na ndipo mtalia na kusaga meno." Niliondoka nikawapigia Sammy na Robin simu. Nilimweleza Robin juu ya hawa watu na jinsi ya kuwafanya. Akasema angefanya kama nilivyomwambia. Na pia akanieleza anahisi kupata fununu ya jambo fulani kwa hiyo lazima nimwone asubuhi hotelini kwake mnamo saa tatu hivi. Pia nilimweleza kuwa sasa naenda kumwona Lulu na nikamwambia Sammy apige huko hotelini kwa Lulu simu itimiapo saa nne hivi. Na kwamba ikifika saa nne na nusu bila ya kuniona aje huko hotelini kwa Lulu, huenda nitakuwa nimo msambweni.

Nilipiga simu kwenye Idara ya Uchunguzi nikawaeleza wanitafutie nambari za simu ambako simu ilipigwa kutoka kwenye simu nambari 21899 mnamo saa kumi na mbili na nusu. Na wakasema hiyo ni kazi rahisi. Pia niliwaambia wanipe jina la mtu mwenye simu hiyo, wakasema pia kuwa hilo lisinitie shida ni kazi ndogo.

Basi hatimaye niliondoka kwenda Hoteli Intercontinental. Nilipokuwa naingia nilimkuta Peter na Wazungu fulani fulani pamoja na wapigania uhuru wengine wakinywa kahawa katika chumba cha kahawa. Aliponipungia mkono nikaenda kuwasalimu. Nilikuta Wazungu wote hao walikuwa Marekani na walikuwa wanatoka katika Baraza la Umoja wa Mataifa, kwenye sehemu inayoshughulika na Afrika Kusini. Ilionekana walikuwa wamekuja kwa mazungumzo na wapigania uhuru.

Walininunulia kahawa, baadaye Peter na hao wageni wake iliwabidi waondoke wakalale maana walikuwa wamechoka. Nilimwuliza Peter kama amemwona Lulu, akasema alimwona akiingia ndani, lakini hajatoka nje. Pia nilimwuliza kama kuna mtu mwingine yeyote aliyekuwa ameingia na Lulu, akasema hakumwona yeyote. Basi tuliagana wao wakaenda zao miye Willy, nikakaza roho kupanda chumbani kwa Lulu.

Vijana wa Robin walikuwa wameishapata hata nambari za chumba cha Lulu. Nilienda moja kwa moja mpaka kwenye kile chumba. Lakini kwanza nilihakikisha hakuna mtu aliyeniona huko juu.

Hoteli Intercontinental ni nzuri sana na ghali. Na kama wee ni 'giriki' nusunusu huwezi, na msichana Lulu anatisha maana mtu wa kukaa katika hoteli hiyo lazima awe 'giriki'hasa. Hiyo ninaweza kusema kwamba Lulu ni 'giriki' hasa, ila sivyo asingeweza. Maana wanawake wengine wote wa kwenye maonyesho hata waliotoka ng'ambo ni yeye tu anayekaa hapa. Na kama kuna mtu aliyempangishia, lazima huyo mtu awe na pesa si mchezo. Na hii nadhani ndiyo  ilikuwa kweli hasa, maana Lulu alikuwa msichana mrembo hasa. Mtu yeyote mwenye fedha angemfanyia lolote analotaka. Ninaamini kwamba, Lulu akikuambia wende ukamwibie fedha ili awe wako, Wallah utakubali ufungwe ikiwa utashikwa, lakini ukaibe.

Nilipofika kwenye kile chumba niligonga mlango. Ulifunguliwa na Lulu huku akitabasamu "Karibu ndani, mbona unakuja kunitazama usiku hivi? Nadhani mchana lingelikuwa jambo zuri zaidi." Alikuwa akisema maneno yote haya huku amenishikilia mkono mpaka kwenye sofa.

"Uh, naweza kukusaidia?" 

"Maonyesho yako yamenipendeza sana mpaka imenibidi nije nikupe heko usiku huu," nilijibu. "Asante sana Joe nimefurahi kuwa umeweza kupendezwa na maonyesho yangu ukiwa kama mwandishi wa habari."

"Loo! Unakaa kwenye hoteli ghali sana Lulu, lazima baba yako awe tajiri sana."

"Hata, baba yangu ameisha kufa, na mama yangu pia."

"Huenda hata baba yako alikuwa tajiri sana, kuwa amekuachia mali nyingi sana. Na huenda kaka zako matajiri sana."

"Kaka yangu alikuwa mmoja tu, lakini alikufa huko Kampala kwa bahati mbaya baada ya kupigwa risasi wakati wa msukosuko kati ya Serikali na Kabaka. Halikuwa kosa la askari maana yeye mwenyewe ndiye alikuwa akizagaa mjini. Sasa niko peke yangu, na baba yangu hakuwa tajiri ila alikuwa anakijishamba kidogo cha kahawa tu, karibu na Kampala.

Tuseme maonyesho ya mavazi ndiyo yanayokuhifadhi kiasi hiki, eti?"

Aah Joe, unataka kuingilia katika maisha yangu? Nadhani ulikuwa ukija kunipa heko kama ulivyosema, lakini inaonekana sivyo. Nadhani utanibusu ukinipongeza!" Alisema kwa sauti ya mshangao sana.

Alisogea karibu yangu akanivuta. Akafungua tai yangu akaingiza mkono wake ndani ya shati langu na kisha akanibusu.

"Nimekupenda sana Joe, tangu nilipokuona siku ya kwanza katika Starlight Klabu. Oh! Sijui kwa nini sikuweza kukuona mapema."

"Kwani sasa unaye mpenzi wa kukuzuia usinipende?"

"Ndiyo nimeisha mpata, na naona siwezi kumwacha," alijibu huku akionyesha huzuni.

"Ni nani huyo?"

"Benny, yule niliyemfahamisha kwenye maonyesho."

"Tangu lini mmeanza mapenzi?"

"Tangu jana."

"Jana! Usinieleze, jana tu mmeisha ahidiana kuoana?"

"Kwani ni ajabu?"

"Mlikuwa mnafahamiana zamani?"

"Ndiyo, nilipokuwa nikija huku mara kwa mara alikuwa akinichukua katika gari lake."

"Ndiye amekupangisha katika hoteli hii naona."

"Ndiyo, Benny ana fedha si mchezo."

Kwa muda sote tukawa kimya. Kisha nikafumbua midomo, 
"Samahani Lulu, ninasikitika kuwa nina jambo la kukuuliza," nilisema taratibu huku moyo wangu ukipiga upesi, maana hata mimi sikupenda kumchukiza msichana Lulu.

"Uliza tu Joe."

"Kwa nini katika maonyesho ukiwa kwenye jukwaa kunatokea mauaji wakati huo huo?"

Aligeuka rangi, nywele zikamsimama. Alikuwa anafunguwa vifungo vya shati langu, akaacha. Alikuwa akinibusu, akaacha! Na hapo hapo midomo yake yenye joto ikiwa baridi. Kisha akajibu " Mimi sijui, maana huwa niko kwenye jukwaa."

Mbona leo wamekubadilisha zamu yako na kutoka mapema? Na ulipotoka tu yakatokea mauaji, hasa wakati watu wakikushangilia?"

"Wewe ni nani mpaka uulize mambo kama hayo? Wewe si Polisi, waachie Polisi, waje wauulize. Sitaki maswali kama hayo. Na kama ndiyo yaliyokuleta humu toka kabla hujajisikitikia kwa nini unauliza maswali kama hayo."

"Sisi waandishi wa habari ni wazungumzaji wa mambo mengi kwa hiyo usijali. Kama hupendi hilo swali sasa nikueleze jambo jingine."

"Jambo gani," alisema huku macho yake yakionyesha hofu tupu.

"Kabla ya maonyesho hayajaanza Benny alikuwa akizungumza na wewe. Na akakueleza kuwa wanataka kuwaua watu fulani fulani. Kwa hiyo wewe utaambiwa uende kwenye jukwaa baada ya zamu kubadilishwa na James, Kijana wa kwenye jukwaa ambaye angepata ishara toka kwake. Kisha wewe utatoka kwenye jukwaa na kuwatia watu moto kwa mikogo yako ya ajabu. Halafu wao watapata muda kwa kuua bila kutambuliwa."

Alianza kutetemeka baada ya kusikia mambo hayo,"Mbwa wa Kishenzi we, nani alikuambia mambo hayo yote? Na kwa nini, unaingilia mambo yasiyokuhusu. Toka humu kabla hujawa maiti." Aliposimama alikuwa ameisha toa bastola iliyofichwa katika gauni lake kifuani, chini ya matiti.

"Toka, toka nje ya chumba changu la sivyo utakufa. Pilipili usiyokula inakuwashia nini?"

Nilimjibu huku nikicheka, "Wasichana wazuri kama wewe, hawafai kuwa na bastola, hebu iweke bibie, huenda tutazungumza vizuri kidogo."

"Unadhani natania, nakuua sasa." Kabla hajafyatua bastola yake, nilikuwa nimeishashika mkono wake. Nikaupinduapindua vizuri sana. Nikaichukua bastola yake na kuiweka ndani ya mfuko wangu wa koti.

"Mama Joe aliniambia usiwadhuru wasichana wazuri bure. Sasa nieleze uhusiano wako na mauaji haya. Na kama hutasema, miye nina ushaidi kamili wa kuweza kukupeleka mahakamani na ukahukumiwa kutiwa kitanzi."

Mlango ulifunguliwa na Benny akaingia pamoja na vijana wengine wanne, wote walikuwa wameshikilia bastola mkononi. Lulu alikimbia mpaka kifuani kwa Benny. 

"Aha, mpenzi naona umeniletea zawadi nzuri sana, maana nilikuwa nimejaribu kuipata nimeshindwa." "Ahsante sana Lulu mpenzi."

"Wananchi waheshimiwa wenzangu, nadhani hamtastaajabu nikiwafahamisha kwa Willy Gamba, Mpelelezi maarufu sana katika Afrika hii. Anafanya kazi katika Idara ya Uchunguzi Tanzania. Naamini kila mtu anamjua kufuatana na usomaji wa habari zake katika magazeti ingawaje si kwa sura. Leo tunafurahi kuwa ndani ya mikono yetu na tunaweza kumfanyia lolote lile."

Alipokuwa akitoa hii hotuba yake fupi, niliona rangi za wengine wote zimebadilika sana hasa ya Lulu, na walionyesha mshangao mkubwa sana.

"Willy, ulikuwa mjinga sana ulipodhani umetufunika kwa kutumia jina la Joe Masanja kwamba ungeweza kutupumbaza! Lakini ujue kuwa kundi letu ni kubwa. Na lina watu wa aina nyingi na hata watu wenye vyeo vikubwa sana serikalini . Kwa vile kupata habari za aina yoyote ni rahisi sana. Hata John alipokuja hapa alijifunika kwa jina la Fred, tulijua mapema zaidi ya tulivyokufahamu wewe."

"Kwa nini ulimwua John?" Nilimwuliza.

"Kwa sababu alikuja kuingilia mipango yetu, jambo hata wewe hilo hilo muda si mrefu."

"Nilicheka hapo kidogo halafu nikamweleza, "Unadhani unaweza kusalimika na tendo hilo? Unajidanganya sana Benny. Ninakusikitikia kijana kama wewe kufa katika umri mdogo kama huu."

"Si mara yangu ya kwanza kufanya jambo kama hili, na nina akili zaidi yako na fedha zaidi ya kila mtu hapa Afrika ya Mashariki hasa itakapofika kesho kutwa nitakuwa na maelfu  ya fedha. Na unajua kila siku fedha zinaweza kuponyesha mtu, kwa hivyo sitadhurika hata chembe. Najua nikiisha kukuua wewe sasa hakutakuwa na kizuizi katika mipango yangu," alisema kwa dharau sana.

"Hizo karatasi ziko wapi Benny?" Niliuliza.

"Hilo siwezi kukuambia, maana hata hawa wengine hawajui zilipo ila mimi tu."

"Lakini jua kuwa ukiniua mimi hapa, Lulu atashikwa sasa hivi maana watu wote wanajua niko hapa kwake," nilimwambia nilipotazama saa yangu na kuona karibu saa nne u nusu Sammy anipigie simu.

"Eh, unadhani miye ni mtoto katika kazi hii! Huwezi kunidanganya kwa jambo hili hata kidogo, maana hata mimi nimewahi kutishia watu na uongo wa namna hiyo !" 

Alipotaka kuendelea kusema simu ililia, Lulu alienda kuijibu. Kisha aligeuka na kusema kuwa ilikuwa simu yangu. Benny alionyesha kuchukia kabla ya kusema, "Haya kaijibu tusikie utaongopa nini, mbwa we."

"Hallo, huyu ni Willy," nilijibu. "Oh, fanya hivi, kama usiponiona kwenye dakika tano hivi hapo basi, piga simu polisi uwajulishe habari yangu, na kwamba waje mpaka katika hiki chumba," niliendelea kusema.

"Ndiyo ndiyo, kumbe wengine wapo hapo chini, haya waambie hivyo. Asante sana kwa heri mpaka tutakapoonana kwenye dakika tano hivi," nilimaliza.

Wakati nikijibu simu, Benny, Lulu na wenziwe walionekana wamechukia sana. Tangu walipoingia wale vijana wanne walikuwa wameshikilia bastola zao tayari kufyatua baada ya kuamriwa tu na Benny. "Unasemaje mpenzi Benny, utaniua ama unaniachia huru niende zangu? Maana ukiniua tu utashikwa mara moja, kumbe hata polisi wengine wako nje ya hii hoteli," nilisema huku nikisimama taratibu kabisa.

"Oh, tutaonana siku nyingine Benny, na siku hiyo tutakapoonana si kama ambavyo tumeonana kirafiki hivi," Ilionekana hawakuwa na njia ila kuniachilia huru tu.

"Na wewe Lulu, siku nitakapokupata nitakupa siafu kwenye hayo mapaja yako wayaumeume, kusudi uweze kujikuna ovyo hata mbele ya baba mkwe wako,"

"Huwezi kuudhi mwanamke namna hiyo, na nitahakikisha kuwa unakufa kabla ya kesho jioni," alisema Lulu huku chuki imemjaa.

Alamsiki nyiye wote, niliondoka na kufunga mlango nyuma yangu.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU