KUFA NA KUPOMA

 SURA YA TISA

Miye na Msaliti

Tulirudi mpaka mjini tukiwa katika hilo gari la polisi. Tulipofika karibu na Pan Afrikani Hoteli, tulimwona daktari Njoroge akiwa ndiyo kwanza anarejea. Siye tuliendelea mpaka mjini. Yule kijana wa polisi alinishusha New Evenue Hoteli. Hapo nikaingia katika gari langu nililokuwa nimeliacha hapo nje ya hoteli. Nilitia moto gari langu na kuendesha mpaka Embassy hoteli.

Nilienda nikamuona Lina, maana nilikuwa nimemwambia asitoke mle ndani ya nyumba. Nilipogonga mlango kwenye chumba sikusikia sauti. Kwa wasiwasi nilifungua mlango taratibu. Nilikutana na tishio jingine, mara hii niliona lingeweza kuniua. Lina alikuwa ameanguka chini huku ametiwa visu, kimoja tumboni, na kingine ubavuni. Sura ya hapa mahala haikupendeza hata kidogo, miye Willy. Nililia kama mama anayemlilia mtoto wake wa pekee anapokufa. Lakini kulia kwangu si kwa kawaida, maana mimi ninapodiriki kulia wewe utakuwa umezimia. silii hovyo.

Niliuangukia mwili wa Lina. Moyo ulikuwa bado unapiga, ingawaje yeye alionekana kama amekufa. Nilivitoa vile visu, damu ikaanza kububujika vibaya sana. Nilitoa vitambaa vyangu, nikaviweka kwenye matundu ya visu. Nilimwagia Lina maji kama anaweza, kabla hajafa kabisa anieleze neno lolote na kilichotokea. Sikuweza kufanikiwa, Lina alionekana hawezi kuziduka hata kidogo.
  
Nilipiga simu kwa Daktari aje mapema iwezekanavyo, ili akiweza amuokoe Lina ambaye moyo wake ulikuwa bado katika mapigo. Pia nilimpigia Sammy simu aje hapa mahala, lakini hakuweko. Niliacha ujumbe kuwa wakati wowote arejeapo aje huku chumbani kwangu. 

Nilimbusu Lina ingawaje alionekana kama maiti. Yeyote aliyefanya jambo hili lazima awe mtu aliyejua kuwa Lina ndiye aliyetutorosha toka nyumbani kwa Benny. Kama unafikiri, unaweza kujionea mwenyewe mambo yanavyonyumbulika, maana tukio hili linaonekana la ajabu sana. Hapo hapo methali moja ya kiswahili ilinijia kichwani, "umudhaniaye siye, na usiyemdhania ndiye." Sijui kama na wewe umeshaona na kukubaliana na tukio hili. 

Daktari alikuja. Alipompima Lina, alisema kwamba bado ulikuwako uhai kidogo ndani yake, lakini hayakuwako matumaini makubwa. Hata hivyo alisema atamchukua Hospitalini kwake akajaribu kumsaidia. "Huyo huenda Mungu tu ndiye ataka aishi, la sivyo ameishakuwa marehemu, maana kisu cha ubavuni kimemchoma kwenye moyo." alisema daktari.

Nilimuomba daktari amshtue kidogo kama anaweza, kusudi huenda naweza kupata kijijambo cha kunisaidia.

Alipomshtua Lina alitoa macho, kisha akafumba tena. Alijaribu kusema lakini akashindwa. 

"Lina ebu niambie kimetokea nini?" nilimuuliza huku nikimtingisha, maana niliona anakufa tu, kwa hiyo afadhali nipate jambo linaloweza kunifanya nimpate muuaji wake.

"Alikuja akanitishatisha, akaniuliza...........umekwenda wapi kisha akatoa visu akanichoma........ mimi nami niliwahi kumpiga risasi lakini hakuumia sana aha........." Lina hakuweza kumaliza ila alizirai tena.

Daktari alimchukua kumpeleka hospitalini kwake na aliniambia angejaribu kila njia kuokoa maisha ya Lina. Na kama haitawezekana itakuwa sababu ya ahadi yake. Nilitoa shilingi mia tano nikampa daktari, na nilimuaidi kumpa nyingine elfu moja akiweza kuokoa maisha ya Lina. 

Lina alikuwa amenipa pigo kubwa sana, moyo wangu ulipata kidonda ambacho Lina akifa akitapona. Nilivyomuona Lina akiondoka na daktari! Basi tu. Mungu ndiye ajuaye, maana yeye na maiti yake hakukuwepo na tofauti.

Punde si punde Sammy alitokea. Nilimweleza mambo yaliyompata Lina, naye akasikitika sana. Ilionekana sasa tumebaki siye wawili tu kufanya kazi hii. Hii ilikuwa kwa sababu ya bahati tu, maana hata siye tumekuwa tukiponea chupuchupu. Hata hapa tulipokuwa tumekaa tukizungumza na Sammy tulikuwa na wasiwasi mwingi, maana wakati wowote tungeweza nasi kuwafuata rafiki zetu John na Robin na huenda dakika hii Lina.

"Sikiliza," alisema Sammy "Tayari nimepata habari ndogo ndogo juu ya watu wanaohusika. Binafsi ninalishuku kundi lote lililotoka Ureno kuja kwenye maonyesho. Kwanza, wale wanawake wa Ureno waliokuwa wakionyesha mavazi walionekana kama kwamba si kazi yao ya kawaida. Pili, wamekuja vijana watatu pamoja na hao wanawake. Vijana hao tangu waje hawajaonekana hata kidogo ila tu wameweza kuonekana hotelini kwao. Tatu, Robin alikuwa amepata habari kamili kuwa wao ndio ambao wamekuja kuchukua hizi karatasi kabla ya mauaji yake. Nne, kijana mmoja wa polisi ambaye tulimweka kumvia Benny, amesema kuwa Benny alienda mchana huo kama mara mbili hivi kukutana na hao waonyeshaji mavazi toka Ureno.

Hizi sababu za Sammy zipo katika usawa wa mia kwa mia. Kwa hivyo sasa lililopo ni kuhakikisha kuwa kwa njia nzuri ama mbaya siye ndiyo tunazichukua hizo karatasi badala yao. 

"Je, yule kijana wa polisi aliyekuwa akimfuata Benny leo hii mchana, alisema lolote juu ya Benny kuja hapa Hotelini kwangu?" nilimuuliza Sammy.

"La, alisema Benny hakusogelea sehemu hizi maana alionekana mwenye shughuli nyingi sana.

Jibu hili lilinipa uhakika wa jambo fulani ambalo nitakapokwambia utastaajabu. Lililokuwepo sasa ni kuwatafuta Benny, Lulu na 'Bosi' kabla hawajafanya upuuzi mwingine wowowte, maana tusipowawahi sisi, wao watatuwahi. 

Kabla hatujafanya jambo lingine lolote ilinibidi niandike ripoti kwa Chifu nikimweleza habari ya mambo yote yalivyo mpaka sasa. Maana sasa tumefikia karibu hatua ya mwisho na hii hatua ndiyo mbaya zaidi, maana kila kundi linapigania kushinda. Na hii ina maana ya vifo vingi sana. Nilimweleza Chifu mambo yote tangu mwanzo mpaka ambapo tumefikia, kisha nikaifunga na kuitia kwenye kisanduku changu cha barua za kutumwa.

Kisha nilivalia ili tuondoke. Tulijitayarisha kufa na kupona. Wote tulivalia furana ambazo risasi haziwezi kupita,'bullet proof' kisha tukavalia juu kama kawaida. Hizi furana tulikuwa tumezipokea mchana huu toka kwa Chifu baada ya kumwomba wakati tunaona hatari zinazidi. Tulipokuwa tunataka kutoka simu ililia.

"Hallo, huyu ni Peter, wasemaje Willy."  

"Miye salama tu mheshimiwa, je una utenzi?"

"Ndiyo nina jambo la kukueleza, na ni la siri zaidi. Ni jambo la kuweza kukusaidia sana."

"Niambie basi Peter mpenzi."

"Hapana, kwenye simu mambo huwa si mazuri sana, kwa hiyo tafadhali njoo hapa."

"Vema nakuja sasa hivi kama muda wa dakika kumi hivi." Tulionelea tusiende wote kwa Peter ila Sammy aende kutalii kama Lulu yupo hapo Hotelini kwake. Na huko akamtishe ili aweze kutoa habari zozote. Kisha baada ya hapo Sammy angekuja hotelini kwa Peter, na hapo ndipo mahala ambapo tungekata jinsi ya kuendelea. Tuliagana tukatakiana bahati njema.

Nilienda zangu mpaka 'New Stanley Hoteli.' Nilipokuwa nikipita hapo chini, niliona jamaa wengi wakijiburudisha katika 'Thorn Tree. Lakini pia nilimuona kijana mmoja miongoni mwa hao watu ambaye aliponiona aliinama kidogo ili nisiweze kumfahamu. Lakini ilivyo macho yangu ni hatari, maana katika nusu nukta, nilikuwa nimeishaona kila mtu mwenye umati wa watu elfu moja. Huyu kijana nilimuona kule hotelini 'Intercontinental' wakati wamekuja na Benny huku wameshikilia bastora. Nilijifanya na mimi sikumuona nikaendelea zangu kumuona mheshimiwa Peter.

Nilipofika kwenye chumba cha Peter niligonga akanikaribisha ndani, "karibu Willy, asante sana kwa kufika!!" alisema akaenda kwenye kabati kuchukua vinywaji.

"Asante sana kwa kunikaribisha Peter, lakini miye sitaki vinywaji vyako maana nina kazi nyingi sana," alikuwa bado akimimina pombe akidhani huenda natania kusema kuwa sitaki, "kwanza lazima nihakikishe kuwa nimewatia nguvuni waalifu wote na wengine kuwaua. Wewe ukiwa wa kwanza wa hao waalifu!" Peter ghafla aliangusha chini chupa ya pombe akageuka kunitazama. Alipogeuka alikuta tayari nimeshatoa bastola mbili kumwangalia. Huenda nikadhaniwa mimi ni mkichaa, lakini la, kila siku nikisema neno au nikishuku neno jua niko sawa. 

"Unamaanisha nini Willy, wewe unajua vema kuwa mimi ni mpigania uhuru halisi, na hasa nimepewa cheo kwa ajili ya uhaminifu wangu!" alisema huku akitetemeka kwa hofu. 

"Ulidhani wewe ni mjanja sana Peter, yakwamba ungeweza kuuza wenzako bila kutambuliwa. Na kweli kidogo ungefaulu katika mambo yako, kama usingefanya makosa fulani fulani, na pia kwa sababu walimweka Willy katika kazi hii ambaye anashuku kila mtu. Hata pia nakusifu kwa akili zako nyingi, lakini nasikitika kwa kushindwa kwako."

"Ulijuaje ya kuwa mimi nilikuwepo kwenye mpango huu?"

"Tangu siku ya kwanza niliyoondoka Dar es Salaam nilijua lazima kuwe na mtu ambaye kwanza ana cheo kikubwa sana kwenye Ofisi ya wapigania uhuru ambaye anashiriki katika tukio hilo. 

"Kabla sijatoka Dar es Salaam nilienda nikakagua ile ofisi yenu iliyobomolewa, na ilionekana kuwa mle ndani vitu vingine vyote havikuguswa ila kabati lile lenye karatasi tu. Hii ilionyesha waziwazi kuwa lazima hawa watu wamepata habari kamili ya mahala karatasi hizo zilimo laasivyo tungekuta vitu vyote humo ndani vimevurugwa vurugwa kutafuta mahali zilipo hizo karatasi. Pia ilinipa wazo kuwa lazima awe afisa mwenye cheo kikubwa sana kujua hata mahala karatasi za siri kama hizo zilipotunzwa, maana afisa wa vivi hivi tu asingeweza kujua.

"Na kama unakumbuka siku ile usiku nilipokuwa nikienda kwa Chifu ulikuwa ukinifuata. Ulijifunga shuka na huku umevaa miwani myeusi. Gari lako halikuwa na nambari. Nilijua tu kuwa huyu mtu lazima ananifahamu ndiyo sababu anajibadili hivi.

"Wewe mwenyewe ulikuwa umekuja na hili kundi la akina Benny. Na baada ya kufanikiwa kuziiba hizo karatasi wao waliondoka wewe ukabaki Dar es Salaam. Ulibaki kwa sababu ulikuwa na wasiwasi ya kwamba wangeweza kuniweka mimi kwenye kazi hii. Hivyo ulivizia uone na ulikuwa sawa.

"Kisha ulinifuata Nairobi baada ya mimi tu kufika. Maana nilikuwa nimeweka mtu wa kuchunguza mpigania uhuru yeyote mwenye cheo ambaye angeingia Nairobi siku ile. Na wewe ulionekana ukitoka Dar es Salaam." Wakati huo huo wote bado nilikuwa nimeshikilia bastora zangu tayari tayari, na Peter alionyesha mshangao wa ajabu machoni mwake.

"Ulipofika hapa." Niliendelea, "Ulimuona John na kwa sababu mlikuwa mkifahamiana. John alikwambia kuwa alikuwa amekuja kwa tukio hilo. Hakusita kukueleza sababu kwamba anajua wewe ni afisa mkubwa sana katika ofisi ya wapigania uhuru. Uliripoti mambo hayo yote kwa Benny na Njoroge, na wao wakakuamuru umuue John. Ulifanya mpango ukamuua John."

"Umejuaje kuwa Daktari Njoroge ndiye 'bosi'" aliuliza.

"Hiyo ni rahisi. ngoja niendelee kukueleza jinsi ambavyo wahalifu hawana akili, hali wakifikiri wana akili sana. Kisha ukamweleza Benny na Njoroge juu yangu - kuwa mimi pia ni hatari zaidi. Kwa hiyo jambo la kufanya ilikuwa wewe ukimbie upesi upesi kujifanya kuwa unatusaidia wakati unatuwinda.

"Nilipohakikisha ya kwamba ni wewe msaliti, hata mimi nilianza kukufanyia ujanja. Siku nilipotoka na Lina pale 'City hall' ni wewe tu uliyejua. Ulienda ukamwambia Benny, Benny akaweka mtu wa kutuvizia. Bahati mbaya miye nilitambua nikamkomesha.

"Wakati ninaenda kwa Lulu jana usiku nilikukuta 'Hotelini Intercontinental' na wageni fulani fulani, na ni wewe tu ulijua miye nimeenda humo. Ukaenda ukampigia Benny simu kuwa niko huko, akanifuata. Lakini mimi nilikuwa nimejua kitambo kuwa wewe utafanya jambo kama hili kwa hivi nikamwahi.

Halafu tulipotoroka kule kwa Benny baada ya kutushika. Benny alikupigia simu akikueleza kuwa tumetoroka lakini hakujua ni nani aliyetusaidia kutoroka, kwa hivi akakwambia unipigie simu kijanja niweze kukueleza. Nami nikiwa na nia ya kuzidi kukupumbaza zaidi nilikueleza habari zote. 

"Ulipomweleza Benny juu ya Lina akakuambia umtafute mpaka umempata uweze kumuua. Yeye hakutaka kufanya jambo kama hili maana kwanza alijua waziwazi kuwa Lina si mchezo, huwezi kumuendea hovyo hovyo. Pili alifikiri Lina anaweza kuwa yupo chumbani kwangu na kama kwa bahati mbaya angetukuta wote chumbani angejua maafa ambayo yangewapata.

"Wewe ilikuwa ni rahisi kuja kwangu, maana kama kwa bahati ungenikuta nipo ungejifanya kuwa unakuja kwenye mazungumzo tu. Bahati nzuri hukunikuta. Ulipofika chumbani kwangu ulimkuta Lina, na kwa vile Lina hakuwa anakufahamu mara moja alikuja juu, lakini ulimuwahi ukamtia visu." Wakati huu alionekana kustaajabu sana juu ya habari hii.

"Lina naye aliwahi kukufyatulia risasi mkononi. Kuona hivyo ukakimbia kabla ya kuhakikisha sawasawa kama Lina amekufa ama vipi." nilimwendea nikamvua shati lake, nikakuta kweli wamemfungafunga kwa vitambaa. Kisha nilijiegemeza kwenye ukuta huku nimeshikilia bastola zangu kama kawaida. "Halafu uliponipigia simu nije nikuone ndicho kilikuwa kifo changu na mimi, maana kuna watu ambao unajua watakuja humu wakati wowote. Wewe hukujua kama mimi najua, hivyo uliwaambia wakae kwa muda kidogo ili uweze kunipa pombe, na nisifikirie habari yoyote kusudi iwe rahisi kwenu kupambana nami. Lakini hapo ndipo ulipopiga chini hasa, maana Willy, alikuwa anajua kila kitu. Kwa hiyo nimekuja kwenye kifo chako si changu. Na nadhani taarifa nitakayoitoa kwa mkurugenzi wa wapigania uhuru itamfanya atoe machozi. Kwani kweli siye waafrika tunakulana kama samaki. Wahenga walisema kikulacho kimo nguoni mwako." Na ni kweli kabisa."

"Mh, kumbe unajidanganya sana Willy unadhani utatoka humu salama? wala usidhani kwamba wahalifu wanapofanya jambo kubwa kama hili huwa wanalifanya kwa pupa. Kwanza wanaambiana njia zote ambazo wanaweza kupita, na jinsi ya kuzuia pasiwepo  na uwezekano wowote wa kuingiliwa." Alisema Peter huku sasa amekaa kitini."

"Wewe walikuahidi kukulipa kiasi gani Peter."

"Lazima waliniaidi fedha nyingi laasivyo nisingelikubali kuhalibu jina langu na kuuza watu wangu."

"Lakini kiasi gani hebu nipe jumla laasivyo naweza kugeuka mbogo sasa hivi, nikakutia marisasi maana unanijua waziwazi nilivyo."

"Wangenilipan shilingi milioni kumi."

"Na malipo yote ya hizo karatasi ni kiasi gani?"

"Ni shilingi milioni mia moja."

'Zimeishafika hapa toka Ureno?"

"Sijui kama zimefika," alijibu huku akiwa na wasiwasi. niliachia risasi moja na kukipiga kiganja chake.

"Sema kweli, maana wewe, Benny na Daktari Njoroge ndiyo mnaojua ukamili wa habari hii."

"Ndiyo imeishafika, ilifika jana usiku, lakini bado walioileta hawajatupa, watatupa leo usiku."

"Watawapea wapi?"

"Kusema kweli hapo sijui," alijibu kwa hofu tena. Nilimtia risasi nyingine ya mkono karibu na pale Lina alipokuwa amempiga. "Wapi, niambie laasivyo utakufa."

"Sijui kwa kweli, lakini nadhani itakuwa wakati wa maonyesho huko 'City hall'."

 "Hizo karatasi zimewekwa wapi?"

"Kule kwa .........." kabla hajamaliza usemi vijana wawili waliingia kupitia dirishani. Nilipogeuka kuwatazama, wengine wanne waliingia mlangoni. Peter alisimama na kukimbia kabatini alikotoa bastola na kuishikilia. Kisha wakaja vijana wengine wanne, wakawa kumi. wawili wengine wakaja lakini wakabaki mlangoni mimi nilikuwa bado nimebaki nimesimama hivyo hivyo na huku bado nimeshikilia bastora zangu wote walikuwa wamejipanga upande mwingine wa ukuta wote wakiwa wameshikilia bastora zao.

"Tupa chini hizo bastola zako Willy, maana naona kifo chako kimefika," alisema Peter kwa sauti ya ujuvi. "Vipi, huwezi ukajihudhunikia mwenyewe, kabla mimi sijafa wewe mwenyewe utakuwa tayari umeishakufa. Ha ha ha ha, mbona nyie wapelelezi hamkubali kushindwa! watu kumi na watatu na wewe mmoja bado unapanua domo lako. Kuzungumza upuuzi mtupu. Wewe utakufa, miye nitapata fedha na hakuna atakayetambua kuwa miye Peter nilihusika na mambo haya."

"Unajidanganya sana. ukiniua mimi lazima Sammy atakupata tu."

"Ohooo! Umechelewa sana rafiki yangu, sammy ameishakamatwa huko chumbani kwa Lulu. Benny amemchukua huenda sasa ameishakuwa majivu," alijibu mmojawapo wa wale watu. 

Niliona kuwa huyu kijana hakuwa anatania. Nilikata shauri mara moja nipambane nao. Ikiwa nitakufa basi, lakini ikiwa nitapona nitahakikisha kuwa nimemponyesha Sammy nikimkuta bado hai.

"Fyatueni bastola zenu sasa mbona mnaogopa? mnaonekana mkitetemeka. Mkichelewa basi nitawamaliza miye kabla hamjanimaliza. Yaonyesha kwamba mnao uwoga wa kike," nilisema hivi kusudi niwatie hasira, maana mtu akipatwa na hasira hawezi kuona sawasawa. Maneno yangu yalifanikiwa maana niliona wanapandwa na hasira hovyo hovyo.

Peter alitoa ishara huku akisema, "Kwa heri Willy, nitahakikisha kuwa nimerithi mali yako yote hata Bella. Fika salama huko ahera."

Walipotaka kuanza kunifyatulia risasi haraka nikawafyatulia mfululizo. Sita tayari chini. Niliipiga risasi mikono ya Peter akaanguka chini bila ya kuwa nayo bastora. Kisha nikawamaliza wale wanne waliobaki. Nilimsikia Peter akitoa sauti ya kuwaita wale wawili wa mlangoni. Walipokuja wakanikuta miye tayari nawangojea. Nikawafyatulia kisha nikawavutia ndani na kufunga mlango kisha nikamfuata Peter.

"Eh, umejua kuwa mimi ni Willy, eh Peter? uhalifu haulipi. Na mshahara wa dhambi wa mauti bali karama ya Mungu ni uzima wa milele."

"Oh Willy nisamehe, nilivutiwa na pesa. Oh nimetubu nimetubu."

"Pesa, pesa Peter! unakubali kuuza Afrika nzima kwa ajili ya pesa, ona sasa umepata nini ndani yake!

Peter alianza kulia.

"Zile karatasi ziko wapi?"

"Kule kwa Daktari Njoroge katika stoo yake. Zimewekwa katika sefu ya chuma humo stoo. Na watazibadilisha leo saa mbili na dakika kumi, lakini sielewi wapi."

"Sasa Peter, kwa heri ya kuonana. Nitakupa risasi sita kwa sababu ndivyo nilivyoaidi nilipokuta John ameuawa. Nitakutia visu viwili kama kisasi kwa ajili ya msichana Lina kama nisingelikuwa nimeapa ningekurudisha Dar es Salaam wakakuweke kitanzi. Kwa heri kwa mara ya pili."

"Ohoo nisamehe Willy..........."

Niliondoka mpaka kwenye mlango kisha nilimuendea na kumtia visu viwili hatimaye nikaachia risasi sita kama yeye alivyoziachia kwa John na kama alivyo mchoma Lina.

Lo. furana yangu "buletproof" ilikuwa imeniokoa vizuri sana.

Niliondoka mle ndani haraka mpaka chini. Mawazo yangu sasa yalikuwa kwa Sammy, kwamba nitamkuta mzima ama vipi. Wameelekea upande gani sijui. Niliona nianzie kule kwa Lulu alikokwenda. Nilienda na gari langu mpaka hoteni kwa Lulu. Nilipanda mpaka kule chumbani kwa Lulu. MLango ulikuwa umefungwa. Nilipoingia ndani niliona kazi ya Sammy. Niliona Maiti nne zote zimekula visu.

Nilikaa kwenye kitanda nikifikiri wapi wamempeleka lakini sikuwa na mwangaza wowote. Nilizunguka huko na huko chumbani. Hofu, wasiwasi, uchungu, fikira, huzuni, vyote hivyo viliusukasuka moyo wangu, chuki na maudhi niliyokuwa nayo yangeweza kunifanya nizimie. Niliona karatasi kwenye kitanda. Nilipoiendea mwandiko haukuwa wa Sammy ila mtu mwingine. UPESI, NAIROBI SOUTH, WILISON AIRPORT, KABLA YA SAA MBILI KWENYE NYUMBA MOJA NAMBARI B 141. RANGI BLUE TAFADHALI UFANYE HARAKA LAA SIVYO UTAJUTA KUCHELEWA KWAKO."

Itaendelea 0784296253


Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU