KUFA NA KUPONA

SURA YA NANE

Mauaji ya kikatili

Baada ya kunifungua mimi, nikavaa upesi upesi, kisha nikachukua bastola moja, nikaenda kulinda mlango wa hiki chumba wakati Lina akimfungua Sammy. Sammy alivaa upesi upesi, nikamtupia bastola moja, na nikamtupia Linna nyingine, mie nikatoa bastola yangu ndogo kwenye mkunjo wa chupi yangu.

Nilifungulia madebe ya petroli halafu, nikayawasha moto, tukakimbia kutoka humo ndani. Tulipofika kwenye mlango, tulikuta walinzi wa nje tayari wamefika. Lakini hawakutuweza maana wote tulikuwa tunafahamu hasa namna ya kutumia bastola, tuliwaua wote. Tulikimbia mpaka kwenye gari la Lina, tukaingia ndani, Lina akaweka moto tukapaa zetu. Tulipokuwa tunaondoka tuliona gari la Benny, Lulu na 'bosi' likiingia. Fikiria kitisho walichokikuta humo ndani!

"Turudi tukawagutue Willy, nadhani tunaweza tukawakamata vizuri sana wakati huu, maana hofu zitakuwa zimewajaa," alisema Sammy.

"Achana nao Sammy. Kama tukiwashika sasa siri nyingine hatutazipata maana miye nataka tulifutilie mbali kundi, lote la wahaini."

"Asante sana Lina, sijui nitakupa nini kwa kuponyesha maisha yetu. Shukrani nilizonazo Maurana ndiye ajuaye. Sikutegemea kama ungeweza kufanya jambo la ajabu kama hili, maana nadhani hata mimi mwenyewe ningeshindwa kufanya jambo lolote kama ulilolifanya." Nilimshukuru Lina. Kusema kweli nilikuwa namwangalia Lina kama Malaika aliyetumwa kutoka mbinguni kuja kutuokoa. Usiku huu alionekana mzuri kuzidi wanawake wote niliokwisha kuwaona. Kila kiungo changu kilimpenda hata kucha zangu zilimpenda.

"Ulijuaje tuko hatarini Lina? Na ulijuaje jambo hili maana mpaka sasa mimi naona kama muujiza tu, hata siziamini akili zangu." Sammy alimuuliza.

"Nitawaeleza lakini sasa si wakati mzuri, maana Benny anaweza akatufuata, kwa hiyo ngoja mpaka tufike hotelini kwa Willy, kwanza." alijibu Lina huku amekaza macho yake mbele ya barabara. Tulikuwa tunaenda maili mia kwa saa kwenye hii 'uhuru Highway'."

Tulienda mpaka hotelini kwangu Embassy, Lina alisimamisha gari lake mbali kidogo na hotelini, kisha akarudi tukaenda chumbani kwangu. Tulikuta kuna pombe, Lina alikuwa amenunua chupa nzima ya 'dry gin' alipokuwa amekuja kukutana nami wakati tuliosemezana. Lina alileta bilauli akaanza kutumiminia pombe. Tukaanza kunywa hali yeye anajilaza kwenye kitanda. Kama kaiwada yake wewe si msahaulifu nilikwambia kuwa msicha huyu hanywi pombe ila soda tu na 'baby-cham'.
 
Lina aliinuka akakaa kwenye kitanda. Kisha akasema. "Sammy ulikuwa na haja sana ya kujua jinsi nilivyofahamu na jinsi nilivyofauru. Willy alikuwa ameniambia tuonane hapa mnamo saa sita u nusu hivi. Miye nikaja hapa wakati huo, maana habari nilizokuwa natafuta nilikuwa nimeishapata kiasi. Nilingoja hapa kwa muda wa nusu saa! Willy alikuwa ameeleza kuwa ataenda kufanya uchunguzi kwenye nyumba ya Benny. Wasiwasi uliniijia nikahisi kuwa lazima Willy yupo taabuni, moyo wangu uliniuma sana kiasi cha kutovumilia, nikaona nimfuate na kama ni kufa tufe wote. Maana Sammy, nimekufa sana kwa Willy. Hilo kwa dhati nakiri.

"Basi nilikata shauri niondoke kwenda kwa Benny. Nilikuwa na bastola yangu, ambayo nilipewa na Benny enzi zake na mimi. Na nilikuwa ninaichezea kila siku hivyo kwamba hata mimi nina shabaha za kutosha. Nilipokagua humu ndani pia niliona imo pia bastola nyingine. na ilikuwa tayari imetiwa risasi, nikaichukua. Nilienda kule hotelini kwangu nikachukua ile bastola yangu nyingine ambayo pia ilikuwa imejaa risasi. Nadhani hamtastajaabu kusikia kuwa mimi naweza kutumia mikono yangu yote miwili barabara, hivyo nilikuwa na bastola mbili nikama watu wawili! Bastola yangu inacho kiwambo cha kupoteza sauti kama ilivyo ya Willy. Nyumba ya Benny ninaielewa sana na ulinzi wake pia ninauelewa. Nilijua lazima mara hii kuna ulinzi wa ajabu, lakini nilijua naweza kubahatisha, nikifa basi nitakuwa ninakufa kwa ajili ya mtu nimpendaye, kwa hiyo nitakuwa nimekufa kifo cha utu. Mtu niliyekuwa namuogopa ni Benny, maana najua ujasili wake akiwa na bastola.

Niliingia kwenye gari langu na kuondoka mpaka mbele ya 'Sclater hosteli'. Nilipoangaza nikaona gari la Willy. Niliposhuka na kulitazama nikakuta magurudumu yote hayana upepo hata kidogo. Hilo lilinipa uhakika kuwa Willy bado yumo ndani ya nyumba na yumo mswambeni. Niliendea nyumba ya Benny nilipofika kwenye wigo, niliona walinzi wengi wakiwa na silaha huku wakinong'onezana. Niliona nikiruka seng'enge nitaanguka ndani kwa kishindo kwa hiyo nikaona nitambae chini ya sang'enge.

"Kama unavyoniona mimi mwili wangu ni mwembamba kidogo. Basi nilitembelea tumbo kama nyoka, nikajivuta chini ya sang'enge nikatokea ndani, kwenye upande ule wa 'sclaters hosteli'. Nilijivuta hivi hivi mpaka kwenye ukuta. Niliposimama, bado hakuwako mtu aliyekuwa ameishaniona, hata yule mlinzi wa upande ule."

"Nilianza kujisogeza polepole mpaka kwenye pembe ya nyumba. Nilipoangalia niliona kuna walinzi wanne kwenye mlango wa nyuma. Kama ilivyo hii gauni yangu rangi yake usiku haionekani. Nikaona siwezi kuingia kwa mlango wa nyuma. Nikarudi kumvizia yule mlinzi wa upande wangu. Nikamtia risasi bila kuniona, nikajiona naweza kunyata harakaharaka kwenda upande wa mbele. Nilipofika kwenye pembe ya mbele nikawaona walinzi watatu. Walikuwa wakizungumza kwa sauti ndogo lakini iliyoniwezesha kusikia. Nilisikia mmoja wao akisema. 'Benny na Bosi'watarudi hapa dakika tatu hivi tangu sasa."

"Moyo wangu ulifurahi kusikia Benny hayupo. Kisha nilikohoa kidogo ili wale watu wa mlangoni waje pembeni yangu kuangalia kilikuwa kitu gani. Kweli wote walipumbazika na ujanja wangu, wote watatu wakaja.'Nia yangu ilikuwa waje ili niwauae bila ya wale wa ndani kujua kuwa wenzao wameishauawa.

"Nilikuwa tayari na bastola zangu, kabla hawajaniona nikawafyatulia, na wote wakaanguka bila ya wa ndani kutambua. Nilipochungulia kwenye kioo niliona kulikuwapo walinzi watatu, wote wameshikilia silaha huku wanatazama kwenye mlango. Nilijua tu, humo ndimo amefungiwa mpenzi wangu Willy. Hii ilinipa moyo na sikuwa na woga tena. Nilifungua mlango wa mbele taratibu kabisa, kabla ya wale walizi wa mlangoni hawajatambua.

"Niliingia sebleni bila kufanya kelele mpaka nikajibanza kwenye ukuta. Kisha nilijivuta taratibu kwenye ukuta na nilipokuwa mahali pazuri pa kuwalisha risasi na wao, mara moja nilijitokeza, na kabla hawajafanya lolote wote nikawaadhili. Ndipo hatimaye nikakimbilia kwenye ile jela yenu. Nikaokota ufunguo kutoka kwenye maiti ya mlinzi mmoja, nikafungua, ndipo nikawaoneni mkiwa mmefungwa pamoja na viti." alimalizia kutueleza Lina, huku akitoa tabasamu lenye huba na ukarimu.

Hatimaye Sammy alimuuliza Lina, "Jambo gani umelipata katika uchunguzi wako?"

"Kweli, karibu nisahau kusema. Sikupata mambo mengi sana ila tu kwamba ile nyumba ambamo Benny anakaa ni ya Daktari Dicksoni Njoroge, tajiri mmoja ambaye ana mashamba makubwa makubwa na ng'ombe wengi sana huko Thika na Nyeri, lakini ajabu ni kwamba Benny, halipi kodi ya nyumba, anakaa tu bure hali hawana ujamaa na Daktari Njoroge ndiyo hayo tu niliyopata sidhani kwamba yanaweza kuwasaidia kwenye mambo fulani." alijibu Lina huku akinitazama.

"Hizo habari zimenipa jambo na sasa lazima tufanye kazi upesi upesi. Nafikili huyu 'bosi' ndiye huyu daktari Dickisoni Njoroge, maana nilipokuwa nakagua katika kabati moja kwenye chumba cha maktaba, nilikuta bahasha imeandikwa 'Dr. Dickisoni Njoroge'. Na sasa nakumbuka ilikuwa na stemp za nchi ya ng'ambo. Na kufuatana na ripoti ya Lina inaonyesha kuwa lazima kuna uhusiano kati ya Benny na Njoroge. Lakini kabla ya kuanza kumfuata Njoroge inatubidi tuhakikishe kuwa ni yeye.

"Tusubiri tujue ni wapi Benny alikuwa akipiga simu alipokuwa kule 'City Hall' wakati wa maonyesho. Tutaulizia, kutoka polisi. Na wakati huu naona tukalale maana inaonekana saa zimekwenda sana, kwani kesho kazi zitakuwa nyingi sana!" Saa yangu ilionyesha saa tisa za usiku. Sammy aliondoka kwenda kulala, akatuacha miye na Lina hapo.

Lina aliniamsha alfajili yapata saa kumi na mbili na dakika arobaini hivi. Ilionekana msichana huyu ni kiumbe cha ajabu maana kichwa chake kinafanya kazi kama mpelelezi pia.

"Lina, mimi naona nitampigia Mkurugenzi wa Upelelezi Tanzania simu akupe kazi kwenye idara yetu maana utakuwa msaidizi mzuri sana kwangu na Sammy," nilimweleza Lina.

"Hapana Willy, mimi nataka tukitoka salama kwenye baa hili, na mimi nikiwa salama tuoane mara moja kabla ya wengine hawajakuzuzua."

Nilianza kuduawa nilipomuwaza mchumba wangu Della ambaye yupo nyumbani kwangu upanga. Na papo, uzuri wa Lina unanizubaisha. Nikamwambia, "Usijali Lina, lolote utakalo miye Willy nitatimiza, maana bila ya wewe mimi sasa hivi nisingekuwa Willy tu lakini jina langu lingeanziwa na 'Marehemu'......"

Kitambo nilipokuwa nikijitayarisha kwenda kuoga simu ililia. Nilipoenda kuijibu nilikuta Peter ndiye alinipigia simu."Unaendeleaje kijana, mambo yanaenda vizuri ama vipi maana ofisi yetu ya Dar es salaam wana wasiwasi mwingi sana, na wamenipigia simu asubuhi hii."

Nilimweleza Peter mambo yote yaliyokuwa yametupata mpaka muda huu, na jinsi tulivyofikiri mambo yetu yataendeleaje.

"Lakini unakaa wapi hapo Peter, ama umeishapata nyumba tayari?"

"Bado Willy, niko hapa 'New Stanley Hoteli' chumba nambari 101, kama ukitaka kuja kuniona." Peter alikata simu, miye na Lina tukaenda maliwatoni kuoga.

Tulipokuwa maliwatoni nilisikia simu ikilia, basi nilitoka huko na kuiendea simu.

"Halloo, Jeo huyu."

"Polisi Stesheni hapa."

"Eh mna ujumbe wangu wowote wazee?"

"Ndiyo, eh'

"Basi hii simu ilikuwa inapigwa huko Livingston Green, kwenye nyumba ya Dr. Dickison Njoroge."

"Asante sana bwana."

Nilikata simu nikarudi maliwatoni kuoga. Kichwa changu kilijenga mawazo kutokana na taarifa hiyo ya Polisi kuhusu simu iliyopigwa.

Baada ya kuoga, tuliletewa kahawa. Na baada ya hapo nikajitayarisha kwa ajili ya kazi za mchana. Nilipolisoma gazeti la 'East Afrikani Standard,' nilikuta taarifa kwamba maonyesho yangeanza saa mbili usiku. Lakini halikutaja zaidi habari za vifo vilivyokuwa vimetokea. Lina aliniambia alikuwa na hofu huenda Benny akafahamu kwamba yeye ndiye aliyetutorosha hivyo akaanza kumwinda. Lakini mimi nilimuhakikishia kuwa hatajua maana watu wake wote tulikuwa tumewahujumu, na watu waliokuwa wanajua ni Sammy na Peter ambaye nilimweleza tulipokuwa tukizungumza katika simu, na watu hawa hawawezi kumzuru.

Sammy alifika hotelini kwangu mnamo saa mbili. Tuliamua kwenda kumuona Robin ambaye tulipanga kukutana saa kama hizo. Lina alisisitiza twende zetu naye kila mahali lakini siye hatukuonelea vizuri. Nilimtaka akae pale pale chumbani kwangu asiende kwake. Nilimwachia bastola moja ili kuitumia itakapobidi.

Tuliondoka na kumwacha Lina mle ndani, tukaanza safari yetu kwenda New Evenue Hoteli ambako Robin alikuwa amepitia. Tulipofika kwenye ghorofa ya kwanza nikaamua kupiga simu Polisi ili kupatiwa vijana fulani fulani wakamvizie Dr. Dickison Njoroge waweze kujua myenendo yake ya siku nzima. Na lazima wawe wakipiga ripoti kwetu baada ya kila dakika 15 hivi kutujulisha myenendo hiyo. Na kama wakiona anafanya jambo fulani ambalo wanalitilia mashaka lazima wapige ripoti mara moja.

Tulipanda mpaka chumbani kwa Robin ambako tuligongagonga mlango. hata hivyo kulikuwa kimya! Sammy alichukua funguo zake akaufungua huo mlango.

Tishio tulilolipata, mwenyezi Mungu aliyetuhuruku ndiye aliyejua! Sammy alishtuka akaanguka chini. Nilipoingia mimi ndani, niliona mauaji ya kikatili ambayo sijawahi kuyaona. Robin alikuwa amelazwa kitandani huku amekufa! alikuwa amekatwakatwa na visu, kama ambavyo ingekatwa nyama. Huzuni iliniingia na uchungu wa ajabu ya kwamba nilianza kutoa machozi.

Hatmaye Sammy alizinduka. Nilimwambia awe macho wakati nikipekua pekua kila mahali humo chumbani mwa Robin, maana huenda wakatufanya kama walivyotufanya wakati wa kifo cha John. Nilipekua kila mahali lakini sikuona lolote. Ilionekana kuwa walimuua Robin na kuchukua kila kitu walichoona kingeweza kutusaidia sisi. Chumba kizima kilikuwa kimevurugwa vibaya sana.

Niliona kijikaratasi kidogo chini ya kitanda, nacho kilikuwa kimendikwa kwa herufi kubwa. Inaonekana hawa watu waliona hakina maana wakakitupa. Kiliandikwa "NENDA RUDI SALAMA UMEFANIKIWA, KWENDA NA MUONYESHAJI WA MAVAZI, LEO USIKU TOKA UADUINI TUNAMOFIKIRI." Nilifikiri sana lakini bado niliona haileti maana. Nilimwita Sammy aje ili naye akisome tuone kama anaweza kutoa maana yoyote kuhusu maneno hayo.

Sammy alipokisoma naye hakuweza kuunganisha maneno hayo na kuweza kutoa maana. Kisha nilishtukia akitabasamu kwa mbali. "Hallo Willy, nadhani hiki kijikaratasi kina maana kubwa sana. Na kila jambo alilokuwa anachunguza Robin liko hapa. Huwenda Robin alijua mambo mabaya yanaweza kumtokea kwa hiyo alionelea atuachie habari kwa njia hii ya hekima hivyo kwamba bila kufikiri sana huwezi kujua ameandika nini. Willy haya maneno ya kwanza. "NENDA RUDI SALAMA UMEFANIKIWA" kama ujuavyo yana maana ya kazi yetu, maana kazi hii inafahamika kati yetu kama 'Operesheni N-R-S-U" yaani 'NENDA RUDI SALAMA UMEFANIKIWA. hivyo basi maneno haya ni kwa ajili yetu kama sikosei, maneno yaliyobaki, Robin anatueleza mambo aliyochunguza na kupata. Nadhani yana maana ya kuwa, Hizi karatasi za siri zitaenda na mmoja wa waonyeshaji mavazi wa Ureno. Yale maneno ya mwisho UADUINI TUNAMOFIKIRI yana maana ya Ureno. Kwa hiyo huyu mwonyeshaji mavazi ndiye ataenda na hizi karatasi huko Ureno leo usiku. Na kufuatana na simu uliyoipata chumbani kwa Benny, nadhani Robin yupo sawa."

Kweli huyu Sammy ana kichwa, la sivyo ingelimchukua mtu mwenye kichwa kinene mwaka mzima kutambua inasema nini.

Tulipiga magoti kwenye kitanda, tukamsalia Robin, Mungu amuweke mahali pema peponi. Halafu tukapaa kuendelea na kazi hii ambayo ilionekana itatumaliza. Tulifunga kile chumba, tukatelemka chini. Tulimpigia simu mkurugenzi wa upelelezi nchini Kenya kumweleza yaliyompata Robin. Alishtushwa sana na habari hizi, lakini alituambia tusife moyo tuzidi kuendelea, maana ilionekana tunaendelea vizuri sana. Alituambia kuwa atazidi kutupa msaada wowote ule tuutakao. Kisha nilipiga simu polisi kusikia kama wamepata jambo lolote juu ya Daktari Njoroge. Polisi walijibu kuwa hawakuona mwenendo wowote mbaya, ila tu ya kwamba Njoroge alitoka nyumbani kwake kama saa tatu kasorobo hivi, akaenda madukani, na akaingia katika duka moja liitwalo 'Stationary & Office Machines Ltd.' huko akanuua mashine moja ambayo inatoa 'Photostat Copies' za barua. Nilimuuliza ulikuwa muda gani umepita, akasema kama dakika kumi hivi zilizopita na kwamba alielekea nyumbani kwake 'Livingstone Green'.

Mara moja nilipata wazo, wazo lenyewe ni kuwa daktari Njoroge ndiye 'bosi' hasa. Lakini kwa sababu yeye ni mtu mheshimiwa, juu ya ule utajiri na kisomo chake, watu hawamfikirii ubaya wowote. Baada ya kusikia utorokaji wetu usiku ameingiwa na wasiwasi sana na anaona tunaweza kumshika kabla hajaweza kupata hela zake. Kwa hiyo sasa anafikiria kufanya 'Photostat Copy' ya hizo karatasi. Na ikiwa tutaweza kuzipata hizo karatasi zenyewe, bado anaweza akapata kiasi fulani cha hela kwa kuuza zile copy.

Tulifikiri sana tuliona jambo kubwa ni kuhakikisha kuwa hizi copy hazitatengenezwa. Na tungeweza tu kufaulu kwa kuiharibu hiyo mashine kabla ya kutengeneza hizi copy. Na pia kuhakikisha kuwa hataweza kununua nyingine. Kwa hivi tulimpigia simu mkurugenzi wa usalama ahakikishe kuwa maduka yote yanayouza mashine za namna hiyo yamefungwa mpaka kesho yake, na ulinzi ufanywe kuhusu hizo mashine. Mkurugenzi alituhakikishia kuwa hayo yatafanyika bila shaka.

Mimi nilikata shauri nimfuate daktari Njoroge huko kwake kabla hajaanza hiyo kazi. Sammy ilimbidi aendelee na uchunguzi wa hawa watu ambao wamekuja kuzichukua hizi karatasi, kusudi tuweze kuzifahamu kabla ya usiku. Nilipiga simu polisi ili waniletee kijana mmoja niende naye.

Kijana wa polisi alipokuja tuliondoka kwenda 'Livingstone Green' huyu kijana niliyepewa alionekana wa aina ninayotaka, mtulivu lakini si mchezo.

Tulikuwa tukitumia gari la Polisi na tulipata habari wakati tukienda kwa Njoroge kwamba yeye Njoroge alifika nyumbani hapo na baada ya dakika kama tano hivi akatoka, na akaelekea pande za mjini tena. Tulipata habari hizi kwa njia ya radio ya polisi ambayo ilikuwa katika hili gari lao. Niliwambia wazidi kutueleza mwenendo wake kwa njia hii hii. Tulikwenda kulisimamisha gari letu kwenye maduka ya 'Livingstone Green'.  Nilimweleza huyo kijana wa polisi abaki katika gari wakati mimi nikienda kwa Njoroge, kusudi aweze kupokea habari, na kama kutakuwa na jambo lolote kabla sijarudi akimbie kunieleza. Akanipa ramani ya mzunguko wa nyumba ya Njoroge.

Nilikwenda bila shida mpaka kwenye hiyo nyumba. Nyumba ilikuwa kubwa na ya kibepari hasa. Kumbuka kwamba wakati huo ilikuwa ni mchana, na mambo ya mchana ni ya mchana saa hizo watu wengi walikuwa kazini nilienda na kupiga hodi. Kijana mmoja umri kama miaka saba hivi alinifungulia.

"Kijana, mimi ni mfanyakazi wa baba yako Njoroge, ambaye huangalia mashamba yake ya Thika. Tumeonana sasa hivi njiani akienda mjini, lakini ameniambia nitakukuta wewe hapa. Na kama ulivyoona alikuja hapa na kasha lililokuwa na vitu. Ameniambia utanionyesha alipoliweka, maana humo imo mashine ambayo ni kwa ajili ya kazi ya mashamba yake huko Thika. Miye nimekuja kuichunguza kama inafaa kwa kazi yetu. Kwa hiyo nionyeshe, maana nina haraka."

Yule mtoto bila wasiwasi alinipeleka kwenye chumba mlimokuwa na mashine nyingi na vitu vingi vya ajabu. Nilimshukuru huyo kijana kisha nikamwambia aendelee na kazi zake. Niliifungua ile mashine na kuiharibu. Kisha nikavichukua vyuma vingine ambavyo ni vya maana. Baadaye nikalifunga kasha hilo tena nikaenda zangu salama usalimini.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU