UCHU

NGUVU YA RUSHWA

III

Simu ilipoita Jean alikuwa amelala. JKS alikuwa amemweleza kuwa vijana walikuwa wamefika salama na kazi ya kumsaka na kumuua Willy Gamba ilikuwa ifanyike usiku ule. Alikuwa amefikiria jinsi Bibiane angeshangaa sana baada ya kuelezwa kuwa Jean ndiye aliyetoa amri ya yeye kumuua. Jean alikuwa mtu aliyefurahia uovu, alikuwa mtu katili afadhali ya mnyama. Alifurahi kusikia mtu akipata maumivu, na hapo ndipo roho yake ilipopata faraja. Pamoja na miaka yoye sita aliyokaa na Bibiane, utafikiri walikuwa mtu na mke wake, yaani mume na mke, bado alipomweleza Col. Gatabazi kuwa lazima Bibiane auawe moyoni mwake hakusikia masikitiko. Kilichomfurahisha na kumridhisha ilikuwa ni pesa na nguvu ya pesa, na si mapenzi. Jean aliabudu pesa kwani aliamini kuwa pesa ndizo zilizompatia uwezo alionao duniani.

Kwa kutumia pesa, Jean aliweza kuwakamata wakuu wa nchi nyingi duniani, hasa katika Afrika na Asia, lakini vilevile viongozi wa ngazi za juu katika serikali za nchi za Ulaya. Alipata kila alichokitaka kwa kutumia pesa. Hivyo, simu ilipolia alijua analetewa habari njema za kuuawa kwa Bibiane na Willy Gamba maana alikuwa amesema alikuwa amesema wakishauawa aelezwe. Kila alipopewa taarifa ya kuuawa kwa mtu alipata faraja ndani ya moyo wake, Ndio sababu maelfu ya Watutsi walipouawa alisikia raha isiyo kifani. Hakika mtu huyu alikuwa mgonjwa, tena mgonjwa sana!.

"Jean", aliitikia kwenye simu.

"Col. Gatabazi hapa".

"Sema Col. Gatabazi".

"Kazi imeharibika".

"Nini?".

"Kazi imeharibika. Vijana wote wameuawa. Bibiane yuko hai na ameokolewa na Willy Gamba. mimi na Nkubana tunaondoka kwenda Kibunda, hatuna muda maana wakati wowote wataanza kutusaka, afadhari tuyaandae majeshi yetu tayari kwa vita", Col. Gatabazi alimwambia Jean.

"Ilikuwaje", Jean aliuliza kwa sauti ya kukata tamaa. Col. Gatabazi alimweleza kwa ufupi kama Nkubazi alivyomweleza.

"Basi tuonane kesho Goma, saa tisa mchana nitakuwa huko, natarajiwa kuja na ndege yangu, lakini nitampitia rafiki yetu Kinshasa", Jean alieleza na kukata simu kabla hata Col. Gatabazi hajajibu kitu.

Jean alipokata simu ya Col. Gatabazi, alitumia muda huo kupiga simu Zambia, Zaire, Afrika Kusini, Angola, Kenya na kumalizia Tanzania.

"Umenipata JKS?", Jean alimuuliza JKS baada ya kumweleza yote yaliyotokea na maelekezo mengine huku JKS akipatwa na shinikizo la damu.

"Nimekupata", JKS alijibu kwa sauti ya kutetemeka.
........................................................................................................................


NGUVU YA RUSHWA

IV

Bibiane alipomaliza kuoga alimkuta Willy amemtengea kikombe.

"Kahawa au chai?"

"Kahawa."

Willy alimmiminia kahawa na alipotaka kumwekea sukari Bibiane alikataa.

"Bila sukari," alisema.

Kwa mara ya kwanza vilevile Bibiane alimuangalia Willy vizuri na kumuona mwanaume mzuri sana, na alipofikiria namna alivyowasambaratisha akina Xavier na kundi lao, mwili wake mara moja ulisisimuka. Halafu, palepale akamfikiria Jean na jinsi alivyompenda na kumfanyia kila kitu lakini akaamua kumuua. Hasira ilimpanda sana, na akaapa kiroho kuwa kwa vile yupo hai atalipiza kisasi.

"Unafikiri nini?" Willy alimwuliza Bibiane.

"Ahera."

"Umeshapona sasa?".

"Xavier alisema mimi na wewe tutaonana ahera baada ya masaa machache, akili yangu inafikiri huenda tupo ahera." wote walicheka.

"Uko tayari kuzungumza lolote," Willy alimuuliza Bibiane huku sauti yake ikiwa imebadilika ghafla na kuwa sauti yenye uzito fulani.

"Niko tayari, nimekuambia kila unachotaka," Bibiane alijibu kwa sauti ya mahaba.

"Wewe ni nani?" Willy alimwuliza.

"Mimi naitwa Bibiane Habyarimana, ni Mnyarwanda, na wewe?".

Willy alishtuka namna alivyo mjibu na kuzidi kuimarisha hisia zake kuwa huyu msichana vilevile alikuwa si mtu wa hivihivi ila alikuwa mtaalamu katika nyanja kama yake. Mara ya kwanza alipohisi, ilikuwa jinsi alivyojirusha nyuma ya kochi pale nyumbani kwake baada ya yeye kuwapiga risasi wale watu wawili, na alivyochupa dirishani kumfuata Xavier. Kwanza alifikiri alikuwa na mafunzo ya kijeshi tu, lakini kutokana na jinsi ya majibizano yao aligundua alikuwa na utaalamu zaidi.

"Willy Gamba, Mtanzania," alijibu na wote wakaangaliana kama wanapimana saizi. "Ningependa nijue historia yako nzima, na usinifiche kitu, mpaka kufikia uhusiano wako na hawa wauaji na hasa huyu aliyekuhukumu kifo bwana Jean", Willy alimwambia Bibiane.

"Nimeshatoa kauli yangu kuwa nitakueleza kila kitu unachotaka niseme. Hivyo, usiwe na wasiwasi nitakueleza, ila itabidi uwe na subira maana ni hadithi ndefu", Bibiane alijibu.

Bibiane alimweleza Willy kwa kirefu maisha yake ya utoto, maisha ya shule, juu ya baba yake na mama yake na akaendelea, "Mwaka nilipoanza kazi baada ya kuhitimu digirii ya kwanza ya lugha katika Chuo Kikuu cha Kigali, wazazi wangu wote wawili walikufa kwa ajali. Nilikuwa nimeanza kazi Wizara ya Mambo ya Nje kama mkalimani.

"Inasemekana kuwa wazazi wangu hawakufa kwa ajali ya kawaida ila waliuawa na vikaragosi vya Watutsi ambao walifikiri kuwa baba yangu alikuwa ndugu yake na Rais. Hivyo waliwaua wazazi wangu ili kumkomoa Rais. Kitendo hicho kiliniuma sana nikawachukia sana Watutsi", Bibiane alieleza.

"Pole sana", Willy alisema kwa sauti ya huruma.

"Kwa kunisikitikia kutokana na yaliyowakuta wazazi wangu, serikali ikanihamishia ofisi ya Rais, huko ndiko nilipokutana na Jean Yves Francois, yeye ni Mfaransa anaishi Paris lakini alikuwa rafiki kipenzi na Rais. Tulionana naye nyumbani kwa Rais ambako alikaribishwa na tulianza urafiki siku hiyohiyo", Bibiane alieleza Willy huku akimwangalia kwa jicho la kuiba.

"Huyu Jean Yves Francois ndiye aliyekufundisha ujasusi?", Willy alimuuliza.

"Umejuaje?".

"Nimehisi".

"Jean ni mfanyabiashara na alikuwa akifanya biashara na kundi la marafiki wa Rais pamoja na familia ya Rais, wakati mimi nafahamiana naye serikali ilikuwa imeanza kuwa na matatizo kwani Watutsi waliokuwa humu ndani na nje, nchini kwenu na Uganda walikuwa wakipigana ili waiangushe serikali. Jean ndiye aliyekuwa akimsaidia Rais kwa kumjenga kijeshi, kiusalama na kiutawala. Huyu Jean ana utajiri usio kifani, kwani ndiye anayezifadhili serikali na wakuu wengi wa nchi za Afrika. Kwa vile mimi pia nilikuwa kwenye himaya yake alinipeleka kwenye mafunzo ya kiusalama sehemu mbalimbali duniani".

"Na ukahitimu vizuri", Willy alidakia.

"Vizuri sana".

"Ehee, endelea".

"Si ni wewe unanikatisha".

"Huu utajiri aliupataje?", Willy aliuliza.

"Sijui mwenyewe ameupataje, ila anashughulika na mambo ya silaha. Hapa alikuwa analeta silaha, halafu anachukua chai yote na kahawa inayolimwa katika nchi. Hili suala ni moja ya malalamiko mengi ya wananchi maana Jean ndiye aliyekuwa akipanga bei anayotaka, na hakukuwa na mtu wa kusema kitu, maana alikuwa akifanya biashara na Rais na kundi lake, lililokuwa likiitwa Akazu. Kusema kweli Jean na hilo kundi la Akazu ndio waliokuwa wanatawala na si baraza la mawaziri au Bunge", Bibiane aliendelea huku sasa Willy akimsikiliza kwa makini zaidi.

"Huoni kuwa hiyo haikuwa sawa?", Willy aliuliza.

"Mimi ningefanya nini, nilibaki kufanya kila nilichoagizwa kama ilivyokuwa kwa wengine wengi maana sasa hii ndio ilikuwa namna ya maisha. Ama uko na Akazu, vinginevyo hupati kitu cha aina yoyote, iwe mali, elimu au kazi ya aina yoyote Rwanda".

"Kwa hiyo rushwa ndio ilitawala utawala uliopita?", Willy aliuliza.

"Inategemea unavyotafasiri rushwa", Bibiane alijibu huku akiwa kama haelewi anasema nini.

"Rushwa ni pale vyombo vya serikali vinaposhindwa kufanya kazi zake, kwa sababu hiyo kushindwa kutoa haki kwa wananchi wake, na kuwafanya wananchi wengi wapoteze imani, utu, uhuru na maadili kwa serikali yao kwani wote sasa huishi kama wanyama ambapo mwenye nguvu na pesa ndiye anayepata anachohitaji", Bibiane alisema.

"Hivyo ndivyo, maana nchi inakosa maendeleo kwani mapato yote ya nchi badala ya kuendeleza watu wote huingia kwenye mifuko ya watu wachache. Na kama ulivyosema uhalali wa serikali kama chombo cha watu unakwisha, badala yale wale wanaofaidika ndio wanakuwa na nguvu zaidi ya serikali yenyewe", Willy alitafasiri rushwa.

"Kwa tafasiri hiyo nakubali kuwa rushwa ndiyo imetawala. Na sasa Watutsi na Wahutu walipoanza kudai demokrasia isingewezekana maana Jean na Akazu hawakutaka kusikia kitu kama hicho kwa vile kingeweza kuingila maslahi yao. Na ndio sababu Watutsi walipokazana na kusikia eti wako tayari hata kupigana na Akazu, kwa kufadhiliwa na Jean, walianza kulifundisha jeshi la wahutu lililoitwa Intarahamwe ili liweze kuwadhibiti Watutsi wa ndani na nje ya Rwanda".

"Kwa hiyo huyu bwanako Jean ndiye alikuwa Rais hapa?".

"Si hapa tu, mimi najuwa nchi nyingi ambako amewakamata wakuu wa nchi na viongozi wa ngazi za juu serikalini na anawajaza mapesa kila wakati".

"Huoni kuwa yeye ndiye ananufaika zaidi, maana anajaza mapesa watu wachache lakini yeye anachukuwa mali za wananchi wengi", Willy alijaribu kumwelimisha Bibiane.

"Najuwa, maana hata huko kwenu Tanzania pia amewakamata wakubwa, ndio sababu nchi yenu imekuwa ikisita juu ya suala hili la Rwanda".

Willy alisitushwa na taarifa hii lakini hakutaka kujionyesha maana kweli msimamo wa serikali ya Tanzania ulikuwa unalegalega kabla na hata baada ya mauaji.

"Ina maana maamzi yoyote ilikuwa lazima Jean akubaliane nao?".

"Ndiyo, na mapesa yalitembea sana kuhusu swala hili na viongozi wengi wamenufaika. Unafikiri kama swala hili lingefanyiwa maamuzi mapema mauaji yangetokea!", Bibiane alimwambia Willy kwa njia ya kushangaza.

"Kwa hiyo huyu Jean ndiye aliamru mauaji haya?".

"Baada ya Rais kuonekana kwamba angekubali mkataba wa Arusha. Jean na Akazu walikasirika sana maana hawakutaka, kama nilivyosema mwanzo, kugawana madaraka na mtu mwingine. Hii ingegusa maslahi yao. Kwa hiyo, kwanza ndio waliamru Rais auawe na pili tayari walikuwa wamewatayarisha na kuwahamasisha Wahutu kuwamaliza Watutsi wote asibaki mtu ili wajihakikishie uwezo wa kutawala milele. Mpango ulikuwa kwamba hata kama jeshi la RPF la Watutsi lingeshinda jeshi lao lazima baada ya kuchukuwa nchi wangeshindwa kutawala maana wangemtawala nani huku Watutsi wote wakiwa wameshauawa, waliobaki ni Wahutu watupu ambao hawawaungi mkono. Hivyo, ingewachukuwa siku chache kuuangusha na kuutokomeza kabisa utawala wa RPF. Hii ingebaki nchi ya Wahutu chini ya utawala wa Jean na Akazu.

Bibiane alipofika hapa ndipo Willy alipoanza kuelewa kwa undani mambo yalivyokuwa. Kumbe mauaji yote haya yalitokana na watu wachache kutaka kulinda maslahi yao ya kunyonya mali ya wananchi, na kutumia hiyo mali kuweza kuwachochea wananchi kuuana!.

Kwa mara ya kwanza Willy aliona jinsi ambavyo nchi zote za Afrika zilivyo hatarini kutokana na rushwa. Kwa vile viongozi wa nchi hizi kuabudu rushwa, hivyo Willy akaamini kuwa tukio kama la Rwanda kumbe linaweza kutokea mahali pengine katika Afrika!.

"Baada ya RPF kushinda na mipango ya Jean kushindwa, wana mikakati gani sasa?", Willy alihoji.

"Kama nilivyosema hawajashindwa. Wewe ndiye umeingilia ndani ya mipango yao, kuna mpango kabambe wa kuisambaratisha serikali ya RPF kutokea jimbo la Kivu, Zaire. Akazu wamekuwa wakiliimarisha jeshi lao katika makambi ya wakimbizi kule Goma na Bukavu, Zaire, huku Jean akiwatumia rafiki zake kutoka Afrika Kusini hasa waliowahi kuwa katika idara ya ujasusi ya makaburu, alikokuwa akinunua silaha na kuzipitishia Angola ya UNITA, Zaire na Zambia kwa kutumia viongozi wa ngazi za juu za serikali za nchi hizo ambao wako kwenye orodha ya malipo kutoka kwa Jean. Kwa hiyo mambo bdo sana Willy, vita ndio sasa karibu vitaanza".

"yaani dunia inafikiri kuwa kambi zilizoko Zaire ni za wakimbizi kumbe ni kambi za jeshi".

"Ni kambi za jeshi na serikali ya Zaire inajua na ndio inayosaidia hata mafunzo. Hata katika kambi zilizoko kwenu Tanzania kuna wanajeshi wa jeshi la zamani na Intarahamwe, na kuna watu wazito katika serikali yenu ambao wanalipwa na huyu Jean ili kuwasaidia hawa watu, kwa hiyo hili si dogo. Kama ulivyosema pesa ni kitu kibaya sana, watu hawaoni tena madhara ya mauaji yaliyotokea bali wanaona pesa tu".

"Swala la rushwa ni swala linalohujumu haki za binadamu, yapaswa lichukuliwe hatua kimataifa katika uzito huo wa haki za binadamu", Willy alijibu kwa hasira.

Bibiane alikaa kimya bila kujibu kitu.

"Wewe ulikuwa uwasaidie vipi Jean na Akazu katika kutekeleza huu mpango wao wa kuivamia tena Rwanda", Willy aliuliza.

"Usije ukanipeleka kwenye mahakama ya mauaji ya Arusha maana mauaji yale sikuyajuwa pia sikushiriki, nilikuwa Nairobi nikitokea kwenye mkutano Arusha. Ila juu ya hili la sasa Jean amekuwa akinituma kupashana habari kati ya kambi za wakimbizi ambazo ni kambi za jeshi lao huko Zaire, yeye na Akazu. Vilevile kuna wanajeshi na viongozi wa RPF ambao tayari wamenunuliwa na wako upande wa Akazu, mmoja wao ndiye anayetarajiwa kuchukua madaraka mara tu jeshi la Akazu litakapotwaa madaraka tena".

Willy hakuamini masikio yake kuwa tayari hata ndani ya RPF kuna wasaliti.

Mara moja Willy alielewa jinsi alivyotaka kuuawa na akagudua kuwa kweli kama anavyosema Bibiane kuna kiongozi wa juu na karibu sana katika serikali ya Tanzania amabye anamtumikia Jean na kundi la Akazu.

"Utasaidia kunipa majina ya watu wote unaowajuwa kuwa wanahusika, maana hiyo ndio njia pekee tunaweza kulikosha jina lako", Willy alimuasa Bibiane.

"Swala la Jean kunisaliti mimi, na kunihukumu kifo, bila kujali yote niliyomtendea kwa hali na mali ikiwa pamoja na kumpa mwili wangu auchezee atakavyo, na jinsi nilivyojitoa kumstarehesha. Willy mimi niko upande wako, kama uko tayari kupambana nao nihesabu na mimi. Jean akishaambiwa kuwa umenichukua ninavyomjua atataka apambane na wewe yeye mwenyewe, ikifika hapo niachie mimi. Majina na mipango yao yote ni juu yako na uongozi wa RPF mjuwe la kufanya kwani jeshi la Akazu, likisaidiwa na viongozi wa nchi kadhaa ambao ni marafiki na Jean watakuwa tayari kuingilia kati. Ni lazima liwahiwe mapema kabla halijajiimarisha sawasawa", Bibiane alieleza.

"Nafikiri swala la vita si letu, ni la serikali ya Rwanda na RPF, mimi nipe hayo majina na kutokea hapo ndipo nitajua kama kazi yangu imeisha au ndio kwanza inaanza", Willy alieleza taratibu.

Bila kuwa ameandika mahali popote, Bibiane alitoa kichwani jina hadi jina akianza na kundi la Akazu mpaka viongozi wa nchi mbalimbali wanaolipwa na Jean huku Willy akiyaandika chini kwa mshangao mkubwa, kwani watu waliokuwa wanatarajiwa wengi wao ni viongozi wanaoheshimika Afrika na kote duniani. Alishangaa zaidi Bibiane alipotaja jina la yule waliyekuwa wakimwita JKS wa Tanzania.

"JKS, hii imenishangaza sana, maana huyu ndiye anayetegemewa kugombea urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu unaokuja," Willy alimweleza Bibiane.

"Najua kabisa, na tayari Jean ameshamtengea mamilioni ya dola za Kimarekani zitakazo msaidia katika kampeni hiyo ya uchaguzi kuusaka urais. Nia ya Jean ni kuwa na marais vibaraka kote Afrika ili yeye na wenzake huko Ulaya, waweze kufanya vile wanavyotaka katika nchi hizi. Jean anaongoza kundi la wafanyabiashara wakubwa wanaomiliki makampuni makubwa ya kimataifa. Na nia yao ni kuhakikisha kuwa Afrika inakuwa soko lao tu, na hata siku moja Afrika isisimame kiuchumi. Ingawaje nchi zao zinapigia kelele rushwa, lakini nchi hizohizo ndizo zinazoyasaidia makampuni makubwa kwa madogo kutoa rushwa kwa nchi zinazoendelea, maana makampuni hayo yakitoa hongo, hongo hii huchukuliwa kama gharama na kutolewa kwenye kodi ya mapato. Hii yote inaonyesha unafiki wa nchi za magharibi, na kila wakati Jean alikuwa akinieleza kuwa kelele zote hizi kuhusu rushwa, demokrasia na soko huria ni kelele za kinafiki tu, lakini huku nyuma katika vikao vya viongozi wa nchi za magharibi ni kuchochea rushwa. Wanajuwa kuwa rushwa ikiisha Afrika basi demokrasia na soko huria vitashamiri na hivyo uchumi wa nchi hizo utakua haraka sana, kitu ambacho hawataki kitokee. Jean anasema, rushwa ndiyo sera inayotumiwa kuendeleza umaskini katika nchi za Afrika ili nchi zilizo endelea ziendelee kuitawala Afrika kiuchumi. Kwa hiyo, iwapo JKS ataitawala Tanzania rushwa itazidi mara dufu, na kutokana na fedha alizotengewa na Jean lazima atashinda, kwani kila walipoweka mtu wao hajawahi kushindwa uchaguzi", Bibiane alieleza.

Sasa Willy alikuwa na picha kamili namna JKS alivyokuwa anahusika na swala zima la Rwanda. na sababu za Tanzania kutokuwa na msimamo dhabiti juu ya swala hili na kuweza kuyumbisha mikutano kule Arusha kiasi cha kutofikia maamzi kwa muda mrefu maana swala hili la Rwanda kwa muda mrefu lilikuwa chini ya Tanzania kwa muda mrefu na JKS alikuwa mmojawapo wa viongozi walioonyesha kuchoshwa na mauaji ya Rwanda. Na alifanya hivyo kwa shinikizo la Jean aliyekuwa akimlipa pesa nyingi na uchu wake wa kutaka madaraka kwa njia ya ruswa ili aweze kuyatumia kwa faida yake na kujinifaisha yeye na rafiki zake. Na ni hii rushwa iliyowanyima Wanyarwanda haki yao mpaka kufikia hatua ya kuuawa vibaya namna ile kweli ni aibu! Aibu sana kwa Afrika nzima.

"Vizazi vijavyo vitakapoyasoma na kuyaelewa matukio haya, hakika hawataamini, watajuwa sisi wote tulikuwa wendawazimu kabisa, kwani ni sisi wote ndio tulioachia hali hii ikafikia hapo ilipo, kwa kuwapa walarushwa madaraka kwa gharama ndogo ya kuuza kura zetu na wao kutumia madaraka tuliyowapa kwa malipo ya fedha kidogo, lazima wayatumie kutuangamiza", Willy alisema kwa uchungu huku akikuna kichwa chake.

Mara moja Willy alimkumbuka Malisa wa Arusha, aliyekuwa mshauri wa JKS katika masuala ya uhusiano wa Kimataifa kabla hajarudi Chuo Kikuu. Hivyo basi, alijuwa Malisa ndiye aliyemweleza JKS kuhusu msimamo na mipango ya PAM na kuteuliwa kwa Willy kufuatilia jambo hili. Willy aliamini kuwa JKS ndiye aliyetoa taarifa za safari ya Rwanda kwa Jean na kundi lake na ndi sababu ndege aliyopanda ikapigwa kabla ya kutua uwanja wa ndege wa Kigali.

"Kwa hiyo JKS ndiye aliyotoa habari zangu zote kwa Jean?", Willy aliuliza kwa shauku.

"Ndio, na ndio sababu Col. Gatabazi aliamru ndege hiyo ipigwe kabla ya kutua uwanja wa ndege, lakini kwa bahati na umahiri wako ukawaponyoka", Bibiane alijibu huku akimwemwesa. Mara mlango wa mbele ukafunguliwa na Col. Gatabazi akaingia ndani.

Willy alipoangalia saa yake ilikuwa yapata saa tisa usiku. Wote walisimama, na Willy akawatambulisha.

"Pole Kanali, leo tumepata mgeni na anaitwa Bibiane, na Bibiane huyu ndiye mwenyeji wetu. Col. Rwivanga, kiongozi katika serikali mpya ya RPF".

"Nashukuru kumfahamu", Col. Rwivanga alijibu.

"Nami nimefurahi kukuona leo, nimekuwa nikisikia sifa zako nyingi kwa muda mrefu, toka kwa Col. Gatabazi kuwa wewe ni mpiganaji hodari, hongera", Bibiane alijibu kwa tabasamu akimwangalia Col. Rwivanga.

"Asante kwa sifa hizo zilizotoka katika kinywa cha msichana mrembo kama wewe", Col. Rwivanga alijibu akaendelea, "Ehe, imekuwaje Willy, hebu nipe habari kamili, maana kazi tumeiona kwa Bibiane, sasa halafu ikawaje hivi", Col. Rwivanga alionekana kuwa wasiwasi na Bibiane.

"Mimi naomba nikalale ili mzungumze vizuri, nionyeshe chumba cha kulala", Bibiane aliomba.

Willy na Col. Rwivanga aliangaliana na Willy ndiye alikuwa wa kwanza kujibu, "Kwa vile nyumba hii ina vyumba viwili tu vya kulala, basi kalale chumbani kwangu, maana tayari hata kuoga umeoga huko. Mimi nitalala hapa sebuleni kwenye kochi hamna taabu".

"Asante", Bibiane aliwaaga na kuelekea chumbani huku wote wakimwangalia. Kisha wakatazamana na kutabasamu.

"Ehe, hebu nipe mambo".

Willy alichukua muda mrefu kumweleza mambo yalivyotokea na mambo mengine yote aliyoelezwa na Bibiane. Col. Rwivanga akasimama na kumshika mkono Willy kwa hatua aliyofikia haraka na kwa umakini mkubwa.


ITAENDELEA 0784296253  

Comments

  1. kazi nzuri sana hii ila nakuomba kaka usikae siku nyingi bila kuiweka

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru