STANBIC BANK YAJA NA AKAUNTI YA HATUA

Dar es Salaam
Stanbic Bank Tanzania imezindua akaunti mpya ijulikanayo kama HATUA, ambayo ni kwa ajili ya watoto yenye lengo la kuwasaidia wazazi kuwawekea akiba watoto wao huku wakiwajengea utamaduni wa kujiwekea akiba.
Kwa kuanzishwa kwa aina hii mpya ya akaunti, Stanbic bank inaendelea kuwapatia wateja wake huduma mpya na bora za kibenki kila siku kuendana na mahitaji ya wateja an hali halisi ya soko.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa akaunti hiyo uliofanyika katika makao makuu ya benki hiyo Kinondoni jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, mkuu wa mauzo wa benki hiyo Shangwe Kisanji amesema kuwa benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuwapatia wateja wake huduma mpya kila mara na nyakati zote huduma hizo huendana na mahitaji ya wateja na mahitaji ya jumla ya soko la huduma za kibenki hapa nchini.
“Wakati wote tumekuwa tukiangalia njia mbalimbali za kuwahudumia vyema wateja wetu katika kutunza fedha zao ikiwemo kuwawekea watoto akiba kwa manufaa yao ya baadae na pia kuwajengea utamaduni wa kujiwekea akiba wawapo wakubwa, utamaduni ambao ni muhimu sana kwa uchumi na maisha yao”
Ameeleza kuwa akaunti hiyo ya HATUA ni muendelezo mzuri wa kuwatoa watoto kwenye utamaduni wa kujiwekea akiba kwenye vibubu na badala yake kuanza utamaduni wa kujiwekea akiba kwa njia rasmi zaidi.

Amesema akaunti hiyo haina makato ya huduma na kiwango cha chini cha amana ni shilingi 20,000 tu. Amebainisha kuwa akaunti hiyo haina masharti magumu ya kuiendesha  na inaruhusu kutolewa kwa fedha mara moja kwa robo ya mwaka ili kusaidia katika majukumu yanayowahusu watoto kama vile ada za shule, sare na kadhalika. Amesema pia akaunti hiyo hujipatia riba kulingana na amana iliyopo.

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU