KUFA NA KUPONA



SURA YA KUMI

'Lililo na mwanzo lina mwisho "Bosi"

Niliwaza harakaharaka kama huu ni mtego ama vipi. Lakini hata kama ni mtego niliona huenda unaweza kunisaidia. Sammy hakuwemo humo chumbani hivyo nikawaza kwamba pengine wanaye huko waliko au ameisha uawa na kutupwa mahala pengine. Zaidi niliona lazima wameenda naye huko waliko. Basi mwishowe nilikata shauri nifanye kama vile ilivyoelekezwa katika kile kikaratasi. Ilikuwa yapata saa moja kasorobo sasa.  

Nilionelea katika hizo dakika kumi na tano nikimbie kule hotelini kwangu, nikaoge upesi upesi kisha nibadilishe mavazi maana shati langu lilikuwa limetobolewa tobolewa kwa risasi. Nilienda nikakoga haraka haraka, nikabadilisha shati na kuondoka zangu kuelekea Nairobi South.

Nilifika "Wilson Airporot" kama saa moja hivi. Kulikuwa na ndege moja tu hapo kiwanjani. Nilisimamisha gari langu, halafu nikatoka na kuanza kutafuta ile nyumba ilikokuwa. Mahala pote palikuwa kimya, baridi ilikuwa kali sana, na moyo ulikuwa unanipiga mno. Nilitafuta kwa muda mrefu kisha ndipo nikaiona. Wakati huo palikuwa pameisha kuwa giza mahala pote.

Moyo wangu ulizidi kupiga na nilinuia usiku huu huu ikiwa nikiwa mzima lazima nihakikishe 'Operesheni N-R-S-U' imefanikiwa. Niliiendea ile nyumba pole pole huku nikichunguza huku na huko. Mawazo yangu yote yalikuwa juu ya Sammy kama ni mzima ama ameuawa.

Nilikuwa nimeisha kata shauri kuua kitu chochote kitakachokuja njiani pangu kabla sijaweza kufahamu nini kimempata Sammy.

Nilijua kama ile karatasi ilikuwa mtego basi watakuwa wananingoja lakini kama hapana basi watakuwa wanadhani kuwa miye nitaenda kumtafuta Sammy kwa Daktari Njoroge huko 'Lavington Green', au kwa Benny huko "Westlands'. Nilipozungukazunguka nikakosa kumuona mtu yoyote hivyo nikadhani huenda hawakuwa wakinitegemea. Nilijibanza kwenye ukuta, halafu nikachungulia kwenye dirisha moja; taa zilikuwa zikiwaa humo ndani ya chumba. Nilipochungulia zaidi humo ndani nilimuona Sammy amelazwa kwenye kitanda na amefungwa kwa kamba. Pia alionekana akiwa bado amezimia. Moyo wangu ulifurahi sana na ukanipa nguvu zaidi kuona Sammy alikuwa bado anaishi, ingawaje chini ya hali ya mateso ya ajabu.

Niliwaza jinsi ya kuweza kuingia humo ndani lakini nilishindwa. Dirisha lilikuwa na vyuma ambavyo nisingeweza kuvifanyia jambo lolote! mwishowe nilijitolea nipitie mlango wa mbele, nilikuwa tayari na bastora zangu. Kijana mmoj alikuja kufungua mlango. Nilimpiga ngumi ya shingoni akazirahi papo hapo hata hakuweza kutoa sauti.

Niliingia ndani nikafika kwenye mlango wa sebuleni. Huu mlango ulikuwa wa mbao lakini juu ulikuwa na kioo, Nilipoangalia ndani nikawaona Benny, Lulu na watu wengine kama kumi hivi wote wakinywa kwa furaha sana. Nilifikiria niingie lakini sikuona jambo la maana, maana 'bosi' hakuwemo na bosi ndiye mwenye vitu ninavyovitaka. Hawa watu humu ndani walionekana wameridhika sana na mambo, ila Lulu mara kwa mara alikuwa akiangaza macho huku na huko.

Kisha wazo likanijia, nikarudi nje taratibu ili nikawe tena kwenye lile dirisha la chumba alimo kuwa amefungiwa Sammy. Kabla sijaenda, nilimbeba yule mlinzi wa mlangoni nikamsukumia kwenye mfereji wa maji halafu nikahakikisha kuwa haamuki mpaka baada ya siku tatu hivi.

Nilipofika pale dirishani, nilikata unyasi mmoja mrefu sana hivi ambao nilijua utamfikia Sammy hapo alipolala kitandani. Kweli ulifika. Niliusukumasukuma sikioni mwake mpaka akazinduka. Alipozinduka alitazama akaniona. Alitaka kusema jambo nikamfanyia ishara anyamaze, maana alionekana akili zake bado hazikuwa zinaweza kuunganisha mambo. Kwa sababu mimi ni namwelewa Sana Sammy, nilijua haitamchukua dakika nyingi kabla ajaweza kuelewa nini ni nini.

Baada ya muda kidogo niliona anaanza kutambua mambo, alinitazama akanitingishia kichwa kuonyesha kuwa sasa anaanza kuelewa mambo. Ilionekana kama akina Benny walikuwa wamemponda vibaya sana Sammy hata kuzirai muda wote ule. Na pia ilionekana akina Benny walijua itamchukua muda mrefu sana Sammy kuzinduka ndiyo sababu hawakuwa na wasiwasi.

Nilishawambieni kuwa Sammy ni maarufu kwa visu. Kwa hiyo alinifanyia ishara nimtupie visu ili aweze kukata zile kamba na kujifungua. Ungeweza kustaajabu angezikataje zile kamba maana hapo mwanzoni nilikuwa nimekwambia kuwa walikuwa wamemfunga vizuri sana. Lakini usitie shaka nitakuelelza sasa hivi.

Kichwa cha Sammy hakikuwa kimefungwa yaani kuanzia shingoni. Basi nilimtupia kisu toka dirishani nacho kikaanguka karibu sana na mahali alipokuwa. akajikurupusha huku na huko hadi akafanikiwa kukiuma kwa midomo. Sammy akakata zile kamba kwa kutumia mdomo. Kile kisu ni kikali sana fahamu, hata niseme zaidi ya wembe. Kisha nilimtupia visu vingine kama sita hivi nilivyokuwa navyo. Tulifanyiana ishara ambazo ni sisi wenyewe tu tunazozifahamu.

Miye nilirudi mpaka kwenye mlango wa mbele nione kama ninaweza kufanya lolote. Ilivyokuwa inaonekana mpaka  sasa, ni kuwa mahala pa kukutania kati ya Benny, Bosi na wale waliotumwa kuja kuzichukua hizi karatasi ni hapo. Na pia ilivyoonekana hawa watu wataondoka na ndege ndogo kuelekea kwao, ndiyo sababu wakachagua nyumba ya kukutania karibu na kiwanja hiki.

Bado nafikiria la kufanya nikasikia sauti nyuma yangu, na nikasikia mdomo wa bastola unanigusa, "Haya tembea mheshimiwa, kama unadhani kuviziavizia nyumba za watu kunasaidia."

Sikuwa na la kufanya ilinibidi nifanye kama nilivyo ambiwa. Mlango ule unaoendea sebuleni ulikuwa umefunguliwa nikaingizwa ndani.

"Karibu Willy, nafurahi sana kukuona tena baada ya kunitoroka jana kwa namna ya ajabu. Nimefurahi kuwa nyie watu hamnipi shida ya kuwatafuta ila mnajileta wenyewe. Kaa chini hapo tuweze kuzungumza kidogo kabla ujashuhudia kwa macho yako jinsi tutakavyofulu." alisema Benny kwa maringo na taratibu sana.

"Asante sana kwa kunikaribisha Benny, lakini nasikitika sana kuwa hutafaulu katika mipango yako, aidha sitakaa nishuhudie ukifanya unyama mimi nikitazama tu." nilimjibu kwa utaratibu mwingi pia.

Nilikuwa nikiwapa maelezo mengi hayo kusudi waweze kumsahau Sammy kwa muda na hii ingempatia muda wa kuweza kujifungua na kujinyooshanyoosha aweze kuwa tayari kwa vitendo.

Ilipofika kama saa mbili kasoro dakika ishirini hivi. Daktari Njoroge akiwa na walinzi kama wanne hivi aliingia.

Huyu Daktari Njoroge ni mtu mwenye umri wa makamo kama miaka arobaini na mitano hivi. Jinsi mwili wake ulivyokaa unaonyesha utajiri mtupu. Nilipata habari kuwa amesoma sana, na amehitimu kama Daktari huko Uingereza. Uso wake uonyesha furaha kila wakati. Pia uonekana kuwa anatoka katika ukoo ulioendelea vizuri sana.

"Karibu 'bosi' nadhani utafurahi sana nikikutambulisha kwa kiumbe ambaye kwa wakati wote huu amekuwa akitutia wasiwasi sana, lakini sasa tena amejileta na yuko chini ya mikono yetu," alisema Benny kwa furaha kubwa.

"Endelea Benny, tuweze kufahamiana kabla hajazikwa," alijibu 'bosi'

"Huyu ni mpelelezi maarufu katika Afrika nzima, bwana Willy Gamba, ambaye anafanya kazi na Idara ya Uchunguzi ya Tanzania, lakini mara nyingi; anafanya kazi bega kwa bega na Idara za aina hii hii za hapa Afrika ya Mashariki."

"Aisii, mimi naitwa Dr. Dickison Njoroge, tajiri sana katika Afrika Mashariki nzima. Na nimekuwa tajiri hivi kwa ajili ya shughuli za namna hii bwana Willy, kwa hiyo kuniingilia kwako kulikuwa kunapoteza muda na fedha yangu. Lakini hata hivyo napenda sana mioyo yenu ilivyo migumu ya kwamba hata naona wivu. Ubaya ni kwamba, ushujaa wako mwisho wake ni hapa. Na kabla sijaona unakufa, nataka kukuonyesha jinsi miye nilivyo na akili nyingi, na jinsi kundi langu lilivyoundwa kwa uimara kabisa." alisema Dr. Dickison Njoroge hali akinitazama kwa furaha.

"Siye tuna chama chetu, nacho ni kikubwa sana, kinao wanachama katika Afrika Mashariki nzima. Pia kina uhusiano na vyama vya namna hii hii katika Afrika na hata nchi nyingine za Ulaya. Hapa Afrika ya Magharibi, mimi ndiye rais wa chama hiki na kesho nategemea kuita mkutano ambao nataka tumchague Benny kama Katibu Mtendaji wa chama badala ya Job ambaye mlimuua katika msukosuko huu. Na pia nataka nikueleze waziwazi kuwa chama hiki kina wanachama pia kutoka hata Serikalini. Watu wenye vyeo vya juu kabisa wana hisa katika chama hiki. Kwa hivi ndiyo sababu kila siku siye hatuwezi kushindwa maana "Zimwi likujualo halikuli likakwisha" walisema waswahili.

Katika wizi wa karatasi hizi, mtindo wetu ni ule ule umetumika. Maafisa wetu wa Tanzania na Uganda wote tulishirikiana bega kwa bega mpaka tukafaulu. Na leo baada ya saa mbili na dakika kumi, chama chetu kitakuwa tajiri kuzidi vyama vingine vyote. Siye tunafanya kazi sawa sawa na jinsi nyie kwenye idara ya upelelezi mnavyofanya. Na pia tuna watu mashuhuri kama wewe na wengine kutoka katika idara yenu.

"Miye najua mpaka sasa mnajua tulivyozipata hizi karatasi, lakini najua hamjui jinsi ambavyo zitapelekwa na wapi zitapelekwa."

"Tunajua Daktari Njoroge usijivunge kuwa akina siye hatujui, hata ambavyo unajidanganya utafanya usiku huu pia tunajua," nilimjibu huku sauti yangu ikionyesha dharau kubwa.

"Kama unajua basi sijali hata chembe, maana wewe sasa ni sawa na maiti, na kama maiti inajua jambo nani huyo atakayejali?

"Ulipokuja kwangu na kuharibu mashine yangu, nilipopata habari nilichukia kiasi kikubwa sana ya kwamba miye mwenyewe nataka kushuhudia kifo chako, na pia kwa sababu wewe ndiye mtu wa kwanza kuweza kunigundua mimi nikiwa kama kiongozi wa kundi la wahalifu. Kwa kifupi Bwana Gamba ni kwamba, muda wa dakika ishirini hivi siye tutakuwa watu tajiri kabisa.

"Hizi karatasi zinanunuliwa na watu wa Ureno kwa kiasi cha shilingi milioni mia moja na siye tumezipata kwa kuuza maisha ya watu wetu wengi. Na Serikali imezitafuta kwa gharama iliyo kubwa kiasi cha kutisha. Kadhalika imepoteza watu wake mashuhuri kwa ajili ya hizi karatasi na bado wasizipate.

"Mnamo saa mbili kamili, wapelelezi fulani toka Ureno tunaonana nao hapa hapa ndani, na naona zimebaki dakika kumi kufika muda huo, na wakati huo nitahakikisha kuwa nyie mtakuwa mmeishakufa. Hao vijana wakitupatia fedha na siye tutawapatia hizi karatasi. Nao wataondoka na ndege yao moja ambayo itawachukua hapa hapa kiwanjani wakiwa kama watu waliokuja katika maonyesho ya mavazi na ambao kwa sasa wanamaliza maonyesho yao na wanarudi nyumbani. Kwa hivyo hakuna binadamu yeyote ambaye atawatilia tuhuma.

"Wakati wakifika Ureno miye na wenzangu tutakuwa tumegawana fedha, tunakula raha tu. Halafu wapigania uhuru watakapoanza kupigwa naweza kutoa kiasi cha shilingi milioni moja kuwasaidia. Na nakwambia nitatangazwa dunia nzima kama mtu mwenye moyo wa pekee na mwafrika safi. Siku moja utakapofufuka ukiwaambia kwamba mimi ndiye niliyewasaliti kwa kuziiba hizi karatasi na kuwapa wareno nao wakapigwa vibaya sana, watakushitaki kwa kusema uongo maana tayari watakuwa wananiabudu kama MUNGU wao mdogo kwa kuwasaidia kiasi hicho. Unaonaje si hekima nzuri sana hiyo?"

"Kwa kweli ni hekima nzuri kama ungefanikiwa, Lakini kwa Sababu hutafanikiwa, hata mimi nakuonea huruma ya ajabu. Ni afadhali usingezaliwa bwana Njoroge maana yatakayokukuta hata watoto wako watajichukia kwa nini walizaliwa na baba kama wewe," nilijibu kwa kiburi sana ingawa sikuwa na bastola hata moja. Bastola zangu walikuwa wameishaninyang'anya.

Nilikuwa na uhakika kuwa, wakati huu lazima Sammy ameishakuwa tayari, alikuwa tu anangoja kuwagutusha. Lulu alikuwa akinitazama kwa macho ambayo yalikuwa yananiambia hadithi za sungura nilizozisoma darasa la tatu. Alikuwa naye ameshikilia bastola mikononi mwake. Benny na vijana wengine walikuwa na furaha ya ajabu maana 'bosi' alikuwa akiwatukuza namna ya jabu.

Kamfungulieni huyo mbwa mwingine humo ndani, nadhani atakuwa bado amezimia, nataka kuwaona wanakula marisasi mbele yangu mwenyewe. Maana naona huyu Gamba ni mshenzi kiasi cha kwamba hanitambui sawa sawa. Kuwa rais wa chama kama hiki, lazima atambue kuwa mimi ni mtu wa pekee, na pia mwenye busara za pekee," alisema 'bosi' huku akimtazama Benny.

Benny alimueleza kijana fulani hapo akafungue mlango - Lulu tu ndiye alionekana hana furaha, huku rangi yake ikizidi kubadilika. Nilidhani huenda anachukia kuona bado naishi. Nilimtazama huku nikitabasamu kisha nikamwambia, "Wewe malaya unachelewa kwenye maonyesho, watu wanakungoja ukawaonyeshe mwili wako huo usio na bei. Mana ni mtu fisadi tu ambaye hathamini mwili wake kiasi cha kuonyesha kwa kila mtu." Lulu hakujibu neno ila tu alitazama chini.

Benny aliniangalia kwa hasira nyingi akasema, "wewe rafiki yangu, huwezi kumwadhiri mke wangu kiasi hicho hali mimi nipo hapa. Hiyo dharau kubwa sana mshenzi wewe."

"Yeeeeeeya, wewe kweli uko nyuma, unadhani huyu fisadi anaweza kukaa na wewe! humjui nini, mbona hukuniuliza zamani nikueleze, maana mimi nina historia yake toka A mpaka Z." nilisema huku nikicheka sana.

Benny alitaka kusema neno lakini kabla hajasema, yule kijana aliyeenda kufungua mlango wa chumba ambamo alifungiwa Sammy alianguka chini na kisu kifuani. Wote walisimama na kuanza kutoa risasi upande ule wa chumba miye niliruka nikaanguka chini ya sofa.

Mle ndani mlikuwa na watu kama kumi na watano hivi wa upande wao. Na miye nilijua Sammy ana visu sita kwa hiyo nilijua watu sita watakuwa wameishakufa kabla hawajatuandama. Lulu alisimama kama anataka kukimbia halafu kwa bahati mbaya akaangusha bastola yake kwenye kichwa changu. Basi niliona sasa tumeishaokoka, maana kama Sammy ataua sita miye wale wengine nitawafanya kazi kabla hizi risasi hazijaisha. Risasi sasa zilikuwa zinapigwa upande wangu na kule mlangoni kwa Sammy. Sammy alifanya mlango kama ngao yake.

Mimi nilianza kazi. Niliposimama niliona watu watano wameishaanguka. Basi miye niliwalisha waliokuwa karibu yangu. Nilipoona mwingine anakula visu nilijua sasa Sammy ameishiwa visu kwa hiyo ilikuwa sasa ni kazi yangu kumuokoa Sammy. Nilijaribu kumpata Benny lakini wapi. Wengi wao walikula risasi mpaka nikaona wamebaki wanne. Benny, Lulu, 'Bosi' na kijana mwingine. Walipoona mambo yamewazidia, walionelea wakimbie. Kweli walikimbia na kupotelea gizani.

Nilimfuata Sammy, nikampa heko kwa kazi yake nzuri aliyokuwa ameifanya kwa wakati huo. Aliniuliza nilipataje bastola nikamweleza iliangushwa na Lulu kwenye kichwa changu wakati nikijificha nyuma ya sofa kuzuia risasi.

"Miye sikubali kuwa aliiangusha kwa bahati mbaya Willy, kila siku nakwambia wanawake wazuri ni sumu huenda ana jambo, maana tangu wanishike kule kwake tabia yake Lulu imenishinda. Jinsi anavyojiheshimu ni ajabu."

"Hata mimi nimemuona hakuwa na furaha wakati wengine wote walipokuwa wanafurahia sana. Sasa tufanye nini Sammy, maana hatujui hawa watu wamekimbilia wapi."

"Mimi nadhani, tukusanye hizi maiti tuzifiche mahala fulani. Kwanza naona bado dakika nne wale wapelelezi wa Ureno wafike hapa. Mimi naona tuwangojee hao hapa maana hawatakuwa na habari kuwa siye ndio tumo humu. Wakija tutawafungulia tukijifanya kama sisi ni walinzi wa Njoroge na kundi lake. Watakapokuwa wameingia ndipo sisi tuwageukie mbogo na kuwaua wote. Lakini lazima tuwe macho maana jua hawa watu pia ni wa kazi kama yetu kwa hiyo lazima wanaweza wakang'amua jambo fulani wakatuwahi kabla hatujawawahi. Pia lazima tuwe tunajua kuwa Benny na kundi lake wanaweza kurudi upesi iwezekanavyo kusudi waje wawazuie hawa watu, au awje na kundi la kuweza kutumalizia mbali. Lakini hii itamchukua muda mrefu kidogo hivyo tutaweza kupata nafasi ya kuwacheza hawa watu."

Mawaidha ya Sammy niliyaona kuwa muruwa kabisa. Tulikusanya zile maiti na kuzitia kwenye chumba fulani. Halafu tukakaa tayari kuwangoja hao binadamu. Nilichukua bastola tatu toka kwa maiti hizo za kundi la Benny, na Sammy pia. Tukajitayarisha vizuri kabisa, maana mara hii tutapambana na watu waliofundishwa kazi hii hii kama sisi.

Mlango uligongwa, miye nilienda kuufungua, Sammy alijificha kwenye chumba kimojawapo, "Come in, the boss is waiting for you," yaani"karibu ndani 'bosi'anawangojea."

Thanks a lot ........" yaani" Asante sana, "walijibu. Walikuwa wavulana wanne na wasichana wawili, nilingoja wote waingie halafu mimi niwatokee kwa nyuma. Yule wa mwisho alipoingia, alitoa bastola mara moja na kuniuliza mahali alipo 'bosi'. Lo, nikaona hapa mambo yatachaga. 

Akaniambia nisitoe sauti, pia akaniuliza idadi ya walinzi wanaomlinda 'bosi'. Nikasema kumi na wanne. Akamweleza na mwenzake akamkubalia kuwa wanaweza kuwashinda tu, ila wakaambiana kuwa lazima wamgutushe 'bosi' na watu wake halafu wachukue hizo karatasi kwa nguvu kisha watoroke.

Unaona sasa mambo yalivyokuwa yanachaga. Miye yaliyokuwa yananitisha sasa. Maana kumbe hawa watu hawakuja na fedha, ila tu walikuwa wamemfanyia 'bosi' akili, waje humu ndani kisha wawanyang'anye hizo karatasi kwa nguvu, halafu wawaue ndipo watoroke na hizo karatasi kwenda zao bila kulipa fedha hata senti moja.

Alitaka kunipiga shingoni na kitako cha bastola, lakini kabla hajaniwahi miye nikakinga kwa mkono na ile bastola ikaruka. Hapo hapo nikatoa zangu vita ikaanza.

Hawa wote sita walionekana watu wanaijua kazi yao barabara. Sammy alitokeza kwa nyuma kwa hiyo tukawaweka mahala pema sana. Fahamu mpaka sasa miye fulana yangu nilikuwa bado ninayo, kwa hiyo ilizidi kunisaidia sana. Mapigano kati yetu na kundi hili yalikuwa makali kupita mengine yote yaliyokuwa yameishapita. Mwishowe tulishinda, wanne wao tulikuwa tumeisha waua na wawili wengine walikuwa wamejeruhiwa vibaya sana.

Tuliwaendea hawa waliojeruhiwa, wakatuuliza siye ni nani, tukawaeleza kila kitu. Nao wakatueleza kuwa kusema kweli nia yao haikuwa kulipa pesa zote hizo, maana serikali yao ni maskini sana kuweza kulipa pesa nyingi namna hiyo. Ila tu walikuwa wamemdanganya Njoroge na chama chake kusudi waweze kuzichukua hizo karatasi bila malipo yoyote.

Sasa lililokuwa limebaki ni kupambana na Njoroge. Tuliona hii itakuwa kazi rahisi zaidi. "Miye Willy naona tungoje hapa maana Benny lazima atarudi, na mimi nataka nimwue Benny maana ndiye aliyemwua Robin, na mimi niliapa nitamwua mtu aliyemwua Robin asiponiua yeye," Alisema Sammy.

"Vema, tutawangoja hapa."

Kidogo tu, simu ililia. "Hallo, ni nani?" Nilijibu huku nikiuliza.

"Sikiliza, njoni karibu na Railway Training School hapa Nairobi South, kuna nyumba moja mfano wa ghorofa chumba nambari saba. Hapa ndipo walipo kwa hiyo msikawie. Bado wanajaribu kukata shauri mahala pa kwenda. "Hii sauti ilikuwa kama ya mwanamke ingawaje ilibadilishwa na kusikika kama ya mwanaume. Tulikata shauri tufanye kama tulivyoambiwa.

Tulienda mpaka karibu na RTS, halafu tukaanza kuitafuta ile nyumba, hii ilituchelewesha sana hata tukadhani tutakuta wameisha toka humo ndani. Mwishoni tukaiona, na hapo tukaenda ndani. Tukaenda mpaka chumba nambari saba. Tulipofika tukapiga mlango kwa nguvu, mpaka ndani. 

Nakwambia tulipoingia hatukuamini hata kidogo. Lulu alikuwa ameshikilia bastola mbili mkononi, Benny na 'bosi' wamekaa huku wameinua mikono juu.
        
"Fanyeni haraka, wamemtuma mtu kuleta kundi jingine la watu. Watafika sasa hivi," alisema Lulu.

"Hii ina maana gani Lulu," aliuliza Benny. 

"Mimi ni mpelelezi kutoka Uganda, ila nilifanya kazi nanyi nikijua tungeweza kuwashika vizuri sana. Tulikuwa na John katika kazi hii. Na ni John tu aliyekuwa akijua kazi yangu. Ulikuwa mpumbavu sana Benny uliponipenda sana. Nami niliwala akili vizuri sana hata wote mkaangukia upande wangu," alisema Lulu huku akimwemweseka.

"Unaona sasa mjomba mambo yalivyozidi kunyumbulika. Kumbe Lulu alikuwa upande wetu. Kwanza siku ile Benny alipotaka kutuchoma na petrol, Lulu alisema wamwendee 'bosi', huku akaponya maisha yetu. Kadhalika na kule chumbani 'Wilson Airport' aliniangushia bastola. Halafu nikiwaambia wasichana ni sumu nyie mnanidhania mimi ni mpumbavu ........."

"Wapi karatasi?" Nilimuuliza Daktari Njoroge.

"Zipo hapa," alizitoa huku akitetemeka.

"Wale Wareno wote tumeisha waua, lakini kabla hujafa nitakueleza kuwa uhalifu haulipi hata kidogo. Wale watu nao walikuwa wamekuzunguka. Nia yao ilikuwa kukunyang'anya hizo karatasi kwa nguvu, halafu wakuue, unaona hiyo," nilimweleza huku nikienda kuzichukua hizo karatasi. Niliziangalia nikahakikisha kuwa kweli zilikuwa zenyewe. 

Hatukutaka kupoteza wakati kwani tulihofia kukutwa na hilo kundi jingine la wahalifu hawa. Hivyo haraka tukapiga simu polisi. Si baadaye motakaa ya polisi ilisimama nje ya jumba hili tulimokuwa, punde askari polisi kadhaa wakaingia tulipokuwa. Nyuso zao ziliainisha ghadhabu iliyokithiri kiwango. Haikosi kila mmoja wao alichukizwa sana na hila za wasaliti hawa ambao ati ni pamoja na wazalendo wa Afrika!

Moyo wangu ulirudi kwa Lina. Kama mwehu, nikawaacha wote na kutia gari moto kwenda kumwona Lina maana mpaka sasa moyo wangu ulikuwa bado ukiniuma kwa ajili yake.

Nilipofika kwa daktari nilingia kwa fujo sana maana nilikuwa na hamu ya kutaka kusikia nini kimempata Lina.

"Daktari, Lina vipi?"

"Naona ataishi, ila kwa sasa usiende kumwona maana unaweza kumsumbua,"

"Hata, lazima nimwone, nisipomwona naweza kuzimia,"

"Hapana usiende kumwona tafadhali."

"Nyamaza daktari." Nilimvuta daktari mkono. Akaona hana la kufanya ila kufanya kama ninavyomwambia.

Nilipoingia Lina alikuwa amesinzia. Nilimwinamia na kuanza kumbusu ovyo. Daktari alicheka akasema. "Naona kweli mapenzi ni hatari-yaweza kuua." Akafunga mlango akaenda zake. Lina alifungua macho yake.

"Oh Willy, nilikuwa nakuota sasa hivi umenikumbatia, kumbe ni kweli. Oh, sasa nimepona kabisa, nibusu Willy nikarejewe na uhai."

"Lina, Lina mpenzi, mimi na wewe mpaka kwa mama Willy kifo ndicho kitakacho tutenganisha."

MWISHO

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU